Header Ads

MWANZO MWISHO: AZIZA WA FACEBOOK

FACEBOOK CHATTING
AZIZA WA FACEBOOK
Na Nyemo Chilongani.

Najisikia nimechoka sana, nimechoka sana kwa sababu nilikuwa nimetoka 
kucheza mpira uwanjani huku nikiwa nimechafuka kupita kawaida. Ninapofika 
nyumbani, ninaoga na kisha kuchukua simu yangu kwa ajili ya kuangalia 
updates za facebook, sikukuta hata meseji 
moja zaidi ya notification tu, tena wala hazikuwa nyingi. Nilichokifanya ni kuanza 
kuzugazuga hapa na pale na kisha kutulia. Mara ghafla nikaona namba moja 
nyekundu kwenye sehemu ya meseji, kulikuwa na meseji imeingia, 
nilichokifanya, nikaifungua na kuanza kuchati na mtu huyo huyo.

EDUADO: Mambo vipi Shahruk Khan.
MIMI: Hahahha! Poa. Inakuwaje wewe mtu.
EDUADO: Kama kawa. Nilikuwa nakusubiri sana hewani. Nilikuwa na mzuka na wewe ile mbaya.
MIMI: Duh! Mzuka na mimi! Kuna nini tena?
EDUADO: Kuna bonge la kazi hapa. Unataka?
MIMI: Kwa nini nisitake? Nipe mawasiliano yao niandike barua ya kuomba kazi fasta.
EDUADO: Hahahaha! Kaka unakosea. Niliposema kazi sikumaanisha hiyo.
MIMI: Wewe ulimaanisha ipi sasa?
EDUADO: Kazi moja hivi. Kazi ambayo watu wengi wameishindwa hasa masharobaro.
MIMI: Hahahaha! Itakuwa kubeba zege hiyo watoto wa mama hawaiwezi. Mimi naiweza, hebu niambie ni jengo gani.
EDUADO: Sio kazi ya kubeba zege. Kuna mtu nataka umfanyie kazi.
MIMI: Mtu gani?
EDUADO: Kuna mrembo fulani nipo nae hapa UDSM ni mkali ile mbaya. Yaani mkali
 mpaka nashindwa kusema ukali wake unafanana na nini.
MIMI: Hebu acha masihala kaka. Kwa hiyo kama mkali mimi nifanyeje nini?
EDUADO: Huyu mrembo anaringa mbaya. Yaani mrembo ananata utafikiri akanyagi ardhi hii tunayochimbia vyoo.
MIMI: Ok! Wazuri wapo wengi na hata wenye maringo wapo wengi pia. Hebu niambie kuhusu huyo. Kwanza anaitwa nani. Nipe maelezo ya kujitosheleza na sio naanza kumtengeneza mrembo
mkali kichwani mwangu ikawa ndivyo sivyo.
EDUADO: Huyu mrembo anaitwa Aziza Moody, anaishi Msasani, baba yake ni
mfanyabiashara mkubwa sana aisee. Ni mrembo fulani pini…yaani ni pini sana.
MIMI: Hebu acha masihala. Sasa inakuwaje watoto wa kisharobaro wamemshindwa.
EDUADO: Huyu mrembo hafagilii muonekano, ni mrembo fulani ambaye anapenda mtu
 anamfuate kama jinsi alivyo. Yaani kama wewe ni mtu wa chini, mfuate hivyo hivyo ila tatizo
watoto wa hapa chuo wanapenda kumfuata kisharobaro kaka.
MIMI: Dah! Kwa hiyo kazi unayotaka kunipa ni ipi?
EDUADO: Umchukue huyu mtoto. Yaani ukifanikiwa, moyo wangu utakuwa mweupeeeeeee
 kama theluji.
MIMI: Hahaha! Usitake kunichekesha EDUADO, hivi unamkumbuka Sikitu?
EDUADO: Sikitu yupi?
MIMI: Si yule mrembo wa mwaka jana ambaye ulikuwa unamsifia sanaaaaa kwamba
 mkali kumbe wala hakuwa mkali kama ulivyokuwa ukimsifia, mbaya zaidi alikuwa anakaa mbali, Musomaaaaaa.
EDUADO: Acha na hayo, yule msahau kwani mimi mwenyewe alinitumia picha ambayo sio
 yake. Ila kaka kiukweli Aziza ni mrembo mmoja mkali sana. Hapa chuo amekuwa
 gumzo kila kona, vijana wengi wamechemka.
MIMI: Sasa kama wengine wamechemka mimi nitaweza vipi?
EDUADO: Hahahaha! Kaka ninakuamini sanaaaa, wewe mtu unaweza sana kuongea,
unaweza sana kuandika. Endapo kazi nikakupa na kisha ukashindwa, haki ya Mungu nitajua kweli
duniani kuna wasichana wagumu.
MIMI: Kwa hiyo kazi yako ina malipo au?
EDUADO: Ikitokea umempata, nitakupa zawadi kaka. Yaani ninachokitaka huyu mrembo
umchukue tu, basiiiiiiii. Anaringa sana, ananata sana, yaani sijui niseme vipi.
MIMI: Ila si anaringa kwa sababu mzuri?
EDUADO: Ndio. Ila yeye kazidi.
MIMI: Ila kwa sasa aisee nahisi nimepoteza kumbukumbu zangu za kuongea na hawa
 watoto wa kike, sijui kama nitaweza.
EDUADO: Acha kunitania kaka. Nakuamini sana kwamba unaweza kuliko mtu yeyote
na ndio maana nikakufuata wewe. Hivi haujiulizi kwa nini sikumfuata Thomas? Thomas
kwenye kuongea mkali sana ila kwenye kuandika hakuna kitu, ila wewe, aisee una kipaji
kila kona, nafikiri hata ukimtokea kiziwi, hachomoiiiiiiiiii.
MIMI: Hahaha! Hebu acha kunipamba. Hebu niambie, huyo mrembo yupo Facebook?
EDUADO: Amejaa teleeee…yaani kajaa teleeee. Anajiita Aziza M Aziza. Ni mrembo mkali sana.
Hebu mcheki kwanza.
MIMI: Sawa.

Sikutaka kuchelewa, tayari kichwa changu kikaanza kujazwa na sura nyingi za wasichana
wazuri huku nikianza kuzigawanya kimakundi kwamba huyu alikuwa Aziza mwenyewe
huyu hakuwa mwenyewe. Nilikuwa namfahamu EDUADO toka tupo katika shule ya
sekondari, alipokuwa akisema msichana fulani ni mzuri, mzuri kweli japokuwa kwa
Sikitu alikuwa ameniingiza choo cha kike. Sikutaka kuremba, mara baada ya kuona
 majina kadhaa, nikamfuata Eduado inbox.
MIMI: Oyaa Akshey.
EDUADO: Vipi ushampata?
MIMI: Wamekuja wakina Aziza wengi hao, mpaka wengine wanakaa India.
EDUADO: Hebu subiri.
Sikujua alikuwa akifanya nini, kwa sababu aliniambia kwamba nisubiri,
wala sikuwa na presha, nikamsubiri nione angeniambia kitu gani baada ya hapo.
Nilimsubiri kwa kipindi kama cha dakika moja hivi, akanijia tena inbox.
EDUADO: Umeiona hiyo picha yenye mdoli wa Barbie?
MIMI: Yeah!
EDUADO: Ndiye yeye huyo. Ibra huyo ni mrembo mkali ambaye sijawahi kuona.
MIMI: Acha utani.
EDUADO: Shua. Unamkumbuka Silvia tuliyesoma nae? Sasa Silvia haingii kwa Aziza.
MIMI: Acha utani kaka. Silvia haingii?
EDUADO: Kweli tena. Tena hagusi hata robo.
MIMI: Sasa mbona hajaweka picha yake, nitamjua vipi kama ni mkali.
Hebu nipe sifa kwanza manake naona picha zake kazipiga pini watu wasio
 marafiki zake wasizione.
EDUADO: Kwanza mrembo ni pini sana, mrembo kwao wana mahela ya kumwaga,
chuo anakuja na gari, Verrosa moja nyeusi, mtoto anamiliki laptop aina ya
Apple ile inaayouzwa milioni tatu, mtoto anamiliki anamiliki iPhone
5 huku akisema kwamba iPhone 6 ikianza kuuzwa atataka kuanza kuitumia
 kwani anapenda kwenda na wakati.
MIMI: Kaka utakuwa unanitania tu.
EDUADO:  Kweli tena. Halafu kuna cha zaidi.
MIMI: Kipi?
EDUADO: Otea.
MIMI: Hebu niambie kipi?
EDUADO: Ugonjwa wako.
MIMI:Unamaanisha nini?
EDUADO: Mtoto Mpemba.
MIMI: Hahahaha! Kaka acha utani, utanifanya nimfuate sasa hivi.
EDUADO: Ndio hivyo. Mtoto ni pini sana, pini ile iliyosimama.
MIMI: Hahaha! Pini kama ya Blackberry vile.
EDUADO: Acha kaka. Mtoto ni pini zaidi ya zile za Blackberry.
Kwanza ukimuona tu, mtoto utampenda. Mavazi yake sasa…weeeeeee.
1
MIMI: Hebu nipe sifa zake kwa ujumla.
EDUADO: Nisikilize. Mtoto ni wa kipemba.
Ana nywele ndefu zinazomfikia chini ya mabega yake,
mtoto ana hipsi zilizopangika, hapa mashavuni mwake ana vijishimo viwili,
lipsi lainiiiii kila wakati zinang’aaaaa.
MIMI: Kingine?
EDUADO: Mtoto ana sura nyembamba, masikio hayaonekani sana,
ifuani hapa kumesimama vizuri sana, mavazi yake huwa ni suruali za jinsi kwa sana.
MIMI: Umesema anaishi wapi?
EDUADO: Anaishi Masaki.
MIMI: Halafu mimi naishi uswahilini Tandale. Umesema anamiliki simu gani?
EDUADO: Anamiliki iPhone 5.
MIMI: Halafu mimi namiliki Nokia ya Tochi. Umesema baba yake ana gari?
EDUADO: Yeah! Yeye mwenyewe analo.
MIMI: Mimi sina gari na baba yangu hana hata gari.
EDUADO: Acha kujizarau Ibra. Mtoto unang’oa huyu.
MIMI: Usijali. Ushawahi kufika kwao?
EDUADO: Yeah kaka. Kwanza hiyo nyumba yao….duh! Kuna watu wanakufuru. Kwanza bonge la nyumba. Limezungushiwa ukuta, jumba lina fensi kwa juu, ndani kuna kamera, nyumba vigae, ukiingia ndani unakutana na bwawa la kuogelea. Kuna ungo wa Dstv, kuna bustani kali ya maua mbalimbali, kuna walinzi wawili ambao wanalinda kwa bunduki kutoka Knight. Yaani wapo full.
MIMI: Ok! Mimi naishi Tandale. Nyumba yetu ndogo, haina ukuta wala fensi, haina mlinzi na kama kuogea, tunaogea bafuni na si kwenye bwawa. Mpaka hapo, nimeshamkosa.
EDUADO: Ibra. Usiniangushe. Yaani mimi lengo langu umchukue huyu mtoto tu.
MIMI: Una namba zake za simu?
EDUADO: Hapana.
MIMI: Basi ngoja nifanye mishe halafu nione itakuwaje. Ila wasiwasi wangu ule ule tu, itakuwa kama Sikitu.
EDUADO:  Usijali kaka. Huyu sio kama Sikitu. Kwanza yule demu mwenyewe alinitaka nikaamua kukurushia wewe. Mimi na mrembo wa mkoa wapi na wapi. Ishi Dar tuwe tunamalizana, mambo ya mikoani haya, tigo pesa zinatumika sanaaaa. Hapa hapa Bongo ndio kuzuri, ukimtaka tu,
 nauli yako sh 400 kwenda, 400 kurudi. 600 soda yako, 600 soda yake. Mwisho wa siku kwa
 gharama zote ukitoa buku tano, michenji inarudi mingi mpaka mfuko unaomba poo kwa kuzidiwa uzito.
MIMI: Hahaha! Umeonaeeeee. Hakuna gharama kabisa. Ila poa, usijali. Ngoja nimtumie friend request halafu nianze kumfanyia uninja. Ila niandalie zawadi yangu.
EDUADO: Usijali kaka. Wewe fanya yako, ukimaliza, niache nami nifanye yangu. Au sio?
MIMI: Poa. Mia mia. Ngoja nianze kazi.
EDUADO: Shwari. Ngoja nifanye yangu. Nataka nimfuate mtoto Magreth hapa.
MIMI: Ndio yupi huyo?
EDUADO: Si yule wa facebook wa kipindi kileeeee.
MIMI: Kwani ushang’oa?
EDUADO: Chezea mimi wewe. Mimi noma…kama ni wembe basi Gilette.
MIMI: Sasa mbona hujamkata Aziza kama ni Gilette.
EDUADO: Aziza ana chembechembe za chuma. Ningemkataje? Huyo nakuachia kama wewe mwenye yale maji ya kuyeyushia vyuma ndio utakwenda nae sawa.
MIMI: Basi poa. Acha nikufanyie kazi yako mkurugenzi. Kazi hii niliachana nayo zamani sana ila kwa ajili yako, navaa gwanda nikukamilishie halafu nisepetue.
EDUADO: Mia mia.

Hapo nikatulia kwanza. Nikaanza kujifikiria ni kwa jinsi gani nilitakiwa kuanza kumfuata msichana Aziza. Kitu ambacho kilikuwa kikiniumiza kichwa changu kwa wakati huo ni kwamba hata Aziza mwenyewe sikuwahi kumuona kwa hiyo niliogopa kuuziwa mbuzi kwenye kiroba kama ilivyokuwa kwa Sikitu. Ngoja nikupe kijistori changu na huyu Sikitu.
Eduado alinifuata inbox na kuniambia kuhusu Sikitu, alimsifia na kumpamba sana, alinifanya nivutiwe nae sana na yeye alitaka nimchukue, nikasema poa. Mzee nikaanza mishemishe zangu kama Michael Scotfield wa Prison Break na kweli ndani ya wiki mbili, mtoto akawa mikononi mwangu. Unajua jinsi mtu anavyokwambia kwamba msichana mzuri hata kama wewe mwenyewe haujamuona unaanza kumtengeneza msichana wako kichwani, hivyo ndivyo nilivyofanya kwa Sikitu. Nikamtengeneza Sikitu wangu kichwani, kumbe nilikuwa namuumba Sikitu wa tofauti bila kujua. Siku aliponitumia picha yake inbox niione mara baada ya kumlazimisha sanaaa, akanitumia. Alikuwa mrembo lakini hakuwa na urembo kama ambao Eduado aliniambia. Nikaachana nae.
Sikitu hakukoma, chating zangu nzuri za inbox za maneno ya hapa na pale alikuwa akizipenda sana, hivyo alitaka tuendelee kuchati. Haikuwezekana tena, nilimkatia maguu mara baada ya kuniambia kwamba anaishi Musoma, mbaya zaidi huku Dar hakuwa hata na ndugu kwa hiyo hakuwa na ndoto za kuja Dar, sasa mimi ningeonania nae wapi? Yaani nisafiri mpaka Musoma kwa ajili yake? Niliona kuwa suala gumu sana kufanyika. Basi ndio hivyo, tukapotezana potezana na hatimae mapenzi kutoweka, siku hizi simuoni, bila shaka, kaniblock.
Baada ya miezi miwili, leo Eduado kaja na mpya, kaja na mrembo mpya ambaye wala sijawahi kumuona, huyu anaitwa Aziza. Sikutaka kufanya vitu kwa presha sana, nilichokifanya ni kumuomba urafiki na kisha kuanza kusubiria majibu. Kila siku nilipokuwa naingia facebook, hakuwa amenikubalia, sikuwa na shaka, niliendelea kusubiria zaidi na zaidi na baada ya siku mbili, akakubali kuwa rafiki yangu, furaha iliyoje? Hapo ndipo nilipoamua kuuanza mchezo wangu, mchezo ule ule ambao ulimfanya Sikitu kuchanganyikiwa kwangu, ila kwa hapa, kutokana na sifa ambazo niliambiwa na Eduado, ilinipasa nitumie mbinu kubwa zaidi, mbinu ambazo zingeendana na uzuri wake, mtoto wa kipemba bwana, hakutakiwa kufuatwa kikawaida, nami nikaanza kumfuata kipemba kipemba na mapenzi ya Kihindi….mtu mzima nikawa najiona kama Shahruk Khan vile.
****
   Mtu mzima nikaingia kazini kwa ajili ya kuanza kazi yangu ambayo nilikuwa nimepewa ya kuhakikisha kwamba mtoto wa Kipemba, Aziza anakuwa wangu. Ni kweli kwa mambo ambayo alikuwa amenieleza Eduado yalikuwa yamekwishanitenga kwa kiasi kikubwa sana kutoka kwa Aziza lakini ilitakiwa pia nifanye yangu katika kipindi hicho.
Kitendo cha Aziza kuukubali urafiki pamoja nami kilionekana kuwa kitu kizuri sana, kwa hiyo nilichokifanya nikajifanya bonge la bwege, nikamfuata kwa wall yake na kuandika ‘Asante A’ na kisha kusikilizia.
Kweli, kama alivyosema Eduado ilikuwa vile vile, mrembo hakuiLIKE asante yangu wala kuitolea comment, nikaona poa, vyote hivi ni mwanzo wa kumbukumbu zangu nitakazompa hapo baadae. Kwa upande wa Eduado, hakutaka kujishika, kila siku alikuwa akinisumbua tu kwa inbox.
EDUADO: Kaka vipi?
MIMI: Kuhusu nini?
EDUADO: Mtoto. Hujaniambia chochote kile. Umefanikiwa au?
MIMI: Wewe umeniambia mambo mengi kuhusiana na huyu mrembo, unadhani ningeweza kumamilisha ndani ya siku tatu?
EDUADO: Hapana. Nilikuwa nauliza manake nimeona hapa sasa hivi u rafiki yake.
MIMI: Yeah! Ni rafiki yangu ila kila kitu kinatakiwa kufanywa kimahesabu.
EDUADO: Usiniangushe basi Sharukh Khan.
MIMI: Hilo usijali.

Katika kipindi hicho nilikuwa nafikiria mambo mengi sana, huyu mtoto kwangu alionekana kuwa na pozi ajabu, yaani nilikuwa nikizipitia post za kizushi alizokuwa akiziweka, watu walikuwa wakicomment halafu yeye hatokei. Hata kama kaweka picha ya mdoli, watu walikuwa wakicomment halafu yeye hatokei na mbaya zaidi kulikuwa na watu wengi wanaolike na kucomment jambo lililonifanya kugundua kwamba kuna siku huyu msichana alikwishawahi kuweka picha na hivyo wanaume kujua ni mzuri na kisha kuzitoa.
Bado kiu yangu ilikuwa ni kuwasiliana na Aziza tu ambaye alionekana kuwa mtu wa mapozi sana. Sikujua ningeanzia wapi ila nilichokifanya ni kuanza kumtumia meseji nione kama angeijibu au kuipotezea.

2

MIMI: Mambo!
Niliituma meseji hiyo, siku ya kwanza, ya pili, ya tatu mpaka wiki hadi mwezi lakini meseji ile moja haikujibiwa, mbaya zaidi nilikuwa namuona yupo hewani. Sikukoma kidume mimi, bado nilikuwa nikimtumia meseji za kumsalimia lakini hali ilikuwa vile vile, hakujibu.
Mtu mzima nikaona naumbuka, kama nilikuwa naitwa Sharukh Khan basi ilibidi niwaonyeshe watu kwamba hawakukosea kuniita jina hilo, nilitaka kuwaonyeshea dhahiri kwamba mama yangu alikuwa mtu wa Tanga, kule ambapo mapenzi yalikuwa yamenogeshwa kwa kuwekewa makorokocho. Nilichoanza kukifanya ni kuanza kumtag picha. Hapa ni lazima ugundue, picha ambazo nilikuwa nikimtag ni zile ambazo zilikuwa na muonekano wa kimapenzi tu. Picha ambazo zilikuwa zikiwaonyesha wapenzi wakibusiana na kukumbatiana, ndizo ambazo nilikuwa nikimtag, tena yeye peke yake.
Hahaha! Ule ukaonekana kama ujinga vile kumbe kwa wakati huo nilikuwa na target zangu kichwani. Niliendelea na mtindo ule ule mpaka siku ambayo akaonekana kuchoka na kukasirika, kwa mara ya kwanza akaja inbox, ila sio kiamani kama nilivyotaka, alikuja kibifu.

AZIZA: Naomba usiwe unanitag mapicha yako.

Niliisoma meseji ile. Kwanza nikacheka, kilichonifanya kucheka ni kwa kumuona kwamba alikuwa msichana mjinga sana, kitendo cha yeye kuniandikia meseji kilionekana kuwa kama kosa kubwa sana, nilichokifanya, nikaanza kuandika meseji ndefu, meseji ambayo ingemfanya kunijibu, meseji ambayo isingemfanya kubaki kimya.

MIMI: Kuna vitu kadhaa Aziza itakupasa uelewe na ninatumaini vitakuongoza katika maisha yako yote. Jitahidi kuishi lakini kamwe usiwe mbinafsi. Unapopata kitu, usitake kukaa nacho, jaribu kuchangia pamoja na wenzako. Unapopata chakula, jaribu kumwangalia yule asiye na chakula na kumgawia, milele atakushukuru kwa ulichomfanyia siku moja tu alipokuwa na njaa. Unapomuona mtu hana nguo, mgawie nguo na ataendelea kukushukuru maisha yake yote. Unaniona mimi, mimi si mbinafsi hata mara moja, katika maisha yangu nimekuwa nikiwapa watu vitu fulani vitu ambavyo hawana katika maisha yao, nikakuangalia wewe, nikakuona kwamba u masikini sana, ukijiangalia, unajiona kuwa tajiri, mwenye fedha labda, lakini bado ni masikini, masikini wa kitu kimoja ambacho ulihitaji mtu mwenye kitu hicho akusaidie, nikakusaidia lakini unaonekana kuukataa msaada wangu. Kuwa makini Aziza, mara nyingine msaada huja mara moja na kupotea, unapoutafuta, inawezekana usiuone tena.


Kwanza nikashusha pumzi nzito, nikaiangalia meseji ile na kisha kuirudia rudia mara nyingi nyingi na kisha kuituma. Niliiona kuwa meseji kali ambayo isingemfanya kubaki kimya kwa kutaka kujua ni kitu gani ambacho alikuwa amekosa katika maisha yake, kilichonifurahisha, akatuma meseji. Kuna nini tena? Meseji ya pili hiyo, hakujua kwamba ndio mwanzo wa chating yetu.

AZIZA: Umemaanisha nini?
MIMI: Nimemaanisha kwamba wewe ni masikini. Tena yule fukara kabisa. Hiyo ndio maana yangu.
AZIZA: Sijakuelewa.
MIMI: Hebu isome vizuri hiyo meseji, utaielewa tu.
AZIZA: Nimeirudia zaidi ya mara tano, sijaielewa, naomba uniambie umemaanisha nini.
MIMI: Nikuulize kitu kimoja?
AZIZA: Niulize.
MIMI: Unaweza kugundua ni umasikini wa aina gani umekuwa nao?
AZIZA: Hapana na ndio maana nikauliza.
MIMI: Inawezekana ukawa na magari, nyumba na fedha ila bado ukawa masikini, unakubaliana nami?
AZIZA: Hapana.
MIMI: Kwa sababu gani?
AZIZA: Mtu ana kila kitu, atakuwaje masikini.
MIMI: Hahahah! Aziza. Ukisema hivyo unakosea. Kuwa na kila kitu haimaanishi kwamba wewe si masikini. Unaniruhusu nikuulize kitu?
AZIZA: Niulize
MIMI: Unaamini katika fedha?
AZIZA: Yeah!
MIMI: Fedha inaweza kukupa kila ukitakacho?
AZIZA: Yeah!
MIMI: Unakosea sana Aziza.
AZIZA: Unapokuwa na fedha unanunua gari ulitakalo, unanunua chakula, unanunua nyumba na mambo mengine. Kwani nimekosea?
MIMI: Umepatia. Ila unavyoona kila mtu mwenye fedha huwa na furaha?
AZIZA: Inawezekana.
MIMI: Umekosea. Umekwishawahi kuwasikia wale matajiri wanaojiua?
AZIZA: Yeah!
MMI: Sasa wamekosa nini wale katika maisha yao? Wana fedha, wanaweza kununua kila kitu, wana magari, wanaweza kwenda sehemu yoyote ile. Ila swali linakuja kwa sababu gani wanajiua?
AZIZA: Mmmh! Sijui.
MIMI: Hahaha! Jibu rahisi sana. Walikosa furaha, amani, wakakosa mapenzi na mambo mengine. Unapokuwa na fedha, utanunua gari ila kumbuka hautoweza kununua furaha, unapokuwa na fedha utaweza kumnunua msichana mtaani lakini ukashindwa kununua mapenzi. Umenipata hapo?
AZIZA: Kidogoooo.
MIMI: Yeah! Kila mtu hunipata kidogo, ila tukiendelea kuchati, utanipata sana tu. Utaniruhusu niwe nachati nawe kwa ajili ya kukuambia mengi usiyoyajua?
AZIZA: Yeah! Ila huwa siwi hewani muda wote.
MIMI: Hilo si tatizo. Unachotakiwa ni kunishtua kila unapokuwa hewani. Utakwenda kufahamu mengi ambayo haujayajua. Kwani unaishi wapi?
AZIZA: Nipo Masaki Dar es Salaam.
MIMI: Ndio maana.
AZIZA: Kwa nini?
MIMI: Usijali. Mtaa unaokaa ndio nitakaoanza nao siku tukianza kuchati. Kwa sasa nahitaji kusoma, naomba uniruhusu niondoke.
AZIZA: Ila pleeeaseeee naomba uniambie.
MIMI: Sijakataa. Nitakwambia tu wala usijali. Wewe ni rafiki yangu, pamoja kuwa na kila kitu, yakupasa kupata vitu vingine ambavyo haupaswi kuvinunua. Nitakwambia namna ya kuvipata na inawezekana hata marafiki zako wakakushangaa.
AZIZA: Mmmh!
MIMI: Usigune. Huo ndio ukweli. Usiku mwema Aziza.
AZIZA: Nawe pia.

Kuna nini tena? Nilichokifanya ni kutoka hewani mpaka saa sita ndio nikaingia tena, Aziza hakuwepo, nikamtafuta Eduado, nikamuona, hata kabla sijamtumia meseji, akaniwahi.
EDUADO: Vipi Sharukh Khan. Imekuwaje au bado?
MIMI: Kwisha habari yake. Anacheza na mwanasaikolojia nini.
EDUADO: Imekuwaje tena?
MIMI: Wewe usijali. Cha msingi andaa zawadi yangu.
EDUADO: Umeanza kufanikisha?
MIMI: Ndio maana yake. Unajua ukimjua mpinzani inakuwa rahisi sana.
EDUADO: Dah! Wewe noma kaka. Yaani hii kazi nimewapa watu saba, naona wengine wanambwela tu, wananiambia kila wakimtumia meseji dogo hajibu.
MIMI: Hahahaha! Hata mimi ilikuwa hivyo hivyo. Nilivyoona anashindwa kujibu, nikatumia plan B. Hapo ndipo nilipompoteza na kuchati nae sana.
EDUADO: Kwa hiyo ulichati nae?
MIMI: Yeah! Tena mimi ndiye nimemkatisha. Chezea mimi wewe.
EDUADO: Hahahah! Ebwana wewe nomaaaaa....sasa hata kukutambulisha kwa mrembo wangu mwingine naogopa.
MIMI: Wewe si ulinipa kazi kaka? Hakuna tatizo. Kazi inafanyika taratibu.
EDUADO: Duh! Kaka nashukuru sana kwa kunisikiliza. Natumaini mtoto ataeleweka tu.
MIMI: Amekwishaeleweka. Dogo amekwishaeleweka.
EDUADO: Hahahah! Basi poa sana, nimefurahi sana.
MIMI: Usijali kaka...hug.
EDUADO: Poa.

Kila kitu kikaonekana kuwa juu ya mstari, meseji moja ambayo alikuwa amenitumia ikaonekana kubadilisha kila kitu. Ile meseji ndio ambayo nilikuwa nikiitaka kuiona na kweli aliituma. Chatting zikawa zimeanza, kwa Aziza, nilihitajika kuwa makini sana kupita kawaida kwani kwa kufanya vile nilikuwa na uhakika wa kumchukua ili kumuonyeshea Eduado kwamba nilikuwa Sharukh Khan.
                        ****
   Sikutaka kuleta shobo tena kwani tayari nilimuona kuku kuwa wangu kwa hiyo sikutakiwa kumshikia manati kwa kuamini kwamba jioni ikifika mwenyewe atarudi bandani. Nilipoingia hewani siku iliyofuatia, msichana Aziza alikuwepo, kajaa tele ila mtu mzima nikaamua kuchuna. Katika hili ngoja nikwambie kitu kimoja rafiki yangu hasa mwanaume kama mimi. Unapoona kwamba kuna msichana fulani unampigia sana misele facebook, hautakiwi kila wakati umuanze wewe tu, sometimes unamchunia uone je ataweza kukutumia meseji au la. Ukiona kwamba kakutumia, basi jua kwamba anautambua mchango wako na hata kwenye ile mishemishe yako anaonekana kuifurahia. Ila ukiona nae anakaa kimya, mtu mzima poteza kwani si unajua warembo wapo wengi! Inawezekana haujapangiwa kuwa na huyo.
   Nilipomuona Aziza hewani, nikamchunia kana kwamba sijamuona huku nikiamini kwamba yeye ndiye alipaswa kunitumia meseji. Ila katika kipindi hiki hasa siku ya leo, meseji zilikuwa zikiingia nyingi nyingi hasa kutoka kwa marafiki zangu wengine, bahati nzuri nilikuwa natumia kompyuta hivyo ilikuwa rahisi kuwajibu.

IBRA: Mambo vipi kaka!
MIMI: Poa. Ni aje mkuu?
IBRA: Kama kawa. Upo wapi?
MIMI: Nipo gheto aiseee nimesizi tu si unajua kijimvua nje kinazingua.
IBRA: Yeah! Hilo kweli kaka. Hivi unamuona mtu wangu hapo hewani?
MIMI: Nani?
IBRA: Tina.
MIMI: Dah! Hapa namuona kwa kuotea, mara anakuja mara anatoka. Kama vipi mcheki kwa whatsapp.
IBRA: Kwani yupo huko?
MIMI: Yeah!
IBRA: Dah! Basi nafikiri kule atakuwa kaniblock mtu mzima. Simuoni kabisa.
MIMI: Hahahah! Kaka pole sana. Umeblockiwa...hahaha! Tatizo lako uliremba sana kwa kujifanya umeoa, full mauhakika.
IBRA: Unajua nini kaka, kila siku naamini kwamba mwenda pole ndiye mla nyama.
MIMI: Usitake kuniambia hivyo. Wahenga wengine walikuwa wakizingua tu, kidogo naweza kumuamini yule aliyesema chelewa chelewa utakuta mwana si wako. Si kwamba unamuona kinyonga anatembea taratibu ukajua hata yeye anajua kwamba anatembea taratibu, mwenzako pale anajiona anakimbia kwa kasi sana. Hahahaha! Na bado...atakublock mpaka whatsapp.
IBRA: Akiniblock na huko tena, nitamuona katili sana kaka.

Huku nikiendelea kupiga stori na Ibra, mara Emmanuel Solo nae akaingia kwa inbox yangu. Sikuwa na jinsi, nilikuwa nachati nao huku nikimuona Aziza hewani ila nami nilikuwa nimemlia pini tu.

SOLO: Kaka.
MIMI: Niambie.
SOLO Upo wapi?
MIMI: Nipo gheto. Wewe upo wapi?
SOLO: Nipo Morogoro kama kawaida yangu.
MIMI: Duh! Wewe noma. Ndani ya wiki moja umetembea mikoa mitatu. Big Up mkuu.
SOLO: Kutafuta kaka. Maisha kutafuta. Si unamuona hata Ndimanga Hassan, anatembea zaidi ya mikoa kumi kwa mwezi, hatutakiwi kukaa sehemu moja. Hadithi imeishia wapi?
MIMI: Ipi? Zipo nyingi tu.
SOLO: Ile ya yule msichana mwimbaji wa kwaya aliyekuwa amepanga mauaji kwa mvulana ambaye alikuwa amemkataa kanisani na kuamua kutaka kumuua nchini Zambia.
MIMI: Bila shaka unaizungumzia HER HIDDEN FACE, si ndio?
SOLO: Yeah!
MIMI: Ile ipo sehemu ya tano. Inaendelea kama kawa.
SOLO: Basi poa. Ngoja niitafute niendelee kuisoma.

EDUADO: Kaka
MIMI: Niambie kijana.
EDUADO: Mtoto leo kaja chuo aisee kapendezaje!
MIMI: Acha utani.
EDUADO: Sure. Mtoto ni noma kaka. Mtoto mrembo mpaka anajishangaa. Namuona hewani, ushatupia mambo?
MIMI: Hapana. Nangoja anianze, asiponianza nampotezea tu kwani si lazima kivile kuchati nae na kumshobokea.
EDUADO: Ila kaka fanya mambo bhana. Huyu mrembo sitaki umkose kabisa.
MIMI: Usijali kaka. Huyu mdogo mdogo mwisho wa siku utamkuta gheto kapumzika. Chezea Tandale wewe.
EDUADO: Hahaha!

AZIZA: Mambo!
MIMIl Mabaya.
AZIZA: Ubaya wake?
MIMI: Naumwa.
AZIZA: Nini tena jamani?
MIMI: Maralia. Yaani mbu mmoja tu jana chumbani kwangu ndio alisababisha majanga yote haya.
AZIZA: umekunywa dawa?
MIMI: Hapana.
AZIZA: Kwa nini sasa jamani?
MIMI: Naogopa sana dawa Aziza. Labda uje uninyweshe kinguvu.
AZIZA: Dah! Pole sana Ibra. Nitakuombea kwa Mungu akuponye.
MIMI: Asante sana. Nitafurahi sana.
AZIZA: Aya nishakushtua. Hebu niambie kuhusu vitu ulivyokuwa ukiniambia.
MIMI: Tatizo lako unajiamini sana Aziza halafu unafanya makosa sana kila unapoona kwamba fedha ndio kila kitu. Yaani haujifikirii kama kuna watoto wa matajiri ambao wanaumwa sana mpaka wanakufa, kama fedha ni kila kitu si wangepona.
AZIZA: Nafahamu.
MIMI: Basi kama unafahamu, fahamu pia kuna kitu ambacho ni kila kitu na si fedha kama unavyofikiria.
AZIZA: Kipi tena.
MIMI: Mungu ndiye kila kitu katika maisha yetu. Bila Mungu, huwezi kuwa na furaha hata kama una fedha, bila Mungu huwezi kupona ugonjwa wako hata kama una fedha na kutibiwa na madaktari wakubwa duniani. Umenipata?
AZIZA: Ndio nimekupata.
MIMI: Au hadi hapo unataka kubishana tena?
AZIZA: Hapana. Ila unaonekana kuwa na hekima sana Ibra.
MIMI: Yeah! Unajua wakati mwingine yatupasa kuutambua ukweli. Hatutakiwi kuamini sana katika fedha. Ila achana na hayo. Wewe ni mama wa nyumbani, mwanafunzi wa sekondari au mwanafunzi wa chuo?
AZIZA: Naonekaje?
MIMI: Profile picha yako ni ya mdoli, sasa nitajua unaonekanaje?
AZIZA: Hahaha! Usijali. Mimi ni mwanachuo.
MIMI: Unasoma wapi?
AZIZA: Mlimani
MIMI: Unasomea nini?
AZIZA: Sheria.
MIMI: Afadhali.
AZIZA: Afadhali ya nini tena?
MIMI: Uje kuwa mwanasheria wangu baadae katika kampuni yangu.
AZIZA: Hahahah! Utaweza kunilipa?
MIMI: Kwa nini nisiweze? Nitakuwa na fedha mbayaaaaaaa....nitamiliki magari ya kifahari na majumba makubwa sana....lol
AZIZA: Yote ni mipango ya Mungu ila napenda ulivyoongea kwa sababu unaonekana una imani ya kupata hivyo, cha msingi yakupasa kujituma tu na kumtanguliza Allah kwa kila kitu. Naomba nikuulize swali.
MIMI: Usijali. Uliza.
AZIZA: Unaishi wapi?
MIMI: Tandale kwa Mtogole.
AZIZA: Kule kwenye wezi wengi na wakabaji?
MIMI: Si wezi wengi tu, kule kunapodharaulika na watu wenye fedha kama nyie.
AZIZA: Hahaha! Usiseme hivyo bwana. Ila mbona umedanganya?
MIMI: Nimedanganya nini?
AZIZA: Kwenye profile lako. Umeandika unaishi Romania. Ulikuwa unataka kujipaisha nini upate wanawake?
MIMI: Hapana Aziza. Hiyo imekuja yenyewe tu.
AZIZA: Kivipi?
MIMI: Nilikuwa nataka kupatambulisha kama home kwetu ni Tandale. Ila nilipokuwa nikiandika Tandale, haikuwa ikitambulika kama ilivyokuwa sehemu nyingine. Matokeo yao wao kama facebook wakaniletea Tandalesti mji fulani kutoka Romania, nikaona sio kesi, nikakubaliana nao, ila ukiangalia kwa makini, Tandale imetokeza katika jina hilo.
AZIZA: Yeah! Nimeona. Hebu naomba uniambie mengi kuhusu Tandale.
MIMI: Kama yapi unataka kufahamu?
AZIZA: Mazingira, watu wa huko na mambo mengine.
MIMI: Tandale kama Tandale mazingira yake mazuri sana, watu full kuyafurahia maisha kama kawa. Kuna watoto wazuri, watoto ambao wanajitambua wao ni nani na kipi cha kufanya maishani mwao. Kuna mambo ya Rusha Roho usiku, yaani kwa kifupi kuhusu maisha, huku tunakula sana bata kuliko kwenu pa kulala saa moja.
AZIZA: Hahaha! Kwani huko kwenu huwa mnalala saa ngapi?
MIMI: Huwa nikiwa mgonjwa sana, nawahi kulala kama saa saba hivi.
AZIZA: Saa saba?
MIMI: Yeah! Ila nikiwa si mgonjwa, mpaka adhana iadhiniwe. Watu tunatransform usiku kuwa mchana na maisha yanasonga.
AZIZA: U must be kidding me Ibra.
MIMI: Huo ndio ukweli Aziza. Siwezi kukutania.

Unaona jinsi mawasiliano yetu yalivyokuwa yakienda? Hapo ndipo nilipokuwa napataka sasa. Nilikuwa namletea sana ucheshi lakini mwisho wa siku kuna kitu nilikuwa nakihitaji kutoka kwake, namba ya simu tu. Unajua katika maisha ya kuchati facebook huwa yanachosha sana, kuna kipindi fulani automatically unatokea kummisi mtu fulani na ungependa sana awe hewani lakini hayupo hewani, unapokuwa na namba ya simu, inakupa wakati mzuri wa kumsikia na kumjulia hali katika kipindi chochote ambacho ungependa kumsikia.
Ucheshi ndio ulikuwa kawaida yangu ila katika kipindi hiki nilikuwa nataka kuuleta ucheshi mpaka katika maandishi. Aziza akaonekana kulifurahia hilo, akaonekana kuanza kunikubali japokuwa hatujawahi kuonana hata siku moja. Nilikuwa bize na chatting na Aziza, sikutaka kuwasiliana na mtu mwingine katika kipindi hicho japokuwa nilimuona Eduado, Ibra Akilimia na Emmanuel Solo walikuwa wamenitumia meseji.
Nilikuwa nikijitahidi sana kumuingiza Aziza kwenye himaya yangu, yaani aingie bila kupenda na mwisho wa siku kila kitu kiwe poa sana. Sikujali alikuwa akiishi wapi, sikujali na mimi nilikuwa nikiishi wapi, kitu ambacho nilikuwa nikikiamini ni kwamba mapenzi wala hayakuwa na hiyana, yalikuwa hayabagui watu kama tulivyo wanadamu.

AZIZA: Nikuulize kitu.
MIMI: Niulize tu.
AZIZA: Unasoma?
MIMI: Hapana.
AZIZA: Unafanya kazi?
MIMI: Hapana.
AZIZA: Sasa unafanya nini?
MIMI: Nipo nipo nyumbani. Nilisoma kidato cha kwanza, sikuwa na fedha za kuniendesha kielimu, nikaachana nayo mpaka sasa hivi. Kuna kipindi nilipata vijisenti mara baada ya kubeba sana mizigo Tandale sokoni, nikaenda kusoma English Course.
AZIZA: Kwa hiyo haufanyi kazi?
MIMI: Yeah! Sifanyi kazi.
AZIZA: Unafanya kitu gani kingine?
MIMI: Sifanyi chochote kile.
AZIZA: Ila niliona kama unaandika hadithi! Au majina yamefanana?
MIMI: Yeah! Huwa ninazipost tu.
AZIZA: Hadithi zile huwa unaandika wewe?
MIMI: Hapana.
AZIZA: Sasa huwa anaandika nani?
MIMI: Anaandika baba na kisha mimi kuzichukua na kuziweka facebook.
AZIZA: Unanidanganya Ibra.
MIMI: Nikudanganye ili iweje? Kuna tuzo ya uongo wanapewa waongo? Huo ndio ukweli.
AZIZA: Mmmh! Basi mpe hongera baba yako.
Mimi: Zimefika.

Wakati mwingine haitakiwi kuwa mkweli kwa kila kitu. Tayari nilikwishaona kwamba kagundua kwamba sisi ni watu tunaoishi sehemu mbili tofauti, madaraja mawili tofauti na katika kichwa chake aliamini kwamba Tandale wanaishi watu masikini japo haikuwa hivyo. Nilichokuwa nikikifanya ni kuendana na akili yake alivyokuwa ameiweka, nami nikaanza kujifanya masikini ambaye sikubahatika kusoma kwa kuwa sikuwa na fedha ya kuniendeleza kielimu. Nikafanikiwa, kwa kiasi fulani aina ya maisha ambayo nilimpa yalimfanya kuamini kwamba kweli nilikuwa mtoto wa uswahilini, nilijivunia kuishi Tandale katika uwepo wake.

Maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida, kuhusu Aziza, wala sikuwa na wasiwasi kwa kuamini kwamba piga ua huyu mtoto ni lazima ningemchukua bila tatizo lolote lile. Kila siku nilikuwa nikiwasiliana nae, alikuwa akionekana kunikubali sana, chatting zangu zilizokuwa zikitabasamu zikaonekana kuuteka moyo wake. Nilikuwa na marafiki wengi facebook lakini nikikaa bila kuchati na Aziza sikuwa nikijisikia furaha kabisa.
Japokuwa Eduado alikuwa amenipa ishu ya kumfuatilia Aziza kama mchezo fulani lakini kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo nami nikazidi kufall inlove. Nilikuwa nikipenda sana Aziza, kila nilipokuwa nikiingia facebook na kumkosa, sikuwa nikijisikia raha kabisa.
Kuna nyakati za shida zikaingia, nyakati ambazo sikuweza kumuona Aziza hewani. Katika nyakati hizo maisha yalikuwa ya tabu sana, nilikuwa nikikosa furaha hata katika maisha ya kawaida. Nilimzoea sana Aziza, nilimpenda sana Aziza kwa hiyo kutokuuona uwepo wake machoni mwangu kilikuwa ni kitu ambacho kiliniumiza sana.

MIMI: Eduado vipi?
EDUADO: Poa. Inakuwaje?
MIMI: Kama kawa. Mbona Aziza simuoni siku hizi?
EDUADO: Tupo kwenye mitihani kaka.
MIMI: Sasa mkiwa kwenye mitihani ndio haruhusiwi kuwa hewani? Mbona wewe upo?
EDUADO: Mimi si unajua mbishi kaka.
MIMI: Dah! Nimemmisi sana Aziza. Nimemmisi ile mbaya kaka.
EDUADO: Usijali kaka. Mitihani ikiisha atakurudi hewani tu.
MIMI: Poa. Ila mnamaliza lini?
EDUADO: Wiki ijayo.
MIMI: Duh!
EDUADO: Nini tena kaka?
MIMI: Nahisi kama nitakufa kwa mawazo. Nahisi nitaweza kufa kaka.
EDUADO: Usijali kaka. Wewe vumilia tu utakula mbivu.
MIMI: Poa kaka.

Katika kipindi hicho ndicho nikajua kwamba moyo wangu ulikuwa ukimpenda sana Aziza. Huyu Aziza ndiye ambaye alinifanya niwaone wasichana wote kuwa wa kawaida sana, yeye ndiye aliyenifanya nimuone kuwa msichana mzuri kuliko wasichana wote duniani. Uwepo wake katika mtandao wa facebook bado nilikuwa nauhitaji sana, nilikuwa nikijisikia mpweke kupita kawaida. Aziza...Aziza...Aziza...upo wapi wewe msichana uje kuupoza moyo wangu ulio kwenye maumivu makali?
Siku zikaendelea kukatika na hatimae siku ambayo ilionekana kunifurahisha ikawadia. Siku hiyo nikawa kama nimepigwa na mshtuko mkubwa moyoni, sikuamini kile ambacho kilikuwa kikionekana machoni mwangu, Aziza alikuwa hewani. Sikutaka kupoteza muda, sikutaka kuleta pozi, kwa haraka sana nikamtumia meseji.

MIMI: Mungu wangu!
AZIZA: Nini tena.
MIMI: Umekuja at last.
AZIZA: Yeah! Nilipotea kwa kipindi fulani hivi, si unajua mitihani wangu.
MIMI: Pole sana. Mmekwishamaliza?
AZIZA: Yeah! Tumekwishamaliza. Ila nami nilikumisi sana.
MIMI: Nashukuru kwa kunimis, ila ulimiss nini kutoka kwangu?
AZIZA: Chatting zako, meseji zako zimekaa kitofauti sana na watu wengine.
MIMI: Kivipi?
AZIZA: Zipo kitofauti sana. Katika maisha yangu nimewahi kuchati na watu wengi sana, ila zako...dah!
MIMI: Bado haujaniambia kivipi.
AZIZA: Kwanza hauandiki kimkato kama neno ‘sijui kuliandika cjui’, yaani maneno ya mikato huwa hauitumii kabisa.
MIMI: Kwani hiyo nayo ni sababu?
AZIZA: Ngoja nikwambie kitu Ibra. Hii ni siri ambayo wanaume wengi wamekuwa hawaielewi na ndipo wanapofanya makosa kila siku.
MIMI: Siri gani?
AZIZA: Unajua unapochati na msichana yeyote ambaye haujawahi kuonana nae, unatakiwa kuonyesha nidhamu ya hali ya juu, hiyo ndio sifa moja kubwa ya kumteka msichana kwa sababu hisia zetu hazitekwi na mambo makubwaaa, hapana, hivi vitu vidogo vidogo ambavyo wavulana wanavipuuzia ndio vinatuteka.
MIMI: Kama vitu gani.
AZIZA: Cha kwanza salamu Ibra. Hivi unajua kwa sababu gani meseji yako ya kwanza kabisa uliyowahi kunitumia sijakujibu?
MIMI: Hapana. Sijajua kwa nini.
AZIZA: Salamu. Wanawake wengi wanalichukulia tofauti neno ‘mambo’. Unapomsalimia msichana kwa mara ya kwanza kwa kumwambia ‘Mambo’, wanaojibu ni wachache sana.
MIMI: Kwa nini sasa?
AZIZA: Kwa sababu mwanamke anapenda kufuatwa kinidhamu.
MIMI: Sasa nilitakiwa kukusalimia vipi ili ujibu?
AZIZA: Unapomfuata msichana yeyote duniani, anza kwa kumsalimia ‘Habari yako’ au salamu yoyote iliyokaa kinidhamu. Kidogo ukisalimia hivyo, kuna asilimia kubwa sana ya msichana kukujibu.
MIMI: Duh! Kumbeee!
AZIZA: Yeah! Hiyo ni siri ya kwanza Ibra, wavulana wengi huwa wanafeli hapo tu kitu ambacho kinawafanya kila siku kulalamika kwamba wasichana tuna mapozi kujibu salamu zao, hapana, hatuna mapozi bali wanakosea kusalimia, wanakosa nidhamu katika kusalimia.
MIMI: Nimekuelewa. Naomba siri nyingine.
AZIZA: Chatting. Unajua usipende kuchati na msichana kifupi kama nilivyokueleza toka mwanzo. Andika neno lote kwa ujumla, unajua unapoandika kifupi, unaupa kazi ubongo wa mtu kulifikiria neno na matokeo yake akili yake inachoka na kukatisha chatting na wewe.
MIMI: Ila mimi sijawahi kuchati namna hiyo Aziza.
AZIZA: Najua. Ila ninakumegea siri juu ya vitu ambavyo msichana anavipenda na vile asivyovipenda.
MIMI: Dah! Umeifungua akili yangu.
AZIZA: Ila wewe..dah! Wewe mtu noma.
MIMI: Kwa nini?
AZIZA: Kama kuna msichana ulichati nae halafu akaonekana kuchoka na chatting zako, basi hakika hatoweza kuridhika na chatting za mtu yeyote yule duniani.
MIMI: Hahaha! Kwa nini?
AZIZA: Unaandika maneno kwa ujumla, hauandiki vifupi, cha kushangaza sasa
MIMI: Kipi?
AZIZA: Unafuatilia mpaka alama za maandishi. Penye kiulizo, unaweka, penye nukta, unaweka, penye mkato, unaweka, penye alama ya mshangao, unaweka. Nimekuvulia kofia.
MIMI: Hahaha! Ni kawaida sana Aziza. Napenda kuchati na mtu katika staili ya kuandika hadithi.
AZIZA: Hongera yako. Naomba nikuulize swali.
MIMI: Uliza tu.
AZIZA: Ulinimis?
MIMI: Sana tu.
AZIZA: Ulimiss nini kutoka kwangu?
MIMI: Chatting na mambo mengine.
AZIZA: Kama yapi?
MIMI: Uzuri...koh koh koh
AZIZA: Hahaha! Hebu acha kunitania, umewahi kuniona mpaka useme mimi mzuri?
MIMI: Unajua unapoongea na msichana usiyemfahamu simuni halafu ukasikia sauti yake, unajua tu kwamba huyu mzuri na huyu mbaya.
AZIZA: Sasa kwani mimi umeisikia sauti yangu?
MIMI: Hata unapochati na mtu, mwandiko wake unajionyesha kwamba huyu mzuri na huyu mbaya. Ila kuna kingine pia.
AZIZA: Kipi?
MIMI: Nilichogundua ni kitu kimoja. Wasichana wengi wanaoweka profile picha zao picha za wanawake maarufu wazuri, huwa wabaya. Ila walioweka picha za profile zao kama maua au midoli, huwa ni wanawake wazuri.
AZIZA: Hahaha!
MIMI: Yeah! Hii ni kwa sababu yule msichana mbaya kamuweka Rihanna kwa sababu anataka kutuonyesha kwamba yeye ni mzuri ila yule aliyoweka picha ya ua anataka kutuonyesha kwamba yeye ni mtu wa thamani, mzuri na ananukia kama ua au mdoli. Nililifuatilia hilo kwa marafiki zangu wengi na nikaligundua.
AZIZA: Kweli wewe mfuatiliaji. Kwa hiyo ukagundua mimi kuwa ni mzuri?
MIMI: Yeah! Nimegundua hilo kiasi ambacho kama nitaambiwa niombe kitu kimoja duniani nacho kitafanikiwa, basi ningeomba kuwa na wewe, basi.
AZIZA: Hahah! Acha utani Ibra.
MIMI: Kwani naonekana kutania?
AZIZA: Yeah!
MIMI: Huwa sifurahii pale ninapokuwa serious halafu mtu ananiona natania. Nipo serius Aziza.
AZIZA: Sasa umenipendea nini? Hujawahi kuniona wala nini.
MIMI: Ngoja nikwambie kitu Aziza. Mapenzi ni hisia, mapenzi hayajalishi uwe umemuona mtu au haujamuona, vyote hutokea moyoni. Unapotumia kipindi kirefu kuchati na msichana fulani, automatical moyoni unafall inlove, hicho ni kitu ambacho hutokea kwa binadamu wengi wenye moyo wa nyama kama wa Ibra.
AZIZA: Duuh! Hivi naomba nikuulize kitu.
MIMI: Uliza.
AZIZA: Unaongea mambo mengi sana mazuri Ibra. Unaonekana kuwa una kitu cha ziada kichwani mwako.
MIMI: Hapana, sina kitu cha ziada. Akili nilizonazo mimi ndizo ambazo hata mtu mwingine anazo, tofauti kwenye kuzitumia hizo akili tu.
AZIZA: Unaonaaa. Kila unachoongea point. Ibra una kitu cha ziada akilini mwako. Matumizi ya akili yako nayaona kuwa tofauti sana. Wewe genius.
MIMI: Genius! Acha utani. Niwe vipi Genius na wakati shuleni sijawahi kuingia hata kumi bora?
AZIZA: Sikiliza Ibra. Kuna wale genious wa darasani. Haimaanishi ukiwa genious darasani basi hata kwenye kuongea na kuandika utakuwa genious, haiko hivyo. Kwa magenious wamegawanyika. Kuna wale wa darasani na wale wa sehemu nyingine kwenye maisha. Unaweza ukawa genius darasani lakini katika maisha ukawa mbumbumbu. Unakubaliana nami?
MIMI: Kiasi.
AZIZA: Hahaha! Usijali. Utanielewa tu. Turudi kwenye mada yetu.
MIMI: Kwa hiyo hivyo ndivyo mapenzi yalivyo Aziza.
AZIZA: Nimekuelewa Ibra.
 MIMI: Naomba nikuulize swali moja tu.
AZIZA: Uliza.
MIMI: Ushawahi kujisikia kitu chochote romantic moyoni mwako juu yangu?
AZIZA: Swali gumu kujibika Ibra.
MIMI: Najua. Hata mwalimu anapoamua kutoa mtihani mgumu, kuna wengine wanafaulu japokuwa ni mgumu. Najua swali langu gumu lakini naona linaweza kujibika kirahisi sana.
AZIZAl Swali gumu Ibra.
MIMI: OK! Ngoja nibadilishe swali. Unanipenda?
AZIZA: Ninakupenda sana Ibra. Nahisi katika marafiki zangu wote facebook. U are the best.
MIMI: Dah! Ushatoka nje ya mada.
AZIZA: Kivipi?
MIMI: Hebu turudi ndani ya mada. Unanipenda?

Swali lile likaonekana kuwa gumu kwa upande wake, nikaona ukimya ukiwa umetawala mahali hapo, nikawa naisubiria meseji yake huku nikionekana kuwa na kiu kubwa ya kutaka kusikia kitu chochote kutoka kwake, hasa jibu la swali ambalo nilikuwa nimemuuliza.

AZIZA: Mhh!
MIMI: Nini tena?
AZIZA: Una haraka sana Ibra. Maswali yako mengine yanakufanya nikuone mtu wa haraka mno.
MIMI: Tatizo muda Aziza. Nahofia kwamba nikichelewa, nitakuta ushachukuliwa kitu ambacho sitaki kitokee.
AZIZA: Hahaha! What if nikisema sikupendi?
MIMI: Nafikiria litakuwa neno baya ambalo sijawahi kulisikia katika maisha yangu.
AZIZA: Hahaha! Ibra una maneno sana. Hivi unayatoa wapi hayo yote?
MIMI: Kutoka moyoni mwangu Aziza. Nimetokea kukupenda sana.
AZIZA: Lakini bado mapema sana.
MIMI: Najua. Najua kwamba mapema ila kumbuka kwamba vitu vingine ni lazima vifanyike mapema. Nadhani sina makosa juu ya hilo.
AZIZA: Nikuulize swali?
MIMI: Niulize.
AZIZA: Una mpenzi?
MIMI: Nadhani ningekuwa na mpenzi nisingeweza kukwambia kwamba nakupenda na kukuhitaji.
AZIZA: Kwa nini usiweze?
MIMI: Uaminifu. Napenda sana kuwa mwaminifu hasa kwa mtu nimpendae.....thats all.
AZIZA: Sawa. Ila mbona haujaniuliza kama nina mpenzi au la?
MIMI: Nadhani sitakiwi kujua kwani kwa upande mwingine nikitokea kujua, nitaumia kitu ambacho sitaki kitokee moyoni mwangu.
AZIZA: Nakuonea huruma Ibra.
MIMI: Kwa nini?
AZIZA: Unampenda mtu usiyewahi kumuona.
MIMI: Hahaha! Hilo si tatizo Aziza. Kukuona haijalishi. Kitu kinachojalisha ni wewe na mimi kuwa pamoja tu.
AZIZA: Sasa kama nina mpenzi itakuwaje?
MIMI: Sijajua itakuwaje lakini kitu ninachokihitaji ni kimoja tu, kupata nafasi moyoni mwako, kuthaminiwa na kupewa kipaumbele.
AZIZA: Kwa hiyo mpenzi wangu nimuache kwa sababu yako?
MIMI: Simaanishi hivyo Aziza.
AZIZA: Hiyo ndio maana yake. Yaani nimuache mpenzi wangu.
MIMI: Wakati mwingine inawezekana. Ngoja nikupe kijistori cha kizushi.
AZIZA: Aya nipe.
MIMI: Kuna mwanamke mmoja alikwenda kuchota maji siku moja, alikuwa amechoka na kuchafuka sana. Sehemu alipokuwa amechota maji kulikuwa mbali sana, kichwani alikuwa na ndoo na mkononi alikuwa na kidumu. Bahati mbaya, akajikwaa, ndoo ikadondoka na kupasuka, maji yakamwagika na kushindwa kuzoleka.
AZIZA: Dah! Alifanya nini sasa?
MIMI: Kurudi bombani kulikuwa mbali sana na alikuwa amechoka kupita kawaida. Kile kidumu ambacho alikuwa nacho mkononi ndicho kilichomsaidia kuoga.
AZIZA: Stori nzuri.
MIMI: Yeah! Ni nzuri na iliyojaa mafunzo. Umejifunza nini?
AZIZA: Nimejifunza kwamba yatupasa kuwa na kidumu pia katika kipindi tunachokwenda kuchota maji.
MIMI: Umekuwa mwerevu sana. Nadhani ushajua nimemaanisha nini.
AZIZA: Hahaha! Kumbe ndio umemaanisha hivyo? Yaani nina ndoo na unataka niwe na kidumu?
MIMI: Yeah! Ila naomba ufahamu kitu kimoja. Wakati ndoo inapopasuka, kidumu kitaweza kufanya kazi kama ndoo. Kwa hiyo ni muhimu kuwa na kidumu pia japokuwa haulazimishwa kufanya hivyo.
AZIZA: Ibra unanifundisha tabia mbaya.
MIMI: Hapana. Sikufundishi tabia mbaya ila nakupa tekniki nyingine ya maisha. Njia ambazo unaweza kufanya plan B mara plan A inapoonekana kuharibika.
AZIZA: Ok! Nimekuelewa.
MIMI: Sasa umechukua hatua gani baada ya kunielewa?
AZIZA: Inabidi unipe muda wa kufikiria kwanza manake duh! Kuwa na kidumu inahitaji moyo.
MIMI: Nisikilize Aziza. Unataka kwenda kuomba ushauri wapi? Kwa mama?
AZIZA: Hapana Ibra, ila nahitaji kujifikiria juu ya hilo.
MIMI: Kwani moyo wako unakwambia nini sasa hivi juu yangu?
AZIZA: Hauniambii kitu chochote.
MIMI: Unanidanganya Aziza. Hautakiwi kulifikiria jambo hili, unapoamua kufanya maamuzi ya maisha yako yakutakiwa kuwa peke yako Aziza.
AZIZA: Najua. Sasa wewe unafikiri natakiwa kumuomba ushauri nani zaidi ya mama?
MIMI: Niombe ushauri mimi.
AZIZA: Hahaha! Aya basi nishauri juu ya hili. Unaonaje, niwe na Ibra au?
MIMI: Hahah! Ninachokushauri ni kwamba inakupasa kuwa nae kwani kwa muonekano wake tu anaonekana kukupenda na kukuhitaji sana tofauti ya unavyofikiria Aziza. Usimuumize, mpende, kama ameamua kukupenda, kuutoa moyo wake kwa ajili yako, mfanyie the same.
AZIZA: Hahaha! U mshauri mbaya sana.
MIMI: Kwa nini?
AZIZA: Unanishauri vitu vibaya. Ila ok! Naomba nikufikirie kwani sitaki kukuumiza. Nikisema nitoe jibu langu sasa hivi, utaumia na mimi sitaki uumie.
MIMI: Sawa. Kama unaona ukitoa jibu la papo kwa papo utaniumiza, basi usifanye hivyo. Kwa hiyo lini utanijibu.
AZIZA: Wewe unataka lini?
MIMI: Sasa hivi....lol!!
AZIZA: Utaumia. Naomba unipe muda. Bado tuna nafasi kubwa ya kuzidi kuwasiliana Ibra.
MIMI: Poa. Kama ndio hivyo hakuna noma, acha tuzidi kuwa na nafasi zaidi.
AZIZA: Umekasirika?
MIMI: Hapana. Sijakasirika. Kwani umeongea neno lolote la kunikasirisha?
AZIZA: Hapana ila wanaume wengine huwa ukiwakataa wanakasirika sana na kesho wanakuwekea post.
MIMI: Acha nao. Hawajui mapenzi, mapenzi yanahitaji subira, mapenzi yanahitaji kujitoa kwa kila kitu, hautakiwi kukata tamaa ila mapenzi pia yanahitajiiiii........
AZIZA: Yanahitaji nini?
MIMI: Kuyafuatilia sana kama unafuatilia kazi.
AZIZA: Hahaha! Una maneno wewe mtoto.
MIMI: Kawaida tu. Ila kiukweli...dah! hongera.
AZIZA: Hongera ya nini?
MIMI: U mzuri sana. Yaani dah! Sijui niseme nini. Kuna mengine nikisema naona kama nitaonekana muongo.
AZIZA: Hahaha! Kivipi? Niambie tu.
MIMI: Jana nilipokuwa nikinywa maji, nilikuona kwenye glasi, nilipokuwa najitazama kwenye kioo, nilikuona wewe. Usiku silali, nakuota wewe tu.
AZIZA: Hahaha!
MIMI: Maneno ya zamani hayo. Wanawake wa zamani ulikuwa ukiwaambia hivyo....fasta unamchukua. Ila nyie wa siku hizi mmejanjaruka sana.
AZIZA: Hahaha! Kwa sasa hivi tunajua ukweli kwamba huwezi kuniona kwenye maji.
MIMI: Ok! Tuachane na hayo. Hivi tunaweza kuonana?
AZIZA: Kuonana. Mbona mapema sana!
MIMI: Poa, usijali. Tutaonana tukizeeka kwa sababu ndio utakuwa muda muafaka.
AZIZA: Hahaha!
MIMI: Hiyo ndio maana yake. Yaani kuonana tu unataka tupeane kalenda. Kweli makubwa.
AZIZA: Usijali. Tutaonana soon. Ngoja nikamilishe vitu fulani hivi vya kifamilia.
MIMI: Ok! Hakuna tatizo. Unaweza kuchukua muda gani?
AZIZA: Si muda mrefu, kama siku mbili tatu hivi. Unatamani kuonana na mimi?
MIMI: Yeah! Ninatamani sana Aziza.
AZIZA: Ok! Hakuna tatizo. Utaonana na mimi kwa masharti.
MIMI: Masharti gani?
AZIZA: Uje nyumbani.
MIMI: Mh!
AZIZA: Nini tena?
MIMI: Kwa nini usije nyumbani. Au unaogopa matope, unaogopa kuchafuka kutokana na matope ya uswahilini?
AZIZA: Hapana. Nitakuhitaji uje nyumbani.
MIMI: Unataka nife nini?
AZIZA: Kwa nini?

5
MIMI: Baba yako. Nadhani ataniua.
AZIZA: Usijali. Ninapokwambia uje nyumbani, namaanisha kwamba siku hiyo itakuwa poa na hakutokuwa na tatizo.
MIMI: Sawa. Ukiwa na nafasi naomba uniambie. Shida yangu nikuone tu.
AZIZA: Sawa. Usijali. Tutaonana tu.

Siku hiyo tulichati sana mpaka saa saba usiku muda ambao alitaka kulala, niliridhika na hivyo kumruhusu kwa moyo mmoja kulala. Siku zikakatika mpaka kufikia siku ambayo Aziza akataka kuonana na mimi. Nakumbuka siku hiyo ilikuwa kama ndoto kwangu, baada ya miezi miwili ya mawasiliano bila kuonana leo hii Aziza akaniambia kwamba alikuwa akitaka kuniona, nilitamani kurukaruka kwa furaha.
Siku ya tukio ilipofika, nikaoga na kujiweka makini, nikachukua jinzi yangu na kuivaa, nikachukua raba zangu za kawaida na kuzivaa huku kofia yangu ikiwa kichwani mwangu. Kutoka nyumbani mpaka kwao Masaki wala hakukuwa mbali, nilitegemea kuchukua daladala na hatimae kwenda nyumbani kwao. Mara baada ya kumaliza kujiandaa, nikaingia facebook na kisha kuanza kuwasiliana nae.

MIMI: Nipo tayari.
AZIZA: Ok! Chukua namba yangu. Hii hapa. 0718 069 269.
MIMI: Ok! Ndio najiandaa kwenda kituoni sasa hivi.
AZIZA: Kwani umeshatoka nyumbani?
MIMI: Bado.
AZIZA: Basi usijali. Nielekeze nije kukuchukua.
MIMI: Uje kunichukua?
AZIZA: Yeah! Kuna ubaya?
MIMI: Yeah! Sijawahi kufuatwa na gari toka nizaliwe.
AZIZA: Usijali. Leo nitakuwa wa kwanza kukufuata. Umesema Tandale, napafahamu kidogo, nitakuja mpaka kwa Mtogole then unielekeze.
MIMI: Hakuna tatizo. Nakusubiria.

Sijui niseme nini aisee, huyu mtoto alikuwa akijiandaa kuja kunichukua nyumbani kwa ajili ya kuelekea nyumbani kwao, nilikuwa na presha sana, sikuwa nikijiamini kwamba nilikuwa mimi Ibra. Moyo wangu ukawa na dukuduku kupita kawaida, mavazi niliyoyavaa niliyaona kutokuwa fresh hali iliyonifanya kubadilisha mara kwa mara. Sikujua Aziza alikuwa akifanana vipi, uzuri ambao aliusema Eduado, leo nilikuwa nakwenda kuuona kwa macho yangu.

Kwa sababu aliniambia kwamba angekuja mpaka kwa Tandale Kwa Mtogole wala sikuwa na wasiwasi, nilichokifanya ni kuelekea katika sehemu ya Mafyoso Camp ambapo vijana wengi tulikuwa tukitumia kukaa na kutulia. Siku hiyo, mawazo yangu yote yalikuwa juu ya msichana Aziza ambaye alitarajiwa kufika muda si mrefu, sikutaka kumwambia mtu, nilichotaka kukifanya nilitaka kiwe sapraizi kwa kila mtu mahali pale. Ilipofika saa tisa na robo alasili, simu yangu ikaanza kuita, nikaipokea na kisha kuipeleka sikioni.

AZIZA: Nimekwishafika hapa kwa Mtogole.
MIMI: Ok! Unaiona hiyo njia ya vumbi kushoto kwako?
5
AZIZA: Nimetokea huku Kijitonyama Sayansi.
MIMI: Haina noma. Vuka barabara ya lami na kisha ingia katika barabara ya vumbi, nyoosha, hapo mbele njia imegawanyika, panda na hiyo ya kushoto moja kwa moja utanikuta mtu mzima nimejaa tele na wanangu.
AZIZA: Ok! Nakuja.

Mapigo ya moyo yakaanza kudunda, kila nilipokuwa nikimfikiria Aziza nilikuwa nakosa amani. Nilikuwa nikijiangalia, japokuwa nilipendeza sana kama siku za sikukuu lakini kwa macho yangu nilijiona bado kabisa. Kwangu, Aziza akaonekana kuwa kama malkia fulani ambaye alikuwa akisubiriwa kwa mbwembwe zote kwangu. Macho yangu hayakutulia, yalikuwa yakiangalia ile barabara ya vumbi ambayo ilionganisha mpaka kwa Mtogole.
Baada ya muda, kwa mbaliiiii niliweza kuliona gari moja dogo, Verrosa nyeusi, bila shaka lilikuwa gari la Aziza ambalo alikuwa akilitumia. Ebwana sikufichi rafiki yangu, nilipigwa na butwaa, nikakosa kujiamini. Sikutaka kuwaambia washikaji juu ya Aziza kwa sababu unaweza kuwatambia halafu mwisho wa siku msichana mwenyewe akaonekana kuwa si mzuri, mtu mzima ukaona noma.
Gari lile likaendelea kuja, lilipofika karibu na pale tulipokaa, nikasimama na kisha kulisimamisha kwa kupunga mkono. Kwanza washikaji wakaonekana kunishangaa, hawakuwa wakifahamu kitu chochote kile kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Nilibaki nikiwa nimesimama nje ya mlango hasa baada ya Aziza kusimamisha gari, sikuweza kumuona kwa sababu vioo vilikuwa tinted. Aliposhusha kioo...MUNGU WANGU!
Ngoja nikwambie kitu rafiki yangu. Kati ya majini wote wanaojigeuza kuwa warembo na kuua wanaume nyakati za usiku umewahi kuwaona? Kabla sijaendelea, ngoja nikwambie kitu fulani. Mimi kama mimi nilikwishawahi kukutana na msichana ambaye alikuwa jini nyakati za usiku, tena nakumbuka ilikuwa mkoani Kilimanjaro katika kipindi ambacho kulikuwa na tetesi nyingi kuhusiana na majini ambao walikuwa wakiua watu nyakati za usiku, bila shaka ilikuwa 2006 au 2007.
Usijiulize nilijuaje kwamba huyo mwanamke alikuwa jini. Nilikutana nae usiku katika kipindi ambacho nilikuwa nikielekea Majengo katika kipindi cha likizo, nakumbuka ilikuwa saa mbili usiku, tulifunga shule na kuja Dar es Salaam niliona ningetumia gharama kubwa.
Nilikutana na huyo msichana, asikwambie mtu, alikuwa mrembo mkali sana, ukali wa msichana yule jini sikuwahi kuuona kwa msichana yeyote yule toka nizaliwe, hata mrembo wangu alikuwa haingii ndani.
Nilipopishana nae, alikuwa akinukia manukato mazuri sana, nywele zake zilikuwa ndefu, nilitamani kumsalimia, ila nilikuwa dogo, nadhani kama ningekuwa mkubwa, siku hiyo na mimi lazima ningeuliwa tu...yaani ni LAZIMA. Unamwacha vipi msichana mrembo unayepishana nae? Ukimwangalia, mwarabu si mwarabu, mzungu si mzungu na mtu mweusi si mtu mweusi. Nilipopishana nae, nilipiga kama hatua tano, nilipogeuka nyuma ili niangalie umbo lake la nyuma, kajazia vipi, sikumuona, kilichofuata...ni kutoka nduki tu huku nikipiga kelele.
Nilipokuwa nikiwangalia Aziza katika kipindi hicho nilikuwa nikimfikiria yule mwanamke jini wa kule Kilimanjaro. Aziza, aisee Aziza....Mhh! Nadhani Eduado alikuwa mchoyo, hakutoa sifa ambazo alistahili kuwa nazo Aziza, Aziza alikuwa msichana mzuri sana, msichana ambaye....dah! Sijui nizungumze vipi.
Hahaha! Kwanza kwa washikaji. Walipoona kwamba nimelisimamisha gari lile, wakataka kuangalia ndani kujua kuna nani, nilikuwa nimewapa mgongo, mlango ulipofunguliwa, Aziza akatoka nje...aiseeee. Si kwa watoto, watu wazima, mababu, wala warembo wengine, wote wakabaki wakimshangaa Aziza, alikuwa mkali mpaka mtu mzima nikawa najipa mapungufu.
Ukiachana na zile sifa za uchoyo ambazo alikuwa amezitoa Eduado juu ya Aziza, acha nikwambie jinsi alivyo, umtengeneze Aziza wako kichwani mwako na uone ni jinsi gani alikuwa mrembo.
Kwanza Aziza alikuwa Mpemba, kwa hapo sitaki nizungumze sana kwa kuwa wote mnaamini kwamba wapemba wamebarikiwa kwa urembo, mtoto alionekana kuwa baba yake alikuwa mwarabu, tena wa Dubai, mama yake alikuwa Mlangi, vuta picha mtu mzima. Mtoto alikuwa na nywele nyingi sana, hapo ndipo nilipogundua mapungufu ya sifa za Eduado. Mtoto hakuwa na nywele zilizoishia kwenye mabega, mtoto minywele ilikuwa hiyooo mpaka mgongoni huku zikiwa zinang’aa sana. Uso wake ulikuwa mwembamba ambao ulikuwa ukizungukwa na tabasamu pana ambalo lilikuwa likiyafanya meno yake meupeeee kuonekana. Ukiachana na hayo, huyu mtoto alikuwa na kidoti aisee, tena kile kidoto kilichokuwa karibu na pua, kilimfanya kupendeza sana.
Ukiachana na uso wake uliomfanya kuonekana kama malaika, umbo lake lilikuwa zuri sana. Huwa wapemba ni kama waarabu au wachina, hawana makalio hayoooo tofauti na wanawake wetu weusi, yeye alikuwa mwembamba wa wastani, kifua chake kilikuwa kimesimama. Kwa sababu alikuwa amevaa sketi fupi kiasi, miguu yake haikuwa miguu ya bia, ilikuwa miguu ya wastani kidogo. Kila nilipokuwa nikimwangalia, mtoto hakuwa na kovu lolote lile, yaani alionekana kama katengenezwa kupitia Adobe Photoshop na kisha kuja kwangu.

AZIZA: Wao Ibraaaaaa.

 Aliniambia kwa furaha na kisha kunikumbatia. Watu wote ambao walikuwa wakimwangalia Aziza wakaanza kutushangaa, Aziza alionekana kama mzungu, nilionekana kuokota embe katika mti wa mlimao au kujenga nyumba kubwa angani. Aziza alikuwa akinukia vizuri sana, harufu ya manukato yake ikanifanya nifall inlove zaidi na zaidi. Nilitamani kumbeba juu juu. Warembo wa pale mtaani ambao walikuwa wakiniringia sanaaaaaa, katika kipindi hiki walionekana kushikwa na wivu huku mioyo yao ikiukubali uzuri wa Aziza.

MIMI: Mzima wewe cheupe?
AZIZA: Mimi mzima.
MIMI: kweli nilipatia, sikutoka nje hata mara moja.
AZIZA: Ulipatia nini?
MIMI: Wanawake mnaoweka picha za midoli na maua huwa mnakuwa wakali sana.
AZIZA: Kwani mimi mzuri?
MIMI: Nilikuwa najiuliza kwamba hivi umezaliwa hapa duniani au umeshushwa kutoka hukooooo.
AZIZA: Hahaha! Acha hizo Ibra.
MIMI: Mtoto unaonekana kuwa mrembo sana, mtoto una mvuto wa ajabu, mtoto unaonekana zaidi ya malkia Cleopatra aiseee...dah! Ulivyonikazia kuwa na mimi sawasawa tu manake ungenisababishia kifo.
AZIZA: Kivipi?
MIMI: Mmh! Hapa kifo nje nje aiseee. Tena bora ulivyokuwa na gari manake ungekuwa unatembea kwa miguu, utawafanya hata wale wanaokwenda msikitini kuswali wakatishe safari zao, utawafanya mpaka wale wanaokwenda kanisani kusali wakatishe safari zao kwa muda wakuangalie wewe. Kama vitabu vya dini vinavyosema kwamba ukimwangalia mwanamke na kumtani utakuwa umeshazini nae, haki ya Mungu nina uhakika wewe umeshazini na watu wengi maishani mwako. Umeshazini na mimi, umezini na wale marafiki zangu, umezini na wale mababu waliokaa pale chini wakicheza bao, mbaya zaidi, umezini mpaka na wasichana wenzako....hahahaha! Wamekusaga.
AZIZA: Yaani yote hiyo kwa sababu wamenitamani?
MIMI: Ndio. Hebu jiangalie, hivi unaweza kujilinganisha na nani? Hata Beyonce haingiii, labda Alicia Keys ndiye anaweza kuifikia nusu yako.
AZIZA: Hahaha! Ibra una maneno matamu. Hebu nisubiri kidogo niende hapo dukani.
AZIZA: Unakwenda kununua nini? Hakuna pizza wala baga hapa Tandale.
AZIZA: Hahaha! Hebu acha utani.

Huyu Aziza. Aisee bora alivyoweka picha ya mdoli katika akaunti yake ya facebook manake kama angeweka picha yake basi ingekuwa balaa. Mwendo wake ulikuwa ni wa mapozi kupita kawaida, alionekana kutembea kwa tahadhali ardhini. Nilichokifanya nikayapeleka macho yangu kwa washikaji waliokuwa pale kijiweni, nilijua tu kwamba walikuwa na dukuduku mioyoni mwao.

JAFARI: Kaka heshima. Kaka heshima yako...kuanzia leo...hauna mpinzani hapa mtaani aiseeee...duh!
MIMI: Hahaha! Mtoto umemuonaje.
JAFARI: Kwanza huyu mtoto umemtoa wapi?
MIMI: Facebook.
JAFARI: Duh! Kaka naomba na mimi uniunganishe manake dah!
MIMI: Kaka mambo hayapo rahisi kama unavyofikiri. Mpaka nimempata huyu mtoto, nimepitia kwenye mabonde, mito majabari mpaka wewe kumuona hapa. Usifikiri ukijiunga leo kesho unampata, unaweza ukawa babu hujaambulia chochote.
ALLY: Kwani huyu ni wa facebook?
MIMI: Yeah! Tena yupo mpaka Twitter...yupo kotekote.
HUSSENI: Ila huyu mrembo sio mgeni machoni mwangu, nadhani nilishawahi kumuona sehemu.
MIMI: Acha uongo. Wapi?
ALLY: Daah! Nshajichanganya. Kumbe kichwani mwangu ilikuwa inakuja picha ya Kajool, yule mrembo muigizaji wa Kihindi.
MIMI: Hahaha!
JAFARI: Ila Ibra. Daah! Unapokuwa na mtoto kama huyu, hivi kweli unaweza kutembea nje ya ndoa?
MIMI: Kaka, sisi wanaume hatufai, hata upewe mrembo mzuri kama malaika, kesho unalala na rafiki yake...hahaha!

AZIZA: Ibra.
MIMI: Niambie (Huku nikimfuata)
AZIZA: Tuondoke.
MIMI: Bila ya kukanyaga nyumbani? Hebu acha zako, twende home.
AZIZA: Ibra...nataka tuwahi nyumbani.
MIMI: Hata kama. Twende mara moja tu.

Lengo kubwa la kumtaka Aziza twende nyumbani lilikuwa moja tu, kutaka kuwaonyeshea wale wasichana ambao walikuwa wakileta mapozi kwamba huyu msichana alikuja kwa ajili yangu kwani kama nisingefanya hivyo, wangejua kwamba alikuwa mpita njia ambaye alikuwa amesimama kutaka kuulizia kitu fulani. Kwa sababu alikuwa amelipaki gari pembeni, nikawaambia washikaji waliangalie na mimi kuanza kuondoka na Aziza kwenda nyumbani.
Watu walikuwa wakinitolea macho, wengine walikuwa wakiniangalia kisiri na kunipigia saluti. Aziza alionekana kukimbiza kupita kawaida, urembo wake ulikuwa ni mkubwa kiasi ambacho hakukuwa na mtu aliyefikiria kama ningeweza kuja na msichana mzuri kiasi kile.

AZIZA: Mazingira ya huku nimeyapenda.
MIMI: Umeyapendea nini?
AZIZA: Yametulia sana. Halafu kumechangamka.
MIMI: Hahaha! Nyie si mmezoea mazingira ya kwenu yapo kimya utafikiri jangwani.
AZIZA: Yeah! Unajua kule sijui kupo vipi, huwa kunaboa kweli.

Katika kipindi chote ambacho tulikuwa tukiongea huku tukielekea nyumbani, kichwa changu kilikuwa kikimfikiria baba. Nilijua kabisa kwamba katika kipindi hicho alikuwa nyumbani, kichwa changu kilikuwa kikifikiria uongo ambao nilitakiwa kumpa, uongo ambao ungeendana na ukweli. Nilipofikiria kwa kipindi fulani, nikapata jibu, nikapata kile nilichotakiwa kumwambia baba.
Kweli tukafika home, majirani wote wakawa wananiangalia kwa macho ya kunishangaa, Aziza, kwao alionekana kuwa tofauti sana, uzuri ambao alikuwa nao ulionekana kuwa wa kipekee sana. Nikaufungua mlango, tulipoingia ndani tu, kizaazaa, baba alikuwa kwenye kochi akiangalia televisheni.

Nikamkaribisha Aziza, akamsalimia baba na kutulia kochini. Nikamwangalia baba huku lengo langu likiwa ni kutaka kumsoma, hiyo ndio ilikuwa tabia ya nyumbani, muda mwingi watu huwa tunasomana kabla ya kuongea kitu chochote kile. Baba akaonekana kufahamu nilichokuwa nikikifikiria. Akaniwahi.

BABA: Unaonekana unataka kuniambia jambo, halafu hilo jambo la uongo, hebu niambie sasa nikusikilize.
MIMI: Hahaha! Tatizo mzee Akilimia una presha sana. Wewe subiri kwanza, mbona unakuwa na wasiwasi?
BABA: Huo mtazamo wako unaoutumia kunitazama. Ok! Karibu mgeni. Sijui unatumia kinywaji gani?
AZIZA: Hapana. Nimeshiba.
BABA: Kwani ukinywa kinywaji chochote utavimbiwa?
AZIZ: Hapana. Nimekwishakunywa.
BABA: Ibra, ni kweli anayoyasema?
MIMI: Hapana. Hapo kakupiga fix.
AZIZA: Hahaha!
BABA: Jisikie huru. Uletewe kinywaji gani?
AZIZA: Maji tu yanatosha.
MIMI: Ok! Ila kuna maji ya chumvi...utakunywa?
AZIZA: Mmmh! Maji ya chumvi?
MIMI: Sasa unashangaa nini? Au haujui kama Dar es Salaam kuna bahari ya Indi?
AZIZA: Niletee hata hayo nitakunywa tu.

6

Mtu mzima nikanyanyuka, kumbuka hapo bado sikuanza kumtambulisha Aziza kwa mzee kwamba alikuwa nani na alifuata nini nyumbani. Juu ya hilo, sikuwa na wasiwasi sana kwani kwa umri ambao nilikuwa nimefikia, mzee hakuwa muongeaji sana zaidi ya kunitaka kuwa makini kila siku kwa kila nikifanyacho. Nilipochukua maji, nikamletea, tena kwa makusudi, nikamletea kwenye kikombe cha plastiki, nilichokuwa nikikihitaji ni kumuonyeshea maisha fulani ya tofauti sana, maisha ambayo alikuwa akiyaamini kichwani mwake kwamba yalikuwa yakiishiwa na watu waliokuwa wakikaa Tandale uswahilini.

MIMI: Baba huyu ni rafiki yangu anaitwa Judith. Nilisomanae Faraja Seminari ila nilimuacha darasa moja. Kwa sasa yupo hapo I.F.M anasomea sheria.
BABA: Asante kwa kumfahamu. Karibu Judith na jisikie huru.
AZIZA: Asante.
MIMI: Judith, huyu ndio mzee Akilimia. Huyu ndiye ambaye nimemuibia hiki kipaji cha kuandikaandika.
AZIZA: Nashukuru kumfahamu.

Kwa sababu tulikuwa na safari, hatukutaka kukaa sana mahali hapo, tukasimama na kisha kuaga na kuondoka. Njiani, Aziza alionekana kushangaa sana, hakuamini kama nilikuwa na uhuru mkubwa wa kuongea na mzazi kwa kiasi kile.

AZIZA: Mbona baba yako unaongea nae namna ile?
MIMI: Kivipi?
AZIZA: Ulivyokuwa ukiongea. Yaani kama unaongea na vijana wenzako.
MIMI: Nisikilize Aziza, mzazi ni rafiki, hautakiwi kumuogopa sana mzazi mpaka kukosa uhuru, wazazi wetu hawakutulea katika mazingira hayo, walitulea katika mazingira ya kirafiki zaidi, mazingira ambayo yametufanya kuwa huru kwao.
AZIZA: Basi hongereni. Mzee wangu ukae chini na kuongea nae namna ile, mh! Mtu hujiamini. Kwanza akirudi tu, amani nakosa, muda wote utasikia Azizaaaa.
MIMI: Hahaha! Ila hao wazee ndio fresh. Mzee unakuwa bandidu kama hivyo, hakuna utani, hakuna masihala...hahaha!
AZIZA: Kuna uzuri gani? Baba akirudi unajificha chooni. Ngoja nikuulize swali.
MIMI: Uliza.
AZIZA: Kwa nini umemdanganya jina langu na kila kitu kuhusu mimi?
MIMI: Pale ningemwambia unaitwa Aziza, angeshtukia mchezo.
AZIZA: Kivipi?
MIMI: Unajua nimesoma seminari, sasa niliposema kwamba nimesoma na wewe, kidogo angetilia mashaka. Nilichokifanya ni kucheza na akili yake kabla ya yeye kucheza na akili yangu, nikamuwahi. Hahaha!
AZIZA: Ibra una visa sana.

Tuliendelea kwenda mtaa wa juu, tulipofika, watu wengine bado walikuwa wakishangaa, wala sikutaka kuwa na wasiwasi, kama kuuza tayari nilikuwa nimeuza sana, nilichokifanya ni kushukuru kwa niaba yake kwa washikaji waliokuwa wakililinda gari na kisha kuingia garini.

AZIZA: Sasa hapa safari ni kwenda nyumbani. Unatakiwa kuwa huru, baba yangu ni mkali sana ila kwa sasa hayupo. Jiamini, usiwe na wasiwasi. Umenisikia.
MIMI: Ooopsss...nimekuelewa. Sasa kama akirudi ghafla?
AZIZA: Usiwe na wasiwasi. Kila kitu kipo under control.
MIMI: Mmmh! Aya bhana japokuwa huwa ninahofia sana kwenda nyumbani kwa mwanamke.
AZIZA: Hahaha! Kwa nini unaogopa?
MIMI: Unaweza kugeuzwa mwanamke....hahaha
AZIZA: Usijali Ibra. Hakuna mtu anayeishi nyumbani ambaye ametokea Mombasa. Kuwa na amani.
MIMI: Aya (Nilisema na Aziza kuwasha gari na kuondoka mahali hapo huku nikiwa nimezoa maksi nyingi sana kwa kila aliyeniona na Aziza).
Ila pamoja na hayo yote yaliyokuwa yakiendelea, nadhani sikutakiwa kwenda kwa kina Aziza. Mungu ametufumba macho kutojua mambo yanayotokea mbele yetu, kama angetupa uwezo, nadhani nisinge kwenda kwa kina Aziza kwani hali ilikuwa ni balaa tofauti na uhakika ambao alikuwa amenipa.....chezea wazee wa kiarabu kwa mabinti zao

MIMI: Mmmh! Mbona mapigo ya moyo yananidunda hivi?
AZIZA: Hahaha! Uoga wako tu. Au una BP?
MIMI: Hapana. Yaani kama kuna jambo baya linakwenda kunitokea.
AZIZA: Jambo gani na wakati nimekwishakwambia kwamba baba hayupo, nipo peke yangu.
MIMI: Na mama je?
AZIZA: Nae hayupo. Yaani kurudi kwao mpaka saa mbili usiku.
MIMI: Hapo mwakemwake.

Kiukweli nilikuwa na wasiwasi sana ila Aziza alijitahidi sana kuniondoa wasiwasi. Ngoja nikwambie kitu kimoja, hakuna wazee ambao ninawaogopa kwa mabinti zao kama wazee wa Kiarabu. Huwa hawataki utani kabisa, huwa hawataki ulete masihala kwa mabinti zao hata mara moja.
Kukutoa roho kwa sababu umemfuata binti yake wala haoni tatizo hata mara moja. Kwa Aziza, akajitahidi sana kuniondoa wasiwasi lakini sikufichi rafiki yangu, hofu bado ilikuwa ikiendelea moyoni mwangu.
Nikaona haina noma, mzee wa Kiarabu angenitishaje mimi mtoto wa Tandale na wakati kama fujo nimekwishazizoea? Mzee wa Kiarabu angenitishaje mtoto wa Tandale na wakati kama ugomvi tushazoea ? Nilikuwa nikijipa moyo ila nilipofikiria kwamba wazee wa Kiarabu walikuwa wakitumia hata bunduki kukudedisha, nikaona mweeeee...kazi ipo.
AZIZA: Tumekwishafika nyumbani. Karibu.
MIMI: Asante.

Mlinzi akafungua geti na kisha Aziza kuliingiza gari ndani. Nikabaki nikishangaa tu, sikuamini kama hapa Tanzania kulikuwa na watu ambao walikuwa wakiishi katika majumba makubwa kama ule mjengo aisee. Kulikuwa na bonge la bwawa la kuogelea, bustani kubwa ya maua pamoja na sehemu ya kuegesha magari. Mazingira ya nyumba yakanivutia sana, tukateremka na kisha kuanza kuangalia huku na kule, nilitaka kuyazoea mazingira japokuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kwangu.
AZIZA: Mbona unaangalia hivyo.
MIMI: Lazima niyazoee mazingira, naangalia vichochoro vya kufanyia uninja wangu mara mzee wako atakapotokea ghafla.
AZIZA: Acha hizo bwana. Mzee harudi sasa hivi, mpaka saa mbili usiku.
MIMI: Basi hakuna noma. Kuna nani mwingine ndani ya nyumba?
AZIZA: Mfanyakazi wa ndani. Wadogo zangu wote wapo shule nchini Kenya.
MIMI: Hakuna noma.

Tukaingia ndani na kisha kutulia. Macho yangu hayakutulia sehemu moja, yalikuwa yakiangalia huku na kule kama mtu ambaye nilikuwa natafuta jambo fulani. Sebule ilikuwa nzuri, ilivutia na kupendesha macho ya kila aliyekuwa akiiangalia. Nikakaribishwa katika mkochi mmoja mkubwaaaa, ile kukaa tu, nikayahisi makalio yakiingia ndani kabisa na kuzama kochini.

AZIZA: Hapa ndipo nyumbani. Karibu
MIMI: Asante
AZIZA: Nikuletee nini?
MIMI: Kwani kuna nini na nini?
AZIZA: Kuna juisi, soda, maziwa na maji.
MIMI: Kwa sababu nyumbani ni ngumu sana kunywa maziwa, hebu niletee maziwa.
AZIZA: Hahaha! Aya. Kuna kingine unachokitaka?
MIMI: Kama kuna vitafunio itakuwa full mzuka.
AZIZA: Unataka vitafunio gani?
MIMI:Kwani kuna nini na nini?
AZIZA: Kuna keki, mandazi, baga, pizza, chapati
MIMI: Duh! Utafikiri nimeingia hotelini. Fanya hivi. Kwa sababu sijawahi kula baga zaidi ya kuisikia kwa watu, hebu niletee hiyo na kwa sababu nasikia sikia watu wakitamba facebook sijui pizza tamu, nami niletee kwanza.
AZIZA: Utamaliza vyote Ibra?
MIMI: Kwani vikibaki si nitabeba! Au hairuhusiwi kubeba?
AZIZA: Inaruhusiwa.
MIMI: Basi niletee.

Usinishangae aiseee, hivi ndivyo nilivyo na nilikwishazoea kuishi maisha ya namna hiyo. Tandale hakukuwa na sehemu inayouza baga wala pizza, kwa hiyo kwa nini nisiagize baga na pizza nami nitoe ushamba mdomoni mwangu? Nikaletewa vitu nilivyovitaka, aiseee, kwanza nikajifanya kutokujua baga ipi pizza ipi, ikanibidi niulize.
MIMI: Pizza ipi na baga ipi?
AZIZA: Pizza hiyo ya duara na baga ni huo mkate wenye vitu mbalimbali.
MIMI: Mweee...kazi ipo. Nahisi leo nitaumwa sana tumbo.
AZIZA: Kwa nini?
MIMI: Tumbo langu halijazoea kula vitu hivi Aziza.
AZIZA: Usiogope, vitu vya kawaida tu.

Nikaanza kula buana, vilikuwa vitamu sana, tofauti na Aziza alivyofikiria kwamba ningebakisha, haikuwa hivyo, nikala vyote na kushushia na maziwa. Muda wote Aziza alikuwa akiniangalia, sijui alinionaje, sikutaka kujali, nilichokijali ni kupiga msosi tu.
Hayo ndio yalikuwa matukio ambayo niliyafanya mahali hapo, bado nilikuwa nikitaka kumuonyeshea Aziza kwamba mimi nilikuwa mtoto wa uswahili. Najua wale masharobaro wangeomba maji na pia kama wangeambiwa kuhusu chakula wangesema wameshiba, ila kwangu mimi mtu nisiyekuwa sharobaro, hahaha! Nikaagiza vitu ambavyo vilikuwa adimu kupatikana Tandale.
Nilichokuwa nikikifanya ni kucheza na akili ya Aziza tu, unajua unapoona umekuwa na msichana wa matawi ya juu halafu wewe unatoka uswahilini, usijifanye matawi sana na wakati kwenu ni wababaishaji tu. Nilitaka kumtia kipofu Aziza, nikajifanya sijawahi kula pizza na wakati mara nyingi nilikuwa nakwenda kuzinunua Magomeni karibu na msikiti wa Kichangani. Nikajifanya kwamba hata baga sijawahi kula na wakati nilikuwa nikipenda kuzinunua pale Kijitonyama katika sheli ya mafuta karibu kabisa na jengo la TTCL. Aziza akaniona kwamba kweli nilikuwa mtoto wa uswahilini

MIMI: Nashukuru kwa chakula chako na kinywaji chako. Nadhani sasa ni wakati.
AZIZA: Asante kwa kushukuru. Wakati gani?
MIMI: Wa kuniambia kile ambacho kila siku nilikuwa nikikihitaji sana kwako.
AZIZA: Kipi?
MIMI: Kuwa msichana wangu wa dhati.
AZIZA: Hahaha! Hausahau?
MIMI: Nitasahau vipi na wakati ninakupenda. Then ukiona nakumbuka basi jua kwamba wewe ni mtu muhimu sana kwangu. Kama usingekuwa muhimu, nisingekumbuka.
AZIZA: Hahaha! Nisikilize Ibra, najua kwamba unanipenda ila...
MIMI: Ila nini tena?
AZIZA: Nahofia.
MIMI: Unahofia nini?
AZIZA: Kuwa na wewe. Naweza kufa kwa presha.
MIMI: Haha! Hakuna kitu kama hicho. Nahitaji kuwa na wewe tu. Hebu fikiria muda wote ambao nimeupoteza kwa ajili yako Aziza, umekuwa rafiki yangu mkubwa, rafiki ambaye sikutaka kumpoteza katika maisha yangu yote.
AZIZA: Najua. Tuendelee kuwa marafiki.
MIMI: Nisikilize Aziza. Kila kitu kinakwenda na nyakati pamoja na mabadiliko. Najua kabisa kwamba kabla ya baba yako kumuoa mama yako walikuwa marafiki, si ndio?
AZIZA: Ndio.
MIMI: Baadae wakabadilika na kuwa wapenzi, si ndio?
AZIZA: Ndio.
MIMIl Na mwisho kabisa wakawa mke na mume. Nimekosea?
AZIZA: Haujakosea.
MIMI: Yeah! Hayo ndio maisha yalivyo. Tumekuwa marafiki kwa kipindi kirefu, inatupasa tubadilishe kila kitu kwa wakati huu, kutoka kwenye urafiki mpaka kuwa wapenzi, tukitoka hapo, itatupasa tubadilike pia, tuje kuwa wachumba na hatimae mke na mume.
AZIZA: Mmmh! Ibra una malego ya mbali.
MIMI: Yeah! Hayo ndio maisha yanavyotakiwa kuwa. Hatutakiwi kila siku tufikirie kuhusu hapa tulipo, yatupasa tufikirie kule tutakapokuwa kesho. Ukiona mtu anafikiria zaidi hapa, kidogo atakuwa na matatizo fulani kichwani.
AZIZA: Naomba nikuulize swali. Unanipenda?
MIMI: Nadhani macho yangu yanaelezea kila kitu. Siku zote mapenzi ya msichana huonekana katika tabasamu lake ila mapenzi ya mvulana huonekana machoni mwake. Unaona nini machoni mwangu?
AZIZA: Mapenzi.
MIMI: Yeah! Hicho ndicho kitu kilichomo moyoni mwako juu yako. Nakupenda sana.
AZIZA: Najua.
MIMI: Naomba kitu kimoja Aziza.
AZIZA: Kitu gani?
MIMI: Lipsi zako.
AZIZA: Zimefanyaje?
MIMI: Nataka kuona ni jinsi gani zilivyo laini.
MIMI: Unamaanisha nini?
MIMI: Haujajua namaanisha nini? Subiri.

Nikainuka pale nilipokuwa na kisha kumsogelea. Lengo langu kubwa mahali hapo lilikuwa ni moja tu, kubadilishana mate na kisha nione lipsi zake zilikuwa laini kiasi gani. Hakuonekana kuwa mchoyo, akanipokea, huku lipsi zetu zikiwa zinatamaniana tu, ghaflaaaaa....tukasikia honi ya gari getini. Kwa haraka sana Aziza akainuka na kisha kuchungulia dirishani, geti lilipofunguliwa, alikuwa baba yake.
AZIZA: Mungu wangu! Baba!
MIMI: Unasemaje?
AZIZA: Baba. Baba amerudi.
MIMI: Amerudi (Nikainuka na kwenda kuchungulia dirishani, gari aina ya Range la baba yake lilikuwa linaingia)
AZIZA: Mungu wangu! Sijui nifanye nini.
MIMI: Wewe si ulisema baba yako anarudi saa mbili usiku?
AZIZA: Ndio. Sijui leo imekuwaje.
MIMI: Mmmh! Hiki kifo (Nilijisemea moyoni huku nikitetemeka na haja ndogo ikitaka kunitoka)

Aziza alionekana kama kupigwa ganzi, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati huo, nilimuona akianza kutetemeka huku kwa mbali kijasho chembamba kikianza kumtoka. Hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa akikiona mahali pale.

MIMI: Kwa hiyo?
AZIZA: Sijui nifanye nini.
MIMI: Chumba chako kipo wapi?
AZIZA: Njoo.

Nikaanza kumfuata kule aliponiambia nimfuate, chumbani. Nilijua fika kwamba katika kipindi hicho akili yake haikuwa sawa, mimi kama ninja nikatakiwa kufanya manuva. Tukaenda mpaka chumbani kwake, alikuwa akiendelea kutetemeka tu. Baada ya kufika chumbani, mtu mzima nikabaki nikikiangalia chumba kile, kilionekana kuwa na mvuto sana.

AZIZA: Kwa hiyo.
MIMI: Daah! Ngoja nizame chini ya kitanda (Sikutaka kuchelewa hata sekunde kumi, mtu mzima nikazama chini ya kitanda)

Huko chini kulionekana kusafi ajabu, kitanda kile kikubwa cha chuma kilikuwa na nafasi ya kutosha kabisa. Kitu cha kwanza nilichokifanya ni kuichukua simu yangu na kisha kuiweka katika silent. Nilibaki nikijiuliza sana kwamba kwa nini jambo kama lile lilikuwa likinitokea? Kwa nini Aziza alikuwa ameniaminisha sana mimi kwenda kwao mpaka kutaka kuniletea msala? Kila nilichojiuliza nikakosa jibu. Kule chini ya kitanda nikaanza kuchati na Eduado kupitia sms za kawaida.

EDUADO: Ibra umefikia wapi?
MIMI: Kaka acha. Nipo kwao.
EDUADO: Du! Upo kwao? Wewe noma. Ilikuwaje kuwaje hadi umefika kwao?
MIMI: Alikuja kunichukua home.
EDUADO: Sikupatii picha mtu mzima. Leo malovee hapo hapo chumbani kwake.
MIMI: Haha! Kaka acha, huku msala. Nipo uvunguni.
EDUADO: Uvunguni! Kivipi tena?
MIMI: Baba yake amefika na wakati dogo alisema kwamba anarudi saa mbili usiku. Karudi kwa kushtukiza, yaani hapa nimeingia chumbani kwake na kujificha uvunguni.
EDUADO: Hahaha! Kaka hiyo kweli noma, sikupatii picha aisee ulivyojipinda huko mtu mzima, kama dawa ya mbu.
MIMI: Kaka wewe acha tu, huku ni noma. Ukisikia nimepigwa risasi, usishangae.
EDUADO: Dah! Ngoja nikuombee Mungu akuokoe.
MIMI: Wewe unafikiri Mungu atanisaidia hapa?
EDUADO: Atakusaidia tu.
MIMI: Kunisaidia anaweza ila dah! Kaka mimi ni mwenye dhambi. Nafikiri atataka nikamatwe ili nisirudie mchezo wangu wa kusalandia watoto wa watu.
EDUADO: Kaka pole sana. Sasa mtoto anasemaje?
MIMI: Yaani hapa ni kujiokoa mwenyewe. Aziza anazingua, anaonekana kuogopa sana.
EDUADO: Kwa hiyo utatokaje humo uvunguni?
MIMI: Ngoja kwanza giza liingie manake huku mtu unaweza kufa.

Mtu mzima nilikuwa nazidi kutetemeka chini ya uvungu wa kitanda, Aziza hakuwa akitulia, mara aingie, mara atokea hali ambayo ikanionyeshea angetoa boko muda wowote ule. Nilichokifanya nikachukua simu yangu na kisha kuanza kumtumia meseji.

MIMI: Nini kinaendelea hapo?
AZIZA: Baba amekaa sebuleni, amekuja na wageni. Tena wageni ambao watalala hapa hapa nyumbani.
MIMI: Hilo sio tatizo sana. Wa kike au wa kiume?
AZIZA: Wa kike.
MIMI: Duuh! Ila si watalala chumba cha wageni?
AZIZA: Yeah! Ila wengine watalala katika chumba changu. Mbaya zaidi baba ameniambia nije kusogeza kitanda ili kiingizwe kitanda cha pili.
MIMI: Duuuh! Leo kazi ipo.
AZIZA: Mbaya kuliko zote amemwambia mdogo wangu aje kufagia chumbani.
MIMI: Wewe si ulisema wadogo zako wapo shule bording?
AZIZA: Nilikuwa nimekudanganya.
MIMI: Mungu wangu! Nimekwisha.
AZIZA: Naomba uniambie nifanye nini Ibra.
MIMI: Kwanza kabla ya yote punguza presha.
AZIZA: Sawa.
MIMI: Najua kwamba leo nakwenda kukamatwa, kabla sijakamatwa naomba uniambie kitu kimoja.
AZIZA: Kitu gani?
MIMI: Unanipenda?
AZIZA: Nakupenda Ibra.
MIMI: Upo tayari tuingie katika mahusiano kwa muda mchache uliobakia kabla sijauawa na baba yako?
AZIZA: Ibra usiseme hivyo.
MIMI: Wewe unafikiri nitasemaje? Naomba unijibu. Upo tayari?
AZIZA: Nipo tayari lakini jua hautokwenda kuuawa.
MIMI: Nimefanya kila kitu kwa ajili yako, nilihisi mambo haya yatatokea tu toka tulipokuwa tukija. Ila usijali. Ngoja nikuonyeshe jinsi mchezo unavyofanyika Aziza. Nataka nikuonyeshe kwamba huwa sikamatwi kijinga jinga.
AZIZA: Utafanya nini sasa?
MIMI: Cha kwanza hakikisha mdogo wako haji kusafisha chumba, akifika chumbani mpokonye fagio, ng’ang’ania kusafisha chumba chako.
AZIZA: Sawa. Cha pili?
MIMI: Hakikisha kila unapotoka chumbani, unafunga mlango kwa ufunguo, cha tatu, uache mlango wa jikoni wazi, cha nne mpe taarifa baba yako kwamba kuna mtu alikuja kumuulizia.
AZIZA: Mmmh! Huyo mtu nani?
MIMI: Ibra...ila leo niite jina la Ahmed.
AZIZA: Akisema yupo vipi?
MIMI: Mwambie kama jinsi nilivyo. Usitie shaka.
AZIZA: Kingine nisemeje?
MIMI: Mwambie kwamba ningekuja baadae kumuulizia tena.
AZIZA: Mhh!
MIMI: Usijali. Kila kitu kipo under control.
AZIZA: Sawa.

Baada ya dakika kadhaa, nikasikia mlango ukifunguliwa, nikasikia vishindo vikija kwa kasi, alikuwa mdogo wake ambaye alitaka kusafisha chumba kwa kukifagia, Aziza akafika na kisha kumpokonya ufagio kwa kutaka kufagia yeye mwenyewe. Mdogo wake alipoondoka, akakiinamisha kichwa na kisha kukutana nami.

MIMI: Vipi huko?
AZIZA: Bado hali ni ngumu.
MIMI: Daah! Sikamatwi kijinga hapa. Fanya kama nilivyokwambia, umesikia?
AZIZA: Sawa.
MIMI: Nakupenda mpenzi.
AZIZA: Nakupenda pia (Tukafanya kile tulichotaka kukifanya pale sebuleni....lol)

Aziza akaondoka, nikaona sio ishu, niliendelea kukaa uvunguni mule. Nazo dakika zilikuwa zikisogea tu, zilisogea zaidi na zaidi, mpaka saa moja usiku inaingia, mtu mzima nilikuwa mule mule ndani, chini ya uvungu. Saa mbili kasoro nikaona ungekuwa ujinga, nikamtumia Aziza meseji.

MIMI: Njoo uvunguni kwanza.
AZIZA: Sawa.
MIMI: Ila kabla ya kuja, cheki kuna nani jikoni.
AZIZA: Yupo mama.
MIMI: Vizuri sana
AZIZA: Vizuri?
MIMI: Yeah! Njoo kwanza huku uvunguni.

Baada ya muda, Aziza akafika, hakuonekana kuwa na amani.

AZIZA: Unasemaje baby?
MIMI: Hapa naondoka na kuelekea jikoni, cha msingi kamtoe mama yako jikoni.
AZIZA: Mmmh! Nitamtoa vipi?
MIMI: Kamwambie kwamba baba yako anamuita.
AZIZA: Eeeh!
MIMI: Fanya hivyo. Una dakika moja ya kufanya hivyo. Nakwenda na muda.
AZIZA: Halafu?
MIMI: Wewe kamwambie hivyo. Akija sebuleni mimi utanikuta nje ambapo huko sebuleni utamwambia baba yako kwamba kulikuwa na mtu alikuja kumuulizia. Umesikia
AZIZA: Na mama akifika sebuleni na kusema kwamba kaitwa kumbe hajaitwa?
MIMI: Mwambie uliskia vibaya.
AZIZA: Sawa. Umeifungua
MIMI: Kwenye ile dakika moja, umebakisha sekunde arobaini. Nenda, ukitoka zima taa ya humu chumbani na uuache mlango wazi kidogo
AZIZA: Sawa.

Aziza akaondoka mahali hapo, na kweli akaelekea jikoni na kumwambia mama yake kwamba alikuwa akiitwa na baba yake, nilipomuona mama yake akipita ukumbini kueleka sebuleni, nikaufungua mlango na kupita kuelekea jikoni kwa kasi huku nikihakikisha sisikiki, nikaufungua mlango na kutoka nje kwa nyuma, nikaanza kuambaa ambaa mpaka pembeni ya gari lao.

MAMA AZIZA: Nimekuja mume wangu.
BABA AZIZA: Kuna nini?
MAMA AZIZA: Aziza amekuja na kuniambia unaniita.
BABA AZIZA: Mimi! Hapana, labda kasikia vibaya.
AZIZA: Si nimesikia unamuita mama.
BABA AZIZA: Hapana.
AZIZA: Basi samahani nilisikia vibaya
MAMA AZIZA: Usijali. Nipo jikoni naandaa chakula kwa sababu dada wa kazi anaumwa, amelala na huyu Aziza asije akatoa chakula kibichi
BABA AZIZA: Sawa. Aziza, wapeleke chumbani wageni hawa.
AZIZA: Sawa. Ila leo kuna mtu alikuja kukuulizia.
BABA AZIZA: Nani?
AZIZA: Sijui, ila alisema atarudi usiku.
BABA AZIZA: Yupo vipi?
AZIZA: Mrefu kidogo, maji ya kunde halafu ana.........!

MLANGO: Ngo ngo ngo ngo (Nilikuwa nikipiga hodi huku mlinzi akionekana kunishangaa kwani aliniona ninavyoingia na Aziza, alikuwa hajui sababu kwa nini nilikuwa nimetokea nyuma ya nyumba na kuanza kugonga mlango. Mlango ukafunguliwa, alikuwa Aziza, kama vile sterring, nikaingia ndani, Baba yake Aziza akabaki akiniangalia, sikufichi, nilijiamini kama Van Damme)

Baba yake Aziza alikuwa amenitolea macho pamoja na wageni wote ambao walikuwa sebuleni, mtu mzima sikutaka kuteteleka hata kidogo, nilionyesha uso wa kujiamini kupita kawaida. Kwa Aziza, kwa mbali alionekana kuwa na hofu kwani alidhani kwamba nisingekuwa na ujasiri wa kusimama na kuzungumza.

MIMI: Samahani mzee. Shikamoo.
BABA AZIZA: Marahaba.
MIMI: Nilikuja katika kipindi kilichopita lakini sikukuta.
BABA YAKE AZIZA: Sikuwepo. Sawa, umeshanikuta. Kuna nini?
MIMI: Niliagizwa na mzee Badour wa kule Msasani, ameniambia kwamba leo utatakiwa kufika katika kikao kile cha harusi kinachoendelea (Baba Aziza akaonekana kushtuka)
BABA AZIZA: Kikao gani?
MIMI: Kile cha mtoto wake, Farhia.
BABA AZIZA: Huyo mzee ndiye nani?
MIMI: Mfanyabiashara mwenzako.
BABA AZIZA: (Huku akionekana kushangaa zaidi) Alikutuma uje kwangu?
MIMI: Ndio (Nilijibu huku nikiwa serious)
BABA AZIZA: Una uhakika ni mimi?
MIMI: Ndio.
BABA AZIZA: Yeye alikwambia uende kwa nani?
MIMI: Kwako.
BABA AZIZA: Nani?
MIMI: Mzee Mahmoud.
BABA AZIZA: Hapana. Mimi sio mzee Mahmoud. Mimi ni mzee Mansour.
MIMI: Mmmh! Mbona unanichanganya? Hii si nyumba namba 315?
BABA AZIZA: Hapana. Hii ni nyumba namba 511. Nyumba kuanzia namba 300 zipo kule mbele.
MIMI: Ok! Basi samahani kwa usumbufu mzee wangu. Nikosea namba, ila nilipomuuliza mlinzi alijibu hapa ni kwa mzee Mansour ila jina likanichanganya, si unajua sisi wengine majina ya kiarabu hatuyajui vizuri.
BABA AZIZA: Usijali kijana. Najua vijana wa sasa hivi mnakuwa na mambo mengi vichwani. Sawa. Nenda.
MIMI: Usijali (Nikageuka na kisha kuufungua mlango huku Aziza akibaki kutetemeka tu)
MLINZI: Ebwanaa vipi tena, mbona sikuelewielewi?
MIMI: Hakuna tatizo. Nilikuwa nataka kuonana na mzee Mansour tu, kuna uninja nilikuwa nakamilisha mara moja.
MLINZI: Uninja gani?
MIMI: Wa kucheza na akili za watu
MLINZI: Kivipi?
MIMI: Usijali, hili liko nje ya uwezo wako, ukitaka kulifahamu, utachanganyikiwa.
MLINZI: Mmmh! Sawa! Karibu.
MIMI: Asante.

Nikashusha pumzi ndefu, sikuamini kama niliweza kutoka katika mikono ya mzee yule aliyeonekana kuwa na hasira kupita kawaida. Nilitembea kwa mwendo wa haraka haraka mpaka kituoni ambapo nikapanda gari na kisha kuelekea nyumbani. Garini, mawazo yangu yalikuwa juu ya ule msala ambao nilikuwa nimenusurika, ulikuwa msala mkubwa ambao ungeweza kunitoa roho kama ningeleta ishu za Kisharobaro kama Eduado. Nilipofika nyumbani, nikaanza kuchati na Aziza.

AZIZA: Hakuna kama wewe. Umeshindikana mpenzi. Wewe ni genius.
MIMI: Hahaha! Tena ana bahati leo sikutaka kuleta usanii mkubwa zaidi.
AZIZA: Mmh! Kwani ungeweza kuleta zaidi ya ule?
MIMI: Yeah! Yaani mngenibeba pale.
AZIZAl: Hahaha! Hapana chezea wewe mtoto wa Tandale, umeshindikana aisee.
MIMI: Hahaha! Usijali. Kokote kunapokuwa na ishu zinazohitaji mafunzo ya kininja wewe niite tu, usiogope. Hata ukitaka kuingia Ikulu, wewe niite tu na kila kitu kitakuwa poa.
AZIZA: Mmmh! Unajiamini wewe.
MIMI: Acha masihala na mimi.
AZIZA: Ok! Leo sichati sana ila ningependa kuonana na wewe kesho.
MIMI: Wapi?
AZIZA: Popote upendapo.
MIMI: Poa. Tuonane gesti.
AZIZA: Hahaha! Acha masihala.
MIMI: Ndio maana nimekwambia sema wapi. Yaani ni sawa na kuja Tandale halafu nikuulize unakunywa kinywaji gani, je ukisema unataka maziwa, nitayatoa wapi? Ukija huku sikuulizi unakunywa kinywaji gani, nakuuliza unakunywa soda gani.
AZIZA: Hahah! Wewe mtoto wewe. Najivunia kuwa na mtu kama wewe.
MIMI: Usijali. Kuwa serious, tuonane wapi?
AZIZA: Njoo chuo.
MIMI: Saa ngapi?
AZIZA: Muda wowote ule.
MIMI: Poa. Nitakuja saa nne usiku.
AZIZA: Nini?
MIMI: Hebu kuwa serious, nije saa ngapi?
AZIZA: Njoo saa tisa. Unalijua lile jengo la Biashara la UDBS?
MIMI: Yeah! Si pale karibu na kituo cha polisi, opposite na mini-super market?
AZIZA: Yeah!
MIMI: Poa nitakuja.
AZIZA: Usichelewe, kuna bonge la sapraizi nataka kukuonyeshea.
MIMI: Mmmh! Lipi hilo?
AZIZA: Nikikwambia haitokuwa sapraizi. Wewe njoo tu.
MIMI: Poa.

Kuanzia kipindi hicho sikuonekana kuwa na furaha tena, muda wote nilikuwa nafikiria kuhusiana na sapraizi hiyo ambayo Aziza alikuwa ameniahidi. Sikufichi rafiki yangu, usiku ulikuwa mrefu kwangu. Sikutaka kuchati na Aziza, nililala moja kwa moja mkpaka kesho ambapo nikaamka. Kutokana na ubize wa hapa na pale, nikaenda chuo saa tisa na kisha kumuita aje nje ya jengo lile la UDBS, haukuchukua muda, akatoka huku akiwa na Eduado, wote walikuwa wakicheka jambo lililonichanganya.

AZIZA: Karibu mpenzi.
MIMI: Asante. Mbona mnacheka hivyo mtafikiri mnamwangalia Mr Bean?
EDUADO: Ungekufa. Watoto wa Waarabu si wa kwenda kuwavaminia kwao. Matokeo yake ukajificha uvunguni, sikupatii picha, ulijikunja kama dawa ya mbu.
MIMI: Hahaha! Aisee ni noma. Kweli nimeamini mtu akifumaniwa, acha awe mdogo kama panadol.
AZIZA: Kwanza twendeni tukapate lunch, au Ibra umeshiba?
MIMI: Nimekula home ila sijashiba wala nini. Wazo ulilolitoa liko poa. Msosi wapi?
AZIZA: Kule bondeni.
MIMI: Wanapakua kingi au nao wababaishaji.
AZIZA: Kikiwa kidogo utaongeza.
MIMI: Namna hiyo, hayo ndio maneno. Ila hapa nina 400 ya nauli tu.
AZIZA: Usijali. Nitakurudisha na gari.
MIMI: Hapo mzuka zaidi. Itakubidi uniongezee shilingi mia ninunue vocha ya 500 ili niingie facebook baadae.
AZIZA: Usijali. Nitakutumia elfu kumi kabisa.
MIMI: Duh! Sasa simu yangu si itazima
AZIZA: Kwa nini?
MIMI: Haijazoea kuingiza kiasi kikubwa cha hivyo. Sawa na mgonjwa wa Tandale ukampelekea juisi ya shilingi elfu kumi. Anaweza kufa.
AZIZA: Hahaha! Kwa nini?
MIMI: Tumbo limeingiza kitu kigeni kwa hiyo inaweza kuonekana kama asidi.
AZIZA/EDUADO: Hahaha.
MIMI: Huo ndio ukweli. Ila nina swali.
AZIZA: Swali lipi?
MIMI: Nahisi kama mnanificha. Kuna ishu inayoendelea hapa?
AZIZA: Muulize Eduado.
MIMI: Eti kaka kuna nini?
EDUADO: Aziza anakupenda. Alikuwa akikuhitaji toka zamani ila alikuwa akiogopa kukwambia, akaniambia nifanye juu chini mpaka anakupata.
MIMI: Unasemaje?
EDUADO: Ndio hivyo. Anapenda kusoma kila unachokiandika facebook, amekuwa rafiki yako mkubwa, akavutiwa na wewe ila alikuwa akikuhitaji, alichokifanya, akakuunfriend na kisha kujifanya mtu mpya kwako.
MIMI: Aiseee...duh! kwa hiyo kila kilichokuwa kikiendelea kilikuwa kikijulikana?
EDUADO: Yeah! Huo ndio ukweli.
MIMI: Sasa na wewe Aziza ulikuwa unaogopa nini kuniambia?
AZIZA: Maadili.
MIMI: Kivipi?
AZIZA: Msichana hatakiwi kumuanza mvulana.
MIMI: Hahaha! Ningekuwa na girl mwingine je?
AZIZA: Ningepigana mpaka nikupate.
MIMI: Hahaha! Aya buana. Mchezo wenu umefanikiwa na wote mmeshinda. Hebu kwanza ongezeni mwendo washikaji, unajua hapa nina ubao ile mbaya mpaka tumbo linasikia kizunguzungu.
AZIZA: Mmmh! Kwani tunatembea taratibu?
MIMI: Mnatembea kama mnamsindikiza Bibi Harusi.

Hicho ndicho kitu ambacho nilitaka kukwambia kila siku katika maisha yangu. Aziza ndiye alikuwa msichna wangu, nilimpenda na kumthamini sana. Japokuwa alikuwa msichana mwenye uwezo lakini kila alipokuwa pamoja nami alikuwa akionyesha heshima ya hali ya juu japokuwa nilikuwa nikiishi Tandale. Aziza alinipenda, nilimpenda pia, tulifanya mengi sana hasa yale ambayo wapenzi huyafanya faragha. Mpaka leo hii, bado ninampenda mtoto huyu ila cha ajabu....hahaha! hata kwao sitamani kukanyaga.

MWISHO.

 LIKE PAGE YETU HAPA ==>www.facebook.com/2jiachie

No comments