Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 8


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Nancy alimaliza kuisoma kadi hiyo akilia machozi, mashavu yake yalilowa na blauzi aliyovaa pia ilikuwa chepechepe! Yalikuwa maneno makali na ya kuchoma, yaliyoingia moja kwa moja moyoni mwake na kuupiga ganzi, upande mmoja ulimwambia akubali lakini upande mwingine ukamwambia NO! Wanaume kwake walikuwa ni wanaume tu, rangi nyekundu ilikuwa nyekundu tu, hakuna mtu angeweza kumbadili kutoka kwenye msimamo wake.
Aliyanyanyua maua aliyokuwa nayo mkononi pamoja na kadi na kumtupia Danny kifuani kwake na kunyanyuka mahali alipokuwa amepiga magoti akisoma kadi, alimwangalia kwa macho makali! Kumbukumbu za siku yeye na mtoto wa masikini aliyebadilika baada ya kupata umaarufu, Tony walipokuwa wakisafiri kwenda Bagamoyo kwa mganga wa kienyeji ambako alikuwa Yamini mbaya kwamba katika maisha yake asingetembea na mwanaume mwingine isipokuwa Tony! Akamwaga machozi.
“Ninajua utaniacha! Utachukuliwa na wanaume wengine, twende Bagamoyo ukale Yamini kama kweli utanisubiri mpaka nirudi kutoka China!” Yalikuwa ni maneno ya Tony kwa Nancy, yalimiminika kichwani mwake kama filamu! Roho ikazidi kumuuama, hakuna neno kutoka mdomoni kutoka mdomoni kwa mwanaume lingeweza kumbadilisha na kumfanya apende tena.
“Toka! Toka! Toka nyumbani kwetu, sitaki kuona mwanaume, ondoka na maua yako!” Nancy aliongea kwa sauti huku akilia.
Danny aliruka kutoka mahali alipokuwa amekaa na kumfikia Nancy, akamkumbatia kwa nguvu na wote wawili wakaanguka hadi chini.
“Wewee kijana hebu mwachie binti yangu! Unataka kumbaka?” Mama yake Nancy aliongea akijaribu kumvuta Danny.
Tayari mzee Katobe alishakimbia kwenda chumbani kwake na alipotoka alikuwa na gobole lake lenye midomo miwili.
“Mwachie!Mwachie nakuambia, nitakuua” Alifoka mzee Katobe.
Kilichofuata hapo ni mlipuko wa bunduki, chumba kizima kikajaa mwangwi wenye uwezo wa kupasua ngoma ya sikio, mikono ya mama yake Nancy ilikuwa kichwani mwake.
“Baba Nancy umeua!”
Damu ilikuwa imetapakaa chumba kizima, naye Danny alikuwa sakafuni akilia kwa maumivu! Risasi ilikuwa imempenya kwenye mguu wake wa kulia chini kidogo ya goti! Mzee Katobe alikuwa akitetemeka kwa hasira, Nancy pia alikuwepo mikono yake ikiwa kichwani na machozi yakimtoka kwa wingi, pamoja na kutompenda Danny alimwonea huruma na kumlaumu baba yake kwa kitendo alichokifanya.
“Ni hasira!”
“Hasira yako mbaya sana! Sasa si umeishia Jela mume wangu!” Aliongea mama yake Nancy akimsogelea Danny, alipomfikia alipiga magoti pembeni yake na kuanza kumfunga na khanga sehemu iliyokuwa ikivuja damu.
“Mama nipelekeni hospitali nikatibiwe!” Danny alilalamika.
“Danny vipi?”
“Baba yako amenipiga risasi, hata wewe umeshuhudia! Yote hii ni kwa sababu yako Nancy, nakupenda! Na sitakuchukia hata siku moja!”
Ingawa siku zote mzee Katobe alimchunga sana binti yake asiwe na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume aligundua umuhimu wa kumtumia Nancy kuyeyusha tatizo lililokuwa limejitokeza, vinginevyo angefia jela, mara moja alikimbia chumbani kwake na akiwa huko alimwita Nancy kwa sauti ya juu naye alimfuata wakimwacha mama peke yake akiendelea kumfunga Danny na khanga ili kuzuia damu zaidi isivuje.
“Sikiliza mwanangu!” Mzee Katobe alimwambia Nancy.
“Ndiyo baba!”
“Hali ni mbaya na ni wewe peke yake unayeweza kusaidia!”
“Ndiyo! Kusaidiaje?”
“Huyu kijana anakupenda, pamoja na hasira zangu kumpiga risasi ukimwomba asitoboe siri ya kilichotokea ninafikiri anaweza kukusikiliza!”
“Mh! Hilo litawezekana kweli?”
“Linawezekana kabisa! Naomba ukalifanye sasa hivi!”
Nancy alitoka chumbani bila kuongea chochote na kwenda moja kwa moja hadi mahali alipokuwa mama yake, hali ya Danny ilikuwa mbaya alionyesha kupoteza fahamu! Alimtingisha mara kadhaa akijaribu kumwita lakini hakuitika, muda mfupi baadaye baba yake alifuatia na kukuta akihangaika kumtingisha.
“Jamani twendeni tumpeleke hospitali!”
“Mimi naogopa!” Mzee Katobe aliongea, mwili wote ulikuwa ukitetemeka na alionyesha wazi ni kiasi gani alijilaumu kwa kitendo alichokifanya.
“Basi acha sisi tumpeleke, wewe baki hapa nyumbani maana naona anazidi kuzidiwa!”
Mzee Katobe alitingisha kichwa kuonyesha hali ya kukubali, hata hivyo aliwasaidia kumbeba hadi kwenye gari lao, wakampakia na kuondoka naye kuelekea hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, njiani kabla hawajafika hospitali Danny alifumbua macho na kumkuta Nancy amekaa pembeni mwake mama yake akiendesha gari kwa kasi.
“Pole Danny! Naomba umsamehe baba yangu!”
“Kwa sababu yako naweza kufanya lolote, nakupenda Nancy! Wala sitanii!” Aliongea Danny ingawa kwa taabu.
Gari liliegeshwa mbele ya jengo la mapokezi dakika kumi baadaye na wauguzi wakasogea wakiwa na kiti cha matairi, Danny aliteremshwa haraka na kukimbiwa chumba cha daktari, wakati anaingia aliweka kidole chake mdomoni kama ishara ya kuwazuia Nancy na mama yake wasiongee lolote, kwa wakati huo hawakuelewa ni kwanini aliwapa ishara hiyo lakini alipoanza kuongea na daktari walielewa maana yake.
“Nilikuwa natembea huko ufukweni Badeco, wakaja wanaume wawili wakiwa na bastola wakaanza kuninyang’anya kamera yangu pamoja na pesa nilizokuwa nazo! Nilipojaribu kupambana nao ilishindikana wakanipiga risasi mguuni!” Danny aliongea kwa sauti ya chini huku akilia, Nancy na mama yake walibaki mdomo wazi hawakutegemea hayo ndiyo yangekuwa maelezo yake.
“Aisee pole sana! Unahitaji matibabu ya haraka, kwa kawaida kesi kama hii inabidi upate kwanza fomu ya polisi lakini siwezi kusubiri fomu hiyo ndiyo nianze kukutibu, matibabu yatafanyika na fomu itafuata baadaye!”Aliongea daktari huku akichukua kadi na kuanza kuandika maelezo juu yake.
“Nina uhakika mfupa umevunjika, kuna milio fulani naisikia ambayo kwa kweli si ya kawaida! Hivyo naomba mmpelekeni chumba cha X-ray akapigwe picha mara moja na majibu niyapate upesi!” Daktari aliwaeleze wauguzi waliokuwepo chumbani na Danny akasukumwa akiwa juu ya kiti cha matairi hadi chumba cha X-ray ambako mguu wa Danny ulipigwa picha, kutoka hapo alipelekwa moja kwa moja wodini na kusubiri majibu yaliyotoka nusu saa baadaye na kuonyesha kweli mfupa wa Danny ulikuwa umevunjika.
Madaktari walikusanyika na kuijadili hali hiyo, ushauri uliotolewa na daktari bingwa wa mifupa ni Danny kufungwa vyuma kwenye mguu wake uliovunjika ili uungwe kwa urahisi maana kulikuwa vipande kadhaa vilivyosambazwa na risasi iliyopita na kuchimba sakafuni.
Alichukuliwa kutoka wodini kupelekwa chumba cha upasuaji, Nancy na mama yake wakifuata nyuma! Kabla ya kuingia chumba cha upasuaji, Nancy alipinda shingo yake na kumpiga Danny busu usoni akimshukuru kwa kitendo chake cha kumtetea baba yake alichokifanya.
“Sijui jinsi ya kukushukuru!”
“Kitu kimoja tu unaweza kufanya kama shukurani! Ni kukubali kuwa mpenzi wangu, nakupenda Nancy, sijali kuwa baba yako kanipiga risasi ili mradi imetokea wakati nakutafuta wewe! Lakini tofauti na hapo...”
“Tutaliongelea hilo baadaye nenda kwanza katibiwe!”
Danny aliingizwa chumba cha upasuaji ambako alikaa kwa karibu masaa mawili, alipotoka alikuwa katika dawa ya usingizi wala hakuweza kuongea lolote, ilikuwa tayari saa kumi na mbili za jioni ni wakati huo ndipo Nancy na mama yake waliamua kurejea nyumbani kwa muda.
****
Walimkuta mzee Katobe akiwa sebuleni amejishika tama kwa mawazo mengi, kichwa chake kilikuwa kimechanganyikiwa, aliiona milango ya jela zote Tanzania ikiwa wazi na ikimwita ili aingie! Walipomweleza kilichotokea hospitali, kwamba Danny alisema uongo ili kumtetea hakutaka kuamini! Aliruka juu na kushangilia kwa furaha.
“Huyu kijana ni wa aina yake, siwezi kumlinganisha na yule Mbweha aliyeko China! Yaani hakusema kuwa nimempiga risasi?”
“Hajasema!”
“Nafikiri hakutakuwa na matatizo labda hili gari lake ndio linaweza kuleta usumbufu!”
“Usumbufu gani?”
“Si ajabu polisi wanaweza kuuliza limefikaje hapa!”
“Si tutasema tuliliendesha kutoka ufukweni, hapo kuna tatizo gani?” mama yake Nancy alisema.
“Bila shaka hakuna shida!”
Saa moja na nusu ya jioni wote watatu walirejea hospitali na kumkuta Danny akiwa amejilaza kitandani, bado fahamu zake zilikuwa hazijarejea vizuri! Alikuwa akiongea maneno mengi bila kujitambua, dawa za usingizi alizopewa chumba cha upasuaji zilikuwa bado hazijamtoka vizuri! Muda mfupi tu baada ya Nancy na wazazi wake kuwasili, watu watatu waliojitambulisha kama maaskari kanzu walifika kitandani na kumkuta Danny akiendelea kuongea mambo yasiyoeleweka.
“Yaani Nancy, baba yako amenipiga risasi? Sio mbaya ili mradi nimekupenda na sitamwambia mtu yeyote kwamba mzee Katobe ndiye aliyenifanyia kitendo hiki, nitawadanganya polisi kwamba nilipigwa risasi na majamba…!” Yalikuwa maneno hatari kutoka mdomoni kwa Danny, aliyekuwa bado hajarejewa vizuri na fahamu zake.
Nancy aliyekuwa jirani kabisa na kitanda alijaribu kuufunika mdomo wa Danny ili asiendelee kusema maneno ambayo yangemtia baba yake katika matatizo, lakini maaskari waliwahi kumwona na kumwamuru aache kufanya kitendo alichokuwa akifanya na mmoja wa maaskari alisogea karibu na kutoa kirekoda kidogo mfukoni kwake akaanza kuyarekodi maongezi yote aliyoyaongea Danny.
Mzee Katobe alisimama hapo akitetemeka mwili mzima bila kuelewa kitu gani kingetokea, alijuta ni kwanini alikubali kuongozana na mke wake pamoja na mtoto wake kuja wodini! Alifikiria kurudi kinyumenyume na baadaye kutoroka lakini kabla hajafanya hivyo maaskari walianza kuuliza maswali.
“Bila shaka nyinyi ni ndugu wa huyu mgonjwa au siyo?”
“Ndiyo!”
“Mna uhusiano gani na mgonjwa?!”
“Hatuna undugu ili sisi ndio tumemwokota akiwa amepigwa risasi!” Mama yake Nancy aliongea mzee Katobe akiwa kimya.
“Mh!”Mmoja wa maaskari aliguna akimwangalia mzee Katobe usoni, alikuwa mzee maarufu sana wilayani Bagamoyo hata maaskari hao walimtambua, ukorofi wake ulijulikana kwa kila mtu.
“Haiwezekani! Nafikiri mmeyasikia maneno aliyokuwa anayasema huyu mgonjwa!”
“Huyu amechanganyikiwa anaweza kusema lolote! Ina maana mimi naweza kufanya kitendo anachokisema?”Mzee Katobe aliongea kwa sauti ya ukali kama njia ya kujihami
“Hapana! Usitutishe mzee, hapa kuna kitu cha kufuatilia!Afande John hebu mfunge pingu huyu mzee twende naye kituoni!” Aliongea askari mwingine na amri yake ilichukua mkondo, mzee Katobe akafungwa pingu na kuanza kusukumwa kwenda nje mke wake akifuata nyuma, Nancy peke yake ndiye alibaki pembeni mwa kitanda cha Danny. Saa nzima baadaye Danny alirejewa na fahamu zake zote na kumwona Nancy pembeni mwa kitanda akilia.
“Vipi? Mbona unalia?”
“Baba yangu! Wamemchukua!”
“Kumpeleka wapi?”
“Polisi!”
“Kufanya nini wakati mimi nilishasema nimepigwa risasi na majambazi?”
“Kuna kitu kimetokea ukiwa usingizini!”
“Kitu gani?”
“Ulisema maneno yote ya ukweli!” Alisema Nancy na baadaye kumweleza Danny kila kitu alichokisema.
Danny alishika mkono wake mdomoni kama ishara ya kuonyesha mshangao, kweli kumbukumbu zilimwijia kwa mbali sana kuwa alitamka maneno hayo lakini akimwambia Nancy na si polisi.
“Nakumbuka kusema lakini nikikueleza wewe!”
“Polisi walikuwepo!”
“Nitawaruka!”
“Wamerekodi!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
Utamu ndiyo kwanza unaanza!
Unajua nini kiliendelea?
Tukutane Jumatatu mahali hapa!
Unaweza kushare kwa ajili ya marafiki zako!

No comments