Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 34


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Nancy amefanikiwa kuwaokoa wazazi wake pamoja na mzee Mwinyimkuu, waliotekwa na kufichwa shambani kwa mzee Katapila huko Tindiga Kilosa, yote haya yalifanywa na Tonny kama kisasi baada ya kumkataa, kwa juhudi zake Nancy amefanikiwa kuingia ndani ya ngome ya shamba hilo akiwa na Danny, mwanaume ampendaye ambaye kwa bahati mbaya amechomwa mshale na kuanguka chini, kupoteza fahamu jambo lililomfanya Nancy akate tamaa kwamba asingepona!Akiwa ndani ya jengo Nancy anawekwa chini ya ulinzi na Tonny aliyemlenga na bastola yake kwa lengo la kumuua lakini kabla hajafyatua risasi, Tonny anaanguka chini! Amepigwa risasi na maaskari waliokuwa wakiwafutilia Danny na Nancy kutokea Dar Es Salaam!
Nancy anakataa mahojiano yoyote na polisi kwanza anataka wazazi wake pamoja na mzee Mwinyimkuu ambao hali zao ni mbaya kutokana na mateso waliyoyapata wapelekwe hospitali, amesahau kabisa kuwa Danny yupo nyuma tu ya jengo hilo! Maiti ikiwemo ya Tonny zinabebwa na kupakiwa ndani ya gari na wazazi wa Nancy pamoja na mzee Mwinyimkuu wanapakiwa ndani ya gari jingine na safari ya kuelekea Kilosa hospitali inaanza.
Ghafla wakiwa njiani Nancy anajiwa na kumbukumbu za Danny, anagundua amemsahau mpenzi wake! Hapohapo anamwamuru dereva asimame na anafanya hivyo, Nancy anawasimulia kilichotokea baadhi ya maaskari wanaona anachowaeleza ni usumbufu na wanamwambia achague kimoja wazazi au mpenzi wake? Anachanganyikiwa na anashindwa achague lipi kwani wote ni wa muhimu kwake.
Je, nini kinaendelea? Fuatilia.......
“Chagua!” Askari alisema.
“Siwezi kuchagua!”
“Kwanini?”
“Wote ni wa muhimu kwangu!”
“Mshika mbili?”
“Moja humponyoka!” Badala ya Nancy kujibu askari mwingine alidakia.
Nancy alijitahidi kuwabembeleza kwa uwezo wake wote ili wakubali yeye ashuke kwenye gari lililowabeba wazazi wake, apande gari lililobeba maiti ambazo hazikuwa na sababu yoyote ya kuwahishwa hospitali kwa wakati huo ili wazazi wake wapelekwe hospitali haraka na warudi hadi shambani kwa mzee Katapila kumtafuta Danny! Aliwahikikishia kuwa mtu huyo alikuwa wa muhimu kiasi gani kwake, kiasi kwamba asingeweza kumwacha afie porini, wakati msaada ulishapatikana.
“Una uhakika atakuwa hai?”
“Sina uhakika lakini anaweza kuwa hajafa ingawa hali yake ilikuwa mbaya sana!”
“Kwa hiyo turudi?”
“Nitafurahi sana mkichukua uamuzi huo!”
“Ok! Basi nyinyi tangulieni, sisi tutarudi na huyu binti hadi shambani!” Kamanda Yesaya wa kampuni ya Omega alisema na wakakubaliana, gari likageuzwa na kuanza tena kurudi shambani kwa mzee Katapila, Tindiga. nusu saa baadaye walishafika na kuegesha gari, kabla ya kufika langoni walipishana na simba wawili! Mmoja jike na mwingine dume, walitishika kwani hawakutegemea kama wanyama kutoka Mikumi waliweza kufika maeneo hayo! Nancy akawa wa kwanza kurudi akifuatiwa na walinzi wengine wa Omega na kuanza kukimbia kwenda ndani hadi nyuma ya jengo, Nancy aliangua kilio alipokuta mwili wa Danny haupo mahali alipouacha! Alishindwa kuelewa alikuwa amekwenda wapi, alipita huku na kule kuzunguka maeneo hayo bila mafanikio ya kumwona.
“Una uhakika alikuwa hapa?”
“Kweli kabisa!”
“Nilimwacha hapahapa akiwa na mshale mgongoni!”
“Sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Kwa kweli hata mimi sifahamu!” Alijibu Nancy akilia, baada ya hapo wote walianza kuzunguka huku na kule shambani wakimtafuta bila mafanikio mwisho wakakata tamaa kabisa, muda wote huo Nancy alikuwa akilia mfululizo! Pamoja na kazi yote kubwa aliyoifanya kumwokoa Danny na baadaye wazazi wake alikuwa amempoteza mchumba wake! Walinzi wa Omega walimfariji kadri walivyoweza lakini hawakuweza kumzuia asiendelee kulia, saa nzima baadaye waliondoka shambani na kusafiri kwa kasi hadi hospitali ya wilaya ya Kilosa ambako waliwakuta wazazi wa Nancy pamoja na mzee Mwinyimkuu wakiwa wamelazwa chumba cha wagonjwa mahututi, Nancy aliomba kumwona daktari ili ajue nini kilichoendelea.
“Hali zao ni mbaya lakini watapona!”
“Kweli daktari?”
“Kabisa, matumaini yapo, tatizo lao kubwa lilikuwa ni njaa! Kwa muda mrefu sana hawakupata chakula cha kutosha, ndio maana tumewatundikia dripu za glucose ili kuongeza sukari kwenye miili yao, siku mbili kuanzia sasa watakuwa na uwezo wa kuongea vizuri!”
“Ahsante daktari! Lakini bado kuna tatizo moja linanitatiza!”
“Tatizo gani binti?” Aliuliza Dk. Muhombolage, aliyekuwa akiwashughulikia wazazi wa Nancy.
“Mchumba wangu!”
“Amekuwaje?”
“Tulikuwa naye pamoja wakati tunawafuatilia wazazi wangu, akachomwa mshale na kuanguka, nikamwacha sehemu aliyokuwa ameangukia na kuingia ndani ya jengo ambako niliwaokoa wazazi wangu, bahati mbaya sana nikamsahau wakati wa kuondoka kuja hapa hospitali! Nikarudia njiani kumfuata lakini sikumkuta, sasa sielewi ni wapi alipokwenda! Lazima kutakuwa na mtu amemchukua au kaliwa na Simba tuliokutana nao njiani! Maana kama angekufa tungeikuta maiti yake eneo lilelile!” Alieleza Nancy kwa kirefu daktari akimsikiliza, hakuwa na jambo la kumshauri zaidi ya kuulizia hospitali za jirani za eneo walilokuwa, alipiga simu hospitali ya Kilombero na kuulizia kama kulikuwa na mgonjwa wa aina hiyo aliyekuwa amepokelewa, jibu likawa hapana.
“Labda mtoe taarifa polisi!”
“Ninaoshughulika nao hapa ni polisi, wamekwishafanya hivyo mapema!”
“Basi atapatikana!”
“Haiwezekani daktari atakuwa amekufa!” Alijibu Nancy na kuondoka ofisini kwa daktari kurudi chumba cha wagonjwa mahututi ambako wazazi wake walilazwa, alikaa huko mpaka saa tatu na nusu ya asubuhi polisi walipokuja kutaka kuchukua maelezo yake kwa sababu taarifa walizokuwa wamezipokea kutoka mkoani Morogoro kwa Kamanda wa Polisi ni kwamba yeye Nancy pamoja na Danny ndio walikuwa majambazi waliokuwa wakisakwa baada ya kuvamia ghala la mzee Katapila lililopo Vingunguti jijini Dar Es Salaam, kuua watu, kumjeruhi mzee Katapila na kuondoka na kiasi kikubwa cha fedha!
Hivyo ndivyo mzee Katapila alivyowaeleza polisi na kwa sababu ya uwezo wake kifedha na heshima aliyokuwa nayo katika jamii kipindi hicho, aliaminika na Nancy pamoja na Danny kuonekana watu hatari, hapohapo hospitali Nancy alipigwa pingu mikononi na kubebwa mpaka kituo cha polisi cha Wilaya ya Kilosa, hakutakiwa kujibu chochote mara moja alipakiwa ndani ya gari jingine na kusafirishwa kwenda Dar Es Salaam alikotakiwa kujibu kesi ya mauaji. Alijaribu kuongea kadri alivyoweza kuonyesha hakuwa na hatia lakini hakuna mtu aliyemjali, hivyo ndivyo ilivyoeleweka, Nancy alikuwa muuaji.
Jijini alitupwa moja kwa moja mahabusu kituo kikuu cha polisi, alipotolewa baadaye ulikuwa ni wakati wa kutoa maelezo yake juu ya kilichotokea, jopo la maaskari wa ngazi za juu walikuwepo kusikiliza maelezo ya msichana huyo yakichukuliwa! Nancy huku akilia alianza kusimulia kila kitu kilichotokea maishani mwake tangu mwanzo wakiwa Bagamoyo na wazazi wake, walivyompokea Tonny nyumbani kwao, kuishi naye, kumsomesha mpaka nchini China wakitegemea angekuja kuwa mume mwema wa binti yao lakini ghafla akaja kubadilika, akawa nyoka na kumtelekeza Nancy kwa ajili ya msichana mwingine ambaye naye alikwenda kumfanyia unyama wa aina hiyohiyo ndipo akarudi nchini Tanzania na kutaka kumuoa tena Nancy ambaye kwa wakati huo tayari alikuwa na mchumba mwingine. Hakuyasahau mambo ya Bagamoyo kula yamini kwa mganga wa kienyeji ambayo baadaye ilikuja kumfanya awe mwendawazimu.
“Kuna mzee mmoja ambaye yuko Kilosa hospitali pamoja na wazazi wangu, anaitwa mzee Mwinyimkuu huyo ndiye mganga mwenyewe aliyenilisha yamini na baadaye akapatikana na kuiondoa ndio maana akili yangu ikarejea tena kawaida! Tonny akawa ameng’ang’ania kunioa lakini kwa mabaya aliyonifanyia nilikataa na kutaka kuolewa na Danny, hilo lilimkera ndio maana akamkodisha mzee Katapila ili awateke wazazi wangu! Lakini kuna kitu kingine hapohapo, Danny alipoamua kunioa mimi alimwacha msichana aitwaye Agness, huyo naye kwa hasira zake akamfuata mzee Katapila huyohuyo na kumkodi ili amteke Danny! Hilo likafanyika, akatekwa na kufichwa Vingunguti lakini mimi niliapa ni lazima nimkombe Danny, niwakomboe wazazi wangu na mzee Mwinyimkuu na baadaye wadogo zangu ambao walichukuliwa na wazee wawili waishio Kisiwani katikati ya ziwa Tanganyika!” Aliongea Nancy kwa karibu masaa mawili akisimulia kila kitu kuonyesha ni kiasi gani hakuwa na hatia na mtu mbaya alikuwa mzee Katapila.
“Kweli?”
“Sina sababu ya kudanganya! Huo ndio ukweli ila kama mtaamua kunigandamiza mimi sababu ya umasikini wangu, sawa! Sitakuwa na la kufanya ila niliyoyasema ndio ukweli!”
“Hivi sasa mzee Katapila yuko wapi?” Kamanda wa polisi wa mkoa alimuuliza Mkuu wa Upelelezi.
“Bado yuko Muhimbili!”
“Afungwe pingu hapohapo kitandani!”
“Sawa Afande!”
“Huyu msichana hana hatia! Tena ni miongoni mwa wasichana shujaa kuliko ambao nimewahi kukutana nao, amefanya kazi ya kipolisi wakati sisi tuko hapahapa!” Kamanda alifoka.
“Mheshimiwa Kamanda naomba nikueleze ukweli juu ya jambo hili, siku nyingi niliwahi kutoa taarifa kituo cha polisi Bagamoyo lakini hakuna aliyejali, nilionekana muongo! Maaskari wengi wanamuogopa sana mzee Katapila, hilo ndilo linamfanya awe mtu mbaya anayeonea watu kila siku na hachukuliwi hatua yoyote!”
“Suala hili nitaliingilia mwenyewe binti mpaka haki itendeke! Kwa hivi sasa tunakuacha huru, ukimaliza kutoa maelezo yako unaweza kuondoka lakini uripoti hapa siku ya Jumatatu, au mnaonaje?”
“Sawa Mkuu!” Wengi wote waliitikia.
Baada ya maelezo Nancy hakuwa na jambo jingine la kufanya kituoni, alimshukuru Mungu na kutoka nje ambako alikutana na waandishi wa habari wengi wakimsubiri na kuanza kumpiga picha huku wakimuuliza maswali mengi juu ya kilichotokea, aliwasimulia ingawa kwa kifupi na baadaye kuondoka mbio hadi stendi ya daladala ambako alipanda basi lililompeleka hadi kituo cha Mabasi cha Ubungo ambako alipanda basi la Shabiby lililomsafirisha hadi Morogoro ambako alipanda basi jingine lililomfikisha Kilosa, hiyo ikiwa ni siku ya Jumamosi saa kumi na mbili jioni.
Hali ya wazazi wake wodini ilikuwa nzuri, aliweza hata kuongea nao! Wote walimshukuru kwa ujasiri aliouonyesha hata mzee Mwinyimkuu lakini hawakuacha kuuliza wapi alikokuwa Danny, Nancy alilia wakati akiwaeleza alivyochomwa mshale maiti yake kupotea! Mpaka wakati huo aliamini Danny alikuwa marehemu, wazazi wake wote wakiwa kitandani walimwaga machozi hata mzee Mwinyimkuu hakuweza kujizuia, baadaye walikubaliana na ukweli huo na kuyaacha yote mikononi mwa Mungu.
“Yaani kweli Danny amefariki pamoja na wema wote aliokuwa nao? Haiwezekani!” Mama yake Nancy aliongea akiwa kitandani.
“Nina wasiwasi alilia na Simba!” Alisema Nancy.
“Kwanini unawaza hivyo?”
“Tulikutana na Simba wawili kabla hatujafika shambani!”
Je nini kitaedelea?
Tukutane Ijumaa mahali hapa

No comments