Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 25


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Walishuka Bagamoyo saa tisa za alasiri siku ya Jumamosi tarehe kumi na saba mwezi wa nne, watu waliowaona waliwakimbia, hakuna aliyetaka kuongea nao wakiamini walikuwa ni misukule! Hali walizokuwa nazo zilitisha, isitoshe kila mtu wakati huo aliamini walikuwa ni marehemu.
Walinyoosha hadi nyumbani kwao na kukuta nyumba ikiwa imefungwa na hapakuwa na mtu yoyote, majirani jasiri waliwafuata wakitaka kufahamu kama kweli walikuwa ni wao! Mama Nancy alisimulia kila kitu kilichotokea, watu waliangua kilio na wao hawakumficha juu ya kilichokuwa kinaendelea kanisani. Bila kuchelewa gari lilikodishwa, mama Nancy na watoto wake wakapakiwa ndani na safari ya kwenda kanisani ikaanza! Lengo ikiwa ni kuzuia harusi ya Danny na Agness kwa sababu Nancy alikuwa amepatikana.
Gari liliegeshwa mbele ya kanisa, Nancy akionekana mwendawazimu kabisa na mama yake akiwa amechoka, walisaidiwa kushuka na kisha kuongozwa kuingia kanisani! Watu wote walipowaona walianza kupiga kelele wakikimbia kwenda nje, kilikuwa ni kitu cha kutisha! Maneno misukule yalisikika kila upande ndani ya kanisa.
Mama Nancy na watoto wake wakiongozwa na majirani hawakujua kilichokuwa kikiendelea! Walizidi kusonga mbele kwenda Altareni ambako pia watu walionekana kushutushwa na kilichokuwa kimetokea.
“Nini?”Padri aliuliza.
Watu walioaminika kufa maji katika ziwa Tanganyika wanaibuka kutoka Kisiwa cha Galu walikokuwa wamefichwa, ni mama Nancy, mke wa mzee Katobe pomoja na Nancy, binti wa familia hii ambaye pia ni kipenzi wa kijana aitwaye Danny.
Danny na mzee Katobe waliwatafuta sana watu hawa bila mafanikio, hatimaye kukata tamaa na kulazima kuendelea na maisha yao! Tayari Danny ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alishakutana na msichana mwingine aitwaye Agness huyu pia ni mwanafunzi chuo kikuu na leo hii wapo ndani ya kanisa wakifungishwa ndoa.
Ndoa hii imewezekana tu kwa sababu Danny anaamini Nancy ni marehemu ingawa hakuiona maiti yake, vinginevyo asingemwoa Agness na jambo hili alishaliweka wazi kwake kuwa akitokea Nancy akarejea basi atalazimika kumwacha Agness na kuwa naye.
Leo hii wakiwa ndani ya kanisa baada ya padri kumuuliza tu Danny kama alikuwa tayari kumwoa Agness kelele zinasikika nyuma yao, wanageuka na kukuta watu wanakimbia huku na kule wakipiga kelele na kusema “Misukule imeingia kanisani”
Danny na watu wengine walioko madhabahuni pamoja na padri wanapigwa na butwaa kuwaona wanawake wawili, mmoja akiwa mwendawazimu kamili wanaingia kanisani wakiwa wameongozana na watoto wawili na kundi kubwa la watu.
Je, nini kitatokea ndani ya kanisa?
Ndoa itafungwa?
SONGA NAYO
Padri, wazazi wa Dany nao walishindwa kuvumilia na kujikuta wakikimbia kutoka madhabahuni kwa woga, picha ya watu waliokuwa wakija mbele yao hasa wawili kati ya wote, mmoja akiwa amebeba watoto wawili walionekana kuwa wagonjwa iliwashtua.
Watu watatu tu walibaki mbele ya madhabahu, Danny, Agness na mzee Katobe wakiangalia picha iliyokuwa ikiendelea kwa mshangao, hakuna mtu kati yao akina nani walikuwa wakitembea kuelekea mahali walipokuwa wamesimama.
Walifika na kusimama na mama Nancy kuweka watoto wote chini kisha kumsogelea mzee Katobe aliyekuwa wima bila kuelewa nini kilikuwa kikiendelea, hali ya mama Nancy ilishaharibika hakuwa mwanamke yuleyule ambaye mzee katobe alimwona mara ya mwisho! Alikuwa na nywele ndefu sana zilizojisokota pia rangi yake ya ngozi ilikuwa nyeusi kuliko alivyoondoka.
“Katobe!” Alimwita mume wake.
“Ndiyo! wewe nani?”
“Niangalie vizuri usoni utanitambua!”
Mzee Katobe alikaza macho yake na kuyaelekeza usoni kwa mwanamke aliyesimama mbele yake, picha ilimwijia na kugundua alikuwa mke wake lakini badala ya kusimama kumsogelea alianza kukimbia kwenda nje ya kanisa, hakuwa tayari kuamini kuwa yule alikuwa mke wake kweli.
“Tafadhali rudi! Mimi ni mkeo, usiogope nitakueleza kila kitu!”
“Mzee Katobe rudi usikilize, sisi ndio tumemleta huyu si msukule ni mkeo halisi amerudi!”mmoja wa majirani wa mzee Katobe alisema huku akimkimbia hadi kumfikia na kumshika mkono kisha kuanza kurudi naye hadi madhabahuni ambako alimkuta mke wake akiwa amesimama mahali alipomwacha machozi yakimtoka, aliyakaza tena macho yake kumwangalia na kwa unyonge huku akiogopa alimsogelea.
Shughuli ya harusi ilishakoma kabisa ingawa baadhi ya watu waliokimbia nje walianza kuingia tena kanisani, hata padri na wazazi wa Danny walianza kujisogeza.
“Ni wewe?”Mzee Katobe alimuuliza.
“Ndiyo, kwanini huamini?” Mama Nancy aliuliza.
“Ulikufa maji!”
“Si kufa! Nilikuwa hai mahali fulani nikipata mateso!”Aliongea mama Nancy akilia.
“Kweli?”
“Nilikuwa kisiwani Galu!”
“Wapi?”
“Katika ziwa Tanganyika!”
“Haiwezekani! Tulivitembelea visiwa vyote tukikutafuta wewe na mwanangu Nancy! Kwanza yuko wapi? Nikimwona yeye naweza kuamini maneno yako!”
“Yule pale! Alijibu mama Nancy akisonta kidogo kuelekeza mahali alipokaa Nancy akiwa ameinamisha kichwa chake nywele zake ndefu na chafu zilizojisokota ziliufunika uso wake, mwili wake ulikuwa umekonda mno isingewezekana kwa mzee Katobe kuamini kuwa binti yake mrembo ndiye amekuwa mwendawazimu aliyekuwa amekaa chini mbele yake.
“Unanidanganya huyo sio Nancy, namfahamu vizuri mwanangu! Alikuwa na afya njema na sura ya kuvutia hawezi kuwa huyo mwendawazimu!”
“Tafadhali nakusihi usogee na umfunue hizo nywele!’
Tayari watu walishazunguka madhabahu wakishangaa kilichokuwa kikiendelea, haikuwa harusi tena huzuni kama za msiba zilitawala ndani ya kanisa, watu waliokuwa na furaha walikuwa wamebadilika na kuwa wanyonge kupita kiasi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Danny pia, hakuamini mambo aliyokuwa akiyaona.
Mzee Katobe alitembea taratibu hadi mahali alipokuwa amekaa Nancy na kuchuchumaa kisha kukinyanyua kichwa cha binti aliyedaiwa kuwa wake ingawa yeye alimwona mwendawazimu! Macho yake yalithibitisha kuwa alichoambiwa kilikuwa ni kweli! hakuyaamuru machozi yake yatoke bali alishtukia mashavu yake yakilowa.
“Kweli ni mwanangu! Nini kiliwapata? Sogea karibu yangu mke wangu, tupige magoti tumwombe Mungu na kumshukuru kwa kuwarudisha salama!” Aliongea kwa huzuni mzee katobe na mama Nancy alisogea na kufanya kama alivyoelezwa, wote wakaanza kusali wakiwa wamemkumbatia Nancy. Kila mmoja wao alikuwa akilia kwa uchungu, hakika ilikuwa siku ya huzuni kuliko siku nyingine zote maishani mwao.
“Siamini!”
“Kwanini!”
“Kama kweli mmerudi, kila mtu alielewa mlishakufa!”
“Hapana tulikuwa hai katika mateso makubwa!”
“Na hawa watoto ni wa nani?”
Mama Nancy aliangua kilio, hakuwa na maneno ya kutosha kuwaelezea vizuri watoto aliowazaa na mzee Kiwembe bila ridhaa yake, hakutegemea kupewa msamaha wa aina yoyote ingawa siku zote alijiona si mwenye hatia na aliwapenda sana watoto wake.
“Nakuuliza hawa watoto ni wa nani?”
“Nitakueleza baadaye lakini naomba uniahidi msamaha!”Aliongea mama Nancy kwa huzuni kubwa huku akijifuta machozi.
Danny alikuwa amesimama pembeni, mwili wake ukiwa umepigwa na ganzi! Maongezi yote yaliyofanyika kati ya mzee Katobe na mkewe aliyasikia vizuri na hata uso wa Nancy uliponyanyuliwa aliuona na kumtambua!
Kitu kama sinema kiliendelea kichwani mwake na kujikuta akirudishwa moja kwa moja hadi chuo kikuu siku aliyokutana kwa mara ya kwanza na Nancy na kumpenda, bado ubongo wake uliukumbuka uzuri wa Nancy bila kutegemea yeye pia alijikuta akitokwa na machozi ya uchungu.
Alijikuta akitamani kumsogelea Nancy lakini hakuweza kufanya hivyo, mkono wake wa kushoto ulikuwa umekamatwa vizuri na Agness aliyeonakana kukerwa na kilichokuwa kikiendelea.
“Niachie!”
“Uende wapi?”
“Nataka nikamsalimie Nancy!”
“Huyo mwendawazimu?”
“Sijali yukoje, lakini nataka kumsalimia!”
“Hakuna!” Agness alikataa.
“Unakumbuka maneno niliyoongea na wewe kabla hatujaingia katika mapenzi yetu?”
“Maneno gani?”
“Usijifanye kusahau! Nilikueleza kabisa kuwa kama siku moja Nancy angerudi, lazima ingelazimika kuwa naye! Na sasa amerejea kwanini unanizuia kwenda kumsalimia?
“Lazima uelewe kitu kimoja Danny!”
“Kitu gani?”
“Tumekuja hapa kufunga ndoa!”
“Imekwishafungwa?”
“Bado lakini muda ndio huu!”
Tayari padri alishafika madhabahuni na kuwaomba watu waketi kwenye viti ili aendelee na shughuli iliyowakusanya ndani ya kansia, hakuelewa kabisa kilichokuwa kikiendelea kati ya mzee katobe na wanawake wachafu waliokuwemo ndani ya kanisa.
“Mzee Katobe!” Mzee katobe! naomba usogee hapa tuongee kidogo! Padri aliita na mzee katobe alijiondoa mikononi mwa mkewe aliyekuwa bado wamekumbatiana na kuanza kutembea kuelekea madhabahuni ambako aliungana na padri pamoja na wazazi wa Danny kwenda pembeni kuteta, hakuficha kitu katika maelezo yake! KIla kitu kiliwekwa bayana juu ya mke na mtoto wake walioaminika kufa maji!
“Kwa hiyo wamerudi?”
“Ndiyo! yaani siamini siku zote nilijua familia yangu ilishatangulia ahera!’
“Sasa tuendelee kufungisha ndoa au? Unataka uwapeleke nyumbani kwanza maana wakiwa hapa kanisa haliwezi kutulia!”
“Mtu wa muhimu sana katika ndoa hii hivi sasa ni Danny yeye ndiye mwenye uamuzi!” Aliongea mzee katobe bila padri kuelewa nini ilikuwa maana yake.
“Kwani kuna nini?”
“Kuna jambo kati ya yule binti yangu na bwana harusi mtarajiwa!”
“Jambo gani?” Padri aliuliza.
“Mnahitaji kuongea naye mwenyewe!”
Wakati hayo yakiendelea madhabahuni Danny alikuwa bado ameng’ang’aniwa mkono wake na Agness kiasi cha kushindwa kujiondoa na kwenda kumsalimia Nancy! Pamoja na kuwa mwendawazimu bado mapenzi yake kwa msichana huyo yalikuwa palepale hakuwa na taarifa ni nini kilichomfanya msichana huyo aliyewahi kuwa mrembo kufikia hali iliyokuwa nayo.
“Danny! Hebu sogea hapa kidogo!”Padri aliita.
“Amening’ang’ania hataki kuniachia!”
“Nani?”
“Huyu Agness!”
Ilibidi wazazi pamoja na padri wasogee hadi mahali waliposimama Danny na Agness wakiwa wameng’ang’aniana na kuanza kumuuliza Danny maswali juu ya kama shughuli ya ndoa ilikuwa inaendelea toka ilipoishia au la! Danny hakujibu kitu chochote, alibaki kimya huku macho yake yakiwa yamemwangalia Nancy aliyekuwa amejikunja chini, alionekana kutoelewa hata kitu kimoja kilichoendelea.
“Danny Padri anakuuliza!”
“Baba! Sipendi kuwaudhi nyinyi wala mtu yeyote, nafikiri niliwahi kuwaeleza vizuri juu ya msichana aliyekaa pale chini, anaitwa Nancy, nilimpenda na ndiye niliyetaka awe mke wangu lakini bahati mbaya akapotea na nikaamini alikufa! Kumbe yupo hai na kama amerudi sioni tatizo kuwa naye tena, ili mradi amefika mapema kabla sijavaa pete ya ndoa!”
“Kwahiyo ina maana hutaki kumwoa tena Agness?”
“Hilo ndilo jibu na hata yeye anaelewa, niliwahi kumweleza huko nyuma kuwa kama Nancy angerudi ingelazimu mimi na yeye tuachane!”
“Haweizekani wala usijidanganye, unapoteza muda wako Danny! Huwezi kuniacha dakika za mwisho kiasi hiki, aibu hii nitaificha wapi?”
“Hata mimi nakuunga mkono binti, mwanangu hawezi kuoa au kuishi na mwanamke mwendawazimu! Itakuwa ni aibu kubwa mno!” Mama yake Danny aliongea.
“Hata mimi nipo upande wa mke wangu!” Baba yake Danny aliongeza, mzee katobe alikuwa kimya muda wote wala hakufungua mdomo wake, macho yake yalikuwa yameelekezwa kwa watoto waliokuja na mama Nancy, mzee huyo alionekana kuwa mwenye maswali mengi yasiyokuwa na majibu.
Danny alibaki kimya akiwashangaa wazazi wake kwa uamuzi waliotaka kuufikia, alijikuta njia panda! Hakupenda kuonekana mtoto asiyekuwa na nidhamu lakini pia alitaka apewe uhuru wa kuchagua akiamini kabisa maisha yake ya baadaye yalikuwa yake peke yake na hivyo alihitaji mwanamke ambaye angeiridhisha roho yake na kumletea furaha hata kama angekuwa mwendawazimu.
Alimpenda Nancy na alitaka kuwa naye, huyo ndiye alikuwa chaguo lake si Agness aliyekuja katika kipindi cha upweke, hakumchukia kwa lolote kwani alimsaidia sana kuutuliza moyo wake lakini kwa sababu Nancy alikuwa amerejea ilikuwa ni lazima amwache na kwenda kwa chaguo lake.
Alitumia nguvu nyingi na kujiondoa mikononi mwa Agness kisha kukimbia mpaka mahali alipokuwa amekaa Nancy, akakinyanyua kichwa chake na kumbusu usoni! Watu wote ndani ya kanisa walishangaa lakini kuna wengine walipiga makofi na kushangilia.
Akiwa bado katika hali hiyo bila kujua nini kilikuwa kikifuata, alishtukia kiti cha kanisani kikitua kichwani kwa Nancy! Damu zikaruka, alikuwa Agness akitetemeka kwa hasira, machozi yakimtoka kwa wingi. Nancy hakulia wala hakulalamika alichofanya ni kulala chali sakafuni!
“Agness umefanya nini tena?” Danny alipiga kelele.
Kulikuwa na dalili zote kuwa ndoa ilishashindikana, Nancy alikuwa amelala chini akivuja damu na Danny alikuwa akimfokkea Agness kwa kitendo huku watu wengine akiwemo mzee Katobe pamoja na majirani wakimbeba Nancy kumpeleka nje ya kanisa ambako alipakiwa garini na safari ya hospitali ikaanza.
****
Mama Nancy alibaki kanisani akiwa na watoto wake Catherine na David mikononi mwake, akishuhudia ugomvi mkubwa uliokuwa ukiendelea kati ya Danny na Agness kelele zilizidi kupanda ndani ya kanisa hata padri alijaribu kuwanyamazisha watu haikuwezekana! Ilikuwa ni aibu kwa Agness na wazazi wake, alifunika uso wake akilia.
“Danny”Padri alimwita.
“Naam Padri.”
“Msimamo wako ni upi?”
“Kuhusu nini Padri?”
“Kuhusu ndoa.”
Haiwekani tena hata kama Nancy ni mwendawazimu na nilimwambia Agnes jambo hili toka awali kwa kuwa amerudi akiwa hai ni lazima niwe naye!
“Kwa hiyo hakuna ndoa tena?”
“Kweli kabisa!”
Danny aliongea kwa kujiamini, hakuwaogopa hata wazazi wake, alikuwa amedhamilia kufanya alichokitamka! Ulikuwa ni uamuzi wake kuchagua amuoe nani hata kama baba na mama yake walitaka amuoe Agness lakini yeye alimpenda Nancy na alitaka awe nae maishani.
“Danny umemuona lakini huyo Nancy alivyo?”
“Ndio mama”
“Kwa hiyo utakuwa nae hivyo!”
“ Kweli kabisa”
“K wa nini usimuoe Agness kwa sababu mmeshafikia hatua nzuri?”
“Haiwezekani mama, nakuheshimu sana sana lakini kwa jambo hili naomba uniachie mwenyewe niamue!”Alijibu Danny akimuangalia Agness aliyekuwa pembeni akimwaga machozi, hakuwa na kitu kingine cha kusubiri kanisani alitaka kuelewa ni kitu gani kmimempata Nancy huko alikokuwa amepelekwa,bila hata kuuliza alikuwa na uhakika asilimia kubwa kuwa Nancy alipelekwa hospitali ingawa hakuelewa hospitali gani.
Alitoka akikimbia kwa kasi nje na kuingia ndani ya gari lililokodishwa kwa ajili yake na bibi harusi na kumwamuru dereva aliondoe haraka iwezekanavyo kuwafuata watu waliondoka na gari la mwanzo wazo la harusi tayari lishafutika hakuna alichokiwaza wakatim huo zaidi ya Nancy.
‘’Unafikiri wameelekea hospitali gani?”Aliuliza.
“Hakuna hospitali nyingine wanayoweza kuwa wamekwenda zaidi ya hospitali ya Wilaya”
“Twende huku huko basi”
Dereva aliondoa gari kwa mwendo uliotakiwa na Danny, akibadilisha gia hadi namba nne ingawa walipita katika njia yenye mabonde mengi, dakika na tano baadaye walifika hospitali na kuegesha gari lao. Danny akashuka na kukimbia hadi mapokezi akiwa ndani ya suti yake ya nyeusi. Alipowauliza wafanyakazi wa mapokezi kama walikuwa wamepokea mgonjwa aliyejeruhiwa kichwani, walionyesha mshangao na hatimaye baada ya kusoma ndani ya daftari la wagonjwa walimwambia hapakuwa na mgonjwa wa aina hiyo aliyepokelewa.
“Kwa hiyo yuko wapi?Kuna hospitali gani nyingine kubwa hapa Bagamoyo?
“Nendeni mkajaribu kumwangalia hospitali ya kanisa la Mennonite, ni mpya umejengwa hivi karibuni watu wengi wanakimbilia huko sababu hapa hatuna dawa!.
“Ahsante!”Alijibu Danny na kurudi tena mbio zile zile hadi kwenye gari,alipompa dereva taarifa mara moja alionekana kuielew hospitali hiyo na wakaondoka wakipandisha mlima hadi mahali hospitali ya Mennonite ilipokuwa,kabla hata ya kufika waliliona gari lililopambwa vizuri likiwa nje wakawa na uhakika hapo ndipo Nancy alipopelekwa.
Walishuka na kuingia ndani ambako walimkuta mzee Katobe pamoja na watu wengine wawili wakisubiri,Danny alianza kwa kuomba msamaha kwa yote yaliyotokea kisha akaketi pamoja nao kusubiri mgonjwa arudi kutoa katika chumba cha upasuaji alipokuwa amekwenda kushonwa!
“Vipi huko kanisani?”Mzee Katobe aliuliza.
“Ndoa imeshindikana!”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu ya Nancy!”
“Lakini ni kwa nini usingemuoa Agness? Si umemuona mwanangu alivyo?”
“Hapana baba!Nampenda sana Nancy nipo tayari kuwa naye katika hali hiyo hiyo aliyonayo wakati nikimtafutia tiba mpaka apone kwani hakuna kisichowezekana!”
Je nini kitaendelea?

No comments