Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 26


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Saa nzima baadae Nancy alitolewa chumba cha upasuaji akiwa amenyolewa nywele zote kichwani na kushonwa nyuzi kumi na nne sehemu aliyopasuka, badala ya kuruhusiwa kwenda nyumbani ilibidi apewe kitanda kwa sababu mwili wake ulionekana kuwa dhaifu! Wote walikubaliana na Danny akaamua kubaki na mgonjwa wote wakaondoka, mzee Katobe alirejea tena saa kumi mbili jioni akiongozana na wazazi wa Danny na mama Nancy akiwa na watoto wake! Hakuna aliongelea suala la ndoa tena,wote walijifanya hawakumbuki yaliyotokea mchana ingawa ni kweli yalikuwemo vichwani mwao.
“Vipi hali ya mgonjwa?”Baba yake Danny aliuliza.
“Anaendelea vizuri ila hana kumbukumbu kabisa! Sijui itakuwaje?”
“Hivyo ndivyo ilivyo! Si umechagua mwenyewe bwana ukikoroga ni lazima ulinywe!” Baba yake alimwambia akitabasamu.
Hawakukaa sana wodini, masaa mawili baadae waliaga na kuondoka kurejea nyumbani kwa mzee Katobe ambako pia wazazi wa Danny walifika, hapakuwa na maongezi sana,baada tu ya chakula cha usiku kilichopikwa na mama Nancy akiwa nyumbani kwake tena, waliingia chumbani kulala,mzee Katobe na mke wake walitumia usiku huo kuongea juu ya kilichotokea, mama Nancy alieleza kila kitu akifafanua vizuri juu ya watoto aliokuwa nao! Mzee Katobe hakuweza kuyazuiya machozi, badala ya kuchukia alilia kama mtoto mdogo huku mke wake akimbembeleza.
“Nimekusamehe mke wangu, najua usingeweza kufanya jambo hili kwa makusudi naelewa ni kiasi gani unanipenda na kiasi gani wewe ni mwaminifu!Ulikuwa mateka na ndio maana ukajamiiana na mtu mwingine hatimaye kupata watoto hawa! Hawana hatia yoyote,sina sababu ya kuwachukia!” aliongea mzee Katobe.
Hawakulala mpaka saa kumi na mbili asubuhi waliponyanyuka na kujiandaa kwenda hospitali, mama na Nancy alitayarisha kifungua kinywa na ilipotimia saa moja na nusu ya asubuhi mzee Katobe aliondoka na wageni wao hadi hospitali ambako walikuta hali ya mgonjwa ni ile ile, hapakuwa na mabadiliko yoyote upande wa akili ingawa kidonda chake kinandelea vizuri na kulikuwa na dalili kuwa siku hiyo angeruhusiwa na kuondoka.
Lakini hivyo sivyo ilivyotokea kwani wakati wa raundi madaktari walishauri Nancy ahamishiwe wodi ya wagonjwa wa vichaa na haikuwa katika hospitali hiyo, ilibidi ahamishwe na kupelekwa katika hospitali ya wilaya ambako kulikuwa na wodi ya aina hiyo! Nancy akawa maewekwa kwenye madawa makali ya akili, Danny hakurusiwa kukaa wodini ingawa aliomba jambo hilo lifanyike, alisikitika wakati akiondoka hospitali kurudi nyumbani! Hakuwa na kumbukumbu tena juu ya Agness na hakuelewa hata mahali alipokuwa kipindi hicho.
Siku chache baadaye wazazi wa Danny waliondoka kurejea Canada wakiwa wamesikitishwa na kitendo kilichofanywa na mtoto wao. Nancy aliendelea kulazwa wodini karibu mwezi mzima akipatiwa matibabu ya vichaa lakini hayakumsaidia chochote bado aliendelea na hali yake ya wendawazimu mzee Katobe akashauriwa na marafiki zake kumwondoa hospitali na kumpeleka kwa wataalam wa tiba za jadi.
Kwa sababu alitaka mtoto wake apone, mzee Katobe hakuwa na chaguo lingine, alikubali kila kitu alichoambiwa na kumsafirisha mwanawe akiwa na Danny aliyesitisha masomo yake kwa mara nyingine hadi sehemu za Lushoto mkoani Tanga ambako alitibiwa na mganga wa kienyeji kwa muda wa miezi mitatu bila mafanikio na kuhamishwa tena kwenda kwa mganga mwingine, walizunguka nae sehemu nyingi sana mkoani humo bila mafanikio! Si Danny wala mzee Katobe aliyekuwa tayari kukata tamaa.
“Huyu mpaka mkutane na mganga yule yule aliyemrisha yamini! Vinginevyo hatafunguka, hatokufa mwendawazimu, kwani yuko wapi huyo mganga?”Mganga mmoja maarufu mjini Tanga aliwauliza walipokwenda kwake na kumsimulia historia ya mgonjwa.
“Alikuwa Bagamoyo huko Pwani lakini baadae alihamia Zaire!”
“Nakushauri uende kumtafuta huyo mganga kwanza! Ni kazi ndogo sana akipatikana, yeye anafahamu ni kitabu gani alisoma na akikisoma tena kwa lengo la kumfungua atafunguka! Vinginevyo mtapoteza fedha nyingi na bado mtoto wenu hatapona!”
Maneno hayo yaliwaingia sana akilini na kufikia uamuzi wa Danny kuondoka kwenda Zaire kumtafuta mzeeMwinyimkuu, alirudi Bagamoyo na kupata maelezo ya kutosha kutoka kwa mama yake Nancy juu ya mahali mzee huyo alipoishi nchini Zaire.
“Kabla hajapata tatizo alilonalo, Nancy aliwahi kunitajia kuwa sehemu aliyoishi mzee Mwinyimkuu ni Kalemi!Hivyo ukifika hapo anza kumuulizia”.
“Sawa mama!Nitajaribu kumtafuta kwa nguvu zangu zote.”
Danny hakuwa na chaguo lingine zaidi ya kupewa fedha na kuiacha Bagamoyo hadi Dar es Salaam ambako alipanda treni iliyomfikisha Kigoma baada ya siku tatu na kuvuka ziwa Tanganyika kwa meli hadi upande wa pili nchini Zaire, kazi yake ilikuwa moja tu kumtafuta mtu aliyekuwa na siri ya tatizo la Nancy! Alisafiri hadi Kalemi lakini hakufanikiwa kumpata mzee Mwinyimkuu, watu walimfahamu sana katika eneo hilo lakini walimpa taarifa kuwa alihamia Kinshasa miezi michache kabla.
“Anatumia jina tu?”
“Ndivyo!Na ni mganga maarufu sana utampata tu,anafanya kazi zake sehemu ya stendi kuu ya Kinshasa! Wala usihangaike kuwauliza sana, ofisini kwake kuna bango kubwa lililoandikwa Africana Medicine”
“Ahsante sana”
Danny hakutaka kupumzika asingeweza kufanya hivyo kabla ya kumpata mzee Mwinyimkuu, siku hiyo hiyo alisafiri hadi Kinshasa kwa ndege, bahati mbaya aliingia usiku hakuweza kamtafuta lakini hata muhudumu wa hoteli aliyofikia alilitambua jina la mzee Mwinyimkuu aliyesifika sana kwa dawa za biashara na kuzindika nyumba za watu, alidaiwa kuwa mganga kutoka Tanzania.
Furaha aliyolala nayo siku hiyo ilikuwa kubwa mno na asubuhi kitu cha kwanza kilikuwa ni kwenda stendi ya mabasi alikoelekezwa, bango la Africana Medicine lilionekana wazi juu nyumba kubwa iliyotazamana na stendi, Danny akajua mwisho wa safari yakea ulikuwa umefika, kumpata mzee Mwinyimkuu kulimaanisha kupona kwa Nancy na hatimaye ndoa yake na mwanamke aliyempenda kufanyika.
Aliingia ndani ya nyumba hiyo na kushangazwa na uzuri uliokuwepo, ilikuwa nyumba nzuri iliyopambwa kwa tarazo za kung’aa na kila kitu ndani kilikuwa vioo! Haikuwa rahisi kuamini eti hiyo ilikuwa ofisi ya mganga wa jadi! Msichana mrembo alikaaa nyuma ya kompyuta akichapa vitu fulani fulani, kichwani mwake Danny alihisi maelezo aliyopewa hayakuwa sahihi.
“Habari za leo dada?”
“Nzuri tu kaka nikusaidie?”
“Ndio!Mimi ni mgeni wa mzee Mwinyimkuu sijui hapa ndio ofisisni kwake?”
“Ni hapa ndio!”
“Nimemkuta?”
“Hapana!”
“Yupo wapi?”
“Bahati mbaya sana juzi alipatwa na ajali wakati akitoka hapa kwenda nyumbani kwake, hivi sasa ninavyoongea na wewe yupo chumba cha wagonjwa mahututi cha hospitali ya Mulubwanzi!Hali yake ni mbaya mno,hana fahamu na hawezi kuongea lolote!”
“Unasema kweli?”
“Ndio kaka!”
”Mungu wangu! Nitafanya nini mimi?”
“Kwani kuna nini kaka?”
Danny alisimulia kila kitu kilichotea na kilichofanya yeye kusafiri hadi Zaire, msichana huyo alisikitika sana na kuendelea kusisitiza kuwa jambo ambalo Danny lifanyike lisingewezekana bila mzee Mwinyimkuu kurejewa na fahamu zake kwani hapakuwa na mtu mwingine kwenye kitu hicho aliyekuwa na uwezo wa kusoma vitabu vyake vya uganga.
“Sasa nitafanya nini?”
“Kwa kweli sijui inabidi mimi na wewe tumuombe Mungu amnusuru mzee Mwinyimkuu na kifo!Tofauti na hapo hakuna kinachoweza kufanyika mchumba wako aweze kupona lakini ungemkuta ninakuhakikishia lazima angekuwa tayari kukusaidia”.
“Unaweza kunipeleka hospitalini nikamwone?”
“Hakuna tatizo!”
Msichana huyo ambaye katika mazungumzo yao Danny alifanikiwa kumfahamu kwa jina la Aminata, alikubali kufunga ofisi na wote kwa kutumia gari lake waliongozana hadi hospitali ya Mulubwanzi kumwona mzee Mwinyimkuu, ni kweli alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi! Kichwa chake kikiwa kimefungwa bendeji nyingi, huku mashine za oksjeni zikiwa mdomoni mwake, kwa hali aliyokuwa nayo hapakuwa na matumaini ya kupona.
“Jamani kwa nini mimi nina bahati mbaya? Kwa nini nimempata mzee Mwinyimkuu akiwa katika hali hii? Aliwaza Danny huku machozi yakimlengalenga.
Je nini kitaendelea?
Je wataweza kumuona mzee Mwinyimkuu?
Je ataweza kumrudisha Nancy katika hali yake?

No comments