Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 23ILIPOTOKEA...

Baada ya kuzama ziwani Nancy na mama yake wanajikuta katika kisiwa cha Galu kilichoko katikati ya ziwa Tanganyika, safari yao kuelekea Kongo kumtafuta mzee Mwinyimkuu aliyemlisha Nancy yamini inaonekana kufikia mwisho!
Wapo mikononi mwa wazee wawili, mzee Kiwembe na babu Ayoub. Wazee hao walifika kisiwani hapo miaka mingi iliyopita baada ya kupata ajali majini, wameishia hapo peke yao bila mwanamke! Hivyo kuja kwa Nancy na mama yake kunaonekana kuwa baraka, wanawageuza wake zao.
Mzee Kiwembe alimchagua mama Nancy, pamoja na kutaarifiwa juu ya kiapo ambacho msichana huyo alikula babu Ayoub anaamua kumwingilia Kimwili! Hapohapo Nancy anashikwa na wendawazimu na kuwa mwehu kamili.
Mama yake anasikitika lakini anakosa la kufanya sababu wao ni kama mateka baadaye anaamua kuukubali ukweli na kuendelea kuishi na mzee Kiwembe kama mumewe! Muda mfupi baadaye anakuwa mjamzito, hali inayomchanganya na kumfanya ashindwe kuelewa nini angemwambia mume wake mzee Katobe kama angeondoka kisiwani na kurejea Bagamoyo!
Hali ya mtoto wake ni mbaya, Nancy anazidi kukonda! Wendawazimu unamfanya agome kula chakula, ni mtu mwenye vurugu nyingi jambo linalosababisha afungwe kamba kwenye nguzo kubwa iliyokuwepo kibandani kwa babu Ayoub.
Mama Nancy hakuwa na uhakika kama siku moja angeondoka kisiwani hapo na mtoto wake na hakuwa tayari kushuhudia Nancy akifa! Kila siku aliwalilia mzee Kiwembe na babu Ayoub wamchukue Nancy kwenda Kigoma kwa matibabu zaidi.

SONGA NAYO

Kila siku iliyokuja na kupita mama Nancy alifikiria ni kwa namna gani angeweza kuondoka kisiwani na kufika Kigoma akiwa na mtoto wake, uwezekano ulizidi kupungua kadri siku zilivyozidi kusonga mbele, wakati huohuo hali ya Nancy ilizidi kudhoofika siku hadi siku!
Pamoja na kuwa mjamzito mwanamke huyo hakuogopa kwenda kwa mume wake, alimpenda mzee Katobe na aliamini kama angekutana naye na kumpa maelezo juu ya kilichotokea hakika angemwelewa na kukubali kumsamehe! Mimba hakikuwa kikwazo cha yeye kuondoka, tatizo lilikuwa usafiri na ni kwa namna gani angeweza kumpandisha Nancy katika mtumbwi hata kama angeamua kuondoka na kimtumbwi kidogo cha wazee wale usiku wakiwa wamelala.
“Mtoto mwenyewe wamemharibu akili, nikimsogelea anataka kunipiga! Hataki hata kuniona, sijui wamemfanyia kitu gani mpaka kunisahau mimi mama yake!” Aliwaza mama Nancy.
Mama Nancy alionekana kugota kabisa kimawazo, alikosa mpango au mbinu za kumwondoa kisiwani lakini kila siku akili yake ilifanya kazi! Hakuwa tayari kuona mtoto wake anakata roho wakiwa kisiwani, alikuwa tayari kufia mbele kwa mbele akitafuta usalama wa maisha yao wote wawili.
Miezi ilizidi kukatika taratibu hatimaye mama Nancy akajifungua mtoto wa kiume, mzee kiwembe alimwita mtoto huyo Magurumchumvi, jina la babu yake aliyewahi kuwa mganga maarufu wilayani Kasulu mkoani Kigoma! Pamoja na kumzaa mtoto huyo nje ya ndoa yake, bado mama Nancy alimpenda mtoto huyo, hata siku moja hakuwahi kumwita kwa jina la Magurumchumvi, alimwita David akimfananisha na Daudi wa Biblia aliyempiga na kumuua mtu mwenye nguvu, Goliath.
Hakuna siku iliyopita bila yeye kupanga mkakati wa kuondoka, ilikuwa ni lazima atoroke tena akiwa na watoto wake wote wawili, asingemwacha Nancy kisiwani vinginevyo alikuwa tayari kufa pamoja naye kisiwani Galu! Bado manyanyaso yaliendelea kila siku aliingiliwa na mzee kiwembe na alimsikia Nancy akilia usiku mzima babu Ayoub akimfanyia ukatili bila kujali alikuwa mwendawazimu.
Mtoto akiwa na miezi minne tu alianza kuhisi dalili ya mimba nyingine, kichefuchefu na kutapika asubuhi kwake kulimaanisha ujauzito! Ilikuwa ni kama utani lakini miezi mitatu baadaye mtoto David akiwa na umri wa miezi saba mimba ilionekana wazi, mzee kiwembe hakusikitishwa na hilo kwake ilikuwa furaha kupata watoto wawili katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu! Alijiona shujaa aliyekuwa akifidia muda aliopoteza kisiwani, hilo lilimfanya babu ayoub naye azidishe kasi ya kumwingilia Nancy akitafuta mtoto bila kujali mtu aliyemfanyia kitendo hicho alikuwa mgonjwa na mwendawazimu.
“Najitahidi sana lakini wa kwangu hapati mimba!”
“Pole sana, mimi sasa hivi naelekea kupata wawili!”
“Nimeona!”
“Ongeza juhudi!”
“SItachoka mpaka mtoto apatikane, vinginevyo atafia kwenye kamba!”
Waliongea wazee hao mama Nancy akisikia, aliumia sana moyoni mwake lakini wao hawakujali! Hawakuwachukulia Nancy na mama yake kama binadamu wa kawaida bali watumwa ambao kazi yao ilikuwa ni kuwaridhisha kingono. Kitu kimoja kilimsumbua mama Nancy kichwani mwake, mtumbwi! Alihitaji chombo cha kumsafirishia yeye na watoto wake, ni hapo ndipo alipofikia kuanza kuchonga au kutengeneza kitu chochote cha kuelea majini ambacho angetumia kukatisha ziwa Tanganyika akipiga kasia.
Aliliona wazo hilo la kufaa kabisa, hapakuwa na njia nyingine ya kujiokoa zaidi ya kupata mtumbwi, ni hapo ndipo alipoanza kila siku mzee Kiwembe na babu Ayoub wakiwa ziwani, alikwenda msituni na kukata miti ya Mikule! Iliokuwa kama boya ndani, ilifanana sana na Milingoti ya katani lakini yenyewe ikiwa na unene wa kama nguzo ya umeme, ilikuwa rahisi kuangusha kwa sababu iliota sehemu zenye majimaji!
Alikata miti mingi na kuikata katika vipande vya kama futi sita na kwa kutumia kamba za magome ya miti alianza kuvifunga vipande hivyo pamoja na kufanya kitu kama sakafu ya miti, haikuwa kazi ndogo! Aliifanya taratibu na kila siku alipopata nafasi, alitumia miezi miwili kukamilisha kutengeneza kitu alichokuwa akihitaji ingawa hakuwa na uhakika kama kingeweza kuelea na hatimaye kumvusha kwenda upande wa pili, alikuwa amechoka kuishi kisiwani akishuhudia mwanae akiteseka.
Alikiita kitu alichokitengeneza jina la pantoni na kukisukuma hadi majini akitaka kuona kama kingeelea, hivi ndivyo ilivyokuwa! Kwa macho yake alikiona kikielea majini, alipanda juu yake kuona kama kingezama lakini bado kilielea na hakikuonekana kuelemewa na uzito. Moyo wake ukaanza kurejewa na matumaini ya kuondoka kisiwani hapo, aliporudi nyumbani siku hiyo fikra zake zote zilikuwa ni lini angeondoka! Kila siku haikupatikana kwani babu ayoub alipoondoka kwenda ziwani kuvua aliacha mlango umefungwa.
Angetaka kuondoka peke yake bila Nancy ingekuwa rahisi lakini hakuwa tayari kumwacha mtoto wake hilo ndilo lilimfanya aendelee kukaa kisiwani mpaka akajifungua mtoto wa pili! Huyo alikuwa ni wa kike na mzee Kiwembe alimeita kwa jina la Mategelesi, jina la bibi yake ambaye alikuwa kuwa mganga wa kienyeji hata siku moja mama Nancy hakumwita mtoto wake kwa jina hilo, alimwita Catherine na alimpenda ingawa alizaliwa nje ya ndoa.
Tayari alikuwa na watoto watatu na wote alitaka kuondoka nao kwenda Kigoma au Kongo, alichotaka ni kufika nchi kavu! Huko angeelewa kitu cha kufanya ili hatimaye arejee Dar es Salaam na baadaye Bagamoyo hakuogopa kurudi kwa mzee Katobe na watoto, Mpaka wakati huo hakuelewa ni kwanini akiwa na mumewe hakuwahi kupata ujauzito zaidi ya ule wa Nancy lakini akiwa na mzee Kiwembe alikuwa akipata mimba mfululizo.
“Nitaondoka! Siku yoyote nitakayopata nafasi ya kumwondoa Nancy katika kibanda hicho ndio siku nitakayoondoka hapa kisiwani, itatokea tu! Kosa moja magoli mia kwa sasa wacha nijifanye mnyonge!”Aliwaza mama Nancy.
****
“Siwezi kuoa! Siwezi, tena wazo hili lisinijie tena kichwani mwangu, kama ni kufa kwa huzuni acha nife! Ningemzika mke wangu na kuliona kaburi lake hapo ndio ningefikiria kuoa! Siamini kama kama Nancy na mwanangu kweli wamekufa! Wanaweza kuwa mahali fulani wanaishi au wamekwama, nikaoa halafu siku moja mke wangu akarudi! Nitafanya nini mimi? Nitamwambia nini mke wangu? Haiwezekani nampenda sana mama Nancy na siamini kama kweli yeye na mwanangu wamekufa!” Aliwaza mzee Katobe.
Maisha yake yalikuwa ya huzuni mno, watu waliomfahamu walimwonea huruma! Aliishi peke yake bila hata mfanyakazi, alikonda kwa mawazo.
Marafiki zake wengi walimshauri aoe lakini hakukubali! Hisia kuwa siku moja mke pamoja na mtoto wake wangerudi zilimsumbua kichwani, alivumilia hadi mwaka ukapita na kuahidi kuendelea kuishi peke yake hadi mwisho wa maisha yake labda mke wake atokee.
Kwa Danny ilikuwa tofauti, alipoingia chuoni mara ya kwanza baada ya kutoka Kigoma kumtafuta Nancy na mama yake alikuwa mtu mwenye huzuni sana, mara nyingi alionekana kutokwa na machozi! Hakuamini maisha yake yangekuwa sawa tena, watu wengi waliomfahamu Nancy walihuzunishwa sana na habari za kifo chake lakini kwa wasichana waliomtamani Danny siku zote hali ilikuwa tofauti, baadhi yao walifurahia na kuona hiyo ndiyo ilikuwa nafasi pekee kumpata mwanaume waliyempenda ambaye siku zote alijifanya mgumu.
Mmoja wa wasichana hao alikuwa ni Agness alisoma darasa moja na Danny lakini sababu ya kurudia mwaka Agness alijikuta yupo mbele yake, aliwahi kuwa rafiki mkubwa wa Nancy, lakini pia alimpenda Danny tangu mwanzo hakutaka kuliingilia penzi lao.
Alijifanya kumwonea huruma Danny, muda wote akiwa pembeni yake na kumfariji, lakini hilo halikuwa lengo lake, muda wote alitafuta kuwa naye karibu ili hatimaye aweze kumwingiza katika mtego wa kuwa mpenzi wake! Alichofahamu yeye ni kwamba, kumnasa mwanamume au mwanamke mwenye huzuni kimapenzi kilikuwa kitendo rahisi kuliko kumeza tonge la ugali.
Danny hakuweza kuitafsiri hali hiyo mapema, kila alichofanyiwa na Agness alikiona chema, walisoma pamoja, alipikiwa chakula, alinyooshewa nguo na hata kufuliwa nguo zake! Mambo yaliharibika zaidi Agness alipoomba kuwa anamchua mwili Danny, hilo pia Danny hakulitafsiri kwa upana wake akawa amekubali akifikiri ni huduma ya kawaida hatimaye akajikuta amenaswa kabisa, maisha bila Agness yakaanza kuonekana magumu, alionekana tiba ya huzuni yake.
Penzi lilianza taratibu kati yao, Agness akawa anaingia taratibu na kuzipa tundu lililoachwa na Nancy! Kidonda kikiaanza kupona moyoni, penzi likakomaa mpaka danny kuamua kumtambulisha Agness kwa mzee Katobe aliyemchukulia kama baba yake, bado hakuwa na mawasiliano na wazazi wake.
Mzee katobe hakuwa na kipingamizi, asingeweza kumzuia Danny asiwe na mpenzi au kuoa wakati hakuwa na uhakika mkubwa kama siku moja mwanae angerudi.
“Agness! Kuna kila dalili kuwa ninakupenda na ninafikiria kukufanya mke wangu baadaye! Lakini kuna kitu kimoja kinachonisumbua!”Danny alimwambia Agness wakiwa wamekaa wawili chumbani mwao, waliishi kama mke na mume ingawa walikuwa wanafunzi.
“Kitu gani Danny?”
“Nakumbuka nimewahi kukueleza habari za Nancy!”
“Ndio!”
“Kifo cha Nancy kilitokea lakini sikuwahi kuiona maiti yake, kuna wakati huwa nahisi anaweza kuwa anaishi mahali fulani na mimi ninampenda itakuwaje akirudi!”
“Kwani unafikiri anaweza kurudi?”
“Kwa sababu sikuiona maiti wala kaburi lake!”
“Akirudi basi mimi nitawaacha muendelee!”
“Kweli?”
“Ndio!”
“Ahidi!”
“Naahidi!”
“Mh!”Aliguna Danny.
“Kwanini unaguna?”
“Haiwezi kuwa rahisi kiasi hicho!”
“Huo ndio ukweli siwezi kuwatenganisha watu wanaopenda, unampenda Nancy kuliko mimi eh?” Agness aliuliza.
“Unajua....!”Danny hakuwa na jibu la swali hilo lakini ukweli uliokuwa moyoni mwake ulikuwa ni sehemu ya swali alilouliza Agness.
“Najua nini? Inabidi unithibitishie Danny!”
“Nakupenda Agness, tatizo ni hilo tu!” Nancy akirudi nitalazimika kuwa naye, hapo naomba nieleweke.
“Utanioa?”
“Wakati wowote ukitaka lakini uelewe kuwa Nancy akirudi....!”
“Hilo halina tatizo kwangu! Watu wakienda ahera huwa hawarudi, angekuwa hai lazima angeshajitokeza!”Agness alisema.
“Unataka tufunge ndoa lini?” Mzee katobe yupo tayari kusimamia ndoa yangu.
“Hata mwezi ujao!”
****
Penzi lilizidi kupamba moto, Danny alionekana kupata faraja! Hakulia tena kama ilivyokuwa zamani, kila siku zilivyozidi kwenda ndivyo penzi kati yake Agness lilivyozidi kukua na kufanya mipango ya ndoa ipelekwe kwa kasi ya sauti! Kila mtu alitaka kuwa na mwenzake milele na kifupi kila mtu aliamini walifaa kuwa mke na mume!
Walikuwa kivutio kila walikokwenda, wakitembea mkono kwa mkono bwana mbele na bibi nyuma kiasi cha wanafunzi wenzao kuwabadilisha jina kuwaita kumbikumbi!
Kila siku najaribu kufikiria siku ya ndoa yetu nashindwa kuelewa itakuwaje! Bila shaka itakuwa miongoni mwa harusi kubwa hapa jijini Dar es Salaam maana wanachanga isivyo kawaida na mzee Katobe amedhamiria kuonyesha mfano anataka kuwaonyesha watu kuwa bado yupo katika chati si unajua kuna watu walianza kusema eti amechoka, sasa ameamua kuonyesha uwezo wake kwenye harusi yetu!”
“Ndiyo!”
“Basi itakuwa bomba! Hata baba na mama yangu wamepania kweli ila waliniuliza swali moja!”
“Swali gani darling?”
“Juu ya wazazi wako! Eti ni kwanini usimalize tofauti iliyopo ili harusi yetu ipate baraka zote?”
“Mzee Katobe analishughulikia jambo hili, mambo yanakwenda vizuri kuna uwezekano baba na mama wakaja hapa nchini wakati wa harusi!”
Haya ndiyo yalikuwa maongezi kati ya Danny na Agness kila siku waliyokutana, walikuwa na njaa na hamu kubwa ya harusi ili waweze kuishi pamoja!
Kwa Agness aliona ndoa ndio kitu pekee alichoamini kingemfunga Danny hata kama siku moja Nancy angerudi kutoka katika wafu, aliuteka moyo wa Danny kisawasawa na kumsahaulisha kabisa kama duniani aliweza kuishi na mtu aliyeitwa Nancy, hakumpa nafasi ya kumfikiria.
Karibu kila mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikuwa na taarifa juu ya harusi hiyo, wengi walichanga na kumpongeza Agness kwa kumpata mvulana mgumu kupatikana kuliko mwingine yeyote chuoni. Danny hakuwa mwanaume wa kujirahisisha kwa wanawake! Alijiheshimu lakini wakati yeye aliwatesa waliomtamani naye pia aliteswa na mwanamke aliyeitwa Nancy! Historia hiyo haikuwa rahisi kufutika kichwani mwake.
Mgogoro kati yake na wazazi wake ulimalizika, wazazi wakaja nchini kuonana naye, Danny akapiga magoti na kuwaomba wazazi wake msamaha! Wakashikana mikono na kumaliza tofauti zao.
Hawakuwa na tatizo juu ya mipango ya harusi hasa walipomwona mkamwana wao, Agness aliwavutia sana, hasa mama yake Danny! Alifurahishwa na kila kitu alichokuwa Agness kuanzia maumbile hadi kuongea kwake.
“This is the girl fit to be your wife my dear son!”(Mwanangu mpendwa huyu ndiye mwanamke anayefaa kuwa mke wako!)
“I know mom!”(Nafahamu mama!)
“So you have decided to get married?(Kwa hiyo umeamua kuoa?
“Yes mom!”(Ndio mama)
“You have to remember one thing!”(Ukumbuke kitu kimoja!)
“Nini mama?”
“Never start something you can’t finish!”(Kamwe usianzishe kitu ambacho huwezi kukimaliza!”)Alishauri mama yake Danny katika maongezi yao yakiyofanyika faragha nyumbani kwa mzee Katobe huko Bagamoyo,walishamkubali mzee huyo kama sehemu ya familia yao.
“I agree, but thre is one thing!”(Nakubali, lakini kuna kimoja!)
“What is it?”(Nini hicho!)
“I’m not sure of Nancy’s death!”(Sina uhakika juu ya kifo cha Nancy)
Danny alimwambia mama yake na baadae kutumia karibu masaa mawili kueleza kila kitu kati na msichana huyo na jinsi yeye na mzee Katobe walivyohangaika kumtafuta Nancy na mama yake, alipofika mwisho wa maelezo hayo hapakuwa na neno jingine kutoka kwa wazazi wake zaidi ya kumuhakikishia kuwa si Nancy wala mama yake walikuwa hai na kutaka ndoa yake ifungwe haraka iwezekanavyo.
“Mzee Katobe mmepanga ndoa hii ifungwe lini?”
“Kwa ninavyofahamu kila kitu kinakwenda sawa na tulikuwa tunawasubiri nyinyi tu!”
“Inawezekana kufunga mwezi ujao?”
“Ni wangapi kweli?”Mzee Katobe aliuliza.
“Wa nne!”
“Tarehe ngapi?”
“Katikati ya mwezi baada ya Kwaresma,mfano tarehe kumi na saba mnaionaje?”
“Mimi sina matatizo labda mtoto!”
“Mimi na mwenzangu tunasubiri kauli yenu!”Aliongea Danny kwa sauti ya chini, moyoni mwake kulikuwa na furaha ambayo hakuwahi kuipata maishani, hakutegemea hata kidogo mambo yangekwenda kama yalivyokuwa yakiserereka, ndoa yake Agness ilikuwa hatua chache kutoka dakika hiyo! Kichwani mwake alianza kujiona akiwa baba wa familia, yeye na mke wake wakipenda na baadaye wanapata watoto ambao hakuelewa sura zao zingekuwa nzuri kiasi gani kama wangefanana na wazazi wao.
“Sisi tuna likizo ya mwezi mzima, tunaweza kubaki hapa mpaka harusi itakapofungwa! Tunakuomba mzee Katobe uendelee na mipango kama kawaida sisi tutasaidia kila utakapokwama, nafikiria tuna pesa ya kutosha.

Je Danny na Agnes wataweza kufunga ndoa?
Je mama Nancy ataweza kutoroka kisiwani na mtoto wake?

No comments