Header Ads

Bunge, PAC wavutana uchunguzi wa LugumiSAKATA la mkataba wa Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd, limechukua sura mpya baada ya hadidu rejea zilizotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya hesabu za Serikali (PAC) kwa kamati ndogo iliyoundwa ajili ya kuchunguza mkataba huo, kutofautiana na za Bunge.


Kamati hiyo ndogo iliyoundwa na PAC ikiongozwa na Japhet Hasunga (Vwawa-CCM), imepewa kazi ya kuchunguza undani wa mkataba huo wenye thamani ya Sh. bilioni 37.
Mkataba uliozua utata, uliingiwa mwaka 2011 baina ya jeshi la polisi na kampuni ya Lugumi, kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo vya polisi 108, lakini hadi sasa imefunga vituo 14 na kulipwa Sh. Bilioni 34, sawa na asilimia 99 ya fedha zote, kinyume cha Sheria ya Ununuzi wa Umma.

Baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, Aprili 23, mwaka huu, PAC ilikutana na kuteua wajumbe tisa watakaounda kamati ndogo kuchunguza sakata hilo kwa undani na kuandaa hadidu za rejea za kufanyia kazi.
Baadhi ya adidu za rejea zilizojadiliwa na PAC ni pamoja na kuangalia thamani ya vifaa vilivyonunuliwa na hali halisi ya soko na kama kulikuwa na ulazima wa kutoa kazi hiyo kwa mbia mmoja.

Pia kamati hiyo ilitakiwa kuangalia kama Lugumi ililipa kodi katika fedha ilizolipwa kutokana na mkataba huo. Nyingine ni kupitia mfumo mzima wa utoaji zabuni ikiwa ni pamoja na nyaraka za zabuni alizopewa mzabuni na zile alizojaza, kuangalia uwezo wa kampuni kama ilikuwa na sifa za kupewa kazi hiyo.

Siku moja baada ya kufanyika kwa kikao hicho cha PAC na kutangaza majina ya wajumbe wa kamati ndogo, Ofisi ya Bunge ilitoa taarifa kwa umma ambayo ilisema kamati hiyo ndogo itajigawa kwenye makundi matatu na kupita kwenye maeneo husika kuhakiki kazi iliyopewa.
“.. Kwa mujibu wa hadidu za rejea ambayo ni kufanya uhakiki iwapo vifaa vinavyohusiana na mradi ulioingiwa kati ya jeshi la polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd, kuhusu ufungaji wa vifaa vya utambuzi wa alama za vidole, vilinunuliwa na vilifungwa katika maeneo husika,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Akizungumza na Nipashe jana, Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema hoja ya CAG ilikuwa kufungwa kwa vituo vifaa hivyo kwenye vituo 14 badala ya 108, jambo ambalo ndilo linalotakiwa kufuatiliwa na kamati hiyo ndogo na si vinginevyo.

Alisema kwa sasa suala la sakata la Lugumi linavyochukuliwa ni sawa kwamba kuna mtu anatafutwa, jambo alilosema halipaswi kuwa la Bunge bali mtu anayedhani ana kitu chake binafsi anatakiwa kuwasilisha hoja binafsi bungeni.
“Kukagua kampuni imesajiliwa na vitu vingine si kazi yao. Hiyo inahusiana na hoja ya ukaguzi aliyoitoa CAG? Kama haihusiani na hoja ya CAG hiyo kazi nyingine wanaipata wapi wao? Hoja ya ukaguzi inasema ni kufunga mashine kwenye vituo, sasa wao wanaenda kuchunguza kampuni si ajenda ya CAG tena?

“Kwani wao (PAC) wanachotaka sasa hasa ni nini? Maana mnataka kutuchanganya ninyi waandishi wa habari,” alisema Joel na kuongeza kuwa: “Wanachokwenda kufanya ni kitu gani, kama wanataka kwenda kufanya kazi hiyo (kukagua kama vifaa hivyo kama vimefungwa au la), manake sasa wanakwenda kinyume kwa sababu hiyo haikuwa hoja ya CAG, kwa maana hiyo wao wananzisha hoja yao.

“Hiyo ya kampuni kama ni halali, si halali, imelipa kodi haijalipa kodi, hayo yanatoka wapi? Kwa sababu ingekuwa ndiyo hoja ya CAG ingekuwa sawa. Kama si hoja yake manake sasa kamati inatakiwa ilete taarifa bungeni itoe hoja kwamba kuna kitu fulani halafu Bunge sasa liwakubalie kwamba nendeni mkatuchunguzie hayo mambo.”
Alisema kwa sasa PAC haijatoa taarifa bungeni “halafu inaanza kutafuta kazi? Hiyo si sawa, kwa sababu kamati ile inatakiwa ifanye kazi kwa mujibu wa kanuni.

“Lazima inapokuwa inafanya kazi iangalie majukumu yake na mipaka yake ya kazi, na najua spika amewapa ruhusa ya kuunda hiyo kamati ndogo na amewapa adidu za rejea ni kitu gani cha kwenda kufanya.

“Wakienda huko wakagundua mambo mengine inatakiwa yaje yaombewe kibali bungeni kwa sababu siyo sehemu ya ripoti ya CAG, na kama wanakwenda kufanya hiyo kazi nyingine hakuna sababu ya kumuhusisha CAG wala hazina, wala hata polisi kwa sababu sasa hapo polisi au wizara ya mambo ya ndani inahusika nini kwenye masuala kama hayo?

“Jinsi hii hoja inavyojengwa inajengwa kwa minajili kwamba kuna mtu anatafutwa, kama kuna mtu anatafutwa hiyo isiwe ni issue (jambo) ya Bunge. Ingekuwa issue ya individual (liwe suala binafsi) wakaileta kama hoja binafsi ama waka watavyotaka kufanya lakini kama ni hoja ya CAG wasiweke vitu vingine ambavyo CAG hakuhoji,” alisema Joel.
Makamu Mwenyekiti.

Alivyotafutwa kutolea ufafanuzi suala hilo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilary, alisema kwa sasa kazi ya kufanya uchuguzi huo ameiacha kwa kamati ndogo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ndogo ambaye ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka, aliliambia gazeti hili kuwa mpaka sasa hawajapata hadidu za rejea kutoka Ofisi ya Spika na kuwa wakishakabidhiwa ndiyo watajua nini cha kufanya.

“Lakini kama uambiwe uende Dodoma ukaangalie kama bungeni pale komptuta zilikuwa zimewekwa, lazima ujue mkataba ulitaka ziwekwe ngapi na za aina gani. Details (undani) haziwezi kuandikwa kila mahali. Ni sawa na kufanya utafiti, huwezi kuandika kila kitu lakini kama unavyoenda maswali yanaibuka na vitu vingine ndiyo unapata picha halisi.
“Huwezi kwenda kuchunguza bila kujua unachunguza kitu gani. Lazima uambiwe na si kuambiwa tu kwa maneno,
utaenda kuangalia nini? Unaambiwa uchunguze magari 10, kwa nini unachunguza? Ni kwa sababu kuna tuhuma, kwa hiyo lazima uangalie mkataba unasemaje? Kama umeambiwa 10 mkataba kweli ulikuwa unasema 10 au 15, kwa hiyo mimi nafikiri kutakuwa hakuna tatizo,” alisema Kaboyoka.
Alisema kamati ndogo ikikaa ndiyo itaangalia hadidu za rejea na kisha waone ni nini cha kufanya.
“Unajua uchunguzi inategemea malengo yenu ni nini, je taarifa tuliyo nayo itakuja kutusaidia tunachotaka, utakuja kuandika ripoti gani?

“Kama vimefungwa ni vingapi? Utathibitisha nini maana unaweza kuambiwa taarifa ambayo hujui kama ndivyo mkataba ulivyokuwa unasema na ukatoa taarifa ambayo umeegemea kwenye kitu ambacho hakikuwa sahihi, wewe unaonekana umefanya ile kazi hukuwa makini.
“Ni sawa na uambiwe ukachunguzi ni watoto wangapi wameolewa na umri mdogo, kwani sheria inasema? Lazima uijue, anatakiwa aolewe na umri gani? Lazima uwe na sheria ile.
“Maana vinginevyo utakuwa uncheza tu, lazima upate maelezo ya kila kitu, unapofikia daraja ndo unajua hili daraja naweza kulikwepa ama linaweza kubeba gari langu?” alisisitiza.
Hivi karibuni gazeti hili lilibaini kuwa ajenda ya kukabiliana na ugaidi ilitumika kuidhinisha zabuni hiyo na kuvunjwa kwa sheria za manunuzi.
Mpango huo ulisukwa baada ya baada ya Bunge kupitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya ndani kwa mwaka 2011/12, ambayo ndani yake ilikuwa na kipengele cha ununuzi wa vifaa maalum (specialized equipment).
“Kutokana na hali ya wakati huo ambapo matukio ya uhalifu wa kutisha na viashiria vya ugaidi vilivyokuwa vimeanza kujitokeza, jeshi la polisi liliamua kununua mfumo utakaotumika katika utambuzi wa alama za vidole.
Ununuzi wa mfumo huo ulikuwa muhimu kwa jeshi la polisi kwa ajili ya kuimarisha usalama wa nchi, raia na mali zao
Kwa kuzingatia unyeti wa kazi iliyotegemewa kufanyika kwa mfumo huu ilibidi kutumia njia ya single source (kutumia mdhabuni mmoja bila kushindanisha wengi apatikane mmoja bora) hivyo jeshi la polisi lilikaribisha Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd kufunga mfumo huo,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ambayo Nipashe imeiona.
Inaeleza kuwa, kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 204, polisi kupitia kitengo chake cha PMU, lilianzisha mchakato wa mfumo huo.
Taarifa hiyo inasema kuwa, Septemba 16, 2011, bodi kasimu ya jeshi la polisi iliidhinisha uanze mchakato wa ununuzi ya mfumo huo kwa kutumia njia hiyo ya ‘single source’ na kisha kampuni ya Lugumi ikapewa nyaraka za zabuni.
Inaeleza kuwa Septemba 22, mwaka huo ufunguzi wa zabuni hiyo ulifanyika ambapo uliudhuriwa na mwakilishi wa 

Kampuni ya Lugumi.
Taarifa hiyo inasema, simu iliyofuata (Septemba 23) Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, aliteua kamati ya tathmini iliyokuwa na wajumbe watano.
Siku saba baadaye (Septemba 29), kamati ya zabuni iliwasilisha ripoti ya tathimini ambayo ilipendekeza Kampuni ya Lugumi Enterprises.
Ilipofika Novemba 8, taarifa hiyo inasema bodi kasimu ya zabuni ya jeshi la polisi, ilifanya kikao na kuridhia mapendekezo ya kamati ya tathimini kwa kuiteua kampuni ya Lugumi Enterprises.
Baada ya mchakato huo, taarifa hiyo inasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliidhinisha wizara kuingia mkataba na Lugumi kwa barua yenye kumbukumbu namba JC/A/130/11/1 iliyoandika Novemba 25, 2011.
Licha ya kuharakishwa kwa mchakato wa kumpata mzabuni bila kumshindanisha au kujiridhisha na uwezo wake wa kuleta vifaa bora, taarifa hiyo ya polisi inasema mpaka leo ikiwa ni takribani miaka mitano tangu mzabuni alipopitishwa, kwenye baadhi ya maeneo vifaa hivyo havifanyi kazi.

Taarifa hiyo inasema kwenye maeneo mengi vifaa hivyo havifanyi kazi kwa sababu ya kukosekana kwa mfumo wa mtandao wa intaneti.
Hali iyo inandelea kuzusha maswali mengi ikiwa ni pamoja na je, kwa nini walinunua vifaa vinavyotegemea mfumi huo pekee na kupanga kuvifunga nchi nzima ilihali walijua kabisa hali ya upatikanaji wa mtandao nchini?
Kwa muda mfupi uliotumika kumpata mzabuni bila kumshindanisha, ni kigezo gani kilitumika kuiteua kampuni ya Lugumi Enterprises na siyo nyingine yoyote?
Ikiwa ni miaka takribani sita sasa tangu fedha za kununua vifaa hizo kutolewa na kwenye maeneo mengine bado havijafungwa, viashiria vya ugaidi vilivyotajwa kuwa moja ya sababu ya kuharakisha ununuzi wa vifaa hivyo vimeishia wapi? Ajenda hiyo ilitumika kubariki utolewaji wa fedha haraka?
CHANZO; NIPASHE

No comments