Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 28


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Watu wote ndani ya nyumba walikuwa kimya, mzee Katobe na mkewe walibaki midomo wazi bila kuelewa nini kingetokea! Ilikuwa ni kama ndoto, hawakuamini macho yao kama kweli Nancy alikuwa amerejewa na fahamu zilizopotea kwa muda mrefu, walizidi kumshangaa mzee Mwinyimkuu na walizidi kumshukuru Danny kwa juhudi alizozifanya kwani bila yeye Nancy asingekuwa binadamu wa kawaida tena.
Pamoja na shukrani hizo hawakuwa na uhakika nini kingetokea ndani ya nyumba yao, ilikuwa ni lazima Nancy achague mwanaume mmoja kati ya wawili waliosimama mbele yao hakika ulikuwa mtihani mgumu! Ingekuwa ni wao waliotakiwa kuchagua basi wangemchagua Danny, walilidhishwa na tabia yake na walimpenda kwa namna walivyoishi nae vizuri na kusaidiana katika mambo mengi.
Lakini hawakuwa na uhakika kama chaguo la Nancy lingekuwa lao kwani katika mapenzi kila mtu na kitu akipendacho, kwa hali iliyokuwa imeonekana na jinsi ambavyo Nancy alilitaja jina la Tonny mara nyingi dalili nyingi ziliashiria yeye ndiye angeibuka mshindi jambo ambalo hata mzee Katobe na mkewe hawakulifurahia hata kidogo.
“Haiwezekani!” Mama yake Nancy alimnong’oneza mzee Katobe.
“Haiwezekani nini?”Mzee Katobe aliuliza.
“Mwanangu hawezi kurudiana naTommy tena!”
“Hilo hata mimi nakubaliana nalo lakini tutafanya nini? Inavyoonekana huyu mtoto bado anamkumbuka Tonny na pia anampenda tutafanya nini?” Mzee Katobe aliuliza.
“Lazima uzuie!”
“Wacha kidogo tuone kitakachotokea pengine ni wasiwasi wetu!”
Wakati wakiongea maneno hayo kwa sauti ya chini Nancy alikuwa bado amesimama wima mikono yake ikiwa kichwani na alikuwa akilia kwa uchungu huku akizidi kuwaangalia wanaume waliokuwa mbele yake, kichwa chake kilionekana kuwa na kumbukumbu kidogo na juu ya yaliyotokea maishani mwake akiwa mwendawazimu! Alipogeuza kichwa upande wa pili aliwaona baba na mama yake wakiwa wamesimama, akatabasamu.
“Mama huyu ni Tonny kweli au?”
“Ni yeye!”
“Amekuja lini?”
“Tumemwona leo!”
Baada ya kuongea na mama yake bila hata kuongea kitu chochote na mzee Katobe, Nancy aligeuka upande wa mwanzo na kuwaangalia wanaume wawili wakiwa wamesimama kama askari, uso wa Danny ulionyesha kujawa na huzuni na kwa mbali alikuwa akitokwa na machozi! Mambo machache yaliokuwa yamejitokeza ndani ya nyumba hiyo baada ya Nancy kurejewa na fahamu zake yalitosha kumwonyesha juhudi zake zisingezaa matunda.
“Tonny bado unanipenda?”Nancy aliuliza.
“Hakika ndio maana nimerudi, bado nakupenda sana na ninataka kuwa na wewe tena maishani, nisamehe kwa yote niliyokukosea!”
“Mimi yuko wapi?”
“Alifariki dunia! Nisamehe sana Nancy kwa yaliyotokea na tusiongee tena mambo ya siku za nyuma, yote hayo yalipita hebu tugange yajayo!” Maongezi kati ya Tonny na Nancy yaliendelea kama dakika mbili watu wengine wakiwa kimya.
Kila mtu aliyemwangalia Danny alimwonea huruma hata mzee Mwinyimkuu kwani ni kweli alikuwa ametumia juhudi nyingi sana kuokoa maisha ya Nancy na alistahili kuwa mume wake. Danny alisimama kwa unyonge mikono yake ikiwa imekunjwa kifuani! Machozi yakiendelea kumtoka, hakuwa tayari kukubali Nancy aondolewe mikononi mwake wakati alishapoteza muda mwingi kumshughulikia.
“Tonny!”Danny aliita.
“Yes!”Tonny aliitikia kwa mkato huku macho yake yakimpandisha Danny juu na kumshusha chini kwa dharau.
“Lakini mshikaji si wewe ulimwacha? Sasa kwa nini usiniachie tu mimi niliyemuhangaikia?”
“Nini?”
“Usiniachie mimi, kwa nini tugombane!”
Danny aliongea kwa unyonge akimgeukia Tonny na kupiga magoti chini akimbembeleza ili amwachie Nancy.
“Najua una uwezo wa kumchukua na anakupenda kuliko anavyonipenda mimi nakusihi ndugu yangu uniachie huyu mwanamke, nimehangaika sana! Sitaweza kuishi tena kama Nancy akiondoka maishani mwangu, itakuwa aibu kubwa mno ambayo sitaweza kuivumilia!”
Aliongea Danny kwa sauti ya kutia huruma.
Wazazi wa Nancy walishuhudia kitendo hicho na kuumia moyoni mwao, yalikuwa ni matendo ya kusikitisha na waliamini Danny hakustahili kutendewa hivyo kwa sababu alikuwa mwema sana kwa mtoto wao.
“Ni Danny huyuhuyu aliyepigwa risasi na mzee Katobe lakini akaficha siri kitendo kilichofanya mume wangu aepuke kifungo gerezani, ni Danny huyuhuyu aliyehairisha masomo chuo kikuu mara ya kwanza na sasa mara ya pili ili amtafute Nancy, ni Danny huyuhuyu ndiye aliyemtafuta mzee Mwiyimkuu hatimaye kupatikana na sasa Nancy amerejewa na fahamu zake! Haiwezekani, Nancy hawezi hata siku moja kurejea kwa Tonny, lazima tumsaidie!” Mama Nancy aliunganisha mambo kichwani mwake.
“Toka hapa! Haya mambo ya kutafuta ya kumuhangaikia unayajua mwenyewe hapa ni kura tu?Ukishinda kuchukua mtoto, nikishinda ondoka zako!” aliongea Tonny kisha kumsukuma Danny na kumfanya anguke chali sakafuni.
Nancy alishuhudia kila kitu kilichotokea badala ya kusikitika alichekelea na kisha kutembea kwenda mbele mahali alipokuwa amesimama Tonny akitamka maneno na kuonyesha ni jinsi gani alimpenda na alikuwa amesahau yote yalitokea.
“ Nancy! Kwa nini unanifanyia hivi? Umesahau nilijitoa kwa ajili yako? Nifikirie, utayafupisha maisha yangu”Aliongea Danny lakini Nancy hakujali wala kumsikiliza alichokifanya ni kusonga mbele hadi kumfikia Tonny na kumkumbatia, mama yake Tonny alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni alinyanyuka na kuanza kushangilia huku akipiga vigelegele kwake ulikuwa ushindi.
“We mama hamnazo nini?” Unashangilia kitu gani gani? Hapa kuna jambo la kushangilia, tena kaa kimya vinginevyo uondoke hapa nyumbani kwangu!” Mama yake Nancy alifoka akitembea kwa haraka kuelekea mahali Nancy na Tonny waliposimama wakiwa wamekumbatiana.
Kwa nguvu zake zote alimkamata Nancy na kuanza kumvuta hatimaye kufanikiwa kumwondoa mikononi mwa Tonny akaanza kumvuta kuelekea chumbani ambako alimwingiza na kufunga mlango nyuma yake, Nancy alilalamikia kitendo hicho lakini mama yake alielewa wazi akili yake ilikuwa haijatulia au alikuwa hafahamu mambo yaliyotokea mpaka kufikia siku hiyo.
“Niachie mama! Niachie niende kwa Tonny! Nampenda kwa moyo wangu wote, ndiye mtu niliyemchagua maishani lakini alichukuliwa kutoka kwangu na Mimi lakini sasa Mungu amemrudisha! Niacheni nimchague nimpendaye ni mimi wa kuchagua, siwezi kuchaguliwa! Simpendi Danny hata kidogo nilionyesha mapenzi kwake kwa sababu nilitaka kumwokoa baba yangu na jela!”
Aliongea Nancy kwa uchungu huku akilia, kwa jinsi maneno yalivyomtoka kulikuwa na kila dalili ya kumaanisha alichokisema.
“Sikiliza mwanangu Nancy!Najua unampenda Tonny lakini pia kuna vitu kama natakiwa kukueleza baada ya hapo utakuwa na uamuzi wa kuchukua, nina uhakika huna kumbukumbu juu ya nini kilikutokea, laiti ungefahamu usingediriki kumwacha Danny! Hebu kwanza jiangalie, nenda simama kwenye kile kioo uangalie mwili wake pamoja na nywele zako ya hapo nitakueleza kila kitu!”
Mama yake aliongea kwa huzuni, alifahamu wazi Nancy hakuelewa kitu chichote juu ya wendawazimu uliomtesa na alitaka hilo lifahamike kwanza ndipo aanze kumsimulia.
“Mama nilikuwaje?”
“Ni habari ndefu! Unawakumbuka mzee Kiwembe na Babu Ayoub?”
Nancy aliinamisha kichwa chake chini na kuzama katika fikra nzito akijaribu kuyazungusha majina ubongoni mwake ili kuona kwamba kumbukumbu zake zilikuwepo,muda mfupi baadae alinyanyua kichwa chake na kumuangalia mama yake.
“Ndiyo mama, nayakumbuka majina hayo, tulikuwa kisiwani, baba na Danny hawakuwepo! Nashangaa leo wapo na ameongezeka Tonny, walikuja lini? Nakumbuka babu Ayoub ndiye alinifanyia kitendo kibaya ambacho nilizuiliwa kukifanya na mtu yoyote isipokuwa Tonny!T ena aliyenizuia yupo hapa ndani! Wamekujaje watu wote hawa hapa kisiwani Galu?”
“Hapa hatupo Galu mwanangu tupo Bagamoyo? Na sijui kama unakumbuka kilichotokea baada ya babu Ayoub kukufanyia kitendo cha ukatili”.
“Sikumbuki mama!”
“Kwa sababu ni wajibu wangu kukuambia basi nitakueleza ukweli!”
Alipoongea mama Nancy alijiweka vizuri kitandani.
Wakati maongezi yakiendelea kati ya mama na mtoto kelele nyingi zilisikika sebuleni, kulikuwa na kila dalili kuwa watu walikuwa wakigombana!
Sauti ya mzee Katobe ilisikika ikiita jina la Danny na kumzuia asifanye kitendo alichotaka kukifanya.
“Danny! Danny! Usifanye hivyo mwanangu, acha kabisa utaua halafu utakwenda jela!”
“Sijali kitu ni bora nimuue kabisa huyu mshenzi halafu na mimi nife! Hawezi kunionyesha dharau kiasi hiki!”
“Baba nakuomba uniachie!” ilikuwa sauti ya Danny na muda mfupi baadae Tonny alisikika akilia kwa sauti ya juu kuomba msaada akidai amechomwa kisu mbavuni mama Nancy aliposikia maneno hayo alikatisha maongezi na kuondoka chumbani mbio kwenda sebuleni, hakuamini alipokuta damu imetapakaa sakafuni! Tonny alilala sakafuni akijitupa huku na kule damu ikizidi kumwagika.
Je nini kitaendelea?

No comments