Header Ads

APR kwa Yanga lazima mkae leo


MSHINDI wa leo kati ya Yanga na APR katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika atacheza ama na Al Ahly ya Misri au Recreativo do Libolo ya Angola, hilo halimsumbui hata kidogo Kocha Hans van Der Pluijm.
 

Yanga inacheza na APR jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 2-1 katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) wiki iliyopita huko Kigali, Rwanda.
 

Ili isonge mbele, Yanga inahitaji sare yoyote au ushindi iweze kusonga mbele, lakini kocha wake, Pluijm raia wa Uholanzi ameliambia Championi Jumamosi kuwa; “Hilo linawezekana.”
Pluijm alisema tangu waliporejea nchini wikiendi iliyopita kutoka Rwanda katika mchezo wao wa kwanza, amefanya maandalizi kabambe na wachezaji wake na sasa wapo tayari kwa mchezo.
 

“Licha ya kuifunga nyumbani kwao, APR ni timu kubwa na najua wanakuja kutafuta ushindi ili wasonge mbele, sisi tumejiandaa kufanya vizuri na tayari tumefanyia kazi upungufu tuliouona Kigali licha ya kushinda.
 

“Lengo tuliyojiwekea mwaka huu kwenye michuano hii ya kimataifa tunayoshiriki ni kusonga mbele zaidi ili tufika mahali pazuri na siyo kuishia katika mechi hizi za mwanzoni.
“Tunacheza nyumbani na faida ya mashabiki tofauti na awali tulipokuwa ugenini, ni wakati wa Wanayanga wote na Watanzania kutuunga mkono naamini tutasonga mbele,” alisema Pluijm raia wa Uholanzi.
 

Kwa upande wake, Kocha wa APR, Nizar Khanfir ameahidi vijana wake kucheza kwa bidii ili wasonge mbele kwani wameshafanyia kazi makosa yaliyowafanya wafungwe nyumbani.
Khanfir raia wa Tunisia anayeiongoza APR katika mechi ya pili tangu aanze kazi wiki iliyopita, alisema katika mechi ya awali kipa na mabeki hawakufanya vizuri ndiyo maana Yanga ilishinda lakini sasa wapo fiti.
 

“Ni ngumu kuzungumzia mchezo huu, tunacheza na timu nzuri lakini awali tulifanya makosa mawili na wapinzani wetu wakayatumia kupata mabao mawili. Tumere-kebisha makosa na sasa tunataka ushindi ugenini.
“Bado nafasi ya kusonga mbele tunayo kwani bao moja tulilofunga nyumbani limetupa nguvu ya kupambana zaidi, tuna morali ya hali ya juu na tunajiamini kwa mechi ya leo,” alisema Khanfir.
 

“Katika mchezo kwanza, kipa na mabeki hawakuwa na uelewano ndiyo maana walifanya makosa mawili na tukafungwa, sasa kama Yanga ilishinda ugenini, sisi pia tunaweza kufanya hivyo hapa.”
 

Mwamuzi wa mchezo wa leo ni Bernard Camille wa Shelisheli ambaye alichezesha mechi ya robo fainali ya Kombe la Afrika, mwaka jana kati ya Congo na DR Congo mjini Bata huko Equatorial Guinea ambapo DR Congo ilishinda 4-2.
 

Yanga itaingia uwanjani ikimkosa beki wake wa kulia Juma Abdul ambaye ana kadi mbili za njano lakini nguvu ya ushambuliaji kwake itabaki kwa MTN inayoundwa na Simon Msuva, Amissi Tambwe na Donald Ngoma huku viungo Thabani Kamusoko na Haruna Niyonzima wakitarajiwa kufanya vizuri pia.
 

Wakati Yanga ikitegemea nyota wake hao, APR inayomilikiwa na Jeshi la Rwanda yenyewe itawategemea mabeki Abdul Rwatubyaye na Emery Bayisenge na viungo Yannick Mukunzi na Jean Claude Iranzi na mshambuliaji Patrick Sibomana.
Mshindi wa leo atacheza ama na Al Ahyl ya Misri au Libolo ya Angola ambazo zinarudiana leo kwenye Uwanja wa Borg El Arab huko Alexandria, Misri baada ya wiki iliyopita kutoka suluhu mjini Calulo, Angola.

No comments