Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 14


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
“Kizuzi? Kizuizi gani?” Aliuliza Danny kwa sauti ya juu akijifuta machozi, kila mtu ndani ya chumba alishindwa kuelewa barua hiyo ilitoka wapi, mama yake alianza kukisogelea kitanda kwa lengo la kuichukua barua hiyo ili aisome lakini kabla hajafika Danny aliikunja na kuitupa mdomoni mwake na kuanza kuitafuna.
“Barua ya nani?”
“Siwezi kusema mama! Ila kwa sasa niko tayari kuongea na polisi!”
“Ongea nao basi!”
“Siku ya tukio nilikuwa nikitembea ufukweni mwa bahari ya Hindi eneo la Bagamoyo, nilikuwa na kamera yangu mkononi! Mara baada ya kupita Badeco Beach nikielekea Chuo cha Sanaa bagamoyo watu watatu walinifuata kwa nyuma wakiwa na Bastola mkononi na kuanza kuninyang’anya kamera yangu, sikukubali nikaanza kupambana nao, unaandika lakini?” Danny alimuuliza askari.
“Ndiyo!”
“Katika kupambana nao mmoja wao akanipiga risasi nikaanguka chi....!”
“Funga mdomo wako! Kwanini unafanya ujinga kwa faida ya nani sisi tunaondoka na tangu leo wewe ni mtoto we....!” aliongea baba yake Danny, yeye na mke wake walitoka nje na kufunga mlango nyuma yake.
Moyo wa Danny uliumia kupita kiasi, alikuwa katika wakati mgumu! Asingeweza kumsaliti Nancy, alimpenda kupita kiasi na aliamini huyo ndiye angekuwa mke wake, wawe na familia na kuzaa watoto pamoja!
Alikuwa ni yeye wa kuchagua kati ya wazazi wake na Nancy na alikuwa amemchagua Nancy na kuwaudhi wazazi wake, alikuwa tayari kwa lolote ili mradi awe na Nancy! Aliyokuwa nayo hayakuwa mapenzi ya uongo bali ya ukweli tupu!
Alipotoka hospitali mama yake Nancy alikwenda moja kwa moja mahabusu ambako aliomba kuonana na mume wake angalau kwa dakika tano, kwa jinsi alivyokuwa anafahamika mjini Bagamoyo aliruhusiwa kuingia na mzee Katobe akawa ameitwa, hali aliyokuwa nayo mke wake ilimtisha.
“Vipi? Mbona unalia!”
“Nancy!”
“Amekuwaje? Amekufa?”
“Hapana, yupo Kigoma!”
“Kigoma? Anafanya nini?”
“Anamtafuta mtu ambaye hakumtaja ni nani na anatarajia kuvuka kwenda Zaire, nimekuja kukuaga kesho ni lazima nimfuate!”
“Umejuaje kama yuko Kigoma?”
“Unamfahamu jirani yetu mzee Daudi Kamizo?”
“Yule Mkandarasi?”
“Ndiyo! Ameniletea barua hii kutoka Kigoma, alikutana na Nancy jana kabda hajaondoka, nikitoka hapa nitapita nyumbani kwake anieleze vizuri mahali alipomwona maana anadai hata pesa alizokuwa nazo zote zimeibiwa!”Aliongea mama Nancy akimkabidhi mume wake barua naye akaisoma, masikitiko yaliyoonekana machoni mwake yalikuwa makubwa mno.
Dakika kumi na tano baadaye mzee katobe alitakiwa kurudi mahabusu na mama Nancy akaondoka moja kwa moja hadi ofisini kwa mzee Kamizo, huko alielezwa kila kitu juu ya mahali mtoto wake alipoonekana.
“Nilimwona palepale bandarini, hali yake haikuwa nzuri ni mimi niliyempa hata pesa ya kula lakini nilipotaka arudi nyumbani alikataa na nilipomuuliza kulikuwa na tatizo gani hakutaka kuniambia!”
“Nitaondoka kesho kwenda Kigoma, ni matumaini yangu nitampata!”
“Kama atakuwa hajaondoka utampata!”
“Ahsante sana! Nashukuru kwa msaada wako na wewe unahitaji zawadi maana tulitangaza!”
“Ah! Jirani achana nayo uhusiano wetu ni bora zaidi!
“Kwa heri!”
Kutoka hapo alipitia benki ya Taifa ya Biashara mjini Bagamoyo na kuchukua kwenye akaunti ya familia ya kiasi cha shilingi milioni tano kwa ajili ya kumtafuta mtoto wake, muda wote akiendesha gari na hata akiwa benki alikuwa akilia, watu wengi walifikiri labda alikuwa amefiwa.
Siku hiyo alilala jijini Dar es Salaam asubuhi iliyofauta alipanda ndege ya shirika la ndege la Precions moja kwa moja hadi Kigoma, kitu cha kwanza alichofanya aliposhuka uwanja wa ndege ni kukodisha teksi iliyompeleka moja kwa moja hadi bandarini umbali wa kilometa zaidi ya thelathini kutoka uwanja wa ndege.
Akiwa bandarini alianza kutembea na picha ya Nancy mkononi akimuuliza karibu kila mtu aliyekutana naye kama alikuwa amemwona mahali popote msichana huyo, wengi wao alipowauliza walioenakan kutomfahamu Nancy hata chini kwenye majahazi na vyombo mbalimbali vya usafiri.
“ha! Huyo? Mbona alikuwepo hapa? Hebu subiri kidogo!” Aliongea kijana wa kwanza tu aliyemuuliza na kuondoka mbio akiwa na picha mkononi kwenda kwenye kundi la vijana wengine waliokuwa pembeni wakitengeneza nyavu zao, mama Nancy hakutaka kusimama sehemu moja alimfuata kijana huyo hadi alipokuwa.
“Eh! Ndiyo alikuwa anaulizia usafiri wa kwenda Kongo, tukamwelekeza jahazi lililoondoka nusu saa iliyopita!” kijana mmoja alsiema, mwili wa mama Nancy uliishiwa nguvu na kujikuta akikaa kwenye mchanga! Alishindewa kuelewa ni kwa namna gani angempata mtoto wake.
“Alisema anakwenda sehemu gani huko kongo?”
“Hakusema!”
“Kuna namna yoyote naweza kusafiri?”
“Sasa hivi?”
“Labda boti ya kokudi zile za injini ziendazo kwa kasi!”
“Naweza kupata wapi?’
“Kwa waarabu!”
“Nani anaweza kunipeleka?
“Twende!Lakini utaweza bei?”
“Wewe twende kwanza mwanangu!”
Waliondoka hadi kwenye ofisi iliyokuwa juu ya mlango wake imeandikwa Tanganyika Marines, hapo mama Nancy alikodisha boti ya kwenda kwa kasi kwa shilingi laki mbili, akapewa dereva na kwa pamoja wakaanza kuyakata maji ya ziwa Tanganyika akimfuata mtoto wake, hali ilikuwa mbaya kweli ziwani! Hata dereva aliyekuwa naye alishangaa, boti yao ilirushwa huku na kule na mawimbi mpaka dereva akawa na wasiwasi.
Hali katika ziwa Tanganyika ilikuwa chafu kupita kiasi, mawimbi yalikuwa mengi na makubwa yalioupiga mtumbwi kutoka upande mmoja hadi mwingine na kuzidisha wasiwasi kwa mama Nancy na Nahodha wa mtumbwi, usalama ulikuwa mdogo. Wingu lilikuwa kubwa angani na ingawa ilikuwa mchana hali ya giza ilianza kuonekana! Miungurumo ya radi ilisikika angani na muda mfupi baadaye mvua kubwa tena ya mawe ilianza kunyesha na kuwaloanisha wote.
Pamoja na hali hiyo bado mtumbwi ulizidi kuyakata mawimbi na kusonga mbele, mara mbili au tatu ukitaka kubinuka na kuwamwaga ndani ya maji, moyo wa mama Nancy ulikuwa ukienda mbio, alikosa uhakika wa kufika upande wa pili wa ziwa kama wasingefanikiwa kulipata jahazi katikati ya maji.
“Tutafika?” Mama Nancy alimuuliza Nahodha.
“Hata mimi hali inanishtua, nashindwa kukuahidi chochote! Turudi?” Aliuliza.
“Haiwezekani, siwezi kurudi bila kumpata mwanangu”
“Sasa?”
“Twende tu kama ni kuzama basi tuzame na nife maji!”
“Unajua kuogelea?”
“Hapana mimi ni kama shilingi ikidumbukizwa ndani ya maji, utanikuta hapo hapo nilipozamia!”
“Kama ni hivyo nashauri turudi!”
“Sitaki, safari lazima iendelee!”
Nahodha wa mtumbwi alitii amri ya mteja wake na safari ikaendelea, mtumbwi haukwenda kwa kasi kubwa tena, mawimbi na mvua kubwa ya upepo yaliuzuia kusonga katika mwendo wa kawaida. Kila walipokutana na wimbi kubwa mtumbwi ulitaka kuwamwaga majini, mama Nancy aliushika kwa nguvu zake zote hilo ndilo jambo lililomsaidia.
Hakuwa na matumaini ya kunusurika kwa jinsi hali ilivyokuwa lakini bado hakukata tamaa, alitaka kusonga mbele! Safari iliendelea karibu masaa wawili lakini hawakufanikiwa kuliona jahazi mbele yao na bado hali ya ziwa ilikuwa mbaya, mama Nancy alishatapika mara nyingi, jambo lililosababisha mwili wake kuishiwa nguvu na kulegea.
“Hivi kuna uwezekano jahazi likaiacha boti yenye injini au tumekosea njia!” mama Nancy alimuuliza Nahodha wa boti.
“Majahazi huwa yanakwenda kwa kasi sana, hasa kunapokuwa na upepo kama huu! Sababu yanatumia kitambaa, sisi tunazuiliwa na mawimbi makubwa yaliopo!” “Tutawapata kweli?”
“Hali ikitulia tutawapata!”
“Ninaanza kukata tamaa!”
“Usikate tamaa, tulikotoka ni mbali vumilia, hata kama itabidi tufike upande wa pili, huko utamwona tu binti yako!” Nahodha wa mtumbwi alimfariji mama Nancy.
Je nini kitaendelea?
Tukutane Jumatano mahali hapa.
Unaruhusiwa kushare hadithi hii ili watu wengi waweze kuiona zaidi na kujifunza.

No comments