Header Ads

Mastaa vifo tena 2016...Nabii Nicolas Suguye asema itatokea Juni - DesembaKufuatia wasanii watano Bongo kupoteza maisha mwaka huu, Nabii wa Kanisa la Huduma ya Neno la Upatanisho (WRM) la jijini Dar es Salaam, Nicolas Suguye ameibuka na kuweka wazi hali ya wasanii na mastaa Bongo kwa mwaka 2016, tembea na Amani.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum mwishoni mwa wiki iliyopita katika huduma yake iliyopo Ukumbi wa Utoji, Sinza-Mapambano jijini Dar, Nabii Suguye (pichani)  ambaye pia ni askofu (mwangalizi mkuu wa makanisa yake), alisema:
“Mungu amenifunulia makubwa mwaka huu wa 2016 kuhusu wasanii, hasa wakubwa. Mwaka huu, kuanzia Juni mpaka Desemba, tutapoteza wasanii wakubwa nchini na ni jambo ambalo linakuja.”

AWATAJA WATAKAOGUSWA
Nabii Suguye aliwataja wasanii watakaokumbwa na mauti hayo kuwa ni wale wanaotumia uchawi au makafara katika kufanikisha kazi zao.
“Kuna wale wasanii ambao, ili kazi zao ziende mbele ndiyo watakaohusika zaidi. Maono yananiambia hawa, wako katika hatari kubwa.”

ITAKUWA GHAFLA
Suguye ambaye pia ana huduma Kivule jijini Dar, alizidi kusema kuwa, katika maono hayo pia ameelekezwa kuwa roho ya mauti itatoka baharini na kuingia mitaani na kuwafuata wasanii wenye tabia ya uchawi na kufanya kafara hivyo watakufa ghafla.

PIA WATAPATA VICHAA
Nabii huyo, aliendelea kuweka wazi kwamba, wasanii watakaokumbwa na roho hiyo ya mauti wataweza kupata vichaa na kuumwa vifua lakini watakapokwenda hospitalini na kupimwa, magonjwa yao hayataonekana.
“Haya ni maono yangu sahihi kabisa kwa mwaka huu wa 2016 kwa upande wa wasanii. Kwa upande wa mambo mengine, yakiwemo ya serikali na utawala wake, sitasema leo, kuna siku nitaweka wazi,” alisema nabii huyo.

ILI KUJINASUA
Suguye alisema ili kunusuru uhai wao, wasanii, hususan wenye majina makubwa wanatakiwa kumrudia Mungu kwa nguvu zao na kuachana na agano na wachawi au kafara katika kazi zao huku wakikumbuka kutoa zaka kamili kwa Mungu ikiwemo kuwasaidia wasiojiweza.
Pia alisema wanaweza kupakwa mafuta na kuombewa katika makanisa mbalimbali ya kiroho nchini, likiwemo kanisa lake lililopo Sinza- Mapambano.

WASANII WALIOTANGULIA MBELE ZA HAKI
Mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni, wasanii waliokwishatangulia mbele ya haki kwa mwaka huu ni Maneno Gongo ‘Mr Gongo’ (Februari 20, mwaka huu-presha), Jennifer Vincent ‘Mama Utajiju (Februari 15, mwaka huu-kuugua ghafla), Kasim Mapili (Februari 25, mwaka huu-kuugua ghafla), Michael Mhina ‘John Woka (Februari 16, mwaka huu-majeraha kichwani baada ya kulipukiwa na mtungi wa gesi) na aliyejulikana kwa jina moja  la Salim Athuman ‘Mzee Tofi’ (Machi 6, mwaka huu-aliugua muda mrefu).

AMANI NA MASTAA
Baada ya taarifa hizo, gazeti hili liliwasaka mastaa na wasanii wa tasnia mbalimbali nchini ili kuwasikia wanasemaje kuhusu maono ya nabii huyo.

JACOB STEVEN ‘JB’
“Ujue siwezi kukataa kila mmoja ana maono yake.”

ASHA SALUM ‘KIDOA’
“Ni kweli imefika wakati kwa mastaa hasa kwa upande wa sisi wasanii kumrudia Mungu. Kusali na kuwasaidia wasiojiweza.”

SABRINA OMARY ‘SABBY’
“Hayo maneno aliyoongea mchungaji yana ukweli. Cha muhimu ni kumrudia Mungu, utakumbuka marehemu Shehe Yahya aliwahi kutamka hivihivi na baada ya kipindi kifupi vifo vikaanza upya.”

MAHSEIN AWADH ‘DK. CHENI’
“Sisi wote ni binadamu tumeandikiwa kuzaliwa na kufa. Na hakuna ubaya kwa mtu hasa wa Mungu kutoa maono yake.”

ROSE NDAUKA
“Ni kweli imefika wakati wasanii kumrudia Mungu. Alichosema mchungaji mimi namuunga mkono maana kweli ukiangalia vifo vinaendelea kutokea kwa wasanii.”

MRISHO MPOTO ‘MJOMBA’
“Mjomba, mchungaji kanena ukweli kabisa, watu wanatakiwa kubadilika na kumrudia Mungu. Huu ni wakati wa kufanya maombi.”
Mwaka 2015, wasanii mbalimbali nchini walifariki dunia katika matukio tofauti, ikiwemo ajali hali iliyotabiriwa na mchungaji mmoja wa kiroho jijini Dar es Salaam hivyo kuzua mjadala miongoni mwa wadau.

CHANZO: GPL

No comments