Header Ads

AY: Asimulia alivyopokewa Uganda na Bob Wine

Wiki iliyopita niliishia pale nilipokuwa namshukuru mmoja wa wasomaji ambaye alinipa ushauri, lakini nawashukuru mashabiki na wasomaji wa makala haya kwani ninyi ndiyo haswaaa mlionifanya nifike hapa nilipo.
Wiki hii nitaendelea kuzungumzia harakati zangu za kimuziki hasa nje ya Bongo kwani soko na heshima kama msanii wa Kitanzania nilikuwa nimeishaijenga. Hivyo nilitamani sana kufungua mipaka, kichwani mwangu wazo la kwanza likiwa moja ya nchi ya Afrika Mashariki.
Songa nami…

“Nilianza kuwa na ndoto za kuuendeleza muziki wangu au Muziki wa Bongo Fleva kwa ujumla na kuupeleka ngazi ya kimataifa.

“Hiyo ilikuwa mwaka 2003 ambapo nilikuwa nikiumiza sana kichwa kufikiria kuwa ina maana muziki wangu utakuwa ni kwa ajili ya Watanzania pekee yake, jibu nililolipata ni hapana,  napaswa nifanye kitu kuutambulisha Muziki wa Bongo Fleva nje ya mipaka, baada ya maswali ya muda mrefu mwisho nikapata jibu ndipo niliamua kuanza harakati zangu.

“Mwaka huo nakumbuka kwa mara ya kwanza nilifunga safari ya kwenda nchini Uganda wakati huo nikiwa sina ndugu, rafiki wala jamaa na nilikuwa sijawahi kufika huko, niliondoka kwa basi hadi Uganda, nilipofika nikapata bahati ya kupokelewa na kijana mmoja wa Kitanzania aliyekuwa anafahamiana na Bob Wine nchini humo.

“Wakati naingia Uganda nilikuwa nautazama kwa shauku sana mji ule na nikajikuta nikijisemea kimoyomoyo ni lazima watu wa mji huu wanitambue vizuri kwamba (AY) ni nani?

“Kwa wakati ule nilipata changamoto sana kwani hata kaka yangu aliyechangia kwa sehemu kubwa katika harakati zangu ni DJ mkongwe nchini, DJ Venture niliyewahi kumwambia kuwa ndoto zangu ni kufika ngazi za kimataifa lakini kwa mazingira na kipindi kile alinishangaa sana na tukawa kama tunabishana, na kuniambia kuwa nafikiriaje kuutoa muziki wa Kibongo, Tanzania na kuupeleka nje ya mipaka, nikamwambia ndivyo dhamira yangu inanituma kufanya hivyo ila kwa sasa kuna wakati huwa tukikaa tunaanza kucheka sana kwani nilikuwa nimeshatimiza.

“Baada ya kufika Uganda na kupokelewa na Bob Wine na yule Mtanzania wakanitambulisha  kwa Ma-dj, watangazaji, waandishi wa magazeti na kesho yake nikapafomu kwenye klabu moja inaitwa Silk na watu walipenda sana baada ya kama mwezi mmoja nikaitwa kwa ajili ya shoo, hapo ndipo nilipoanza harakati zangu, na baadaye nikaenda Kenya kufanya kazi na wasanii wengine kama nilivyowahi kueleza matoleo yaliyopita.

“Naweza sema Uganda na Kenya ni kama nyumbani (Tanzania) kwani Ma-dj, wafanyabiashara, mashabiki, marafiki watangazaji wote nafahamikana na kufanya nao kazi kama ninavyofanya kazi ninapokuwa Dar.
“Baada ya albamu yangu ya kwanza ambayo niliitoa kwa ajili ya Watanzania niliamua kufanya uzinduzi wa albamu yangu ya pili ya Hisia Zangu sambamba na albamu ya msanii, Khalid Mohamed T.I.D ya Burudani na kufanya tamasha lile tulipe jina la Hisia za Burudani, ilikuwa ni mwaka 2005 na nakumbuka tulifanyia Diamond Jubilee jijini Dar.

“Naweza kusema Tamasha la Hisia za Burudani liliwakutanisha wasanii wengi wa Afrika Mashariki akiwemo msanii, Naziz (wa Kundi la Necessary Noise), Prezzo, Tatuu (Kenya),  Maurice Kirya (Uganda)  na wengineo.
“Baada ya harakati hizo ndiyo hapo saa nilipopata hamu nyingine ya kuendelea kusonga mbele hadi nikafanikiwa kushirikiana na wasanii kutoka Nigeria, Jamaika, Marekani na kwingineko
“Kimsingi kazi zangu nazipanga kwa hatua, ambapo mpaka sasa kuna mikakati mingine naendelea kufikiria kwa sababu nyumbani, Afrika Mashariki na sehemu zingine za dunia tayari, kiukweli kuna baadhi ya wanamuziki wa mataifa mengine tunawapa presha na ninaamini kama tutakuwa na bidii pamoja na nidhamu tutafika mbali sana kikubwa ni kuwa na ushirikiano katika kuonesha namna ya kuzitumia fursa zinazopatikana.

Usikose tena wiki ijayo kwenye simulizi hii nzuri ya msanii nguli Ambweye Yessaya.

No comments