Header Ads

WAKALA WA SHETANI - 15MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Hakuwa mbaguzi alikuwa akijitoa yeye kwa wenzake ili kutatua matatizo yao hata kutoa sehemu ya posho yake kuwasaidia wenzake. Japokuwa picha ilifanana kwa asilimia mia bado shoga zake walisema sio yeye. Lakini kizungumkuti kikabakia kama sio yeye yupo wapi?
Lilibakia fumbo zito vichwani mwao wasijue Malimi kipenzi chao amekwenda wapi.
SASA ENDELEA...
****
Kusekwa aliposhtuka alijikuta amelala kwenye kitanda cha kamba, alipozungusha macho alijikuta yupo kwenye chumba cha nyumba ya udongo. Alijiuliza pale ni wapi na amefikaje. Alisikia sauti za watu wakizungumza nje ya chumba.
“Dogo lazima atakuwa ameamka.”
“Ngoja nikamcheki.”
Kusekwa aliangalia mlangoni na kumuona mtu mmoja akiingia, walipokutanisha macho alisema kwa sauti:
“Ameamka.”
“Poa, njoo naye apate uji na viazi inaonekana hajala tokea jana,” sauti toka nje ilisema.
“Hakuna tatizo, dogo amka,” jamaa alisema na kumfanya Kusekwa anyanyuke kitandani.
Alitoka nje ya chumba na kukuta sebuleni kuna watu wengine wawili.
“Hujambo dogo?” walimsalimia.
“Sijambo, shikamoni.”
“Marahaba.”
Walimpatia uji na viazi vya kuchemsha, baada ya kula walimuuliza sehemu waliyomuokota amefikaje alikuwa ana toka wapi. Kusekwa aliwaleza yote yaliyomkuta baada ya kuamini wale ni watu wema wake kutokana na walivyomuokoa na kumtunza kama mdogo wao.
Jamaa alishtuka na kumpa pole huku wakimhakikishia kuishi naye maisha mazuri pale na kumtafutia shule yenye usalama. Aliwashukuru kwa kumuokoa na kuwa tayari kumlea.Siku ilipita wakimlea kama mtoto wao kwa kumuonesha upendo wa hali ya juu.
Usiku ulipofika walikwenda kulala na Kusekwa alipewa chumba chake, majira ya wa manane Kusekwa alishtuka usingizi baada ya kuvamiwa na kuzibwa mdomo. Ghafla alisikia maumivu makali mkono wake wa kushoto. Alitaka kupiga kelele lakini mdomo ulikuwa umezibwa.
Alihisi maumivu makali na kupoteza damu nyingi, aliteseka bila msaada wowote huku akijiuliza wenyeji wake wapo wapi mpaka watu wale wabaya wameingia na kumkata mkono. Baada ya kutoka damu nyingi alipoteza fahamu.
Alliposhtuka alijikuta yupo hospitali lakini hakuwa na mkono mmoja, aliangua kilio kitu kilichomfanya wauguzi wafike na kumbembeleza. Baada ya kutulia alielezea yote tangu kuchukuliwa na Mr Brown na kukosa kukatwa viungo na siku aliyovamiwa na watu wabaya kumkata mkono wake wa kushoto.
Kwa vile ilikuwa hospitali ya dini walimpa malezi mazuri ya kumfajiri, aliendelea kuuguza jeraha ya mkono. Baada ya siku mbili zilipatikana taarifa kuna watu wamekamatwa na mkono wa albino. Kwa vile Kusekwa alikua amekatwa mkono siku chache.
Alichukuliwa kwenda kuwatambua watu wale japokuwa aliamini kwa usiku alivyovamiwa asingeweza kuwajua. Lakini alipofika polisi ilikuwa tofauti na alivyofikiria, watu waliomuokota na kumuahidi kumtunza ndiyo aliokamatwa na mkono wake.
Roho ilimuuma na kuona hakuna kiumbe cha kuaminiwa diniani, kama waliomuokota ndiyo aliomtenda. Alirudishwa hospitali na watu wale walifunguliwa mashtaka ya kukutwa na mkono wa mtu. Kusekwa naye aliendelea vizuri na jeraha lake ambalo kila siku lilonesha maendeleo vizuri. Baada ya kupata nafuu alihamishwa toka wodini na kupelekwa kwenye kituo kidogo cha kulelea yatima ambao huchukuliwa na wafadhiri mbalimbali.
Alikaa pale kwa mwezi mmoja akitunzwa na kupata mafunzo ya awali ambayo alianza kuyapata kwenye mgodi wa Mr Brown. Siku zote alijenga chuki kwa watu, kiumbe aliyemuamini alikuwa mwanamke peke yake. Lakini wanaume wote aliwaogopa kwa kuwaona wana sura za furaha lakini mioyo yao ilikuwa na nia mbaya kwao.
Alizidi kuwachukia baada ya kuwasikia mganga mkuu na msaidizi wake wakizungumza juu ya wao maalbino kutolewa kafara kwa ajili ya utajiri wa watu. Hakuamini kama kweli Mungu aliwaumba wawe dawa ya utajiri bali viumbe wenye haki ya kuishi kama wengine.
Alijuliza haki yake itapatikana wapi kwa vile wale wanaoonekana wema mbele ya watu ya watu ndio haohao walio mstari wa mbele kusaka roho zao kwa udi na uvumba.
Baada ya mwezi kupia huku afya yake ya jeraha ikizidi kuimalika, alipewa taarifa ambazo kwa wengine waliamini ni njema lakini kwake haikuwa hivyo. Walielezwa mfadhiri atakuja kuwachukua watoto wawili mmoja akiwepo yeye Kusekwa.
Kilichomshangaza ni kuchaguliwa yeye na mwenzake ambaye alikuwa albino aliyekuwa na umri mdogo kuliko yeye. Alikumbuka jinsi alivyochukuliwa kwenye kambi ya Father Joe na Mr Brown kuwa anakwenda kumtunza kumbe kumtoa roho.
Alitaka kukataa kwenda popote lakini bado hakutakiwa kuonesha kiburi kwa vile kuna watu wenye roho nzuri kama Father Joe. Hakuwa na uwezo wa kukataa kwenda kwa huyo mfadhiri. Alikubali kwa shingo upande huku uhai wake akimkabidhi mwenyezi Mungu.
Siku ya kuja kuchukuliwa ilipofika ilikuta akiwa amejipumzisha kwa vile haikuwa siku ya masomo. Aliliona gari likija halikuwa geni machoni mwake, baada ya wageni kushuka jicho lake lilitua kwa hasimu wake mkubwa Mr Brown.
Akiteremka kwenye gari akiwa na wapambe wake wale wale aliokwenda nao kumchukua kwa Father Joe. Aliamini kabisa Mr Brown hakujua anayemfuata ni Kusekwa, angejua ni yeye asingekuja yeye zaidi ya kuwatuma wapambe wake.
Alimuona akitembea kuelekea ofisini kwa mkuu wa kituo kile cha Misheni chenye hospitali kubwa. Moyo ulimlipuka na kujua alichokuwa akikiwaza kilikuwa kimetimia Mr Brown alikuwa amemfuata kwa kivuli cha wema wa kuwasaidi huku wengi wakijua ni viumbe kama yeye wanapewa upendeleo wa kwenda nje ya nchi kusoma.
Kumbe safari ya kuzimu yenye maumivu makali ya kukatwa viungo bila ganzi, akiwa bado anatafakari, dada mlezi wa kituo kile alimfuata.
“Kusekwa jiandae basi wageni wameishafika, tena una bahati nasikia watu wa aina yenu ndio hupata nafasi ya kwenda nje kusoma.”
Kusekwa hakujibu zaidi ya kutokwa machozi, Sister Anna alimshangaa Kusekwa alikuwa tofauti na Albino mwenzake aliyekuwa na furaha.
“Kusekwa mbona unalia hukufurahia safari hii?”
“Hii dada si safari ya Ulaya bali ya kifo.”
“Kusekwa una maana gani?”
“Dada ni hadithi ndefu ya maisha yangu, nimeweza kuruka mkojo nikakanyaka kinyesi.”
“Kusekwa una siri gani ya muda mrefu uliyoiweka moyoni mwako?”
“Wee acha, maisha yangu yamezungukwa na shetani wa mauti.”
“Ni kweli, sasa hivi mmekuwa akitafutwa sana na watu wabaya kwa ajili ya kuwatoa kafara. Ndio maana tumekuwa makini kuwalinda kwa nguvu zote ndani ya kituo chetu, muda wote mmepewa kipa umbele hata wafadhiri wanapokuja ninyi ndio mnaotakiwa kuondoka.
“Huoni wenzako wana miaka miwili hawakupata nafasi hiyo, lakini wewe na mwenzako mmepewa upendeleo. Huyu mfadhiri aliyekuja ni mtu tunaye muamini amekuwa akiwachukua watoto wengi hasa wenye hali kama yako na baada ya muda hutuletea taarifa kuwa amewapeleka nje kusoma.”
“Dada mpaka sasa mmeishampa watoto wenye hali kama yangu wangapi?” Kusekwa aliuliza.
“Ni wengi hata thelathini wanafika.”
“Mungu wangu!” Kusekwa alishika kichwa.
“Kwani vipi mbona unanitisha Kusekwa?” Sister Anna alishtuka.
“Mna dhambi ya kutoa roho ya watu wote hao na kesho kwa Mungu mna la kujibu,” Kusemwa alisema kwa uchungu.
“Kusekwa kwanini unasema hivyo?”
“Wote uliompa Mr Brown sasa hivi ni nyama ya udongo wakiwa na viungo nusu.”
“Mungu wangu, unasema kweli! na umemjuaje Mr Brown?”
“Ndio ushangae kumjua Mr Brown, ni kiumbe mbaya kuliko nyoka aliyelaaniwa na Mungu, cheko lake nyuma alimeficha madhambi ya damu za watu wasio na hatia. Kama hapa ameua watu zaidi ya thelathini unafikiri vituo vingine wameua watu wangapi?”
“Kusekwa unayosema ni kweli?” Sister Anna alizidi kumshangaa.
“Chanzo cha mimi kukatwa mkono kilikuwa yeye, nilikuwa nimepona kwenye kinywa cha mauti na kuangukia kwenye mikono ya viumbe wenye uchu. Nashukuru nimekatwa mkono lakini kwa Mr Brown ningebakia kiwiliwili kisicho na mikono na miguu.”
“Wewee!!”
“Dada yangu shangaa ya Musa uyaone ya Firauni.”
“Kusekwa, ilikuwaje?”
Kusekwa alimweleza toka alipokuwa katika kituo cha kulelea watoto wenye matatizo, na chanzo cha yeye kuwa pale. Kutokana na historia aliyopewa mama yake alitoroka baada ya kulipa kisasi cha kuua wanakijiji walio muua baba yake pamoja kuchukua mali zao kinguvu yakiwemo mashamba na mifugo.
Sister Anna alibakia mdomo wazi huku muda ukiwa umekwenda.
“Lazima nikiri Mungu mkubwa ndiye aliyeniokoa na mauti yale, nilikuwa nimeisha fungwa kwenye mashine tayari kukatwa viungo bila ganzi. Tena kibaya wanaofanya hivyo ni miongoni mwa ndugu zetu tunaoishi nao sehemu moja kwa vile ya tamaa ya pesa wanakosa utu ndani ya mioyo yao na kututoa uhai wetu ambao hatukupewa kimakosa na Mungu.”
Maneno mazito yaliyochanganyikana na kilio yalimfanya sister Anna kutokwa ma machozi bila kujijua, akiwa hajapata cha kumwambia Kusekwa, walishtuliwa na mkuu wa kituo aliyewafuata baada ya kuona wanachelewa.
“Anna unafanya nini, mtoto mmoja tayari huyo unafanya naye nini muda wote niliokutuma?” mkuu wa kituo aliuliza kwa ukali.
“Samahani mkuu, anakwenda kuoga sasa hivi,” alimjibu bila kugeuka.
“Kwa vile hajachafuka kambadilishe nguo tu umlete haraka.”
“Sawa.”
“Haya fanyeni haraka,” baada ya kusema vile aligeuka na kuondoka akimuacha Sister Anna akitazamana na Kusekwa. Kama mkuu wa kituo angemuangalia vizuri Anna usoni angegundua kitu, lakini haraka yake ilimfanya afikishe ujumbe kuliko kumwangalia wahusika.
Sister Anna alikuwa akitokwa na machozi kwa maneno mazito ya Kusekwa juu ya vijana maalbino wengi waliopoteza maisha yao bila hatia kwa kisingizio cha kupelekewa nje ya nchi kusoma. Alimtazama Kusekwa na kukosa cha kumwambia kwani aliamini kabisa hatakubali kuondoka na Mr Brown baada ya kunusulika kwenye kinywa cha mauti.
“Sasa Kusekwa tufanye nini?” Sister Anna alimuuliza Kusemwa.
“Dada Anna mimi huko siendi labda mauti yangu, siwezi kurudi ndani ya kinywa cha mauti kwa mara ya pili.”
“Sawa, sasa tutafanyaje na muda unakwenda?”
“Mimi natoroka siendi huko.”
“Hata mimi sikushauri uyafuate mauti tena uliyakimbia kwa muujiza wa Mungu , lakini nitamweleza nini mkuu anielewe?”
“Mweleze ukweli wala usimfiche, wacha niondoke eneo hili kabla hajaja tena.”
Kusekwa alikwenda chumbani kwake na kuvaa nguo zito na viatu na kuondoka eneo la kambi aliyokuwa karibu msitu wa miti ya asili, iliyopandwa kwa ajili ya kulinda mazingira na kutengeneza vyanzo vya maji.
Kusekwa akiwa amevaa nguo zake za baridi aliingia porini na kuanza kukimbia kukimbilia katikati ya msitu akiwa na mkono wake mmoja lakini alikuwa ameisha uzoea.
Itaendelea

No comments