Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI -13


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
“Hapana! hajafa ila alipatwa na matatizo makubwa sana!”
“Tatizo gani?” Nancy aliuliza.
“Masuala ya mvua, ilikuja kugundulika kuwa eti alikuwa akiloga mvua sababu tangu ahamie hapa kijijini mvua imegoma kabisa, wananchi wenye hasira walimvamia nyumbani kwake wakaichoma nyumba yake na kumfukuza kabisa hapa kijijini! Nasikia yuko Kigoma anafanya shughuli zake za tiba kwenye soko la Ujiji!”
Kusikia alikuwa hai kulimfurahisha sana Nancy na asubuhi hiyo hiyo aliaga na kurudi hadi Tabora ambako jioni ya siku hiyo alipanda treni kwenda Kigoma, masaa arobaini na sita baadaye tayari aliwasili, kama ilivyokuwa kwa Tabora hakumfahamu mtu hivyo alichofanya ni kukodisha gari iliyompeleka hadi soko la Ujiji ambako alianza kuzunguka huku na kule akimtafuta mzee Mwinyimkuu, haikumchukua muda mrefu sana akawa ameelekezwa mahali alipofikia palipodaiwa kuwa ni kwa dada yake.
“Mimi ni dada yake, ndio nimemwachia ziwa! Ni kweli alikuwa hapa lakini biashara yake ikawa si nzuri akavuka ziwa Tanganyika kwenda sehemu iitwayo Kalemii huko Jamhuri wa watu wa Kongo, kwa hiyo kama una shida naye unaweza kumfuata huko!”
“Usafiri unapatikana?”
“Ndiyo! Iko Meli na pia majahazi, meli ni kila siku ya Jumapili na Jumatano, leo hii hakuna usafiri labda upande majahazi!”
“Nauli huwa shilingi ngapi?”
“Shilingi elfu kumi na tano!”
Hazikuwa pesa nyingi kwa Nancy, kwani kiasi cha pesa alichotoka nacho nyumbani kilimtosha kabisa! Ghafla alijikuta akitamani kuhesabu pesa yake na alitaka kuchukua kiasi ampe dada yake na mzee Mwinyimkuu shukrani kwa kueleza habari za ukweli. Alinyanyuka na kuingiza mkono wake kwenye mfuko wa suruali ya jeans aliyovaa, humo ndimo aliweka pesa zake
Katika hali isiyo ya kawaida alishangaa kuona vidole vyake vikitokeza nje, akainamisha macho kuangalia, suruali yake ilikuwa imechanwa na pesa zote zimeibiwa, alikaa chini na kuanza kulia machozi, kiasi cha kumshangaza dada yake mzee Mwinyimkuu aliyeitwa Mwanahawa!
“Pole sana! Nafikiri umeibiwa kwenye treni!”
“Sasa sijui nitafanyaje wakati ni lazima nifike huko Kongo, lazima nionane na mzee Mwinyimkuu! Nina tatizo kubwa sana!”
“Ni tatizo gani?”
Nancy alimsimulia mama huyo kila kitu naye akaonyesha masikitiko makubwa sana, hakuna kitu alichomshauri zaidi ya kuvuka ziwa kuingia Kongo na kumuasa asijaribu kukutana na mwanaume mwingine yeyote mpaka atakapompata mzee Mwinyimkuu na kumrekebisha.
“Ni kazi rahisi sana kama tu utakutana naye!”
“Sasa nitafikaje huko Kalemi?”
“Kwa kweli mimi sina msaada! Nipo kama unavyoniona!”
“Ahsante sana, nakwenda Bandarini kujaribu bahati yangu!” Alisema Nancy, akaaga na kuondoka zake hadi bandarini ambako alianza kutafuta usafiri, njaa ilimuuma kupita kiasi lakini hakuwa hata na pesa kidogo kununua chakula. Kumbukumbu za nyumbani zilizidi kutawala ubongo wake, alielewa ni kiasi gani walimtafuta hasa aliposikia matangazo katika redio, alimwonea huruma sana mama yake lakini hakuwa na la kufanya ilikuwa ni lazima amtafute mzee Mwinyimkuu mpaka ampate, hapo ndipo angeweza kutulia.
Akiwa bandarini alikutana na mzee waliyeishi mtaa mmoja, aliitwa mzee Daudi Kamizo! Alifurahi kupita kiasi na kuamua kuandika barua fupi kwenda kwa mama yake kumjulisha mahali alikokuwa na pia aliandika barua nyingine kwa Danny akimbembeleza asimtie baba yake hatiani.
“Naomba umfikishie mama yangu hii barua na mpe salamu nyingi, mwambie kuna kitu nakitafuta na siku nikikipata nitarudi nyumbani kwetu, mwambie nampenda mama na pia baba yangu!”
***
Wazazi wa Danny waliwasili wodini dakika tano tu baada ya mama Nancy kuondoka na kuwakuta maaskari wawili wakiwa wameketi pembeni mwa kitanda cha Danny, mafaili na kalamu zao zikiwa mkononi! Walielewa kilichokuwa kikifanyika, maelezo ya Danny juu ya nani alimpiga risasi yalikuwa yakichukuliwa.
Danny alikuwa amedhamiria kuusema ukweli akiamini Nancy alikuwa amefichwa na mama yake, muda wa wiki tatu aliokuwa ametoa ulikuwa umetosha kuvumilia hakutaka kuendelea zaidi! Kwa sababu walikuwa wameshindwa kumkabidhi Nancy mikononi mwake ili siku moja amuoe na kuwa mume wake naye alikuwa amedhamiria kumfungisha mzee katobe kwa kosa la kumpiga risasi.
“Taja jina lako kamili, la baba yako, kazi na umri wako!”
Aliwaeleza kila kitu walichokihitaji katika maelezo ya awali lakini walipofika katika maelezo kamili Danny alisita, uso wake ulionekana kuwa wa mtu mwenye mawazo mengi.
“Ilikuwaje siku ya tukio?”
“Subiri kwanza Afande!” Danny aliongea akiwa ameinamisha kichwa chake chini, mawazo yake yalikuwa yamrejesha tena kwa Nancy, alijua jambo alilotaka kufanya lingemuumiza na pengine kufanya uwezekano wa kuwa naye maishani uwe mgumu.
“wee mtoto, hebu waeleze polisi ukweli, hatuwezi kukaa hapa Tanzania kwa muda mrefu tuna kazi nyingi Uswisi, tafadhali eleza ukweli ili huyu mzee achukuliwe hatua!’
“Ukweli gani baba?”
“Kwani umesahau ulichotueleza alivyokufanyia?”
“Sikumbuki!”
“Namna mzee Katobe alivyokufanyia!”
“Bado sikumbuki!’
“Kuhusu risasi!”
“Risasi? Kivipi baba? Labda nilikuwa nimechanganyikiwa au akili yangu ilikuwa haijakaa sawa!”
“Enewei ongea unachokifahamu!”
Maaskari walisogea karibu zaidi na kitanda cha Danny alikuwa ameinamisha uso wake akionekana mwenye mawazo mengi zaidi! Alichotaka kukisema kingemgombanisha na wazazi wake alikuwa njia panda kumsaliti Nancy na kuungana na wazazi wake au kuwasaliti wazazi ili kumfurahisha msichana aliyempenda.
“Siwezi kuwasaliti wazazi wangu, lazima niseme ukweli, hapa nilipofika si pakupindisha tena!”Aliwaza Danny.
“Vipi tuanze?” Askari mmoja alimuuliza.
“hakuna tatizo!”Alijibu Danny akiwaangalia wazazi wake nyuso zao zilionyeshwa kuchukizwa na kilichokuwa kikitokea ndani ya chumba.
“Danny unataka kutuudhi wazazi wako?” Mama yake aliuliza.
“hapana mama!Nitasema ukweli!”
“Ukweli gani?”
“Juu ya mzee Katobe!”
***
Mama yake Nancy alizipokea barua zote mbili na kuanza kuziangalia mwandiko juu ya bahasha ulionyesha moja kwa moja mahali barua hizo zilikotoka bila hata kuuliza swali! Zilikuwa barua za Nancy, furaha iliyomja mama huyo moyoni mwake haikuwa na maelezo aliruka juu mara mbili akishangilia.
“Baba yako amezitoa wapi?” Alimuuliza mtoto wa mzee Daudi Kamizo.
“Alikuwa Kigoma!”
“Ina maana mwanangu yuko Kigoma?”
“Sijui labda umuulize baba!”
Hakukumbuka kuongea kitu chochote zaidi na mtoto huyo, alichofanya ni kuifungua barua yake kisha kuanza kuisoma ni kweli ilikuwa barua ya mwanae Nancy! Hakuyaamuru machozi yatoke bali yalitiririka yenyewe kama chemchem.
Mpendwa mama,
Nakuandikia barua hii nikiwa katika masikitiko makubwa sana, najua sikukuaga na hilo lazima lilikuudhi sana, naomba unisamehe.
Mama, nipo Kigoma, najua hili pia litakushangaza sana imekuwaje nimekuja huku! Nipo katika matatizo makubwa mno, lakini nayaita matatizo haya ya kujitakia mwenyewe! Sikuambii ni tatizo gani mpaka siku nitakapompata ninayemtafuta! Nafanya hivi kwa sababu ya baba ili nije nimtoke katika hatari kama anachotaka Danny ni kunioa!
Pesa zote nilizochukua kabatini nimeibiwa lakini nipo safarini kuelekea Zaire, kumfuata huyo mtu ninayemtafuta! Nakupenda mama na pia baba yangu, nasikitika yupo mahabusu mwambie asinichukie kwani yote ninayofanya ni kwa ajili yake.
Tutaonana kama kuna uhai, likitokea lolote basi tutaonana mbinguni! Niombee sana.
Ni mimi mwanao ninayeteseka
Nancy.
Wakati anamaliza kuisoma barua hiyo sehemu ya mbele ya kifua chake ilikuwa imelowa, alishindwa kuelewa ni kitu gani kilichomfanya Nancy atoroke kwenda Kigoma! Alizungusha akili yake huku na kule lakini hakufanikiwa kilichomfurahisha pamoja na masikitiko yote aliyoyapata na kufahamu kuwa mwanae alikuwa bado akipumua.
Aliigeuza bahasha nyingine aliyokuwa nayo,juu yake iliandikwa jina la Danny na neno jingine “Haraka sana” lilikuwa pembeni mwa jina, hakutaka kupoteza wakati na hapohapo alitoka hadi nje na kuingia danani ya gari, safari ya kurejea hospitali ikaanza, dakika tano tu alikuwa akigesha gari lake mbele ya hospitali ya wilaya ya Bagamoyo na kutoka bila hata kufunga mlango akitembea hadi kwenye wodi aliyolazwa Danny.
Alifungua mlango bila hata kubisha hodi na kuwakuta wazazi wa Danny pamoja na wanaume wawili aliowaacha, kila mtu alishtuka lakini mama Nancy hakutaka kuogea lolote, alikwenda moja kwa moja hadi kitandani na kumkabidhi Danny bahasha kisha akaondoka kimya kimya. Mara moja Danny aliifungua barua hiyo na kutoa karatasi iliyokuwa ndani mwake na akawa kimya akiisoma barua hiyo lakini muda mfupi baadaye wote walishtuka kumwona anatokwa na machozi.
Danny,
Nipo katika matatizo, najua unanipenda lakini kuna kitu kinachonizuia kushirikiana na wewe kimwili! Siwezi kukueleza kwa sasa, mara nitakaposhughulikia jambo hilo nitakuwa tayari kwa lolote! Wewe ni mvulana mzuri pengine kuliko hata Tonny lakini nashindwa kufikia uamuzi wa kukuvulia nguo yangu ya ndani, najua nitapata matatizo makubwa sana na pengine utanihurumia.
Tafadhali nakusihi sana univumilie baada ya muda si mrefu nitarudi tena Bagamoyo, kwa hivi sasa nipo Kigoma natafuta suluhisho la tatizo langu.
Nipo chini ya miguu yako, nakulilia usimwingize baba yangu katika matatizo na kumfanya afungwe, hilo litaniumiza sana na linaweza kufanya mimi na wewe tusiwe unavyotaka!
NI mimi nikupenyaye lakini mwenye kizuizi.
Nancy.
Je nini kitaendelea?

No comments