Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 9


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Mzee Katobe alipofikishwa kituoni alitoa maelezo yake huku akitetemeka na kubabaika na kuwafanya askari wawe na wasiwasi zaidi juu ya tukio hilo, ilibidi atupwe mahabusu na polisi wakamchukua mke wake kwenda nyumbani kufanya upekuzi! Njia nzima mama huyo alikuwa akilia lakini upande mwingine wa moyo wake aliamini nyumbani wasingepata kitu chochote cha kuwasaidia polisi, kama ni bunduki mzee Katobe alikuwa akiimiliki kihalali. Wasiwasi wake ulikuwa ni damu iliyokuwa imetapakaa sakafuni.
“Kama wataikuta ile damu kwa kweli lazima baba Nancy atakuwa kwenye matatizo, sikumbuki tuliporudi nyumbani kama niliangalia vizuri sebuleni!” Aliwaza mama Nancy akijaribu kukumbuka.
Walipofika mama yake Nancy alifungua mlango macho yake yakiwa sakafuni, hakuna hata tone la damu! Mzee Katobe alisafisha wakiwa hospitali, furaha ikamjaa moyoni mwake na maaskari zaidi ya watano wakamiminika ndani ya nyumba na kuanza shughuli ya kupekua wakimulika tochi kila mahali, bunduki ilipatikana chumbani walipoomba kitabu cha kumiliki, mama alikifuata mahali kilipokuwa na kuwakabidhi.
“Ilitumika mara ya mwisho lini?”
“Mimi sifahamu! Sijaona ikitumika!”
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”
Upekuzi uliendelea sebuleni, makochi yalinyanyuliwa na uhamishwa sehemu yalipokuwa! Kwa dakika kumi na nzima maaskari walikuwa sebuleni, wakikaribia kuondoka baada ya kutokupata kitu chochote cha kuwasaidia! Askari mmoja alipiga kelele wote wakageuka na kumwangalia.
“Vipi?”
“ Ganda la risasi!” Alisema askari huyo na wote wakamkimbilia!
“Wee mama unatudanganya?”
“Ah! Unajua….. Unajua!….!” Mama Nancy alikosa cha kuwaeleza!
“Sema ukweli?”
“Kwa kweli sifahamu haya mambo labda muulize mwenyewe!” Aliongea Mama Nancy na baadaye akaanza kulia machozi.
Ganda la risasi lililopatikana lilitosha kabisa kuunganisha na maelezo ya Danny ili kumtia mzee Katobe hatiani, walirudi kituoni na kutoa taarifa kwa mkuu wa kituo! Hawakuwa na shida tena na mama Nancy hivyo walimwachia aondoke zake, hakukuwa na dhamana yoyote kwa mzee Katobe.
****
Ilikuwa tayari saa sita ya usiku wakati mama Nancy anaondoka kituoni, hakutaka kwenda nyumbani tena wakati huo bali wodini ambako aliamini mtoto wake Nancy alikuwepo na pia alitaka kufahamu hali ya Danny kwa wakati huo, ni yeye peke yake aliyekuwa tegemeo katika tatizo lililokuwa linamkabili mzee Katobe! Kama angesema kweli alipigwa risasi na mzee Katobe basi mume wake angefia jela na huo ndio ungekuwa mwisho wa kila kitu lakini kama angekanusha, ni wazi hata kama polisi wangefanya kitu gani wasingekuwa na uwezo wa kumtia mume wake hatiani lazima mzee Katobe angeachiwa huru.
Wodini kama alivyokuwa amefikiria alimkuta Nancy akiwa amekaa pembeni mwa kitanda cha Danny, alikuwa akilia machozi.
“Vipi mwanangu?”
“Hamna tatizo mama!”
“Mbona sasa unalia?”
“Danny amebadilika!”
“Amebadilika!”
“Ndiyo!”
“Kwanini?”
“Anasema kama siwezi kukubali kufanya naye ngono na mwisho kuwa mke wake, atasema ukweli kuwa baba ndiye alimpiga risasi!” Aliongea Nancy kwa uchungu akijifuta machozi.
Neno ngono lilikuwa marufuku katika maisha yake, kiapo alichokula kwa mganga bado alikikumbuka! Hakuwa na ruhusa ya kufanya tendo la ndoa na mwanaume mwingine yeyote isipokuwa Tony! Kama angediriki kufanya hivyo lazima angepata madhara na madhara yenyewe aliyakumbuka, ni kufa au kuwa mwendawazimu.
Ni kweli alimpenda baba yake lakini asingediriki kumvulia Danny nguo yake ya ndani na kufanya naye mapenzi, alikuwa katika wakati mgumu kupita kiasi kufanya maamuzi! Aidha afanye ngono awe mwendawazimu au agome kufanya ngono Danny aseme ukweli juu ya kilichotokea na baba yake, ngome yake na kila kitu kwake apatikane na hatia na kufia jela! Nancy alimwaga machozi mbele ya mama yake.
“Unasema kweli?”
“Kweli kabisa mama! Ndivyo alivyoniambia!”
Mama yake Nancy alimgeukia Danny na kumwangalia kwa macho ya huruma kisha kuanza kumuuliza kama yaliyosemwa na Nancy yalikuwa na ukweli wowote, Danny alikiri na kumwambia mama yake Nancy juu ya mapenzi aliyokuwa nayo kwa mtoto wake na hiyo ndiyo ilikuwa nafasi pekee ya kumpata.
“Baba! Baba! Baba! Nakubembeleza tafadhali, usifanye hivyo!”
“Kwanini mama? Kwani kuna tatizo gani mimi kuwa na mwanao? Hivi nyinyi hamuoni kama mmeniumiza? Kwa kweli kama Nancy hatakubali kufanya hivyo nitasema ukweli, sidanganyi!” Alimaliza Danny na kugeukia ukutani.
Nancy aliinamisha kichwa chake chini, alijuta ni kwanini alikula yamini kwa mganga! Alitamani kubadilisha mambo, awe huru na kukubali kufanya ngono na Danny ili kumwokoa baba yake, maisha ya baba yake yalikuwa mikononi mwake!
“Kesho nitakwenda Mlingotini nikamtafute huyo mganga, nimweleze yote yaliyotokea na kama kuna namna yoyote ya kuniondolea Yamini hii ili niokoe maisha ya baba yangu basi ifanyike kwa gharama yoyote ile!”
Saa tisa na nusu ya usiku aliondoka hospitalini na kwenda hadi nyumbani, Nancy hakulala! Saa kumi na mbili ya asubuhi bila kumuaga mama yake aliondoka nyumbani akitembea kwa miguu kwenda Mlingotini, bado alikumbuka mahali nyumba ilipokuwa! Jua lilipochomoza tayari alikuwa kijijini Mlingotini, alishangazwa na hali aliyoikuta nyumbani kwa mganga. Nyumba ilikuwa imeanguka na hapakuwa na dalili ya mtu yeyote kuendesha maisha katika eneo hilo.
Hakuelewa nini cha kufanya, alianguka chini na kulia kwa uchungu! Dunia ilikuwa imembadilikia, kila kitu katika maisha yake kilikuwa kimejisokota kuanzia kwa Tony hadi kwa Danny na baba yake mzazi!
Akiwa amelala chini aliweza kuona makaburi mawili pembeni yake, akawa na uhakika kuwa pengine mganga wa kienyeji alifariki dunia!
“Nitafanya nini mimi?”
Nancy aliendelea kulia akiwa amelala ardhini, mawazo yalimjaa kichwani na alishindwa kuelewa angefanya kitu gani kama mganga aliyemlisha yamini asingepatikana! Alitamani kufa na kuiacha dunia lakini alipofikiria sana aliona hilo halikuwa jibu sahihi la kutatua matatizo yake ukizingatia tayari baba yake mzazi alikuwa mahabusu na alitakiwa kufanya lolote ili atoke.
“Inavyoonekana Danny hatanii na sijui ni kwanini baba naye alimpiga risasi? Amedhamiria nifanye naye ngono, lakini mimi siwezi mpaka niondolewe yamini!” Aliendelea kuwaza huku akilia.
Mara ghafla alisikia sauti za wanawake wakiongea nyuma yake, akanyanyuka na kukaa kitako, wanawake watatu walisimama njiani wakiwa na ndoo mikononi mwao jambo lililoashiria walikuwa wakienda kisimani kuteka maji. Walisimama hapo kwa muda bila kusema chochote na Nancy wakiendelea kunong’ona wao kwa wao kwa sauti za chini.
Baadaye aliwashuhudia wakikatisha njia na kutembea kwenda mahali alipokuwa amekaa.
“Vipi binti?” Walimuuliza baada ya salamu.
“Nina shida na mzee aliyekuwa akiishi katika nyumba hii!”
“Yule mganga?”
“Ndiyo! Jina lake nimelisahau kidogo!”
“Mzee Mwinyimkuu!”
“Ndiyo!”
“Mbona hayupo muda mrefu!” Aliongea mwanamke mmoja, taarifa hiyo ilimpa matumaini Nancy aliyehisi mganga alishafariki dunia.
“Kwa hiyo kumbe hajafariki?”
“Haya makaburi unayoyaona ni ya mke na mtoto wake, walifariki ghafla yeye akadai wachawi wa Bagamoyo wanamchezea akaamua kuhama!”
“Alihamia wapi?”
“Tabora!”
“Mjini?”
“Hapana! Kijiji kimoja kinaitwa Kisanga!”
“Una uhakika?”Aliuliza Nancy
“Uhakika ninao si alikuwa jirani yetu na alituaga wakati wa kuondoka! Kwani una shida gani naye?”
“Matatizo ndugu yangu!”
“Matatizo gani?”
Badala ya kujibu Nancy aliangua kilio tena jambo lililowafanya akinamama hao watamani kudadisi zaidi na zaidi ili kuelewa kilichokuwa kinamsumbua, mara ya kwanza alisita kueleza lakini baadaye alijikuta akilazimika kufungua mdomo wake na kusema ukweli! Wote walishika mikono vichwani mwao na kumsikitikia.
“Pole sana shoga! Kwanini ulikubali kufanya hivyo?”
“Mapenzi! Nilimpenda sana mpenzi wangu”
“Yuko wapi kwa sasa?”
Nancy akaangua kilio kwa mara nyingine tena, swali hilo lilimkumbusha Tonny mwanaume katili asiye na shukurani aliyemfanyia unyama mkubwa kuliko mwingine wowote katika maisha yake! Maumivu makali yaliuchoma moyo wake. Wanawake wale walizidi kumbana wakitaka kufahamu.
“Aliniacha! Sababu ya mwanamke mwingine ndiyo maana nahangaika kuiondoa hii yamini ili niweze kupata mchumba mwingine na kuolewa”
“Shoga! Acha nikupe ushauri, usijaribu kufanya tendo la ndoa na mwanaume mwingine kabla hujaiondoa yamini! Nimeshaona wengi sana hapa Bagamoyo na hata Dar es Salaam wakiokota makopo sababu ya kukiuka kiapo!”
“Sasa mimi nifanye nini jamani?” Aliuliza Nancy!
“Nakushauri uende Tabora ukamtafute mganga wako, uongee naye ili akuondolee! Narudia tena usijaribu kufanya tendo la ndoa na mwanaume mwingine tofauti na yule wa mwanzo!”
“Wa mwanzo hanitaki kabisa!”
“Basi nenda kamtafute mganga wako, tena simama upesi uondoke usifanye mchezo!” Alimaliza mwanamke mwingine.
“Unaitwa nani dada?” Nancy aliuliza wakati akisimama.
“Naitwa Mwamtumu! Wewe je?”
“Naitwa Nancy!”
“Unaishi Dar es Salaam?”
“Ndiyo!” Aliitikia tu ingawa alijua si jibu la swali alilokuwa ameulizwa.
Nancy hakuwa na la kufanya, mwili wake wote ulikuwa umelegea na akili yake yote kuchanganyikiwa! Alihisi hakuna msaada kutoka mahali popote zaidi ya mganga wa kienyeji aliyepandikiza yamini mwilini mwake, huyo ndiye mtu pekee ambaye angeweza kutatua matatizo yake kwa wakati huo.
Je nini kitaendelea?
Je Nancy atampata mganga huyo?

No comments