Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 29


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Lilikuwa tukio la kutisha na kusikitisha sana, moyo wa kila mtu aliyekuwepo sebuleni kwa mzee Katobe ulikuwa ukidunda kwa nguvu! Nancy alikuwa bado amelala sakafuni uso wake ukiwa umechimbiwa katikati ya viganja mikono yake yote miwili, pamoja na kusikia wazazi wake wakiongea bado hakuamini kama majambazi walikuwa wameondoka.
“Kwa hiyo wamemteka?”Mzee Mwinyimkuu aliuliza.
“Ndivyo inavyoonekana!”
“Unahisi watakuwa ni akinanani?”
“Hakuna mtu mwingine wa kufanya kitendo hiki isipokuwa Tonny!”
“Inawezekana! Basi pigeni simu polisi tuwataarifu pia jambo hili”
“Sawa!”
Wakati mzee Katobe anaisogelea simu ili apige kituo cha polisi, Nancy alinyanyuka sakafuni na kusimama wima! Maongezi kati ya baba yake na mzee Mwinyimkuu ndiyo yaliyomshtua, alitaka kuelewa ni nani aliyekuwa ametekwa, kichwani mwake aliwafikiria watu wawili tu, kama si mama yake basi alikuwa Danny maana kabla majambazi hayajaingia sebuleni walipokuwa wameketi wakijiandaa kwenda kanisani kulikuwa na watu watano peke yake, watoto Catherine na David walikuwa chumbani.
“Nani ametekwa?”Aliuliza Nancy.
“Danny!” Mzee Katobe alijibu.
“Haiwezekani! Yumo humuhumu ndani labda amejificha mahali fulani!”
“Hapana! Lazima tuukubali ukweli kuwa hawa watu wameondoka na Danny! Si unakumbuka walivyoingia walisema wamekuja kumtafuta mtu mmoja, sasa kukosekana kwa Danny hapa ndani kunamaanisha nini Nancy?”Mzee Katobe aliuliza.
“Inawezekana kweli katekwa, tutafanyaje sasa kumpata?”
“Nataka kupiga simu polisi niwataarifu juu ya tukio hili!”
“Baba subiri kwanza, naelewa aliyefanya kitendo hiki si mwingine bali ni Tonny! Acha nikazungumze naye, nina uhakika atamrudisha!” Aliongea Nancy akijaribu kumshawishi mzee Katobe asitoe taarifa polisi kwanza.
Baada ya maongezi ya karibu dakika kumi mama yake Nancy akipinga wazo lililotolewa na binti yake akidai hapakuwa na sababu ya kusubiri, wote walikubaliana na Nancy akatoka mbio hadi nje akipitia ufunguo wa gari ya baba yake juu ya kabati, aliingia ndani na kuwasha kisha kugeuza na kuondoka kwa kasi ya ajabu akitimua vumbi nyuma yake hadi nyumbani kwao na Tonny!
Aliegesha gari mbele ya nyumba ndogo ya matope, akashuka na kutembea hadi mlangoni ambako alianza kugonga, hakuna mtu aliyemwitikia na hapakuwa na dalili za watu kuwemo ndani ya nyumba hiyo! Aliendelea kugonga karibu dakika tano huku watu wakipita njiani na kumshangaa, hakuelewa ni kwanini.
“Nyumba hiyo haina watu dada walishahama muda mrefu!” Mpitanjia mmoja alimwambia.
“Wako wapi?”
“Miaka mingi hawakuwepo ila nasikia walirudi kutoka Marekani na kufikia hapa lakini baadaye wakahamia kwenye hoteli moja huko ufukweni inaitwa Badeco!”
“Ahsante sana!” Nancy aliitikia na kurudi hadi kwenye gari na kuondoka zake kuelekea kwenye hoteli aliyoelekezwa, aliifahamu vizuri sana Badeco Hoteli, ndio hoteli pekee ya kitalii iliyotisha kwa uzuri mjini Bagamoyo kipindi hicho. Kutoka nyumbani kwa akina Tonny hadi hotelini ilichukua muda wa dakika kumi lakini Nancy alitumia dakika tano, tayari akawa anaegesha gari lake mbele ya hoteli na kushuka.
“Habari yako dada?” Nancy alimsalimia msichana aliyemkuta mapokezi.
“Nzuri! Nikusaidie?”
“Ndiyo, namuulizia kaka mmoja anaitwa Tonny amepanga hapa?”
“Kweli yupo lakini hivi sasa amepumzika kidogo!”
“Mpigie simu mwambie mimi Nancy niko hapa!”
“Sawa! Karibu ukae kwenye kiti wakati nikikushughulikia!”
Nancy alilisogelea kochi lililokuwa jirani na kuketi bila kusema kitu, moyo wake ulikuwa ukienda kasi na hasira ilizidi kumpanda ingawa hakutaka kumwonyesha msichana wa mapokezi hasira zake. Akiwa kwenye kochi aliendelea kumshuhudia msichana akiongea na simu na alipoiweka chini alimwonyesha ishara kwamba amsogelee.
“Nifuate!” Alisema msichana wa mapokezi.
Nancy alimfuata msichana huyo nyuma bila kusema chochote na wote wakatembea pamoja hadi pembeni kabisa mwa hoteli kulikokuwa na nyumba nzuri iliyoezekwa kwa makuti msichana wa mapokezi alibonyeza kengele iliyokuwa juu pembeni mwa mlango, sekunde chache baadaye mlango ulifunguliwa, Tonny akatokeza uso wake haukuonekana kuwa na mshangao mkubwa sana, alikuwa kama mtu aliyemtegemea Nancy afike chumbani kwake muda huo.
“Karibu sana!”
“A...h..s..an..te!”Aliitikia Nancy kwikwi za kulia zikiwa zimemkaba kooni, hasira yake iliongezeka maradufu alipouona uso wa Tonny! Alimchukia sana kijana na hakuwa na mapenzi naye tena kufuatia kitendo cha kikatili alichomfanyia Danny.
“Tonny kwanini umenifanyia hivi?” Alianza kuongea kabla hata ya salamu.
“Vipi?”
“Kwanini umetuma watu kuja kumteka Danny?”
“Nini? Nani kakuambia nimefanya hivyo?” Aliuliza Tonny uso wake ukionyesha mshtuko ambao akili ya Nancy iliutafsiri kama maigizo.
“Usinifanyie maigizo Tonny, nipo siriasi kabisa! Hicho ndicho kitu ulichoahidi kukifanya wakati unaondoka nyumbani tafadhali naomba umrudishe Danny kwangu, usininyanganye mtu ambaye kwa sasa ninampenda huo ni ukatili Tonny, nitatoa taarifa polisi!” Aliongea Nancy akionyesha hasira.
“Sijafanya hivyo Nancy! Siku ile niliposema ilikuwa ni hasira tu, kamwe siwezi kumteka mtu!”
“Siangalii unachokisema sasa hivi, maneno yako ya siku ile ndiyo yaliyonifanya nikufikirie wewe! Tafadhali naomba umrudishe Danny kwangu! Vinginevyo nakwenda polisi”
“Ukienda polisi ujue ndio utakuwa umenichokoza, hapo ndipo nitalazimika kulipa kisasi!”
“Nakwenda, fanya lolote utakalo!”
“Huo ni uamuzi wako lakini yatakayotokea baada ya hapo usinilaumu!”
Nancy aliubamiza mlango wakati akitoka nje na dakika moja baadaye muungurumo wa gari likiondoka kwa kasi ulisikika kulikuwa na kila dalili kuwa kilichotoka mdomoni kwa Nancy hakikuwa utani, alimaanisha alichokisema na tayari kulikuwa na vita kali kati ya Nancy na Tonny ambayo mwisho wake usingekuwa rahisi kufikiri.
“Kama anakwenda polisi basi mimi pia nawasiliana na mzee Katapila! Tuone nani ni mjanja kati yangu mimi na yeye!” aliongea Tonny akiisogelea simu iliyokuwa pembeni mwa kitanda chake, kabla hajabonyeza namba yoyote mama yake aliyekuwa akiishi naye hotelini aliingia akitaka kufahamu nini kilikuwa kimetokea.
“Nancy, amekuja hapa anadai nimemteka Danny!”
“Umemteka Danny?” Mama yake aliuliza kwa mshangao.
“Ndiyo!”
“Ni kweli?”
“Hapana mama siwezi kufanya hivyo!”
“Sasa?”
“Kwa sababu ameamua kunipa jina la utekaji basi nimeamua kufanya kweli!” Tonny aliongea uso wake ukiwa umefura kwa hasira, mara nyingi akiwa katika hali hiyo hata mama yake alimwogopa. Kwa harakaharaka alibonyeza namba kadhaa kwenye simu kisha kuanza kuongea na mtu ambaye mama yake hakumfahamu.
“Naongea na mzee Katapila?...Sawasawa....sasa hebu sikiliza, ninachotaka ufanye ni kuhakikisha wote wanatekwa na utawapeleka hukohuko Tindiga ulikosema, wafiche huko kwa muda mrefu lakini usiwaue mpaka nitakapoona nao na ninaomba uje haraka hapa hotelini nikukabidhi hundi yako ili uchukue pesa benki......tafadhali wahi maana ukichelewa nitakuwa nimeshakamatwa na polisi....ndiyo ....Nancy amekwenda kushtaki!....najua watanichukua lakini wataniachia, ukishawakamata kaa nao siku nikitoka nitaamua nini cha kufanya juu ya watu hao! Nataka Nancy aelewe mimi si mtu wa kuchezea, nimeishi Marekani na ninajua visasi!” Aliongea Tonny huku mkono wake wa kuume ukipiga piga meza mara kwa mara, mama yake alibaki mdomo wazi akielewa tayari matatizo yalikuwa yametokea! Watu walikuwa wanatekwa kwenda kuuawa, kichwani mwake hakuwa na picha za watu wengine zaidi ya familia ya mzee Katobe.
*******
“Una uhakika ni yeye?”
“Asilimia mia moja kwani ndio kitu alichokisema!”
“Unao ushahidi?”
“Nina uhakika akihojiwa ataeleza ukweli!”
Nancy alitoa maelezo yote polisi kuanzia uhusiano wake na Tonny, alivyomwacha na kurejea kwa Danny jambo aliloamini lilimfanya alipe kisasi, maelezo yake ya karibu saa nzima yaliwafanya polisi waamini alichokisema na kuondoka haraka kwenda hotelini kwa Tonny, gari la polisi lilikuwa mbele likiwa na askari zaidi ya saba na Nancy alikuwa nyuma ndani ya gari la baba yake, hakuna kilichomfurahisha moyoni mwake wakati huo kama kukamatwa kwa Tonny na kufikishwa mbele ya sheria ili hatimaye aseme ni wapi alikompeleka Danny baada ya kumteka.
Walipofika hotelini, Tonny alikamatwa na kupigwa pingu kisha kuchukuliwa hadi kituoni, maelezo aliyoyatoa hayakutosha kuwafanya askari wamuachie huru, akawa ametupwa mahabusu ili aisaidie polisi katika upelelezi! Nafsi ya Nancy iliridhika kwa kitendo hicho na aliwaomba maaskari wamtese Tonny sana ili hatimaye aeleze ni wapi mchumba wake alikokuwa amefichwa.
“Hakyanani nitawapa pesa nzuri! Mkipiga kofi moja mia tano, teke elfu moja, kifuti elfu mbili, kila kirungu kitakachotua mwilini mwake elfu mbili na mia tano! Kazaneni kumpiga na mtunze kumbukumbu zenu ili nikija asubuhi niwakeshi mafaranga yenu!” Aliongea Nancy akitabasamu na maaskari wote waliokuwa wakimsikiliza waliitikia, jambo lililoonyesha wazi Tonny angeteswa usiku mzima mpaka aeleze ni wapi alikokuwa Danny.
Je nini kitaendelea?

No comments