Header Ads

WAKALA WA SHETANI - 14

 
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’ ILIPOISHIA:
Alishangazwa na sehemu moja iliyokuwa na mwinuko. Bila kusema neno alisogea hadi kwenye mwinuko na kufunua. Alipofunua turubai alishtuka kumuona mtoto Alibino akiwa nyuma amejifunika turubai lile. Alipigwa na bumbuwazi na kujiuliza yule mtoto mbona yumo kwenye ile gari tena kajificha, alishangaa kumuona mtoto akimuomba msamaha kwa kukutanisha mikono yake bila kusema neno huku machozi yakimtoka.
SASA ENDELEA...
Alikumbuka taarifa ambazo alizipata juujuu kuhusu mauaji ya walemavu wa ngozi Albino kwa imani za ushirikina katika mgodi wa Mr Brown. Aliamini kabisa kijana yule alikuwa akitoroka.
Alishindwa aseme nini alibaki akimtazama kwa huruma. Dereva baada ya kuona muda unakatika kwa ukaguzi wa dakika mbili kuwa mwaka mzima aliuliza:
“Mzee Kondo mbona unauweka usiku umekuta nini naona ameganda?”
“Hakuna kitu, mnaweza kwenda,” alisema huku akirudisha turubai na kumuacha yule mtoto Albino kwenye gari.
Alimruhusu dereva ambaye aliondoa gari na kutoka nje ya mgodi bila kujua nyuma ya gari kuna mtu. Kusekwa alimshukuru Mungu gari kutoka salama mgodini. Gari lilikwenda kwa mwendo mrefu bila Kusekwa kuelewa alikuwa akielekea wapi na yeye kuendelea kujificha kwenye turubai kutokana na upepo mkali.
Sehemu moja gari lilisimama na kusikia wale jamaa wakizungumza.
“Bwana eeeh tuchimbe dawa hapa.”
“Sio mbaya.”
Kusekwa alitulia akijua jamaa wameteremka kwenda kujisaidia haja ndogo, wakati wanaingia kwenye gari ili waondoke, Kusekwa aliteremka haraka na kuliacha gari liende. Sehemu aliyoshuka ilikuwa ngeni kwake. Kulikuwa na vichaka ambavyo hakuwa usalama wake.
Lakini baada ya kutoka ndani ya kinywa cha mauti ulikuwa usalama tosha, wakati akitafakari afanye nini mara kwa mbali aliona gari likija na kuwasha taa. Kwa woga alikimbia na kujificha nyuma ya kichaka ili wenye gari wasimuone. Gari lilipopita bila kumuona na kumfanya abaki na sitafahamu afanye nini.
Baridi la alfajiri ile ilikuwa kubwa lakini kwake haikuwa shida kwa vile furaha ya kubakia hai ilikuwa zaidi ya baridi ile. Kutokana na kiza cha usiku ule aliamua kujilaza pembeni ya kichaka ambacho hakujua usalama wake upo kiasi gani.
Pamoja na kutetemeka alimuomba Mungu aipambazue ili ajue yupo wapi na afanye nini. Pamoja na kuwaogopa wanadamu, lakini aliamini wapo wenye roho nzuri kama Father Joe ambaye alionesha upendo wa hali ya juu.
Lakini aliwachukia wanadamu kama Mr Brown ambao hujionesha wana roho nzuri usoni lakini moyoni wana roho mbaya zaidi ya nyoka. Pia aliamini kabisa Father Joe hajui chochote toka kwa rafiki yake mkubwa Mr John Brown kuwa anawachukua watoto wenye ulemavu wa ngozi na kwenda kuwakata viungo na kudanganya kawapeleka ulaya na kumbe ulaya yenyewe ni kuzimu.
Kutokana na akili yake kufanya kazi na kujua haki ya mwanadamu inapatikana wapi alipanga kama atapona katika kile kifo basi atakwenda kwenye vyombo vya sheria. Alikumbuka siku moja walielezwa na Father Joe kuwa kila kitu kinaongozwa na sheria na chombo kinacholinda raia ni jeshi la polisi.
Alimuomba Mungu aweze kufika polisi kufichua uovu ule wa Mr Brown, kila alipojaribu kufumba macho jinamizi la kutaka kukatwa viungo lilimjia na kumfanya akae macho mpaka kuna pambazuka.
Kutokana na baridi kuwa mkali ilibidi Kusekwa ajiingize katikati ya kichaka ili kupunguza ukali wa baridi lile la usiku ule. Kwa bahati mbaya sehemu aliyoingia kulikuwa na nyoka amelala ambaye alimkanyaga, nyoka katika kujitetea alimgonga mguuni.
Kusekwa alishtuka na kupiga kelele za maumivu wakati huo nyoka alikuwa akikimbie eneo lile kwa kutoa mlio wa kutambaa. Alitoka kichakani mule mbio huku akishilia mguu na kusogea barabarani. Baada ya kwenda mwendo mfupi kuondoka eneo la tukio kuogopa kushambuliwa zaidi na nyoka.
Alianza kusikia kizunguzungu ambacho kiliongezwa na mwanga mkali wa gari uliompiga usoni na kumfanya aanguke chini na kilichoendelea hakujua.
MIAKA SABA NYUMA
Ng’wana Bupilipili akiwa katika kijiji cha Sangema kwenye kituo cha kuwatunza watu wenye maisha magumu, baada ya kupata hifadhi pale hapakuwa na tofauti ya kituo alichokimbia.
Shughuli zilikuwa zile zile za kazi za mikono, kutokana na uzoefu alioupata alijikuta akipewa kipaumbele na mkuu wa kituo Mr Harison kuwa kiongozi na mwalimu msaidizi.
Kutokana na kupewa uongozi alijikuta akipata posho ndogo ndogo tofauti na kituo cha awali alikokuwa kula na kulala. Alijikuta akifurahia maisha kule kila siku dua zake zote alizielekeza kwa mwanaye Kusekwa ili bwana amtangulie na kumkinga na roho mbaya za watu na kumpa maisha marefu.
Aliendelea kuwa mwalimu mwanafunzi pale kituoni kujifunza asichokijua na kuwafundisha wenzake wanachokijua. Kila siku zilivyosonga naye ndivyo alivyokuwa akiongeza ujuzi wa kazi yake. Siku moja akiwa darasani juu ya meza ya mwalimu wao kulikuwa na gazeti.
Ng’wana Bupilipili alilichukua lile gazeti na kuanza kulisoma, ndani ya lile gazeti alikutana na picha yake iliyokuwa robo ukurasa wenye maandishi makubwa. ANATAFUTWA, chini ya picha kulikuwa na maneno yaliyosema Mtuhumiwa hapo juu anayetambulika kwa jina la Rozalia Bupilipili au maarufu kwa jina la Ng’wana Bupilipili anatafutwa na jeshi la polisi kwa mauaji ya wana kijiji cha Nyasha pamoja na askari wawili. Ni mwanamke hatari sana mwenye mafunzo ya kigaidi. Yoyote atakaye muona atoe taarifa kituo chochote cha polisi ZAWADI NONO itatolewa.
Tangazo lile alishtuka Ng’wana Bupilipili kuona picha yake kwenye gazeti huku akituumiwa kufanya mauaji ya kutisha katika kijiji cha Nyasha pamoja na askari wawili. Aliamini usalama wake upo mashakani, kwani kwa yoyote atakaye bahatika kuiona ndani ya kituo kile lazima atamuogopa na kisha kulipoti polisi na kukamatwa.
Ilionekana gazeti lile lilikuwa la siku ile hata mkuu wa kituo kile Mr Harison alikuwa bado hajaliperuzi. Alipata wazo la kulichana lakini wasiwasi wake ilikuwa mtu yeyote atakaye bahatika kuliona lile gazeti lazima angemtambua. Kwa ajili ya kuhofia maisha yake alipata wazo la kutoroka eneo lile ili kujiokoa.
Alitoka darasani taratibu na kuelekea chumbani kwake, alichukua vitu muhimu tu na kuondoka eneo la kituo bila mtu kujua. Alijitanda khanga na kuuficha uso wake kwa sehemu kubwa kisha alikwenda hadi kituo cha basi ambako alipanda gari kuelekea asikokujua ikiwa anatafuta sehemu za kijiji zaidi ambazo magazeti kufika baada ya muda mrefu au yasifike kabisa.
Mr Harison baada ya kumaliza shughuli zake ndogo ndogo alirudi darasani kuulizia wamefikia wapi. Lakini alishangaa kutomkuta Malimi, ilibidi amuulize kwa wenzake:
“ Mwalimu wenu yupo wapi?”
“Mmh! Alikuwa anasoma gazeti hapo kisha alitoka nje huenda amekwenda msalani.”
Mr Harison alichukua gazeti lake na kuanza kulisoma taratibu, alipofika kwenye ukurasa uliokuwa na picha ya Malimi alishtuka. Aliiangalia ile picha kwa muda ambayo ilionesha ni ya Malimi, aliisoma na kushtushwa na habari yake iliyoonesha mtu yule ni hatari sana.
Ili kutaka ukweli alitoka na lile gazeti hadi kwa wenzake ambao aliwaonesha ile picha kila mmoja alisema ni Malimi. Kwa vile walijua amekwenda msalani walimsubiri ili wambane na kumuuliza kuhusu uhusiano na ile picha, lakini ajabu muda ulikuwa ukikatika bila kuonekana.
Ilibidi ufanyike msako wa siri kutaka kubaini Malimi yupo wapi, lakini hakukuwa na taarifa zozote. Mr Harison alikumbuka kauli za wanawake waliokuwa kwenye mafunzo kwamba baada ya kusoma lile gazeti alitoka darasani.
Aliamini kabisa ni mwenyewe ambaye baada ya kuiona picha yake ameamua kukimbia. Waliongeza msako kila kona lakini waliambulia patupu Ng’wana Bupilipili alikuwa ameisha potea eneo lile. Taarifa zile alizirudisha kwa wenzake ambao walipigwa butwaa wasiamini tuhuma zile kuwa zake kutokana na tabia yake ya upole tena yenye huruma na mapenzi kwa watu wote.
Hakuwa mbaguzi alikuwa akijitoa yeye kwa wenzake ili kutatua matatizo yao hata kutoa sehemu ya posho yake kuwasaidia wenzake. Japokuwa picha ilifanana kwa asilimia mia bado shoga zake walisema sio yeye. Lakini kizungumkuti kikabakia kama sio yeye yupo wapi?
Lilibakia fumbo zito vichwani mwao wasijue Malimi kipenzi chao amekwenda wapi.

ITAENDELEA

No comments