Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 11


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Walitembea hadi barabarani ambako wote waliingia tena ndani ya teksi waliyotoka nayo Tabora na kuendelea na safari yao kwenye majengo mawili makubwa ya bati, Mariam akamwamuru dereva asimame.
“Simama hapo pembeni ya hizo nyumba!”
“Hapa ndio nyumbani kwenu?”
“Ndiyo! Baba yangu ni mganga katika hii hospitali!”
“Wewe ni mtoto wa Mabula na mke wake Elizabeth?” Dereva aliuliza
“Ndiyo! Unawafahamu?” Aliitikia Mariam
“Mimi ni mtu wa Sikonge na hakuna mtu asiyewafahamu watu hawa katika wilaya yetu! Tiba zao zimewasaidia wengi sana!”
“Basi hao ndio wazazi wangu na mimi naishi nao hapa nyumbani ila nilikuwa nimekwenda kumtembelea mjomba wangu Mikumi huko Morogoro, karibu sana!” Aliongea Mariam akisaidia kushusha mizigo kwenye gari.
Wakati wakiongea hayo Nancy alikuwa kimya, kichwa chake kilijaa tani kadhaa za mawazo, alishindwa kuielewa hati yake kama asingempata mzee Mwinyimkuu, alitamani kufa badala ya kuendelea na maisha ya mateso. Kumbukumbu za wazazi wake zilizidi kumchanganya na kuna wakati Tonny aliingilia kati, alimtupia kila aina ya lawama kama mtu aliyeharibu maisha yake yote.
“Tonny! Sijui kama naweza kumsamehe!” Aliwaza Nancy wakati akishuka na wote wakaagana na dereva wa teksi na kuongoza kwenda mbele ya nyumba iliyokuwa pembeni, Mariam akagonga kwa muda wa karibu dakika kumi ndipo mlango ukafunguliwa.
“Wawooooo! Karibu tulimo mkaya!”(Haooooo! Karibuni ndani!) Mama yake Mariam alisema wakati akiwapokea mizigo yao na kuwakaribisha ndani ambako salamu ziliendelea.
Baba yake Mariam baadaye aliungana nao ikawa ni furaha kubwa katikati ya usiku, kama ilivyo kawaida ya Wanyamwezi mama yake Mariam alinyanyuka akitaka kwenda jikoni kuandaa chakula lakini mwanae akamzuia akidai ulikuwa ni usiku mkubwa mno wangeweza kuvumilia.
“Sasa wewe unaongea, je kama mgeni ana njaa?” Mama yake Mariam aliongea huku akitabasamu.
“Hapana mama, sijisikii kula kabisa!” Nancy aliingilia kati ni kweli kwa mawazo aliyokuwa nayo kichwani mwake asingeweza kutia kitu chochote mdomoni, alichohitaji wakati huo hakikuwa chakula, kinywaji au kitu chochote cha kupitia mdomoni! Alichohitaji ni mzee Mwinyimkuu, bila yeye aliamini maisha yake yasingekuwepo tena hivyo hapakuwa na haja ya kula chakula.
Hawakuongea kitu chochote zaidi, kilichofanyika ni kuwaandalia mahali pa kulala na wote wakaingia chumbani bila hata kuoga na kujitupa vitandani mwao.
Mariam akilala na mtoto wake na Nancy peke yake, hakupata hata lepe la usingizi hadi asubuhi, kazi yake ilikuwa ni kuhesabu mabati huku akiwafikiria wazazi wake na maisha yake mara milioni na zaidi, alitamani kuche haraka ili aulizie mahali alipohamia mzee Mwinyimkuu lakini masaa yalikwenda kwa mwendo wa kinyonga.
Mpaka asubuhi, Nancy alikuwa bado akilia na alikuwa mtu wa kwanza kunyanyuka kitandani na kuketi na nusu saa baadaye Mariam alifuatia baada ya mtoto wake kuanza kulia.
“Hujalala kabisa Nancy!”
“Hata kidogo! Mawazo yangu yote yako kwa huyu mzee, lazima nimpate kama si hapa mahali pengine popote lakini namwomba Mungu sana ili asaidie nimpate hapahapa kijijini, tofauti na hapo nitahangaika kwa sababu siko tayari kurudi nyumbani kabla ya kumwona!”
“Nimeshakuelewa ila acha baba na mama waamke tutawauliza, mimi bado naamini mzee Mwinyimkuu yuko hapa hapa kijijini hawezi kwenda popote!”
“Hivi ni Mnyamwezi yule?”
“Hapana si Mnyamwezi ni mtu wa Kigoma lakini wengine huwa wanasema ni mtu wa Zaire aliyekuja hapa nchini miaka mingi kutibu watu na dawa zake za asili, sina uhakika sana!”
****
Nancy alikuwa amechakaa na afya yake kuporomoka, mawazo aliyokuwa nayo yalitosha kumkondesha! Kama ungejaliwa kukutana naye usingeamini kuwa msichana huyo alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu, ngozi yake ilikuwa imepauka kwa sababu ya kutokuoga, alijichukia mwenyewe lakini hakujali! Haikuwa rahisi kugundua aliwahi kuwa ni msichana mzuri siku za nyuma.
Alikaa kitandani akiwa amejishika shavu, akisubiri wazazi wa Mariam waamke! Alikuwa na hamu kubwa ya wakati huo, jibu la wazazi wa Mariam ndilo lingemwezesha kuelewa kama angekaa Kisanga zaidi au angesonga mbele kumtafuta mzee Mwinyimkuu.
Muda mfupi baadaye akiwa katika mawazo hayo, mlango wa chumbani kwao uligongwa na sauti ya mama yake na Mariam ilisikika akiwasalimia.
“Mwangaluka Mariam!”
“Mwangaluka!”
“Mwalala mpola?”
“Mpola duhu!” Walisalimiana kwa Kinyamwezi Nancy akiwasikiliza, ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kuwasikia Wanyamwezi wakisalimiana kwa karibu, kabila yao ilimvutia hasa walivyovuta maneno na kupandisha sauti na kushusha, ulikuwa ni kama muziki na alitamani waendelee kuongea zaidi. Zamu yake kusalimiwa ilipofika kiswahili kilitumika, ilifanyika hivyohivyo hata kwa baba yake Mariam.
Dakika chache baadaye wote walitoka chumbani na kwenda kuungana na wazazi wa Mariam waliokuwa sebuleni, moyo wa Nancy ulikuwa ukienda kwa kasi kubwa! Alitamani sana kusikilia ambacho angeambiwa, aliamini kwa vyovyote wazee hao walikuwa wanaelewa kilichompata mzee Mwinyimkuu na wapo alikokuwa kwa wakati huo.
“Baba na mama!” Mariam aliita kwa heshima.
“Naam!” Wakaitika wote kwa pamoja.
“Huyu ni rafiki yangu anaitwa Nancy! Tulikutana naye Tabora lakini yeye amekuja hapa kijijini kumtafuta mzee Mwinyimkuu, nafikiri mnamfahamu yule mganga wa pale kwenye kona ya kwenda Sikonge!”
“Ndiyo tunamfahamu! Hebu njoo kwanza hapa tutete kidogo mwanangu!” Mama yake Mariam alinyanyuka na kumchukua Mariam hadi pembeni ambako alianza kuongea kwa sauti ya chini, hiyo pekee ilitosha kumshtua Nancy na kumfanya aelekeze masikio yake yote walipokuwa wamesimama!
“Kwani huyu binti ni nani yake? Maana yaliyompata mzee Mwinyimkuu ni ya kusikitisha sana!” Mama yake Mariam aliuliza akifikiri Nancy asingesikia bila kuelewa kuwa maneno yote yalikuwa yakiingia masikioni mwa Nancy na kati hali ya kushangaza alimwona Nancy akinyanyuka mahali alipokuwa amekaa na kuwafuata tena akilia machozi.
“NIAMBIENI TU! NINI KIMEMPATA? AU KAFA? TAFADHALI NIELEZENI NIJUE MOJA! HAKUNA HAJA YA KUONGELEA PEMBENI MIMI NI MTU MZIMA!” Aliongea Nancy kwa sauti ya huzuni.
Je nini kitaendelea?
Je ni kweli mzee Mwinyimkuu amefariki?

No comments