Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 30


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Mzee Katapila alikuwa ni jambazi aliyeutingisha mkoa wa Dar es Salaam miaka ya sitini na sabini, alijipatia mali nyingi sana kwa njia haramu hatimaye kujikuta ametajirika! Lakini pamoja na kuwa na mali nyingi bado hakuisahau kazi yake ya ujambazi, akawa ameunda genge lililofanya kazi ya kuvamia mabenki, watu binafsi na kuwaibia! Kundi hili aliliita Lambadamu.
Lilikuwa ni kundi maarufu kwa vitendo vya uharamia, hata polisi walilifahamu lakini halikuchukuliwa hatua yoyote kwa sababu tajiri mzee Katapila alilikingia kifua! Watu wengi waliotaka kulipa kisasi walimfuata mzee huyu na kumlalamikia, kwa malipo kidogo tu aliwakamilishia kazi zao.
Ni kwa mzee huyu ndiko Tonny alikwenda kueleza shida yake, akalipa kiasi cha pesa ili amfundishe Nancy adabu akidai kitendo alichofanyiwa kilikuwa cha kudhalilisha mno, akiwa amesahau ukatili aliomfanyia Nancy nchini China na kitendo cha kumlisha Yamini na kuharibu kabisa maisha yake.
Kuua, kuteka na kutesa ilikuwa kazi rahisi sana kwa kundi hilo la Lambadamu hivyo baada ya mzee Katapila kupokea maagizo kutoka kwa Tonny na kukabidhiwa hundi yake ya milioni mbili kukiwa na salio la milioni moja aliwaamuru vijana wake kuingia kazini muda huohuo.
********
Alipotoka kituoni Nancy alinyoosha moja kwa moja nyumbani kwao, moyoni mwake akiwa na furaha kwa sababu ya kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na polisi! Alitamani kufika nyumbani mapema ili awasimulie wazazi wake juu ya kilichotokea, alitegemea wangefurahi kama alivyokuwa amefurahi yeye kwani matumaini ya Danny kurejea yalikuwa makubwa!
Hali aliyoikuta nyumbani kwao ilimshangaza, kulikuwa na idadi kubwa sana ya majirani pamoja na maaskari! Moyo wake ulipasuka kwa mshtuko, hakuelewa ni nini kilikuwa kimetokea kwani kulikuwa na kila dalili ya jambo baya. Aliegesha gari upande wa pili wa barabara na kushuka kisha kuanza kutembea kwa haraka kuelekea nyumbani kwao.
“Vipi kimetokea nini?” Nancy alimuuliza mmoja wa majirani.
“Aiseee! Sisi tulifikiri hata wewe umo?”
“Nimo wapi?”
“Walikuja watu na gari, wakaanza kurusha risasi hewani hapahapa nyumbani kwenu kisha tukawaona wakitoka ndani pamoja na watu watatu, wawili niliwatambua, alikuwa baba pamoja na mama yako lakini watatu sikumwelewa! Baada ya hapo niliingia uvunguni mwa kitanda polisi walipokuja ndipo nikajitokeza! Nilifikiri na wewe umetekwa!”
Nancy hakujibu kitu, alimwaga machozi hapohapo na kuanza kutembea kwenda ndani, maaskari wakimfuata kwa nyuma! Sebuleni kwao kulijaa damu, kulikuwa na picha ya wazi kuwa wazazi wake walipigwa risasi kabla ya kutekwa! Alihisi kuishiwa nguvu miguuni, akaketi kwenye kiti na kuendelea kuwaza juu ya yaliyokuwa yakitokea! Ghafla alisikia sauti za watu wakiongea chumbani, alitoka mbio na kufungua mlango! Wadogo zake David na Catherine walilala kitandani wakiwa wamejifunika shuka.
Aliwachukua na kuanza kutembea nao kwenda nje ya nyumba huku yeye na wadogo zake wakiendelea kulia machozi, ilikuwa hali ya kusikitisha! Maisha ya Nancy yalikuwa yameingia kwenye dhoruba nyingine baada ya kutoka katika wendawazimu.
“Kwa mkono wangu nitawaokoa baba, mama, Danny na mzee Mwinyimkuu, nasema damu itamwagika!” Aliongea kwa uchungu Nancy.
Nancy alikuwa amechanganyikiwa kabisa, mambo yalionekana kumtokea kwa ghafla mno! Hakutegemea baba na mama yake wangetekwa, muda wote alikuwa akilia wadogo zake David na Catherine wakiwa mikononi mwake! Hakuacha kuapiza kwamba kwa mkono wake angewaokoa wazazi wake hata kama Polisi wangeshindwa kuwapata, alikuwa tayari kumwaga damu ili mradi wazazi paoja na mume wake mtarajiwa Danny warudi kutoka walikokuwa wamepelekwa.
“Kwa mkono wangu mimi Nancy nitawakomboa, ni bora mimi pia nipoteze maisha yangu! Sitaweza kuishi duniani bila mama na baba yangu!” Aliongea Nancy kwa jazba, hasira kali ilikuwa imemkamata, alielewa wazi yote yaliyotokea yalifanywa na Tonny kama kisasi cha kumkataa, hata hivyo kilikuwa kisasi kikubwa mno.
Baadaye Polisi walimchukua Nancy na wadogo zake hadi kituoni ambako alitoa maelezo ya nyongeza juu ya tukio lililojitokeza, Polisi waliahidi kufanya kila kilichowezekana kumpata mtu aliyefanya tukio hilo, walimhakikisha isingechukua hata siku tatu kabla mzee Katobe, mke wake pamoja na Danny hawajapatikana.
“Ah! Hii kazi ni ndogo kabisa wala usiwe na wasiwasi, wewe tulia sisi tutawaleta wazazi wako nyumbani na mhalifu tutamtia nguvuni! Hii ndio kazi yetu tulia!” Mmoja wa maaskari alisema.
“Nafurahi sana kusikia hivyo! Sijui nitawashukuruje lakini lazima kutakuwa na namna fulani ya kuwapeni shukurani zangu kama baba, mama na mchumba wangu watarudi, huyuhuyu Tonny mliyenaye mahabusu anaelewa kila kitu!”
“Atasema tu wala usiwe na wasiwasi! Tutakupigia”
Nancy aliondoka kituoni na wadogo zake kwenda nyumbani ambako aliendelea kusubiri taarifa za kukamatwa kwa majambazi waliowateka wazazi wake pamoja na mchumba wake Danny, hakubanduka pembeni mwa simu akisubiri simu kutoka kituo cha polisi cha Bagamoyo lakini hakuna simu iliyoingia kutoka Polisi zaidi ya zilizopigwa na watu waliompa pole.
Siku hiyo alilala mpaka asubuhi bila taarifa yoyote na ikapita hadi siku iliyofuata, siku ya tatu saa sita mchana simu iliita! Wakati huo alikuwa ametoka kwenda msalani, alikatisha starehe yake na kukurupuka hivyohivyo hadi sebuleni, kweli simu hiyo ilitoka Polisi.
“Tunakuhitaji uje mara moja hapa kituoni, hili ni agizo kutoka kwa Mkuu wa Kituo!”
“Nipe dakika tano nitakuwa hapo!”
“Tafadhali usichelewe!”
“Nakuja!”
Kabla ya kuondoka alikwenda chumbani kuangalia wadogo zake na kukuta wapo katikati ya usingizi, hakutaka kuwashtua kwani aliamini asingechelewa sana kituoni! Aliinamana na kuwabusu wote wawili usoni kisha kutembea hadi nje ambako aliwasha gari na kuondoka kwa kasi kuelekea kituo cha Polisi.
“Karibu Nancy!” Askari wa kike aliyekuwa mapokezi alimkaribisha, alishafahamika kwa maaskari wengi kituoni hapo
“Ahsante!”
“Umekuja kumwona Mkuu?”
“Ndiyo nimepigiwa simu!”
“Zunguka basi upande huu nikupeleke!”
Nancy alifanya kama alivyoombwa na kuongozwa hadi ofisini kwa Mkuu wa kituo, mzee mfupi mnene alikaa nyuma ya meza akiwa amevaa magwanda ya jeshi la Polisi, alimkaribisha Nancy kitini na baadaye askari aliyempeleka aliondoka na kuwaacha wawili.
Baada ya salamu maongezi kati yao yalianza, mzee huyo aliyejitambulisha kwa jina la Afande Alphonce alianza kumuuliza Nancy maswali juu ya tukio zima ambayo hayakutofautiana sana na maswali aliyokwishakuulizwa na maaskari wa upelelezi kabla. Yote aliyajibu kutegemea na ufahamu aliokuwa nao na mkuu wa kituo alimweleza hatua waliyokuwa wamefikia katika kazi ya kupeleleza.
“Unamhisi nani?”
“Hakuna mtu mwingine ninayemhisi zaidi ya Tonny!”
“Tumemhoji sana lakini inavyoonekana hakuna anachokifahamu na amedhaminiwa na mzee Katapila nafikiri unamfahamu yule tajiri mkubwa jijini Dar es Salaam!”
“Yaani amempa Tonny dhamana?”
“Ni haki yake kudhaminiwa!”
“Hapa lazima kuna kitu kimetendeka sio bure! Mtampaje dhamana wakati wazazi wangu, mzee Mwinyimkuu bado hawajapatikana!” Aliongea Nancy kwa sauti ya juu akisimama na kukiacha kiti, kifua chake kikiwa kimejaa pumzi na kumfanya ashindwe kuongea vizuri
“Nancy...! Tulia kidogo, tafadhali shusha jazba ili tuongee kwa utaratibu, hakuna ushahidi wa kutosha kuwa Tonny ndiye ameshiriki katika kuwateka wazazi wako!”
“Sawa tu! Lakini haki lazima itatendeka na nitahakikisha Tonny na wote walioshiriki wanaingia mikononi mwa sheria!”
“Tutashukuru sana kama utatusaidia maana hii kazi inaonekana kuwa ngumu, vijana wangu wanajitahidi sana lakini hawafanikiwi hata kupata picha ya mahali wazazi wako walipopelekwa na hatuna uhakika kama wapo hai ama wamekufa! Hata hivyo hatujakata tamaa, bado tunaendelea na kazi”
Nancy hakuwa na la kusema tena, muda wote alikuwa akilia! Alikuwa ameingia katika matatizo mengine mazito zaidi baada ya tu ya kuibuka katika tatizo la wendawazimu na yamini aliyokula! Alimlaumu Tonny kwa kila kitu kilichotokea maishani mwake, yeye ndiye alikuwa mkandarasi wa mabaya yote yaliyokuwa yakimtokea.
“Tonny hastahili kuishi!” Aliongea kwa sauti akiketi kitini na baadaye kunyanyuka tena na kumpa mkono mkuu wa Kituo ili waagane.
“Nakushukuru sana kwa kuja binti!”
“Ahsante sana Mkuu, kuna jambo jingine la kuongelea kabla sijaondoka?”
“Hapana! Nenda kama kuna kitu kitajitokeza tutakupigia simu tena”
“Ahsante!”
Nancy alitoka ofisini kwa mkuu wa kituo akijifuta machozi, moyo wake ulikuwa umeongezewa kidonda kingine! Kitendo cha Tonny kuwekewa dhamana na tajiri wakati yeye Nancy alikuwa na uhakika asilimia mia moja ndiye aliyehusika kila kitu juu ya kutekwa kwa wazazi wake, kiliashiria mazingira ya rushwa! Roho ilimuuma sana kugundua hata Polisi aliowategemea kuwa walinzi wa usalama wa Raia walionekana kutokuwa upande wake.
“Sina la kufanya kwa sasa lakini haki lazima itatendeka!” Aliwaza akiingia ndani ya gari akawasha na kuondoka zake akitimua vumbi, moyo wake ulijaa hasira na alikuwa na wasiwasi mwingi moyoni! Kwani maisha yake yalikuwa hatarini kama Tonny alikuwa huru, aliamini angeweza kumfanya chochote lakini yote alimwachia Mungu na tayari alishaanza kukata tamaa.
Aliendesha gari akilia hadi nyumbani kwao ambako aliegesha na kuingia ndani na kujimwaga kwenye kochi ambako aliendelea kulia akiwakumbuka wazazi wake pamoja Danny! Dunia ilikuwa imebadilika kupita kiasi, kwake hapakuwa mahali pa kuishi tena bali jehanamu ndogo. Alishindwa kuelewa angefanya nini kubadilisha hali iliyokuwepo ili mambo yarejee kuwa kama zamani, awe mke wa Danny na arudi Chuo Kikuu kuendelea na masomo yake.
Alikaa sebuleni hadi akapitiwa na usingizi, alipozinduka ilikuwa saa kumi na mbili ya jioni! Alishangaa kuona wadogo zake hawapo sebuleni, kwani kwa wakati huo mara nyingi walizoea kukaa sebuleni wakicheza! Kwa sababu wakati anaondoka kwenda kituoni walikuwa wamealala aliamini bado wapo chumbani, swala hili halikupitishwa moja kwa moja kichwani mwake kwani haikuwa kawaida ya David na Catherine kuwa chumbani muda huo ni hapo ndipo alipoamua kunyanyuka kwenda chumbani kuangalia.
Mlango ulikuwa wazi na kitandani hapakuwa na kitu! David na Catherine hawakuwepo, alitoka mbio na kuanza kukagua vyumba vingine vyote hadi chooni lakini bado hakuwaona! Wasiwasi ulianza kumwingia kuwa huenda akiwa kituoni, baada ya Tonny kupewa dhamana alikwenda nyumbani kwao na kuwateka watoto.
Alitoka ndani ya nyumba na kukimbia nyumba ya jirani kuulizia kama kuna gari lilifika nyumbani kwao mchana akiwa kituoni, hakuna aliyeonakana kufahamu! Nancy alizidi kuchanganyikiwa, alirudi tena ndani na kuendelea kupekua lakini David na Catherine hawakuwepo! Alilia kwa uchungu.
Hakuwa na la kufanya zaidi ya kupiga simu polisi kuwataarifu juu ya kilichotokea, aliunganishwa moja kwa moja na mkuu wa kituo na kumweleza mambo yaliyotokea akilitupia lawama jeshi la Polisi kwa kumwachia Tonny ili aende kuwateka wadogo zake pia.
“Hivyo ndivyo unavyofikiri?” Mkuu wa Kituo aliuliza.
“Ndio!”
“Basi shauri yako!” Aliongea Mkuu wa Kituo na kukata simu.
Nancy alibaki akilia machozi na aliendelea usiku mzima hadi asubuhi saa kumi na mbili aliposhtuliwa na mlio wa simu akanyanyuka na kuikimbilia akitegemea ingekuwa ni taarifa ya Polisi wakimweleza mahali baba, mama, Danny, wadogo zake na mzee Mwinyimkuu walikokuwa.
“Haloo!” Ilikuwa sauti ya mtoto mdogo na kwa kuisikiliza mara moja Nancy aliweza kuitambua, alikuwa mtoto David.
“Ndiyo! Mko wapi?”
“Tuko...!Tuko...!” Mtoto hakuweza kueleza, sauti nzito ya mwanaume ilisikika.
“Nancy za siku nyingi?”
“Nzuri nani anaongea?”
“Mimi? Umenisahau?”
“Siwezi kukumbuka kwenye simu mpaka uniambie unaitwa nani?”
“Unakikumbuka kisiwa cha Galu?”
“Ndiyo!”
“Unakumbuka wazee wawili wanaoitwa Mzee Kiwembe na Babu Ayoub?”
“Ndiyo!”
“Basi tulikuja kuchukua watoto wetu na hivi sasa tuko njiani kurejea kwetu!”
“Mlipafahamu vipi nyumbani na namba ya simu mmeitoa wapi?”
“Hiyo siyo kazi ngumu sana kwetu, tumekaa Bagamoyo kwa wiki nzima!”
“Kwa hiyo hata wazazi wangu mmewateka nyinyi?”
“Hapana, hatujahusika! Hatukuwa na sababu ya kufanya hivyo! Sisi pia tulisikia tu baba na mama yako wametekwa na watu wasiojulika.....!”
Simu ilikatika na Nancy alibaki kusubiri ilie tena lakini jambo hilo halikutokea, aliendelea kuwalilia wadogo zake! Alishawazoea na hakuwa tayari kuwaacha warejee mikononi mwa wazee hao hatari, aliamini siku moja lazima angewakomboa ingawa hakuelewa ni kwa njia zipi.
Saa nne na nusu za asubuhi simu ililia tena, alinyanyua na kuipokea akiamini ilitoka kituo cha Polisi, ilikuwa sauti ya mwanamke akiongea kwa nyodo!
“Halooo wewe ni nani?”
“Unataka kunifahamu?”
“Ndiyo!”
“Ni mimi mke mwenzio! Mambo uliyonifanyia kanisani sijayasahau, aibu niliyoipata siku hiyo sitoisahau pia ndio maana niliamua kuacha chuo ili nimfundishe adabu huyu mwendawazimu! Hebu kwanza ongea naye” Aliongea mwanamke huyo bila kutaja jina lake.
Sekunde chache baadaye sauti ya kiume ilisikika, alikuwa Danny akiongea huku akilia! Damu katika mwili wa Nancy ilikwenda kasi huku moja ukimdunda kwa nguvu kama uliotaka kuchomoka kifuani kwake! Danny alielezea mateso aliyokuwa akipata huku akilia, Nancy alishindwa kujizuia naye akajikuta akibubujikwa na machozi.
“Uko wapi?”
“Sijui mahali nilipo maana wakati naletwa hapa nilikuwa nimefungwa na kitambaa cheusi usoni!”
“Uko na baba na mama yangu?”
“Hapana!”
“Huyo mwanamke ni nani?”
“Ni Agness! Niliyemwacha kanisani siku ya ndoa kwa sababu yako, aliamua kukodisha watu kunileta hapa kuteswa! Kama unaweza kuja kuniokoa tafadhali fanya hivyo, wataarifu polisi kama wewe huwe......!”Hakuyamalizia maneno yake, kukatokea ukimya wa sekunde kadhaa ndipo baadaye ikaibuka sauti ya kike.
“Usijisumbue kutoa taarifa polisi! Kaa mbali na jambo hili kama unataka kuishi, vinginevyo utapoteza uhai wako!”
“Huwezi kuniua! Malaya mkubwa weee! Na ninakueleza kwa mkono wangu nitakufikisha mbele ya sheria na nitamkomboa Danny kabla hujamfanya lolote!”
“Unanitukana mimi? Unataka nikufanyizie?”
“Fanya lolote unalotaka!”
“Poa!” Agness alijibu na simu kukatika akimwacha Nancy mwenye wasiwasi mwingi juu ya maisha yake.
Je nini kitaendelea?
Je Nancy ataweza kuwaokoa wazazi wake?

No comments