Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 27


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Ni mtu mmoja tu aliyehitajika kuokoa maisha ya Nancy, huyo hakuwa mwingine bali mzee Mwinyimkuu, ni yeye ndiye aliyemlisha Nancy Yamini! juhudi za mwanzo kumpata zilizofanywa na Nancy na mama yake zilishindikana lakini Danny alifanikiwa kufika hadi Kinshasa, kuiona zahanati ya tiba za jadi iliyomilikiwa na mzee huyo aliyekuwa maarufu sana katika jiji hilo.
Dany alilia machozi ya uchungu baada ya kupewa taarifa juu ya ajali mbaya iliyompata mzee Mwinyimkuu, kwake ulikuwa ni mkosi na balaa kubwa! Alishindwa kuelewa ni kwanini ajali ilitokea wakati huo na siku nyingi kabla!
“Ng’ombe wa masikini hazai!” Aliwaza Danny akimwangalia mzee Mwinyimkuu aliyelala kitandani kichwa chake kikiwa kimefungwa na bendeji nyingi.
Nyuma ya Danny alikuwepo Aminata, msichana aliyefanya kazi katika zahanati ya mzee Mwinyimkuu yeye pia uso wake ulijawa na huzuni kubwa! Alikuwa haamini kilichokuwa mbele yake, alimhitaji sana mzee Mwinyimkuu katika shughuli zake kama yeye angekufa basi hata zanahati yao ingekuwa imefikia mwisho na maisha ya Aminata yangekuwa magumu kupita kiasi tangu siku hiyo.
Daktari alipoingia alimkuta Dany akijifuta machozi na hivyo ndivyo alivyofanya Aminata! Daktari aliwahurumia sana kiasi kwamba alipomaliza tu kumpima mzee Mwinyimkuu akaanza kuongea nao juu ya hali ya mgonjwa.
“Hali ya mgonjwa sio nzuri! Ajali aliyoipata imeharibu ubongo wake, kichwa chake kilijipigiza kwenye chuma, damu imevuja chini ya kichwa! Tunategemea kumfanyia upasuaji baada ya mapigo yake ya moyo yakikaa vizuri ili kujaribu kuondoa damu iliyoganda!”Daktari aliongea akiwaangalia Danny na Aminata usoni.
“Atapona?”
“Siwezi kusema sana kwani hali yake haileti matumaini makubwa, lakini hata kama atapona kuna uwezekano mkubwa sana wa kupoteza kumbukumbu zake zote za nyuma na sehemu yake ya mwili kupooza!’
Jibu la daktari lilimshtua sana Danny pengine kuliko lilivyofanya kwa Aminata, hakuna kitu alichohitaji kutokwa ka mzee Mwinyimkuu kama kumkumbuka Nancy na mambo aliyomfanyia, kwake haikuwa na maana yoyote kama mzee huyo angepona lakini asiweze kukumbuka yaliyotokea nyuma yake.
“Daktari hakuna njia yoyote unayoweza kufanya ili apone na kumbukumbu zake ziwe kawaida!’
“Sidhani! Ubongo wake umeharibika sana!’
“Mungu wangu hizo kumbukumbu zake ndizo ninazohitaji zaidi!”
“Sio uhai wake?”
“Vyote pamoja!”
“Lakini kwanini kumbukumbu zaidi?”Daktari aliuliza na Danny akalazimika kumsimulia stori nzima juu ya yaliyotokea Tanzania na kwanini alikwenda nchini Zaire kumfuata mzee Mwinyimkuu, daktari alibaki mdomo wazi akionekana kutoamini kama mambo ya kula Yamini yalikuwa na uwezo wa kuharibu akili ya mtu.
“Haya mambo huwa nayasikia lakini hata siku moja sikuwahi kuamini kama kweli yanaweza kufanya lolote kumdhuru mtu!”
“Hicho ndicho kilitokea! Ndio maana namhitaji sana huyu mzee, kurejewa kwake na fahamu pamoja na kumbukumbu kutaamanisha maisha ya mtu mwingine nchini Tanzania, tafadhali daktari nisaidie!”
“Lakini hilo liko nje ya uwezo wangu ni suala la mwili wenyewe kupona, ninachotegemea mimi atapoteza fahamu lakini hawezi kujua asili inaweza kutenda kazi yake kusiwe na mambo yote ninayosema!”
“Jitahidi daktari!”
“Nitafanya kadri niwezavyo!’
Danny aliwasiliana na Tanzania na kuwajulisha mambo yote aliyoyafikia nchini Zaire, wote walisikitika kusikia kwamba alimpata mzee Mwinyimkuu lakini akiwa katika hali mbaya! Hakuweza tena kuondoka ikabidi abaki Kinshasa akisubiri mzee Mwinyimkuu apate nafuu lakini haikuwa hivyo mpaka mwezi mmoja baadaye alikuwa bado hajaweza kuongea ingawa aliweza kufumbua macho! Mambo yote yaliyosemwa na daktari ndiyo yaliyojitokeza, upande mmoja wa mwili wake ulikuwa umepooza.
Danny alikataa tamaa kabisa na kuamua kurudi Tanzania akiwa amechukua namba ya simu ya Aminata ili aendelee kuwasiliana naye juu ya maendeleo ya mgonjwa, hilo ndilo lililofanyika, lakini mpaka miezi mitatu baadaye Nancy akizidi kuwa mwendawazimu, hali ya mzee Mwinyimkuu ilikuwa bado mbaya.
“Anaweza kunyanyuka kitandani lakini bado hawezi kusema chochote!”
“Daktari anasemaje?”
“Anadai kuna maendeleo kidogo na ana matumaini fahamu zitamrejea baada ya muda!”
“Kweli?”
“Ndiyo!’
“Kwa hiyo nije?”
“Hapana, subiri tu hukohuko Tanzania kwa sababu tunaweza kuwasiliana kwa simu nitakujulisha kila kitu kinachoendelea!”
“Ahsante sana Aminata!’
Furaha aliyokuwa nayo Danny siku hiyo ilikuwa kubwa mno, alipowataarifu mzee Katobe na mkewe juu ya hali ya mzee Mwinyimkuu nao walifurahi kupita kiasi, maisha yao yalikuwa mazuri na yenye furaha kama vile hakikutokea kitu! Walishasameheana mambo yote yaliyotokea ili mradi hayakufanyika kwa mapenzi yao, mzee Katobe aliwapenda na kuwakubali watoto Catherine na David! Kwake walikuwa ni kama watoto wa kuzaa.
Mwezi mmoja baadaye ikiwa ni siku ya Jumapili baada tu ya kutoka kanisani simu ya mkononi ya Danny ililia, kabla ya kuipokea alitupa macho yake kwenye kioo cha simu na kugundua ilikuwa simu ya Aminata, moyo wake ulienda kasi kwani alikuwa na muda mrefu tangu apokee simu kutoka Zaire alishindwa kuelewa ni nini kilikuwa kimetokea.
“Hallo habari yako?”
“Safi! Nipe habari ya huko!”
“Leo nina habari mzuri!”
“Habari gani hiyo?”
“Mzee alitoka ku-hospitali jana!”
“Unasema?”
“Mzee alitoka mu-hospitali jana!”
“Unasema kweli? Ina maana amepona?”
“Huwezi amini!Amepona kabisa ingawa bado pande moja ya mwili ina matatizo!”
“Kumbukumbu zake je?”
“Iko safi! Na nimemweleza juu ya stori yote uliyoniambia na amemkumbuka Nancy vizuri, amesikitika sana na amesema mtu yeyote anaweza kuja kumchukua baada ya mwezi moja!”
“Unasema kweli?”
“Kabisa!”
Danny alirukaruka juu akilia kwa furaha, haikuwa rahisi kuamini alichokuwa amekisikia! Hata masikio yake mwenyewe aliona yamemdanganya hivyo kuendelea kuuuliza mara kadhaa akitaka kufahamu kama kilichosemwa ni kweli au Aminata aliendelea kumsisitiza kuwa mzee Mwinyimkuu alikuwa na afya nje kabisa na tayari alikuwa akisafiri kuja Tanzania kumrekebisha Nancy!
“Ahsante sana! Nashukuru sana! Msalimie sana Mwambie tunampenda sana, inawezekana baada ya mwezi mmoja nitakuja mwenyewe kumchukua!”
Simu ilipokatika Danny alikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa mzee Katobe na kuwapa taarifa juu ya simu aliyoongea nayo kutoka Kinshasa familia nzima ilifurahi, mama aliruka juu na kushangilia kwa furaha.
“Itakuwa vyema! Ili mwanangu arejewe na akili zake!”
“Nafikiri tutaweza hata kufunga ndoa!”
“Unastahili hili Danny umemvumilia sana mwenzi wako!”
“Hakuna matatizo mama! Ulikuwa ni wajibu wangu!”
SIku hiyo hiyo ilifanyika sherehe, wala Nancy hakuwa na habari juu ya kilichoendelea muda wote, alikuwa akiongea peke yake na kucheka! Jina Tonny halikukosekana katika maongezi yake jambo lililoonyesha kuwa pamoja na kuchanganyikiwa alikuwa bado akimkumbuka, mara chache sna alimtaja Danny.
Danny alibaki akisubiri mwezi mmoja ufike na ulipotimia alipewa nauli na mzee Katobe na kusafiri hadi Dar es Salaam ambako alipanda ndege iliyomfikisha Kinshasa siku hiyo hiyo.
*****
Maisha hayakuwa kama yalivyotegemewa kwa Tonny ni kweli baada ya kumaliza Chuo Kikuu cha Beijing yeye na Mimi walihamia Marekani ambako baba yake Mimi, mfanyabiashara maarufu nchini marekani alimkubali Tonny awe mume wa mtoto wake na ndoa kubwa ya kifahari ikafungwa!
Walipewa nyumba kubwa ya kifahari katika Jiji la New York ambako Tonny na Mimi waliishi pamoja wakifurahia maisha. Tonny alimhamisha mama yake kutoka Tanzania na kumpeleka Marekani! Hakuwa na kumbukumbu hata kidogo juu ya Nancy na hata aliposikia kuwa msichana huyo alishikwa na wendawazimu alicheka ingawa alielewa kabisa ni yeye ndiye aliyesababisha yote hayo.
“Shauri yake kwanini hakuweza kuvumilia! Au kurudi kwa mganga amwondolee?” alijiuliza Tonny.
Maisha yalikuwa na kila dalili yangeendelea vizuri katika familia ya Tonny! Hakuamini kama siku moja angerudi tena Tanzania, alijihesabu Mmarekani mweusi na hakutaka watu wafahamu alitokea Afrika Mashariki katika nchi ya ulimwengu wa tatu.
Aliaminiwa na baba mkwe wake na kupewa nafasi kubwa katika kampuni! Kichwa chake kikavimba na kujiona yeye ndiye kila kitu katika kampuni hiyo ya kutengeneza matairi ya TrenTyre, wafanyakazi wote walimheshimu kwani alikuwa mtu wa karibu sana na tajiri yao.
Miaka mitano baadaye mambo yalibadilika ghafla, wazazi wa Mimi pamoja na Mimi mwenyewe walifariji katika ajali mbaya ya gari wakisafiri kutoka Miami walikokuwa wamekwenda kwa mapumziko ya Pasaka kurudi New York, Tonny alikuwa nchini Canada kushughulikia masoko ya matairi! Alipopata taarifa za msiba huo alirudi haraka na kukuta mambo yamebadilika.
Nyumba yake ilikuwa imefungwa mama yake akiwa nje, hakuruhusiwa kufika kwenye msiba kwani familia ilidai hakutambuliwa! Kiburi alichokipata kufuatia madaraka aliyopewa kilimgombanisha na wana ukoo! SIku hiyo hiyo mipango ilifanywa uhamiaji akawa amepewa masaa ishirini na nne aondoke nchini Marekani.
Uchungu mkubwa ulimshika ni hapo ndipo alimpomkumbuka mwanamke wake wa zamani, Nancy! Alitamani kuwa naye tena akiamini huyo ndiye mwanamke aliyepangiwa na Mungu, alimweleza mama yake kuhusu jambo hilo na alimshauri wakirudi nyumbani amtafute, Tonny hakuwa na ubishi alikubaliana na mama yake moja kwa moja.
Walisafirishwa kutoka Marekani hadi Tanzania chini ya uangalizi maalum, waliposhushwa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam waliachwa waende zao na wakiwa hawana hata mzigo walipanda teksi iliyowapeleka moja kwa moja hadi Bagamoyo, watu walipomwona Tonny walishangaa sana.
Kitu cha kwanza alichokifanya Tonny baada ya kufika Bagamoyo akiwa haamini kama kweli alikuwa amerudi ni kumuulizia Nancy, alipewa taarifa zote na kusikitika lakini alikuwa tayari kuwa naye hivyo hivyo alivyokuwa! Alihisi bado anampenda na alihitaji sana kumwomba msamaha kwa makosa aliyomfanyia.
Mchana wa siku iliyofuata alisindikizwa na mama yake kwenda nyumbani kwa mzee Katobe, walipokelewa vizuri si mzee Katobe wala mkewe walioonyesha chuki! Tonny alipiga magoti chini na kuomba msamaha lakini wazazi wa Nancy walimwambia wazi hawakuwa tayari kumpa msamaha kwa sababu alisababisha mtoto wao tatizo kubwa! Tonny alilia kama mtoto mdogo na baadaye kumfuata Nancy mahali alipokaa akiongea peke yake kwa kupiga magoti akimwomba msamaha pia, kama kawaida ya wendawazimu Nancy alicheka bila kuelewa alichokuwa akifanya.
Muda mfupi baadaye akiwa bado amepiga magoti mlango ulifunguliwa, Danny akaingia akiongozana na mzee aliyetembea akichechemea, alikuwa mzee Mwinyimkuu! Danny aliwasalimia watu wote waliokuwepo ndani ya nyumba na baadaye kutambulishwa kwa Tonny na mama yake.
“Huyu kijana tuliishi naye hapa, aliwahi kuwa mchumba wa Nancy! Kifupi ni yeye ndiye aliyemharibia maisha mtoto wetu, anaitwa Tonny! Ana bahati siku hizi sina silaha ningemmaliza!” Mzee Katobe aliongea.
Danny alimwangalia Tonny na kucheka, hakutaka kuonyesha chuki ingawa ni kweli alimchukia sana! Alimsogelea na kumpa mkono na wakasalimia bila kinyongo. Mzee mwinyimkuu alisalimiana familia nzima kisha kupewa pole na baada ya hapo akaeleza nia ya safari yake na kuomba nafasi afanye kazi yake ili kumrejesha Nancy katika hali ya kawaida.
Aliletewa begi lake akatoa vitabu viwili na kuanza kusoma Nancy akiwa ameketishwa mbele yake, alisoma cha kwanza mpaka akamaliza kisha akachukua cha pili kilichokuwa na rangi nyeupe na kuanza kukisoma, alipofika katikati yake tu Nancy alianza kutoa macho kisha kuanguka chini na kuanza kutoa mapovu mdomoni kama mtu mwenye kifafa, walipotaka kumwangia maji aliwazuia na kuendelea kusoma hadi mwisho wa kitabu.
Wakati huo Nancy alikuwa usingizini fofofo, Danny na Tonny walikuwepo wakishuhudia! Nusu saa baadaye alizinduka akiwa mwenye akili timamu mbele yake aliwaona wanaume wawili, Danny na Tonny.
“Tonny......Danny!” Aliita Nancy kwa wakati moja huku akizungusha macho yake kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine! Alionekana kutoamini kilichokuwa mbele yake, baada ya hapo aliendelea kuita jina la Tonny mara nyingi zaidi kuliko Danny!
Je nini kitaendelea mahali hapo?
Je Nancy atamchagua nani?

No comments