Header Ads

WAKALA WA SHETANI -16MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Mweleze ukweli wala usimfiche, wacha niondoke eneo hili kabla hajaja tena.”
Kusekwa alikwenda chumbani kwake na kuvaa nguo zito na viatu na kuondoka eneo la kambi aliyokuwa karibu msitu wa miti ya asili, iliyopandwa kwa ajili ya kulinda mazingira na kutengeneza vyanzo vya maji.
Kusekwa akiwa amevaa nguo zake za baridi aliingia porini na kuanza kukimbia kukimbilia katikati ya msitu akiwa na mkono wake mmoja lakini alikuwa ameisha uzoea.
SASA ENDELEA...
****
Baada ya Kusekwa kukimbia na kuondoka eneo la kambi ile, Sister Anna alijikuta akitafuta cha kumwambia mkuu wake. Alikwenda taratibu hadi ofisini ambapo mtoto mwingine albino alikuwa tayari ameandaliwa kwa ajili ya kuondoka na Mr Brown.
Mkuu wake alishangaa kumuona Anna peke yake bila Kusekwa.
“Vipi mbona unakuja peke yako?”
“M..mm...,” Sister Anna alikosa jibu.
“Vipi! Mbona sikuelewi yupo wapi muda unakwenda si unajua wanakaa mbali?”
Anna alishindwa kujibu na kubakia akikapua macho kama kameza mfupa, kitu kilichomfanya mkuu wake anyanyuke kwa kwaomba samahani wageni.
“Jamani samahanini, nakuja.”
“Bila samahani,” walijibu kwa pamoja.
Alimfuata Anna na kutoka naye nje baada kugundua alikuwa na kitu kilichokuwa kikimtatiza haikuwa kawaida yake kuwa vile. Baada ya kutoka naye nje alimuuliza kwa sauti ya upole.
“Vipi mbona hivyo, Kusekwa yupo wapi?”
“Kuna tatizo father!”
“Tatizo! Kusekwa kafanya nini?” father alishtuka.
“Father kuna makosa makubwa tutakuwa tumefanya bila kujua.”
“Makosa gani?”
‘Kama ni kweli tutakuwa tumepata dhambi kubwa kwa kutoa roho za albino wasio na hatia.”
“Una maana gani kusema hivyo?”
Anna alimweleza yote aliyoelezwa na Kusekwa na uamuzi aliochukua Kusekwa wa kukimbia.
“Anna unasema kweli!?” Father alishtuka sana kusikia vile.
“Ni kweli Kusekwa amejuaje kama yule mzungu anaitwa Mr Brown?”
“Hapo si ndiyo nashangaa kusikia hivyo!”
“Inaonekana kumbe Albino wote tuliokuwa tukimpa na kusema aliwapeleka nje kusoma kumbe alikuwa akiwakata viungo kwa imani ya kishirikina kwa ajili ya mgodi wake.”
“Lakini watakuwa wanamsingizia, mbona hafanani na tuhuma hizo?”
“Unakumbuka Kusekwa alitueleza kuwa alitoroka katika mgodi, Mr Brown hana mgodi?”
“Anao.”
“Na jina sio lake?”
“Ni lake.”
“Basi father umiza kichwa, la sivyo tutaendelea kuwatoa kafara watoto alibino, kumtoa Filipo tukijua kinacho endelea tutakuwa wauaji.”
“Mmh, hii mpya sasa tutafanya nini maana jamaa anajua anaondoka na albino wawili?”
“Hakuna cha kufanya nini mueleze tumesitisha kuwatoa watoto maalbino.”
“Atanielewa kweli mtu niliisha mkubalia na mtoto tumeisha muandaa na amemuona?”
“Mimi nafikiri suala la uhai wa mtu si la kufumbiwa macho, kama wewe huwezi niachie mimi nitamweleza. Huoni tuna dhambi ya watoto wangapi ambao tuliambiwa wamekwenda Ulaya kusoma kumbe Ulaya ya kuzimu.”
“Mmh! Ipo kazi.”
“Father kama huwezi niachie niwaeleze, roho inaniuma sana kuona watoto wote tuliompa Mr Brown amewaua kikatili kwa kuwakata viungo,” Sister Anna alisema kwa uchungu.
“Okay, nimekuelewa niache nikawaeleze, Filipo haondoki.”
Baada ya mazungumzo ya siri waliongozana hadi kwa wageni, Mkuu wa kituo baada ya kukohoa alisema:
“Samahanini kwa kuwaweka kwa muda.”
“Bila samahani,” walijibu wote.
“Kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu, hatutakupa watoto kwa vile nilipitiwa kuwaeleza watoto kabla ya kuondoka walitakiwa kuonana na wazazi wao.”
“Mkuu mbona unaharibu mambo, si unajua kampuni yangu ina husika na kuwapeleka nje watoto wenye ulemavu wa ngozi?” Mr Brown alilalamika.
“Ni kweli, lakini hata watoto wasio na ulemavu wa ngozi nao wanahitaji kwenda nje,” Father alisema.
“Ni kweli, lakini wenye ulemavu wa ngozi ndio waliopewa kipa umbele kutokana na kusakwa na watu na kuwakata viungo. Hivyo tumewapa kipa umbele wao ili kuwaweka sehemu salama,” Mr Brown alitetea hoja yake.
“Sina hakika kama walemavu wanaoonewa huruma ni wa ngozi mbona wapo wengi?” Sister Anna alihoji.
“Huo ni mpango uliopangwa mwakani kuwachukua watu machanganyiko.”
“Sawa, lakini kama nilivyo kueleza hawawezi kuondoka bila kuonana na wazazi wao,” Father alikataa kuwatoa watoto.
“Wanakuja lini?”
“Hawakusema ila walituma ujumbe lazima waonane na watoto wao.”
“Lakini nina siku moja tu vijana hawa ningeondoka nao leo wangeungana na wengine wanane kuondoka kesho kutwa tena wana bahati ya mtende,” Mr Brown alizidi kuwatia tamaa.
“Ni kweli, lakini hatuwezi kukiuka kauli ya wazazi wao kwa vile sisi ni walezi lakini wenye haki ni wazazi wao.”
“Sasa mkuu, mimi nitakuachia hapa kiasi cha pesa wakija wape ili wasikusumbue.”
“Kama pesa hata mimi ningewapa, lakini naheshimu kauli zao kwa vile wao ni wazazi sisi ni walezi tu, hatuna mamlaka ya kwenda kinyume na makubaliano tuliokubaliana. Mbona waliotangulia tulikupa bila kipingamizi tena wengi kuliko hawa wawili?”
“Kwa hiyo nisubiri mpaka lini?”
“Wakija leo nitakujulisha uje kesho, wakija kesho vilevile nitakujulisha usife moyo.”
“Okay, hatuna jinsi.”
Mr Brown aliondoka amenyong’onyea baada ya kuwakosa wale maalbino wawili, waliingia kwenye gari lao na kuondoka kurudi mgodini. Baada ya kuondoka walibakia mkuu wa kituo na Sister Anna wakijadiliana.
“Father umeona?” Sister Anna aliuliza.
“Nimeona.”
“Anataka kutoa pesa ili awanunue watoto, huoni kama ana masilahi nao?”
“Ni kweli.”
“Sasa hizi taarifa zifike kwenye vyombo vya dola ili wachunguzwe na wakingundulika wachukuliwe hatua kali.”
“Kuna muhimu wa kufanya hivyo, bado siamini kama kweli watoto wote aliowachukua amewaua kwa kuwakata viungo. Kama ni kweli tuna dhambi kubwa ya damu za watoto wale ambao tulijua wapo Ulaya kumbe kuzimu,” Father alisema kwa masikitiko.
“Mkuu hili lisilale ikiwezekana tukalilipoti leoleo.”
“Hapana Anna tusifanye papara, nitampigia mkuu wa makosa ya jinai ni rafiki yangu mkubwa. Atakuja hapa tutamweleza yote nina imani atayafanyia kazi.”
“Kama hivyo itakuwa heri.”
“Sasa Kusekwa atakuwa wapi?”
“Sijui, nina imani akiwaona wameondoka atarudi.”
****
Kusekwa baada ya kutoka eneo la kambi, aliingia porini kutokana na hofu ya maisha yake alikimbia kwa muda wa masaa matatu bila kupumzika. Baada ya kukimbia kwa muda mrefu alijikuta akichoka sana na kuamua kujipumzisha kwenye mti uliokuwa na hewa safi.
Bila kujielewa usingizi mzito ulimpitia, alishtushwa na sauti za watu waliokuwa wakizungumza. Alipofumbua macho hakuamini kumuona Mr Brown akiwa na vijana wake mbele yake.
Itaendelea Jumatano

No comments