Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 15


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Safari iliendelea kwa masaa mawili zaidi hali ikiwa bado mbaya, walikuwa katikati ya ziwa bila kuona kitu upande wowote, iwe Magharibi, Mashariki, Kaskazini ama Kusini! Hakikuonekana hata kisiwa kimoja cha kuleta matumaini ya kuokoa maisha yao, bado hofu ya kuzama ilitanda na muda wote mama Nancy alimwomba Mungu anusuru maisha yake.
Fikra juu ya mume wake aliyemwacha mahabusu mjini Bagamoyo bado zilimwijia kichwani mwake na kumzidishia huzuni, mambo yaliyokuwa yakimtokea hakuwahi kuwaza hata siku moja kuwa yangemtokea maishani! Raha na starehe zote alizowahi kuwa nazo maishani akiwa mke wa mfanyabiashara tajiri hazikuwepo tena, alikuwa akiteseka majini kumfuata mtoto wake mpendwa Nancy, hakujuta mahali popote moyoni mwake ili mradi yote aliyokuwa akiyafanya ni kwa ajili ya mwanaye.
“Mama! Jahazi lile pale!” Nahodha wa boti alisema akisonta mkono wake mbele yao.
“Wapi?”
“Angalia huku mbele yetu!”
“Silioni!”
“Nafikiri kwa sababu ya mawimbi ! Angalia vizuri, kaza macho yako utaliona tu !”
Kichwa cha mama Nancy kilielekezwa mbele, macho yake yote yakiwa yamelenga walikokuwa wakielekea, alitaka kuliona jahazi aliliokuwa akielezwa na dereva juu yake, kwa dakika kama mbili hakufanikiwa lakini baadaye alipotulia aliliona likiwa dogo kabisa kama mita elfu moja na mia tano mbele yao, alishangilia na kuhisi ushindi mkubwa moyoni mwake.
“Hatimaye........mwisho nimempata mtoto wangu!” alisema kwa sauti ya juu. “Tutalipata baada ya dakika ishirini !”
“Ongeza kasi”
“Hapana mama hali ni mbaya sana, siwezi kwenda zaidi ya hapa!”
“Sawa, basi fanya uwezalo !”
Boti ilizidi kwenda kwa mwendo wa taratibu, badala ya dakika ishirini alizosema dereva iliwachukua saa nzima kulifikia, mawimbi yalikuwa bado makali, hali ya hewa ilitishia maisha na mvua kubwa ilikuwa bado ikinyesha na kujaza maji kwenye mtumbwi hivyo kufanya kazi ya mama Nancy kuwa ni kuchota maji kutoka kwenye mtumbwi na kuyamwaga nje.
“Ndiyo lenyewe?” Mama Nancy aliuliza.
“Nafikiri! Kwani katika hao watu waliosimama na kutuangalia mtoto wako hayupo?” “Simuoni !”
“Acha nisogee karibu zaidi uwaulize abiria waliochungulia madirishani !”
Nahodha alisema na kuzidi kulisogelea jahazi. Nalo lilikuwa likiyumbishwa na mawimbi kutoka sehemu moja hadi nyingine, mizigo ya magunia ilionekana kutupwa majini na kuonyesha kuwa hali ilikuwa chafu hata kwa wenye jahazi kiasi cha kuanza kupunguza mizigo waliobeba kwa kuitupa majini ili kuokoa maisha yao, hali ya ziwa ilitishia uhai.
“Kuna msichana anayeitwa Nancy humo ndani?”
“Mimi sielewi !” Alijibu kijana mmoja aliyechungulia dirishani akivuta hewa. “Naomba uniulizie basi kama yupo”
“Subiri !”
Kijana huyo aliondoka na aliporejea dakika mbili baadaye wakati jahazi na boti vikisafiri sambamba, vichwa viwili vilichungulia dirishan! Alirudi na Nancy, aliyeonekana kuchakaa kupita kiasi! Macho ya Nancy na mama yake yaligongana, Nancy akalia machozi, hakuamini kama alichokuwa akikiona kilikuwa kweli, alihisi ni ndoto ambayo muda mfupi baadaye angezinduka.
“Mama!”
“Bee mwanangu!”
“Umefikaje huku!”
“Nakupenda mwanangu Nancy ndiyo maana nimeteseka kiasi hiki kukufuata, nakutaka turudi nyumbani!”
“Nyumbani? Hapana mama! Nakupenda sana mzazi wangu lakini siwezi kurudi!” “Unakwenda wapi?”
“Zaire!”
“Kufanya kitu gani?”
“Kuna mtu namfuata, bila huyo kupatikana maisha yangu hayana maana! Sitaweza kumsaidia baba, kwani anachotaka Danny ni kunioa mimi lakini sina uwezo wa kufanya hivyo, Tonny aliniharibu mwili wangu na mtu aliyetumiwa na Tonny kuniharibu yupo Zaire ndiyo maana ninamfuata! Tafadhali mama nakusihi, niache niende!”
“Haiwezekani, siwezi kukuacha uende peke yako, nitafuatana na wewe hadi mwisho, wewe ni mwanangu! Nataka kuelewa kinachokusumbua!
“Twende mama!”
“Nahodha hebu sogeza boti karibu zaidi na jahazi, nimefika mwisho wangu wa safari! Nakushukuru sana, wewe unaweza kurudi baada ya mimi kupanda jahazi hili!” Aliongea mama Nancy na Nahodha hakuwa na ubishi wowote, alisogeza boti yake karibu na jahazi !
Kwa kupita dirishani Nancy na kijana aliyemuita walinyoosha mikono yao na kuishika mikono ya mama yake, wakaanza kumvuta na kufanikiwa kumuingiza jahazini! Nancy alianguka na kumkumbatia mama yake, wote wakaanza kulia na kuendelea kwa karibu nusu saa nzima.
Walipotulia mama Nancy alitaka kujua kilichompata mtoto wake mpaka kuamua kutoroka kwenda Zaire, Nancy hakuweza kuficha ukweli tena, alieleza kila kitu wazi huku akilia, mama yake alishangazwa na habari aliyoisikia na kumtupia lawama zote Tonny, alimchukia kupita kiasi kijana huyo.
“Kwa nini ulifanya kitendo hicho, kwa nini ulikula Yamini wakati unafahamu ni kitu hatari? Nani alikudanganya? Ulishakutana na mwanaume kimwili tangu ule kiapo kwa mganga wa kienyeji?”
“Hapana mama, ndiyo maana nilishindwa kufanya hivyo na Danny ili nimsaidie baba yangu, hii ndiyo sababu ninasafiri kwenda Zaire kumfuata mganga ili aniondolee kiapo cha Yamini nilichokula ! Ni mapenzi tu, ni utoto tu !”
“Una uhakika huyo mganga yupo Zaire?”
“Ndiyo! Nimemtafuta sana, nimepita Tabora, Kigoma na sasa nakwenda Zaire!”
“Kwa nini ulikwenda Tabora!”
“Niliambiwa yuko huko lakini nilipofika nikaelezwa alihamia Kigoma, hapo napo nikaambiwa amekwenda Zaire ndiyo maana ninasafiri! Ulijuaje niko huku?”
“Barua zako ulizozituma!”
“Zilifika?”
“Ndiyo!”
Wakati wakiendelea kuongea jahazi lilizidi kusonga mbele taratibu huku likipigwa na mawimbi mazito, hali ilikuwa bado mbaya kupita kiasi, boti iliyomleta mama yake Nancy iliishageuza kurudi Kigoma, ghafla upepo mkali kuliko uliokuwepo ulianza kuvuma kama kimbunga ukitokea upande wa Mashariki kuelekea Magharibi, watu wote waliokuwepo ndani ya jahazi waliingiwa na wasiwasi maana upepo huo uliyazungusha maji kama pia.
“Jamani hali ni mbaya! Kila mtu sasa amuombe Mungu wake” Alisikika nahodha wa jahazi hilo akisema.
Watu walianza kutupwa huku na kule ndani ya jahazi Nancy, na mama yake walilala chini kwa hofu wakikumbatiana wakimwomba Mungu abadilishe nia ya shetani iliyotaka kutokea. Dakika tano baadaye walijikuta wamo majini, wakihangaika na kunywa maji mengi, tayari walikuwa wamezama majini na jahazi lilionekana pembeni likiwa limebinuka chini juu, watu wengi walionekana wakitapatapa majini.
Mama Nancy aliuona mkungu wa ndizi ukiwa karibu yao, alichofanya ni kuukamata ili umuokoe yeye na mtoto wake kwa sababu alikuwa na uhakika hawakuwa na uwezo wa kuogelea hata dakika tano mbele yao, kwa nguvu ambazo hakuelewa zilitoka wapi alimvuta Nancy karibu yake na wote wawili wakaushika mkungu huo na kuanza kuelea majini taratibu.
Waliwashuhudia watu waliokuwa na uwezo wa kuogelea, wengi walikuwa wafanyakazi wa kwenye jahazi wakiogelea na kukata maji wakiwaacha wao peke yao, nusu saa baadaye watu wachache waliokuwa abiria wa jahazi walionekana wakielea juu ya maji wakiwa wamekufa!
Matumaini ya mama Nancy na mwanae kuokoka yakazidi kupungua, kwa uwezo wa macho yao hawakuona nchi kavu upande wo wote wa ziwa. Tayari ilikuwa saa tisa na nusu alasiri. Waliendelea kushikilia mkungu wa ndizi ukipelekwa na maji zaidi na zaidi kwenda kusikojulikana, masaa yalizidi kukatika, mawimbi makubwa zaidi yalizidi kuongezeka! mvua kubwa iliendelea kunyesha na baridi kubwa kuendelea kuifisha ganzi miili yao.
Mpaka asubuhi siku iliyofuata walikuwa bado hawajaona mtumbwi wala meli yoyote ikipita karibu yao na walizidi kusukumwa na mkondo wa maji kwenda mbele zaidi, mara kwa mara waliongea maneno machache ya kupeana moyo na kumwomba Mungu katika sala zao pamoja ili awanusuru na kifo, lakini maombi yao yalionekana kutojibiwa!
“Mama tutakufa!”
“Hapana mwanangu, usikate tamaa Mungu atatunusuru!”
“Mikono yangu imekufa ganzi na nimeanza kuchoka!”
“Jikaze mwanangu!”
“Sidhani kama nitaendelea zaidi, ila nikishindwa na wewe ukanusurika, basi utamsalimia baba na kuniombea msamaha kwani niliondoka bila kumwaga lakini yote ninayofanya ni kwa faida yake mwenyewe !”
“Usiseme hivyo mwanangu, hata mimi nimechoka na mikono yangu imeishiwa nguvu lakini bado najipa matumaini! Jipe moyo si ajabu tunaweza kukutana na msaada mahali popote mbele ya safari!”
Haikuwa kama mama yake Nancy alivyofikiria hawakupata msaada wowote na njaa ilizidi kuwasumbua nguvu zilizidi kuwaishia na ilipofika siku ya nne wakiwa majini wameshikilia mkungu, mama yake Nancy hakuwa hata na uwezo wa kuongea jambo lolote, alikuwa kimya muda wote kichwa chake kimeinamishwa kukaribia kabisa kuyagusa maji! Hiyo ilionyesha ni kiasi mama huyo alikuwa amechoka.
“Mama! Mama! Mama!” Nancy aliita aliposhuhudia mama yake akiuachia mkungu wa ndizi na kuzama majini.
Je nini kitaendelea?
Je huo ndiyo mwisho wa mama Nancy?
Tukutane Ijumaa mahali hapa.

No comments