Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 31


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Tayari Nancy amekwishagundua kuwa wadogo zake Catherine na David wametekwa na mzee Kiwembe pamoja na Babu Ayoub! Danny naye ametekwa na Agness, mchumba wake wa zamani aliyemwacha kanisani siku ya ndoa baada ya Nancy kurejea.
Mpaka sasa haelewi mahali wazazi wake walipo na kama wao pia walitekwa na Agness au Tonny! Amechanganyikiwa hajui la kufanya ingawa ni lazima awaokoe wazazi, wadogo, Danny na mzee Mwinyimkuu! Huu ni wajibu wake hawezi kuukwepa na yuko tayari kupoteza maisha yake kama itabidi lakini awaweke watu hawa huru.
Je, nini kinaendelea? Fuatilia...........
Hakuna kilichomuumiza Agness moyo kama kitendo cha kuachwa na Danny kanisani mbele ya Padri kisa kikiwa ni kurudi kwa Nancy! Alilia kwa uchungu na kuondoka kanisani yeye na ndugu zake wakiwa wamejaa gadhabu, hakuna walichokifikiria zaidi ya kisasi kwa Danny kwa aibu aliyosababishia ukoo wao.
“Anastahili kufa! Hakuna kitu kingine kinachostahili kuwa adhabu kwa Danny isipokuwa kifo! Ametufanyia kitendo cha aibu sana katika familia yetu, hakika hastahili kuhurumiwa!” Walisema baadhi ya ndugu wa Agness wakiingia katika magari tayari kwa kuondoka eneo la kanisa.
Ilikuwa aibu iliyomkera kila mtu, Agness hakuwahi kuwaeleza ndugu zake juu ya msimamo wa Danny kuhusu msichana Nancy! Kwamba alikuwa naye lakini kama ingetokea akarudi basi angelazimika kumwacha na kurudiana na mpenzi wake wa zamani. Akiufahamu ukweli huo Agness aliwaunga mkono ndugu zake.
Kikao cha siri kilifanyika usiku wa manane nyumbani kwao Agness Jijini Dar es Salaam, mara tu walipowasili kutoka Bagamoyo! Pamoja na kusafiri umbali wa kilometa zaidi ya hamsini kutoka Bagamoyo mpaka Dar es Salaam bado mioyo ya ndugu wengi wa Agness hata wazazi wake ilijawa na hasira.
Mauaji ya Danny yalitawala mjadala katika kikao hicho, kila mtu alitaka Danny auawe tena kwa mateso makubwa iwe fundisho kwa watu wenye tabia za kudhalilisha watoto wa watu, Agness hakutetea kitu chochote hata yeye alikuwa tayari kuona Danny anakufa, muda wote alikuwa akilia machozi ya uchungu akilaani kitendo alichofanyiwa, hakutaka kukubali ukweli kuwa aliwahi kuelezwa na Danny juu ya Nancy.
“Ni heri tukose wote! Hata huyo mwendawazimu wake pia akose mume!” Aliwaza Agness akibubujikwa na machozi.
Familia ilikubaliana kufanya mauaji ya siri kubwa, mzee Elibariki Shao, baba mdogo wa Agness na mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam aliyemiliki vituo vingi vya mafuta aliahidi kushughulikia suala hilo yeye mwenyewe tena kwa gharama zake bila kushirikisha familia, alionyesha wazi chuki yake kwa Danny na kusema kilichofanyika ilikuwa ni aibu kwa ukoo mzima wa Shao.
Hapakuwa na mtu mwingine wa kutatua tatizo hilo, ni mtu mmoja tu ambaye mzee Shao alimfikiria! Hakuwa mwingine bali mzee Katapila, mtaalam wa mauaji tena kwa gharama nafuu! Baada ya kikao usiku huohuo kwa kutumia simu yake ya mkononi alipiga namba ya mzee Katapila na kupanga kukutana naye siku iliyofuata ili ampe kazi ya kufanya.
“Mtu kakuudhi nini?”
“Ebwanae duniani hapa hata ukitulia watu watakuchokoza!”
“Kakufanya nini?”
“Siwezi kuongea kwenye simu, simu zetu wengine zinasikilizwa nataka kukutana na wewe ana kwa ana!”
“Basi kesho saa nne asubuhi njoo ofisini kwangu!”
“Sawa rafiki!”
Walikuwa marafiki wa siku nyingi sana, waliowahi kushirikiana katika biashara mbalimbali na mzee Shao alikuwa na uhakika kwa kumtumia mzee Katapila kazi yake ingefanyika! Alisifika kwa kazi za ujambazi ingawa alikuwa mtu tajiri pengine katika nafasi ya pili au ya tatu jijini Dar es Salaam.
“Kazi imemalizika! Niachieni kila kitu na nitakifanya kwa uaminifu!” Mzee Shao aliwaambia ndugu wote waliokusanyika kabla hawajasambaa, ilikuwa tayari ni Alfajiri.
*********
Mzee Shao hakulala usingizi wala kukigusa kitanda chake, alichofanya baada ya kufika nyumbani kwake ni kuoga na kujiandaa kwenda ofisini kwake jengo la IPS katika ya jiji la Dar es Salaam, alijishughulisha na biashara ya kusafirisha mizigo ndani ya nje ya Tanzania akiwa na kampuni yake ya East African TransCargo.
Asubuhi hiyo ingawa ilikuwa siku ya Jumapili alikuwa na kazi za kufanya kabla hajaelekea ofisini kwa mzee Katapila na alimaliza kila kitu ilipogonga saa nne kasorobo na taratibu akajikongoja kwa miguu kuelekea kwenye ofisi ya mzee Katapila iliyokuwa ndani ya jengo lake refu la Katapila House lililokuwa mtaa wa Jamhuri.
“Binti naomba kumwona bosi!”
“Nimwambie nani?”
“Rafiki yake Elibariki!”
“Alishanitaarifu juu ya ujio wako, tafadhali karibu anakusubiri!”
“Ahsante!”
Mzee Katapila alimkaribisha mzee Shao ofisini kwake, baada ya salamu hakutaka kupoteza muda, alianza kueleza shida yake mara moja akionekana mwenye jazba aliyepania kufanya mauaji! Muda wote akiongea mzee Katapila alikuwa akitabasamu na kutingisha kichwa chake.
“Aisee! Hiyo ni kazi ndogo lakini lazima uhakikishe kuwa hutoboi siri mahali popote, kama ikitokea ukafanya hivyo basi hata wewe mwenyewe rafiki yangu maisha yako yatakuwa hatarini, nafikiri sifa zangu unazisikia!”
“Ah! Nakufahamu!”
“Nitakusaidia kufanya unavyotaka, lakini uwe tayari kunilipa milioni tano!”
“Hilo sio tatizo!”
“Nielekeze mahali anapoishi, baada ya kufanya kazi ndio utanilipa pesa!”
“Sina uhakika sana anaishi wapi labda jambo hilo nilifanyie kazi baada ya kutoka hapa!”
“Sasa bahati mbaya mimi ninasafiri kwenda Afrika Kusini nitarudi baada ya wiki moja, usiwe na wasiwasi kazi yako nitaifanya baada ya kurudi!”
“Nakutegemea wewe!”
Hapakuwa na maongezi zaidi baada ya hapo, waliagana mzee Shao akarudi ofisini kwake ambako baadaye aliwapigia simu baadhi ya ndugu akiwemo Agness wakakusanyika na kuliongelea suala hilo, kila mtu alikuwa bado amedhamiria kufanya mauaji ya Danny.
Wiki moja baadaye mzee Katapila alirejea na kupewa maelekezo yote juu ya mahali Danny alikoishi, hakuwa mahali pengine zaidi ya nyumbani kwa mzee Katobe akisubiri kufunga ndoa na Nancy! Jambo hilo ndilo lilitaka kuzuiliwa haraka iwezekanavyo, ilikuwa ni lazima Danny atekwe na kuuawa kabla ndoa haijafungwa.
“Ndoa haitafungwa! Leo hiihii nawatuma vijana wangu kwenda kufanya kazi huko huko Bagamoyo! Mnataka tumuue palepale?”
“Hapana! Ni lazima ateswe kwanza!”
“Kwa hiyo baada ya kumteka tumpeleke wapi?”
“Tafuta mahali tumhifadhi!”
“Ninalo ghala langu lililowahi kuwa kiwanda cha Fenicha huko Vingunguti, kwa hivi sasa halitumiki ila kuna walinzi wa Omega Security wanaolinda kwa nje, hawaruhusiwi kuingia ndani kwani kuna vitu vyangu muhimu na vya siri navihifadhi!Ninaweza kutoa chumba kimoja pale ili ateswe vizuri lakini itawalazimu mniongezee shilingi milioni moja!”
“Haina tatizo, tunachotaka sisi ni kutoa mfano, aliyekuwa bibi harusi mtarajiwa amekasirika sana!”
“Basi niachieni mimi, kesho usiku njooni nitawapeleka mahali atakapokuwa!”Mzee Katapila alimwambia mteja wake.
Jambo hilo lilifanyika, Danny akawa ametekwa kutoka nyumbani kwa mzee Katobe na kusafirishwa hadi Vingunguti akafichwa ndani ya ghala la mzee Katapila, siku hiyo hiyo Agness alifika ghalani na baadhi ya ndugu na mateso yakaanza rasmi kabla Danny hajauawa.
*********
Kugundua kuwa Danny hakutekwa na Tonny isipokuwa Agness kulimwongezea Nancy hasira! Aligundua ni kazi kubwa kiasi gani aliyokuwa nayo mbele yake lakini ilikuwa ni lazima aifanye kwani hapakuwa na mtu mwingine wa kuwakomboa wazazi, mchumba, mzee Mwinyimkuu pamoja na wadogo zake waliotekwa.
“Lazima niwakomboe! Hata kama kuna vitisho kiasi gani, Agness ni mwanamke kama mimi! Simjui kwa sura wala umbile lakini nitapambana naye!”Aliwaza Nancy.
Ni kweli hakumkumbuka Agness kwa sababu siku aliyoingia kanisani na kukuta ndoa kati ya Danny na Agness ikiwa mbioni kufungwa, alikuwa ni mwendawazimu ambaye hakuelewa chochote.
Alitamani kuwa mtaalam wa silaha ili aweze kupambana vizuri na alihitaji kuwa na bunduki yake lakini hakuwa na uwezo huo, alielewa wazi kupambana kwa mikono na watu wenye silaha lilikuwa jambo gumu kwake kupata mafanikio! Fikra za mafunzo ya Mgambo zilimwingia na siku hiyo hiyo alianza kufutilia suala hilo, ikawa kama bahati alipofika ofisini kwa mshauri wa Mgambo alikuta watu wakijiandikisha naye alifanya hivyo mara moja.
“Sasa kazi wataipata, mambo yanakwenda kama nilivyopanga!” Aliwaza Nancy.
Siku iliyofuata aliingia uwanja wa shule ya msingi Mwanamakuka, akiwa na kundi la vijana kama themanini na kuanza mafunzo, kwa wiki mbili kazi ilikuwa hiyo na tayari alishafundishwa jinsi ya kutumia bunduki aina ya SMG na hata mazoezi ya kulenga shabaha yalishafanyika, mafunzo yalikwenda haraka kuliko kawaida kwa sababu vijana waliohitaji mafunzo walikuwa wengi.
“Sihitaji kitu zaidi, nilichotaka mimi ni kuelewa kutumia bunduki basi hakuna zaidi!”Aliwaza Nancy.
Tangu siku hiyo hakwenda tena uwanjani, alishinda nyumbani akifikiria ni kitu gani cha kufanya na akiwawazia sana wazazi, wadogo na mchumba wake! Aliamini walikuwa mahali fulani wakisubiri msaada wake kuwaondoa katika mateso, alitamani kumfuata Tonny kumwomba msaada kwani alishagundua wazi hakuwa na hatia.
Akiwa katika mawazo hayo simu iliyokuwa mezani ililia na kwa unyonge alinyanyuka na kuifuata, mawazo yake yote yakaimini ilikuwa ni simu kutoka polisi ambao alikuwa hajasikia kitu chochote kutoka kwao.
“Halow!”Aliita lakini hakuitikiwa, alichokisikia upande wa pili ni kwikwi za mtu akilia kwa uchungu.
“ Wewe nani?” Alizidi kuuliza lakini bado hakujibiwa, wasiwasi ulizidi kumwingia.
“Mimi...! Mimi...!Ni mama yako!”
“Mama! Mama!Mko wapi?”
“Sielewi hapa tulipo ni wapi ila elewa tuko katika mateso makali na tunahitaji msaada wako, baba yako ana hali mbaya sana kama unaweza tafadhali njoo!”
“Mko na Danny?”
“Hapana! Tupo na baba yako pamoja na mzee Mwinyimkuu!”
“Wapi?”
Simu ilikatika kabla hajapewa jibu, Nancy akazidi kuchanganyikiwa na wajibu ukazidi kuongezeka, uchungu mkubwa ulimshika moyoni na kujikuta akiyaona maisha yake hayana thamani yoyote! Alikuwa tayari kufa lakini aokoe maisha ya wazazi wake, hakuna kitu kilichowahi kuumiza moyo wake kama kumsikia mama yake akilia kwa sauti aliyoisikia kwenye simu.
“Kwa ujuzi mdogo nilioupata, hakika nitawakomboa wazazi wangu! Si wazazi wangu tu bali pia Danny, wadogo zangu na mzee Mwinyimkuu!” Aliongea peke yake Nancy akikaa kitini, mwili wake wote ulikuwa ukitetemeka kwa hasira.
“Haiwezekani! Iko namna, lazima nijue hawa watu wanapiga simu kutoka wapi, huo ndio utakuwa mwanzo wa upelelezi wangu, polisi wamenitelekeza lakini nitafanya kazi mwenyewe mpaka niwafikishe wahalifu mbele ya sheria!”Aliwaza Nancy na kuyaona mawazo yake yalikuwa sahihi.
Alitoka nje na kuingia ndani ya gari tena bila kufunga mlango wa nyumba na kuondoka kuelekea ofisi za Kampuni ya Simu. Saa, dakika, sekunde za nyakati ambazo simu zote ziliingia alikuwa nazo kwenye kitabu chake kidogo! Hilo ndilo jambo muhimu alilokumbuka kufanya. Dakika kumi baadaye aliegesha gari mbele ya jengo la Kampuni ya Simu lililo kandokando ya barabara mara tu uingiapo Bagamoyo.
“Dada samahani!” Alianza kumwambia mfanyakazi wa kampuni ya simu baada ya salamu.
“Sema nikusaidie!”
“Naomba uniangalizie, kuna simu tatu zimeingia kwenye nyumbani kwetu, moja leo na nyingine mbili ni wiki mbili zilizopita lakini nakumbuka muda ambao ziliingia!”
“Sasa nikusaidiaje?”
Kabla Nancy hajasema lolote aliingiza mkono wake kwenye mkoba na kuchomoa noti nne za elfu tanotano akaziweka mezani, mfanyakazi wa Kampuni ya Simu alionyesha mshangao wa ajabu, hakuelewa fedha hizo zilikuwa za kazi gani.
“Hiyo siyo Rushwa ni shukrani kwa kazi utakayonisaidia, naomba tu uniangalizie hizo namba ni zipi na zilipigwa kutoka wapi!”
“Sawa lakini hapa siwezi kukusaidia! Hatuna huo mtambo acha nipige Dar es Salaam makao makuu kuna rafiki yangu atakusaidia!”
“Mungu akubariki sana!” Aliongea Nancy akionyesha meno yake nje kama dalili ya tabasamu, moyoni alikuwa akisali ili aweze kubahatisha kuelewa namba hizo zilipigwa kutoka wapi! Huo ndio ungekuwa mwanzo wa kazi yake ndefu.
Mfanyakazi wa Kampuni ya Simu akiwa amefurahishwa na fedha iliyokuwa mezani kwake, alinyanyua simu na kupiga Makao makuu na kuomba kuongea na rafiki yake aitwaye Linda na kumweleza shida yake, alimtajia namba ya simu ya nyumbani kwa mzee Katobe pamoja na nyakati ambazo simu hizo ziliingia. Dakika tano baadaye alikuwa na jibu.
“Hii ya leo ni namba 2181719, inatoka Dar es Salaam, mwenye simu ni Kampuni iitwayo Tanbrand Funitures Ltd na hii namba 0222468 inatoka Kilosa, inamilikiwa na mtu anayeitwa Abdulmarik Issa! Hii ya tatu ilipigwa kutoka Nzega, Shinyanga bahati mbaya jina la mwenye simu halikujulikana mara moja, inavyoonekana ni hizi simu za kupiga kwenye vibanda!”
“Ahsante sana dada! Umenisaidia kuliko unavyofikiria, chukua na hii!” Nancy alimkabidhi noti nyingine ya shilingi elfu tano meno yote thelathini na mbili ya mfanyakazi wa Kampuni ya Simu yakawa nje.
Nancy aliondoka na kurejea nyumbani ambako alijifungia chumbani na kuanza kulia, alielewa kazi iliyokuwa mbele yake ilikuwa ngumu na pengine yenye mateso mengi ambayo yangeweza hata kumgharimu maisha yake! Hakujihurumia hasa alipowafikiria wazazi na wadogo zake na alikuwa tayari kwa lolote.
Alilia usiku mzima mpaka kukacha, asubuhi hiyo alikuwa na azimio moja kichwani mwake! Kuanza na Dar es Salaam kabla hajaenda Kilosa na baadaye ziwa Tanganyika alikoamini wadogo zake walipelekwa.
“NAANZA NA DAR ES SALAAM! DAMU ZA AGNESS NA NDUGU ZAKE WOTE NI HALALI YANGU NI LAZIMA DANNY AWE HURU!”Alisema Nancy kwa uchungu.
Hakuwa na jambo jingine la kufanya Bagamoyo, hakuna kilichosalia kwake! Wazazi hawakuwepo, wadogo zake hawakuwepo na wote pamoja na mchumba wake Danny walikuwa katika mateso, alitoka ndani ya nyumba na kufunga mlango akaingia ndani ya gari la baba yake ambalo wakati huo lilikuwa ni kama mali yake, alipoiangalia nyumba yao machozi yalizidi kumtoka aliamini hiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kuiona nyumba yao.
“Buriani!” Alitamka maneno hayo akiingia garini na kuondoka,hakuwa na uhakika kama angerudi tena Bagamoyo akiwa hai.
Je nini kitaendelea?

No comments