Header Ads

WAKALA WA SHETANI - 13MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Kusekwa alizidi kushangaa watu wale kumfanya vile walikuwa na shida gani tena walionesha sio wema kwake. Baada ya kubanwa na vyuma mashine iliwashwa ili kumkata viungo. Lakini ilikuwa ajabu mashine iligoma kuwaka kitu kilichowachanganya wale jamaa nakujaribu mara ya pili lakini iligoma.
SASA ENDELEA...
“Sasa itakuwaje?” Mmoja aliuliza jasho likimtoka baada ya mtambo kugoma.
“Tatizo hili lilitokea hata mwezi jana tulipotaka kumkata viungo yule albino lakini baadae ilikubali na kufanya kazi yake.”
Kauli ile ilishtua sana Kusekwa na kuona kumbe safari ya Ulaya ni kifo, alianza kulia kwa sauti kuomba msaada. Lakini aliambulia makofi yaliyomfanya anyamaze kusubiri hatima yake. Alimuomba Mungu kwa kila lugha aliyoifahamu.
Aliiomba mizimu ya baba na mama yote imtangulie kuponya katika kinywa kile cha mauti. Walikubaliana kumfungua ili kurekebisha ule mtambo ambao uligoma kukata viungo vya Albino. Walimfungua Kusekwa ambaye alikuwa amepoteza fahamu kwa woga wa kupoteza maisha. Walimlaza chini na kuanza kuufanyia matengenezo mtambo ili uweze kuifanya kazi yake vizuri. Walijitahidi kufanya kazi kwa haraka ili waifanye kazi kwa wakati na kurudisha salamu kwa Mr Brown.
Wakiwa katika hali kutengeneza mtambo walimuacha Kusekwa amelala chini kwenye sakafu akiwa kifua wazi. Kutokana na ubaridi wa kwenye sakafu uliosababishwa na kiyoyozi ulimfanya Kusekwa uzinduke. Alipofumbua macho taratibu, aliwaona wabaya wake wakihangaika na kutengeneza mtambo wa kukatia viungo vya Albino. Alitembeza macho taratibu na kuangalia mandhari ya mule ndani na kugundua kuna mitambo mingine miwili na milango minne kati ya milango hiyo mitatu ilikuwa wazi.
Ndani ya kile chumba kilichokuwa na mtambo mmoja wa kukatia viungo na mitambo mingine ambayo hakuifahamu pia kulikuwa na majokufu yaliyoonekana yana kazi ya kuhifadhi viungo vya Albino.
Chumba kile kilikuwa na milango zaidi ya minne tofauti. Kwa vile walikuwa wamemsahau na akili zao zote zilikuwa katika mashine ambayo iliwagomea kutenganisha viungo vya Kusekwa.
Akiwa bado amejilaza chini bila kujitikisa kwa kuogopa kumuona na kuhamishia mawazo yao kwake. Alipata wazo la kutoroka kwa kunyata huku akimuomba Mungu aweze kutoka salama.
Kabla hajachukua uamuzi ule ambao kwake ilikuwa kama kucheza mchezo wa pata potea. Umeme ulizimika ghafla na wote waliokuwa katika kile chumba walishtuka, alimsikia mmoja akisema.
“Huu mkosi gani mashine ilibakia kidogo kieleweke, kukatika kwa umeme kumeturudisha nyuma kabisa.”
“Unajua kazi hii tunaidharau inaweza kututoa jasho,” mwingine aliongezea.
“Wasiwasi wenu, umeme unawaka na kazi inaendelea tatizo tumeishalijua hatutachukua muda mrefu kulitatua,” wa tatu naye aliwatoa hofu wenzake.
Kusekwa aliwashangaa wale watu ambao hawakuwa na chembe ya huruma kwa kutengeneza mtambo ule haraka ili wamgawanye viungo vyake bila huruma. Akiwa bado amejilaza chini aliwashangaa watu wale pamoja na umeme kukatika hawakumgusia yeye zaidi ya mtambo uwahi kupona na kumtenganisha viungo vyake.
Aliamini muda ule wakati wauaji wasio na huruma wakisubiri umeme uwake naye angejaribu bahati yake ya kutoroka. Alijinyayua taratibu pale chini alipolazwa na kuanza kutembea kwa mwendo wa kunyata. Aliutafuta mmoja wa mlango, alifanikiwa kuupata mlango na kutoka kwa kunyata bila kujua anaelekea wapi.
Aliendelea kutembea kuelekea nje katika giza zito huku akimuomba Mungu amuepushe na kikombe kile. Baada ya kutembea kwa muda huku akipapasa na kuomba Mungu umeme usiwake upesi alijikuta akijigonga kwenye kitu alipopapasa aligundua kitu alichojingonga kilikuwa gari.
Alipopapasa vizuri aligundua ile ni Toyota Pick up, akiwa anajiuliza pale wapi mara umeme uliwakana. Kusekwa alijiona yupo kwenye maegesho ya magari ambayo yalikuwa na magari mengi, kabla hajaamua afanye nini aliwasikia watu wakielekea kwenye ile gari wakizungumza.
“Inabidi tuwahi kuondoka muda huu mzigo umefika toka saa saba.”
“Itakuwa vizuri, Mr Brown alikuwa hana raha kabisa.”
Sauti zile zilimfanya Kusekwa aingie chini ya gari ile na kujificha, akiendelea kumuomba Mungu. Kuwaka kwa umeme kulifanya eneo lote lingae kama mchana na kumfanya Kusekwa aamini lazima atakamatwa kutokana na kuwaona askari wakipisha katika kuhakikisha ulinzi wa mule mgodini.
****
Ndani ya chumba cha kukatia viungo vya Albino baada ya umeme kurudi wauaji wale walishtuka kukuta patupu sehemu waliyomlaza Kusweka hapakuwa na mtu.
“Wazee yule mtoto amekwenda wapi?” Mmoja alishtuka na kuuliza macho yamemtoka pima.
“Si alikuwa amelala hapa?” mmoja alionesha kidole alipokuwa amelala Kusekwa.
“Utani huu au ametoroka?”
“Inawezekana lakini hata akitoroka atafika wapi lazima tutamkamatwa tu.”
“Tatizo si kukamatwa bali kuokoa muda, mtambo bado kidogo tukimaliza tuanze kumtafuta kibaya hatujui katoka na mlango upi.”
“Mmh! Ipo kazi jamani, kila mtu atoke na mlango wake ili kumtafuta.”
Baada ya kupeana majukumu waliingia kwenye kazi ya kumtafuta Kusekwa ambaye alikuwa bado yupo chini ya gari akisikiliza mazungumzo ya dereva na mwenzake.
Kila mmoja alikimbia huku akiulizia walinzi kama wamemuona mtoto Albino akipita maeneo yao. Kila aliyeulizwa alisema hajamuona, kila mmoja alipagawa na kujiuliza atakuwa wapi.
Wazo la kuwatoroka hawakuwa nalo zaidi ya kufikiria kuchelewa kutekeleza kazi yao kwa muda muafaka. Waliamini kabisa mtoto Albino lazima angepatikana asubuhi kama hatajitokeza au kumuona wao sehemu amejificha.
Kusekwa aliiona miguu ya mbaya wake aliyekuwa amesimama karibu yake kabisa kuwauliza wahusika wa lile gari.
“Wazee hamjamuona mtoto Albino?”
“Hatujaona mtu yeyote, tena bahati nzuri tumefika hapa umeme umeishawaka lakini eneo hili hatujaona kiumbe chochote, kwani vipi?”
“Kimetoroka kile kitoto, tulikuwa ndio tunatengeneza mtambo kwa ajili ya issue ya bosi.”
“Sasa?”
“Baada ya umeme kuwaka hatukioni kile kitoto japo tunajua lazima atapatikana.”
“Sasa fanyeni hivi toeni taarifa kisha endeleeni na kuutengeneza mtambo, mnafikiri kitafika wapi lazima atapatikana. Mkianza kumtafuta hamjui mtachukua muda gani na mkikipata ndiyo muanze kazi ya kutengeneza mtambo. Hamuoni mtachukua muda mrefu? Lakini mtambo ukitengemaa na akipatikana mnafanya kazi kwa urahisi,” dereva wa gari alishauri.
“Hapo umesema neno ngoja nitoe taarifa kisha turudi kutengeneza mtambo.”
Maneno yote yale Kusekwa aliyasikia aliendelea kumuomba Mungu japokuwa aliamini kuposa ni sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano. Aliomba Mungu wasiliondoe gari haraka kwani lazima angeonekana.
Wale jamaa baada ya kusema vile waliondoka na kumuacha chini ya lile gari. Baada ya kuondoka Kusekwa alimsikia dereva akisema:
“Wacha tuwahi muda umekwenda.”
Kusekwa alihofia kukanyagwa alitoka chini ya gari kwa taadhari kubwa, alipoliangalia lile gari lilikuwa aina ya Toyota pick up, nyuma lilikuwa na turubai. Wazo la haraka lilikuwa kuingia nyuma ya gari na kujifunika lile turubai huku akimuomba Mungu atoke salama kwenye mgodi wa kifo.
Mara gari lilianza kuondoka, mapigo ya moyo yalikuwa makubwa sana kama mtu angekuwa karibu yake angesikia jinsi moyo unavyodunda. Gari lilipofika getini askari alitaka kulikagua.
“Jamani simameni tukague gari.”
Kauli ile ilimfanya Kalekwa atokwe na haja ndogo kwa wasiwasi, alimuomba Mungu kwa kujua lazima ataonekana. Gari lilisimama na mlinzi alizunguka nyuma ya gari na kuanza kufunua turubai.
Alishangazwa na sehemu moja iliyokuwa na mwinuko. Bila kusema neno alisogea hadi kwenye mwinuko na kufunua. Alipofunua turubai alishtuka kumuona mtoto Alibino akiwa nyuma amejifunika turubai lile.
Alipigwa na bumbuwazi na kujiuliza yule mtoto mbona yumo kwenye ile gari tena kajificha, alishangaa kumuona mtoto akimuomba msamaha kwa kukutanisha mikono yake bila kusema neno huku machozi yakimtoka.
Itaendelea

No comments