Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 33


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Danny amechomwa mshale kwenye mbavu wakiwa ndani ya ngome ya shamba la mzee Katapila,hajitambui na kuna dalili kwamba tayari amekwishakufa! Nancy analia kwa uchungu na kukosa jambo analoweza kufanya ili kuokoa maisha ya mchumba wake, anaichukulia hiyo kama kazi ya Mungu na kuamua kusonga mbele hadi ndani ya jengo walimo wazazi wake pamoja na mzee Mwinyimkuu.
Kwa risasi ameua watu wengi na kuwafikia wazazi wake lakini wakati anawafungua kamba, mwanaume asiyempenda na aliyesababisha matatizo yote yanayompata katika maisha yake, Tonny! Anatokea akiwa na bastola mkononi na kumweka chini ya ulinzi akitaka kumuua, muda mfupi baadaye anasikia mlio wa risasi na anaamini risasi hiyo imemwingia yeye.
Je, nini kimetokea? Fuatilia........
Hali ndani ya ghala la mzee Katapila iliwashangaza maaskari walioingia, maiti nne zililala chini moja ikiwa ya mwanamke ambaye hawakumtambua kwa jina! Hawakuamini macho yao walipomwona mzee Katapila ameanguka pembeni akilia kwa maumivu makali kutokana na risasi aliyopigwa pajani, mmoja wa maaskari alimsogelea na kuanza kumhoji maswali juu ya kilichotokea.
“Vipi mzee?”
“Majambazi!”
“Yamekuvamia?”
“Kabisa! Ina maana hamkukutana nayo?”
“Hapana!”
“Kuna gari mmepishana nayo muda si mrefu ikitokea hapa! Ni gari yangu yameondoka nayo!”
“Yakoje?”
“Siyakumbuki vizuri!”
“Yako mangapi?”
“Mawili tu! Mmoja mwanamke na mwingine mwanaume!”
“Pole sana kwa yaliyokupata maana naona wenzako wamefariki dunia! Inabidi tukupeleke hospitali!”
“Sina jinsi ili naomba kama mtawakamata hao majambazi waueni kabisa, askari atakayewapiga risasi nitampa milioni tano!” Aliongea mzee Katapila.
Alikuwa amedanganya kila kitu alichokisema lengo lake likiwa ni kuuficha ukweli na alitaka Nancy na Danny wauawe kabisa ili kuficha siri ya ukweli uliokuwepo, aliamini kama ingegundulika bado alijishughulisha na shughuli za ujambazi sifa yote aliyojipatia katika jamii ingepotea na angeingia matatizoni na pengine kupelekwa jela jambo ambalo hakutaka kabisa litokee.
“Unafikiri wameelekea wapi?”
“Wamedai wanakwenda Tindiga shambani kwangu kwenda kufanya ujambazi mwingine!” Alizidi kudanganya mzee Katapila lengo lake likiwa ni kuwafikishia maaskari ujumbe wa mahali Nancy na Danny walikokuwa wameelekea, hakuna alichokitamani kama kifo chao.
Maiti zote ikiwemo ya Agness zilisombwa na kupakiwa kwenye gari kisha mzee Katapila akafuatia na gari la polisi likaondoka kuelekea Muhimbili njiani kabla ya kufika hospitali maaskari waliwasiliana na wenzao waliolifuatilia gari lililowabeba Nancy na Danny walioamini lilikuwa la majambazi kwa taarifa walizopewa na mzee Katapila.
“Tumekuta limetelekezwa Kimara lakini tukapewa taarifa na wasamaria wema kwamba waliliacha na kukodisha teksi wakasonga mbele kuelekea Barabara ya Morogoro kama wanakwenda Tindiga basi tutawapata, afande Alphonce anasema anafahamu mahali shamba la mzee Katapila lilipo, msiwe na wasiwasi watatiwa mbaroni tu!”
“Tunawatakia kazi njema ila hali haikuwa nzuri ndani ya ghala la mzee Katapila, watu wanne wameuawa na mzee mwenyewe amepigwa risasi kwenye paja lakini hali yake sio mbaya sana!”
“Mnao wale walinzi wa Omega?”
“Ndiyo!”
“Mkihitaji msaada zaidi mnaweza kuwasiliana na kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro!”
“Sidhani kama tunahitaji msaada ila tafadhali pigeni simu Morogoro muwape taarifa juu yetu!”
Waliagana na maaskari ndani ya gari la polisi lililokuwa safarini kuelekea Morogoro liliongeza kasi nyuma yake likiwepo gari la Kampuni ya Omega Security lililojaza walinzi wenye silaha wakiongozwa na kamanda Yesaya, kijana mwenye mwili mdogo lakini mbinu nyingi za kijeshi. Dereva aliuelewa urefu wa safari iliyokuwa mbele yao.
Nusu saa baadaye walikuwa wakivuka kijiji cha Mgeta, gari lao likitembea kwa kasi ya kilometa mia moja na sitini kwa saa lakini bado walikuwa hawajafanikiwa kulipata wala kuliona mbele yao gari walilokuwa wakilifukuza, walishindwa kuelewa gari hilo liliendeshwa kwa kasi gani! Mpaka wanafika Dumila na kukata kona kuelekea Kilosa bado gari lilikuwa halijaonekana.
“Mh!”mmoja wa maaskari aliguna
“Vipi mbona umeguna?”
“Isijekuwa hawa watu wamenyoosha kuingia Morogoro mjini!”
“Haiwezekani! Nyie twendeni hukohuko Tindiga, kama watakuwa hawajafika tutawasubiri!”
Walikubaliana na kuendelea na safari yao, saa moja na nusu baadaye waliingia Kilosa ikiwa ni katikati ya usiku na kuendelea na safari yao hadi Tindiga shambani kwa mzee Katapila ambako waliegesha gari lao mbele ya lango la kuingilia, walinzi wawili walikuwepo na silaha zao mikononi.
“Habari zenu?”
“Nzuri tu habari yako bwana?” Maaskari walijibu.
“Safi tu! Niwasaidie nini?”
“Sisi ni maofisa wa Polisi!”
“Ndio!”
“Kuna majambazi wamemvamia mzee Katapila huko mjini na kuua vijana wake wanne na wakakimbilia huku, hebu tueleze kuna hali gani hapa? Au umeona jambo lolote lisililo la kawaida?”
“Hapana ila..!”
“Ila nini?”
“Kuna kipindi niliona taa za gari zikija lakini gari hilo halikufika hapa, likageuzia pale chini! Nilishindwa kuelewa ni kwanini nikahisi labda kuna watu wamesahau kitu chao mjini Kilosa!”Alieleza kwa kirefu mmoja wa walinzi hao, ni kweli aliliona gari lililowaleta Nancy na Danny lakini hakuwa na habari kama walipita kwenye nyasi na kuzunguka upande wa pili ambako walipanda ukuta na kuingia ndani kuendeleza mauaji.
“Tunaomba tuingie ndani kukagua!”
“Leteni kwanza vitambulisho vyenu, tutaaminije kuwa nyie ni maaskari!”
Maaskari pamoja na walinzi wa Omega Security Guards waliingiza mikono yao mfukoni, kutoa na kisha kuonyesha vitambulisho vyao, walinzi wote wakaamini lakini wakati bado hawajawaruhusu kuingia mlio wa bunduki aina ya SMG ulisikika ndani ya ngome, wote wakashtuka na kwa pamoja wakaanza kukimbia kuingia ndani silaha zao zikiwa tayari, walinzi wa ngome walishindwa kuelewa ni saa ngapi majambazi yaliingia ndani na kwa kupitia mlango gani.
Mlangoni mwa jengo pekee lililokuwemo ndani ya ngome walikuta maiti mbili, hawakutaka kuchelewa mara moja walisukuma mlango na kuingia ndani, mwanaume mmoja alikuwa amesimama wima akiwa na bastola mkononi iliyomlenga mwanamke aliyechuchuma! Bila kujiuliza mara mbili walielewa huyo alikuwa mmoja wa majambazi na askari mmoja aliachia risasi zilizompata mwanaume huyo moja kwa moja begani akadondosha bastola yake.
*****
Alisikia mlio wa risasi, badala ya kuwa imempenya yeye hakuamini kuona Tonny anaanguka chini! Alishindwa kuelewa ni nani aliyefanya kitendo hicho, fikra zake zilimpeleka kwa Danny lakini alilifuta wazo hilo mara moja alipoifikiria hali aliyomwacha nayo wakati anaondoka, hakuwa mtu wa kunyanyuka na kukamata bunduki.
Mara ghafla aliwaona wanaume wengi wakifika eneo hilo na bunduki zao mkononi, wakikimbia huku na kule kuangalia kama kulikuwa na mtu mwingine! Mmoja wao alimfuata akajitambulisha na kuanza kumhoji juu ya kilichotokea, Nancy alilia machozi ya furaha alipogundua walikuwa ni maaskari.
“Wazazi wangu pamoja na mchumba wangu, walitekwa na mzee Katapila akishirikiana na huyu mliyempiga risasi, anaitwa Tonny! Nilitoa taarifa polisi Bagamoyo lakini sikusaidiwa ndipo nikaamua mimi mwenyewe na mchumba wangu ambaye nilimwokoa huko Dar es Salaam kwenye ghala la mzee Katapi...! Lakini jamani kwanini tuzidishe maongezi, mimi naomba tuwachukue kwanza hawa wazee wangu tuwapeleke hospitali, mambo mengine tutaongea baadaye ni vyema tukaokoa maisha kwanza!” Alisema Nancy baada ya kusita.
Maaskari hawakuwa na ubishi, wote walisaidiana kubeba na kupakia maiti zote zilizokuwemo ndani ya jengo hilo na hata zilizokuwa mlangoni kisha kuwabeba wazazi wa Nancy waliokuwa hoi bin taaban kwenda kwenye gari na mara moja kuondoka kuelekea hospitali ya wilaya ya Kilosa iliyokuwa kama kilometa hamsini kutoka eneo hilo, lilikuwa tukio la kusikitisha lililowakosesha raha hata maaskari, walitaka sana kumhoji Nancy maswali juu ya kilichotokea lakini hakuwa tayari kuongea akidai angeeleza kila kitu baada ya kufika hospitali na wazazi wake kutibiwa. Muda wote alikuwa akilia.
******
Danny alizinduka ghafla baada ya fahamu zake kumrejea, alijaribu kusimama wima akashindwa, mwili wake haukuwa na nguvu kabisa! Alikuwa kama mtu aliyefumbua macho kutoka usingizini, kumbukumbu zake hazikuwa sawa! Alijaribu kuzivuta na kuzisogeza karibu ili alewe mahali alipokuwa ni wapi na alikuwa akifanya nini lakini hakufanikiwa kutuliza ubongo wake, mpaka dakika mbili baadaye alipomfikiria Nancy! Kila kitu kilirejea kichwani mwake.
Alikumbuka alivyopigwa mshale na kuanguka chini na mara ya mwisho alipoongea na Nancy, kwa mbali maneno ya kuagwa yaliyosemwa na mpenzi wake wakati akiwa katika upotevu wa fahamu yalimwijia akaelewa Nancy alikuwa ameondoka na kumwacha eneo lile akifikiri alikuwa amekufa baada ya kuchomwa mshale, hakutaka kukubaliana na fikra hizo na kuanza kuliita jina la Nancy.
“Nancy! Nancy!Nancy!” Aliita mara kadhaa bila kuitikiwa, hapakuwa na mtu kabisa ndani ya ngome hiyo hata walinzi waliondoka na magari ya polisi na Omega security Guard kuelekea hospitali ya Kilosa.
Pamoja na maumivu makali aliyokuwa nayo, Danny hakutaka kukata tamaa akazikusanya nguvu zake zote zilizobaki mwilini na kusimama wima akiyumbayumba na baadaye kuanguka chini, alihisi mshale aliochomwa ulikuwa na sumu sababu ya kizunguzungu alichokuwa nacho.
“Kusimama siwezi acha nitambae kuelekea mbele!” Alijisemea moyoni mwake na kunyanyuka tena, safari hii kama alivyowaza hakutaka kusimama alianza kutambaa kuelekea kweney jengo lililokuwa mbele yake! Moyoni mwake alijawa huzuni akiamini kwa vyovyote hata Nancy alishauawa mawazo hayo ndiyo yalimtia ujasiri zaidi, hakuogopa kulisogelea jengo hilo ili kama ni kuuawa basi wammalizie kabisa kuliko kuendelea na mateso aliyokuwa nayo.
Mbele ya jengo hapakuwa na mtu zaidi ya damu zilizotapakaa kila mahali na Danny hakutaka kuingia ndani, alichofanya ni kunyoosha moja kwa moja kuelekea langoni ambako pia hapakuwa na mtu akatoka hadi nje ya ngome na kwenda kulala katikati ya barabara akitarajia gari lolote ambalo lingepita maeneo hayo lazima lingesimama na kumchukua kumpeleka hospitali. Tayari mwanga wa alfajiri ulishaanza kuonekana.
Ghafla giza nene liliyatanda macho pake, moyo wake ukaanza kunywea taratibu, mapafu yakabana pumzi ikawa haiingii kifuani kama ilivyo kawaida huku mwili wake ukilegea, hakuelewa kitu chochote kilichoendelea baada ya hapo.
*********
Safari kuelekea Kilosa ilikuwa bado ikiendelea, Nancy naye alikuwa bado akibubujikwa na machozi akiwa katikati ya wazazi wake pamoja na mzee Mwinyimkuu waliokuwa hoi bin taaban! Hakuwa na uhakika kama baba yake alikuwa hai, muda wote alimwomba Mungu afanye muujiza.
“Ulisema kwamba ulikuja huku na mchumba wako?” Lilikuwa ni swali kutoka kwa mmoja wa maaskari lililorejesha kumbukumbu sawasawa katika kichwa cha Nancy, akanyanyuka na kusimama wima mikono yake yote miwili ikiwa kichwani kwake.
“Vipi?” Mmoja wa maaskari aliuliza baada ya kuugundua mshtuko aliouonyesha.
“Simamisha gari!” Aliamuru.
“Kwanini?”
“Tumemsahau!”
“Nani?”
“Mchumba wangu!”
“Alikuwa sehemu gani?”
“Nyuma ya jengo akiwa amechomwa mshale!”
“Mama yanguuu! Sasa kwanini hukusema?”
“Nilichanganyikiwa nikasahau! Tafadhali dereva simamisha gari!”
Dereva akakanyaga breki na baadaye kusimama, baadhi ya maaskari walihisi anawachanganya akili zao na kuwapa usumbufu, minongíono ya chinichini ilisikika wakati gari linasimama.
“Sasa tufanye kipi? Tuwapeleke wazazi wako hospitali au turudi kwa mchumba wako? Mbona unataka kutuchanganya? Kwanza mambo yenyewe hayajaeleweka, hebu chagua kitu kimoja tafadhali! Baba na mama au mchumba wako?”Meja Alphonce aliuliza na Nancy kukaa kimya, wote walikuwa na umuhimu mkubwa maishani mwake.
Je nini kitaendelea?

No comments