Header Ads

Mambo 5 yanayoleta uadui kwa wapenzi!


Uhali gani msomaji wangu! Matumaini yangu kwamba unaendelea poa na majukumu yako ya kila siku.
Tunaendelea na mada yetu ya mambo matano yanayosababisha uadui mkubwa kati ya watu waliokuwa wanapendana. Tumeshajadili jambo la kwanza na kuona jinsi kushindwa kumsikiliza mpenzi wako kunavyoweza kumfanya awe adui yako.
Leo tunaendelea na mambo manne yaliyosalia:
2. MAUDHI YA MARA KWA MARA
Wachambuzi wa masuala ya mapenzi, wanaeleza kwamba miongoni mwa sumu ambazo zinaweza kumgeuza mwenzi wako na kuwa adui yako ni kitendo cha kumfanyia maudhi yanayojirudia.
Kama unataka kuishi kwenye uhusiano wenye amani, epuka maudhi ya mara kwa mara kwa mwenzako. Endapo ameshakwambia kwamba jambo fulani halipendi, msikilize na muoneshe kwa vitendo kwamba umebadilika.
3. KUFOKEANA MBELE ZA WATU
Yawezekana amekuudhi kiasi kwamba umeshindwa kuzidhibiti hasira zako, matokeo yake unaanza kumpandishia au kumfokea mbele za marafiki zake, ndugu au watoto. Jambo hili hujenga chuki kali ndani ya moyo wa anayetendewa na taratibu ataanza kukutoa thamani.
Hata kama umechukia kiasi gani, kamwe usimfokee mwenzako mbele za watu, tafuta muda ambao utakuwa umetulia, zungumza naye kwa upole na bila shaka mtafikia muafaka wa kilichokuwa kimekukasirisha.
4. KUSHINDWA KUHESHIMU NDUGU ZAKE
Familia zetu za Kiafrika, tuna kawaida ya kutembeleana mara kwa mara, yaani kama ni mume, ndugu wa mke watakuja nyumbani kwenu na kama ni mke, ndugu wa mume watakuja nyumbani kwenu.
Hakuna jambo baya kama kuonesha chuki kwa ndugu wa mwenzako, hii itamfanya mwenzako aamini kwamba mapenzi yako kwake ni ya msimu. Taratibu ataanza kukushusha thamani.
5. KUKOSA UAMINIFU
Jambo kubwa ambalo ndiyo mhimili wa uhusiano wowote wa kimapenzi ni uaminifu kwa mwenzi wako. Mapenzi ya kweli yanajengwa na uaminifu, kamwe usithubutu kuuchezea kamari moyo wa mwenzako. Yaani yeye anakupenda na kukupa heshima zote unazostahili lakini nyuma ya pazia, unachepuka na mwingine.
Hata kama alikuwa anakupenda vipi, akigundua upendo utabadilika na kuwa chuki kali ndani ya moyo wake ambayo itadumu kwenye moyo wake. Jitahidi kumfanyia mambo mazuri na kamwe usiuumize moyo wake.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.

No comments