Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 24


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
“Sitaki lazima niondoke hawezi kumtesa mtoto wangu kiasi hiki, kila siku anamwingilia pamoja na kwamba ameshamsababishia uwendawazimu, huu ni unyama lazima nitoroke na nitaondoka kwa boya langu hilo hilo hata kama nitakufa mbele ya safari! Ni bora nikifa majini kuliko kuendelea kuteseka kiasi hiki!”
Hayo ndiyo yalikuwa mawazo ya mama Nancy karibu kila siku iliyokuja na kupita, hakukoma kutengeza boya lake mpaka aliporidhika limekaa vizuri zaidi na akabaki kusubiri siku ambayo angeweza kutoroka na watoto wake wote watatu lakini haikupatikana, siku zikazidi kusonga na mateso yakazidi kuongezeka.
Hali ya Nancy ilizidi kuwa mbaya, hakuweza tena kuongea chochote! Alishinda amelala asubuhi mpaka jioni, chakula acholishwa alikitapika na kuzidi kudhoofika zaidi, dalili kwamba angefia kisiwani zilizidi kuonekana wazi. Ni hapo ndipo mama Nancy alipoamua kuondoka mara moja bila kujali jambo lolote ambalo lingetokeza mbele ya safari, hofu yake kubwa ilikuwa ni mawimbi ziwani! Hakuwa na uhakika angeweza kufika upande wa pili lakini aliamua kujaribu.
Hakuelewa ilikuwa ni Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi ama Jumapili kwa sababu hapakuwa na kitu cha kumkumbusha! Nyakati za jioni mzee Kiwembe na babu Ayubu wakiwa ziwani kwa shughuli zao za uvuvi, alivunja mlango wa kibanda cha babu Ayubu na kuanza kakata kamba zilizomfunga mtoto wake kwenye nguzo, mikono ilikuwa imeharibiwa na vidonda vilivyotoa harufu vilivyosababishwa na msuguano kati ya kamba na mwili.
“Naondoka nikafie mbele kwa mbele!”Alisema mama Nancy akimbeba mtoto wake kutoka chini na kumweka begani na kuanza kukimbia naye kwenda upande wa pili wa kisiwa kulikokuwa na boya alilotengeneza.Alikuwa amedhamilia kuondoka hata kama angekufa mbele ya safari.
Alimlaza Nancy haraka juu ya boya hilo, hakuwa na uwezo hata wa kujigeuza akachukua kamba za magome ya miti na kumfunga kwenye boya akipitisha kamba tumboni, alikuwa amekonda mno mtu asingeweza kuamini kuwa yule alikuwa Nancy.
“Nikifika salama baba yake hataamini!”Aliwaza akikimbia tena kurudi kwenye kibanda cha mzee Kiwembe ambako aliwachukua watoto wake wawili na kuanza kukimbia nao kwenda ufukweni, alifanya kila kitu haraka ili mzee Kiwembe na babu Ayubu wasirudi na kumkuta katika pilika hizo, aliamini kuwa kifo ndiyo kingekuwa adhabu yake kwani mzee Kiwembe asingekubali mtu aondoke na watoto wake aliowapenda.
Baada ya kuwa yeye na watoto wake wamekaa vizuri juu ya boya lililotengenezwa kwa miti na lenye uwezo wa kuelea! Alirudi tena kwenye kibanda cha mzee Kiwembe na kuchukua samaki waliokaushwa ili wamsaidie yeye na watoto wake kama chakula njiani, akiwa na uhakika kila kitu kilikuwa sawa, kwa ushujaa kabisa alisukuma boya hadi majini na yeye kukaa juu yake.
Hakumsahau Mungu kwani aliamini bila muujiza asingeweza kufika upande wa pili, hapohapo alifumba macho na kuanza kusali sala ya baba yetu uliye mbinguni’akimuomba Mungu amnususru yeye na watoto wake! Alijisikia kama anamjaribu Mungu, kwani kifo kilionekana kuwa mbele yao na yeye alikuwa akifuata.
Alipofumbua macho tayari alikuwa akilia machozi, akanyoosha mkono wake na kuchukua kasia lilikuwa pembeni! Tayari safari ilikuwa imeiva, uzoefu wa kupiga kasia aliupata kutoka kwa mzee Kiwembe aliamini ungemsaidia kufika upande wa pili ambako hakuelewa kungekuwa Kigoma au Kongo na ingechukua siku ngapi, hakuwa na matumaini ya kuwa mzima katika muda wa siku tatu au nne lakini hiyo haikumvunja moyo.
Alianza kupiga kasia akiyakata maji taratibu alielewa wazi ilikuwa ni lazima awe mvumilivu kwani safari yake ilikuwa ndefu! Masaa manne baadae tayari giza lilishaingia, watoto wake wawili walikuwa wakilia kwa sababu ya baridi lakini Nancy alikuwa kimya kabisa kama aliyekuwa kwenye usingizi mzito! Aliwabembeleza huku akiendelea kupiga kasia kwenda mbele zaidi.
Hali ilikuwa ya giza kila upande, mama Nancy hakuweza hata kutambua ni upande gani alikuwa akielekea, alichoshukuru Mungu hali ya ziwa ilikuwa shwari kupita kiasi jambo lilimfanya kusonga kwake mbele kuwa rahisi zaidi, kwa mara moja hakukitambua lakini alipoangalia vizuri ingawa ilikuwa gizani aliweza kuona kitambaa cheupe na kuelewa kilichokuwa mbele yake lilikuwa jahazi likija kwa kasi kubwa.
Alijaribu kupiga kelele akiomba msaada lakini hakuna aliyemsikia, jahazi lilizidi kumsogelea na kuligonga boya lake! Yeye na watoto wake wakamwagwa majini, alijaribu kuwashika Catherine na David waliokuwa karibu naye na kuanza kuogelea nao akijaribu kutafuta boya ili awaokoe bila mafanikio.
“Nancy!Nancy!Nancy!”Aliita lakini hakuitikiwa na wala kumwona Nancy mahali popote kwa hali aliyokuwa nayo alikuwa na uhakika mwanawe amekufa maji, kwa mara ya pili alikuwa katika hatari za kuzama maji! Kumbukumbu za tukio la awali zilizopelekea yeye na Nancy kujikuta mokononi mwa mzee Kiwembe na babu Ayubu zilimwijia kichwani, alitamani kuokolewa lakini si na wazee hao wawili.
Alizidi kuogelea akimtafuta Nancy lakini hakuonekana, machozi yakamtoka na kumezwa na maji.
*****
Familia za pande zote mbili zilikubaliana juu ya ndoa kufungwa tarehe kumi na saba mwezi wa nne! Danny na Agness walifurahi kupita kiasi, mipango iliendelea kama ilivyopangwa na walibaki wakisubiri siku iliyokuwa umbali kama wa wiki tatu mbele yao kwa hamu kubwa.
Hatimaye siku ya siku ikafika, mamia ya watu wakakusanyika kanisa la Romani Katoliki Mantep huko Bagamoyo, wengi wao wakiwa wanafunzi wa chuo kikuu na watu mbalimbali maarufu jijini Dar es Salaam waliosafiri hadi Bagamoyo kushuhudia ndoa hiyo.
Kila kitu katika harusi hiyo kilifanyika kwa juhudi za mzee Katobe wazazi wa Danny hawakuamini! Ilikuwa ni zaidi ya hata undugu, mapenzi ya mzee Katobe kwa mtoto wao hayakuwa ya kawaida.
Kwa Danny na Agness ilikuwa ni siku ya ndoto yao kutimia! Mioyo yao ilijaa furaha, hapakuwa na kipingamizi tena na kilichokuwa mbele yao wakati huo ni familia, mafanikio na watoto! Ingawa mara chache Danny alikumbushia msimamo wake juu ya Nancy hapakuwa na matumaini tena kuwa msichana huyo angekuwa hai. Walisimama mbele ya Padri, meno yao yakiwa nje kwa tabasamu.
“Danny! Je umekubali kumpokea Agness awe mke wako? Katika shida, raha, magonjwa na kifo?” Padri aliuliza.
****
Wakati akihangaika kuogelea na watoto wake mara alishtukia kuona wanaume watatu wakitokea na kumnyang’anya watoto na mwingine aliyekuwa hajiwezi, alishtuka akifiri tayari alikuwa ameingia mikononi mwa mzee Kiwembe na babu Ayubu! Lakini alipowaangalia vizuri watu hao aligundua walikuwa ni vijana, jahazi alikuonekana kusimama lilikuwa limetia nanga.
“Waleteni! Waleteni!” Sauti nyingine ilisikika kutoa juu ya jahazi na hapo hapo zilianza kutupwa kamba watoto wote walianza kufungwa mmoja baada ya mwingine. Hata Nancy alikuwepo! Yeye ndiye akawa wa mwisho, alikuta vijana hao wakihangaika kumkamua Nancy maji tumboni, mmoja wao alimshika alimshika mkono na kwenda kumlaza pembeni.
“Pumzika!’
“Watoto wangu?”
“Wapo wanashughulikiwa!”
“Watapona?”
“Wawili tuna uhakika, lakini mmoja wao hali yake inasikitisha, amekunywa maji mengi! Hata hivyo bado wanamkamua!”
Baadaye alipopata nguvu alinyanyuka na kusonga mahali walipokuwa watoto, Nancy alikuwa bado taabani ingawa maji yalishaisha tumboni mwake! Alilala chini na kuanza kumpulizia pumzi mdomoni kama huduma ya kwanza hatimaye akaanza kuhema vizuri na matumaini yakarejea tena.
Aliwaeleza vijana hao kila kitu juu ya kilichomkuta katika ziwa Tanganyika, walimhurumia na kuamua kumsaidia! Alishukuru Mungu aliposikia walikuwa safarini kuelekea Kigoma, hali ya Nancy ilikuwa mbaya lakini bado alipumua na moyo wake ulikuwa ukidunda vizuri. Mama Nancy alipiga magoti chini na kubusu ardhi, hakuamini kama alikuwa huru tena.
“Sijui jinsi ya kuwashukuru! Mmeokoa maisha yangu na watoto wangu!” Alisema mama Nancy.
“Usijalia! Acha kwanza tuwapeleke hospitali!”
Hilo ndilo lilifanyika,mama Nancy na watoto wake wakapelekwa hospitali ya mkoa wa Kigoma ambako walilazwa na kuanza kupewa matibabu, Nancy alilazwa wodi ya wagonjwa mahututi na alifanyiwa vipimo aligundulika kuwa na Malaria sugu pamoja na homa ya matumbo.
Alianzishiwa matibabu, katika muda wa siku mbili akarejewa na nguvu zake kama kawaida lakini wendawazimu ukarudi pale pale! Hilo halikumsikitisha mama yake ili mradi mwanawe alikuwa hai, wasamalia waliwanunulia nguo nzuri na mpango wa usafiri kurejea Dar es salaam baadaye ulifanywa.
Je nini kitaendelea?
Je Nancy na mama yake wataweza kurudi Dar salama?
Je harusi itaweza kufungwa?

No comments