Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 32


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Nancy amefanikiwa kumwokoa Danny kutoka katika ghala la mzee Katapila huko Vingunguti, wote wawili wanachukua gari la mzee Katapila hadi Kimara ambako wanakodisha teksi inayowapeleka hadi kijijini Tindiga huko Kilosa shambani kwa mzee Katapila.
Ni huko ndiko wazazi wa Nancy pamoja na mzee Mwinyimkuu wamefungiwa wakiteswa, lengo lao ni kuwaokoa na wanafanikiwa kuingia ndani ya ngome ya shamba hilo, Danny amepigwa mshale mbavuni na Nancy amewekwa chini ya ulinzi na mlinzi wa Kimakonde aliyeuvuta upinde wake sawasawa tayari kwa kuuachia ili uzame katika nyama za msichana huyu jasiri.
Je, nini kinafuata? Atafanikiwa kuwaokoa wazazi wake? Nini hatima ya Danny ambaye mshale umezama mbavuni kwake? Endelea.........
Nancy alibaki amepiga magoti chini pembeni mwa Danny akitetemeka mwili mzima, ingawa hali ilikuwa ya baridi alihisi jasho jembamba likimtoka na kulowanisha nguo zake! Mzee mfupi, mwenye misuli alisimama nyuma yake akiwa ameuvuta upinde wake sawasawa tayari kwa kuachia mshale, kulikuwa na kila dalili kama Nancy angejitingisha au kutotii amri aliyokuwa amepewa, mshale ungezama kifuani kwake na huo ndio ungekuwa mwisho wa maisha yake, yeye na Danny wangekufa kabla hata ya kuwakomboa wazazi wake.
“Mzee naomba usiniue, najua unao uwezo wa kufanya hivyo lakini tafadhali sana nisikilize!” Aliomba lakini mzee huyo hakumjali.
“Huchikii siyo? Nimesema uchijitingiche, uchigeuke, uchikae, uchichimame, uchicheke wala uchiheme!” Aliendelea kusisitiza mzee huyo akimaanisha Nancy asiongee chochote, kulikuwa na kila dalili hapakuwa na utani katika maneno yote aliyoyasema.
Kulikuwa na mambo mawili tu ya kuchagua kwa Nancy, aidha kusubiri kifo kwa mshale au kujaribu kujiokoa kwa namna yoyote ile! Hakuwa na uhakika kama chaguo lake la pili lingefanya kazi lakini pia hakuwa tayari kusubiri kifo chake kama kondoo, nguvu ya ajabu ilimwijia mwilini mwake, ilikuwa ni lazima aitumie bastola iliyokuwa pembeni mwake kujiokoa.
Akili yake ilifanya kazi kwa kasi, akayumba kidogo kuelekea kulia kisha kurudi haraka kushoto, alishangaa kuona mshale ukipita kwa kasi kuelekea mbele, ulikuwa umemkosa kidogo tu! Alimshuhudia mzee huyo akipinda mkono wake mgongoni kuchomoa mshale mwingine lakini kabla hajafanikiwa kufanya hivyo tayari Nancy alishainyakua bastola yake ardhini na risasi moja ilizama katikati ya kifua cha mzee huyo akaanguka chini bila kupiga kelele, kwa Nancy ulikuwa ni ushindi.
“Haleluya!” Nancy alijikuta akitamka maneno haya bila kutegemea, furaha kubwa ilimjaa moyoni kuona amekiepuka kifo.
Bila kuchunguza kulikuwa na walinzi wengine, alimgeukia tena Danny aliyekuwa kimya na kuanza kumwita huku kwa mara nyingine akijaribu kuung’oa mshale! Danny aliyekuwa kimya alipiga kelele kwa maumivu akimwomba auache kama ulivyo.
“Nia..che!Nia..che dar..ling, nenda kaja..ribu kuwaokoa wazazi kwangu mimi imeshindikana!” Aliongea Danny kwa taabu.
“Haiwezekani! Haiwezekani Danny, huwezi kufia hapa!”
“Sasa uta..fanya ki...tu gani?”
“Lazima kuna njia ya kuokoa maisha yake!” Aliwaza Nancy na kwa haraka alimsogelea mzee aliyempiga risasi, akamvua mashuka aliyovaa na kuyafunga mwilini akizifunika nguo alizovaa! Alimalizia kwa kuchukua kofia ya mzee huyo iliyotengenezwa kwa nyasi na kuivaa kichwani.
Nancy alitaka kujibadilisha afanane na walinzi wa shamba la mzee Katapila ili kufanya kazi ya ukombozi iwe rahisi, alikuwa amebakiza hatua moja tu, kuingia ndani ya jengo kubwa lililokuwa mbele yake na kuwakomboa wazazi wake lakini hatua hiyo aliamini ndiyo ilikuwa ngumu kuliko zote zilizotangulia.
Hakuelewa nguvu zilizomiminika mwilini mwake zilitoka wapi kwani hata siku moja hakuwa kutegemea angeweza kumbeba mtu mwenye uzito mkubwa kama Danny lakini alishangaa kuona anamnyanyua na kumweka begani kwake na kukimbia naye kusonga mbele bastola ikiwa mkononi.
Alipokuwa umbali kama wa mita hamsini kutoka kwenye jengo hilo, alimlaza Danny chini kwa uangalifu ili mshale usizidi kuzama, alikuwa kimya kabisa na hata alipomwita hakuitika! Nancy alilia na kupoteza kabisa matumaini ya kumwokoa mwanaume aliyempenda na kumhitaji maishani mwake.
“Danny!Danny! Danny!” Alizidi kumwita lakini bado aliendelea kuwa kimya.
Alinyanyuka na kusimama wima akimwangalia kwa macho ya huruma, muda ulikuwa ukizidi kusonga na giza kupungua, alielewa muda mfupi uliofuata ingekuwa alfajiri na ilikuwa ni lazima afanye kila kitu wakati bado kuna giza! Ni hapo ndipo alipojikuta akiamua kumwacha Danny mahali hapo na kusonga mbele, kila kitu akikikabidhi mkononi mwa Mungu! Aliamini kuna wakati binadamu anatakiwa kuchagua moja na haikuwa rahisi kukiongezea uhai kitu ambacho Mungu mwenyewe alikuwa ameamua kife.
Alipiga magoti tena akainamisha kichwa chake na kusogeza mdomo wake karibu kabisa na sikio la Danny na kuanza kuongea masikioni mwake maneno aliyoamini yalikuwa ya mwisho.
“Danny ninakupenda, najua unanisikia! Nakuacha hapa nasonga mbele, kuna mambo mawili yanayoweza kutokea, aidha ninaweza kuungana na wewe ahera muda huuhuu au ukanitangulia kidogo lakini nina uhakika siku moja lazima tutakutana! Penzi lako kwangu lilikuwa la kweli, hakuna mwanaume atakayenipenda kama ulivyofanya wewe!...” Nancy hakumaliza sentensi yake hasira ikampanda, kifo cha Danny kilimuongezea uchungu.
Alinyanyuka na kuanza kukimbia kusonga mbele, hali ilikuwa kimya na hapakuonekana mlinzi yeyote! Hata hivyo hakutaka kujiingiza hatarini, alianza kutambaa kwa tumbo kuelekea mbele ya nyumba alikoamini kulikuwa na mlango. Alifanya kila kitu kwa uangalifu mkubwa akielewa eneo alilokuwepo lilikuwa ni la hatari, mbele kwenye kona akiwa amelala kifudifudi alichungulia na kuona watu wawili wenye bunduki wakiwa wamesimama na kulilinda lango.
“Hawa hawa ndio naanza nao!” Alijisemea na kunyanyuka kisha kuruka kwenda mbele huku risasi zikifyatuka kutoka kwenye bastola yake, kila kitu kilikwenda kama alivyotaka! Walinzi wote wawili walikuwa chini, Nancy alijishangaa alifanya kazi kama mtu aliyepitia mafunzo ya Ukomandoo.
Alikuwa na uhakika kabisa bastola yake ilikuwa inakaribia kuishiwa risasi, alichofanya akiamini mbele yake kulikuwa na kazi kubwa ni kuchukua moja ya bunduki za walinzi waliolala mbele yake! Hapo akawa na uhakika wa kuendelea na mapambano zaidi.
Akiwa mlangoni alisikia sauti za watu wakilia ndani ya jengo hilo, bila kufikiria mara mbili alizitambua sauti, walikuwa ni baba na mama yake! Kulikuwa na sauti nyingine nzito ambazo hakuzitambua. Nancy aliikosa thamani ya maisha yake mwenyewe, hakuona sababu ya kuendelea kuishi wakati wazazi wake walikuwa ndani ya jengo hilo wakiteseka na wakimtegemea yeye kuwaokoa.
“Ni bora kufa!” Alijisemea maneno hayo alichungulia ndani kupitia kwenye tundu la mlango, kulikuwa na mwanga mkali sana ndani ya jengo hilo uliomfanya awaone wazazi wake wakiwa wamelala chini uchi wa mnyama na mwanaume mmoja mwenye nguvu akiwachapa! Alijaribu kumtambua mwanaume huyo kuona kama alikuwa Tonny lakini haikuwa sura ya mtu aliyemfahamu, alielewa walikuwa ni vijana wa mzee Katapila.
Hasira aliyokuwa nayo moyoni mwake ilikuwa haielezeki, alikuwa ni kama Simba aliyejeruhiwa! Tayari alishaua watu wengi na alikuwa amempoteza mpenzi wake, hivyo hakuona sababu ya kushindwa kuingia ndani ya jengo hilo na kujaribu kuwaokoa wazazi wake, ingawa hakuwa na uhakika wa kupata ushindi alikuwa tayari kujaribu.
“Mh! Kumbe mlango haujafungwa?” Alijiuliza baada ya kugundua mlango ulikuwa wazi na hapo hapo bila kusita aliusukuma na kuingia moja kwa moja ndani, mkono mmoja ukiwa umeshika bunduki aina ya SMG aliyoichukua kwa mmoja wa walinzi na mwingine ukiwa umeshika bastola yake ambayo awali ilimilikiwa na mzee Katapila.
Risasi zilimiminika kutoka kwenye SMG na kuwaangusha watu watatu waliokuwa wamesimama wakiwatesa wazazi wake, akasonga mbele mbio hadi mahali hapo akiangaza huku na kule kuona kama kulikuwa na adui mwingine, hakumwona! Kwa sababu hakuwa na uhakika kama maadui waliokuwa chini walikuwa wamekufa alilazimika kuwaongezea risasi nyingine mbilimbili kutoka kwenye bastola yake, akahakikisha alikuwa salama.
“Nan..cy! Nan..cy!Na..ncy, Nancy mwanangu umefi....” Sauti ya mama yake iliongea kwa taabu, hakuweza kuimaliza sentensi yake.
Wazazi wake walikuwa wamelala sakafuni wakiwa wamefungwa kwenye vipande vya magogo, miili yao ilijaa majeraha ya kuchapwa, mzee Katobe hakuwa hata na uwezo wa kuongea lolote na hata mzee Mwinyimkuu pia alikuwa kimya! Ilivyoonekana wanaume walipigwa zaidi kuliko mama yake.
“Namshukuru Mungu mama! Sikutegemea hata kuwatia machoni, nimepita katika magumu mengi na siamini kama nitaweza kuwaokoa lakini acha nijaribu!”
“Hata tusipookoka si mbaya, ili mradi nimekuona mwanangu, nilikuwa na masi...kitiko makubwa sana kufa bila kukuambia maneno ya mwi...sho, kwa hivi sasa niko tayari kufa!Hata baba yako alitamani sana ku..kuona lakini ba.hati mbay...a tan..gu jana hao...ngei” Aliongea mama yake Nancy kwa taabu.
Nancy hakutaka kupoteza muda zaidi ilikuwa ni lazima awafungue kwenye magogo na kuwaweka huru ingawa hakufahamu angeondoka eneo hilo kwa utaratibu gani! Ndio, aliliona gari aina ya Landrover nje wakati akiingia ndani ya jengo lakini hakuelewa ni nani alikuwa na ufunguo wa gari hilo.
Mara moja alianza kumfungua mama yake, kisha baba yake na mwisho kwa mzee Mwinyimkuu lakini kabla hajamaliza alisikia sauti ya Tonny nyuma yake, akitokea kwenye mlango wa nyuma wa jengo hilo! Alikuwa na bastola mkononi, hasira ya Nancy iliongezeka maradufu, alimchukia mwanaume huyo kuliko kiumbe mwingine yeyote lakini hakuwa na la kufanya kwani hakuwa na bunduki mkononi mwake wakati huo, aliiweka pembeni kipindi akimfungua mama yake kutoka kwenye gogo! Kitendo chochote cha kujaribu kuichukua kingemaanisha kifo chake, Tonny asingemwacha hai.
“Nakupongeza sana Nancy kwa kazi nzuri uliyoifanya, wewe ni mwanamke hodari kwa kweli umejitahidi sana kutaka kuwaokoa wazazi wako lakini nakuhakikishia hautafanikiwa kwa hilo! Mambo yalipofika ni pabaya na kuwaokoa kwako kutamaanisha mimi kuingia matatizoni na hatimaye kwenda jela, sasa ni kipi bora? Kwanini nisikuue wewe, kuwaua wazazi wako na baadaye mimi mwenyewe kujimaliza kwa risasi?”
“Tonny ni lazima ukumbuke kuwa mimi na wewe tuliwahi kuwa wapenzi na tulishirikiana mambo mengi, kwanini leo tumefika hapa?” Nancy alijaribu kubembeleza.
“Usijaribu kunilaghai ili baadaye unigeuzie kibao, lazima ufe Nancy! Tena sasa hivi sikupi hata muda wa kusali sala yako ya mwisho!” Alisema Tonny akiwa amemlenga Nancy katikati ya paji lake la uso.
“PAAAAAAAA!” Ndio mlio uliosikika ndani ya jengo hilo.
Je nini kitaendelea?
Je Nancy amepigwa risasi na kufa?

No comments