Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 35


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
Wazazi wa Nancy pamoja na mzee Mwinyimkuu wamepelekwa hospitali ya wilaya ya Kilosa kwa matibabu baada ya kuokolewa kutoka mikononi mwa wauaji! Hizi ni juhudi za mtoto wao Nancy aliyeapa kupoteza maishani ili kuwaokoa wazazi wake.
Lakini anafanya kosa moja kubwa la kumsahau shambani kwa mzee Katapila mchumba wake Danny aliyechomwa mshale mbavuni, analikumbuka kosa hili wakiwa njiani na kuwataarifu polisi, anawaomba wamrudie na wanakubali lakini walipofika mahali alipomwacha walikuta mwili wa Danny haupo, hisia zao zinawafanya waamini kijana huyo ameliwa na Simba kwa sababu walikutana na Simba wawili njiani.
Ni jambo hili ndilo Nancy anawasimulia wazazi wake baada ya kurudi hospitali kutoka shambani akiwa na uhakika Danny hakuwa hai! Je aliliwa na Simba kweli?
Sasa endelea......
“Kwa hiyo inawezeka aliliwa na Simba?” Mama yake Nancy aliuliza.
“Huo ndio wasiwasi wangu kwa sababu hatujamkuta mahali nilipomwacha akiwa amechomwa mshale!”
Kila mtu alisikitika, wazazi wa Nancy walilia machozi kila walipokifikiria kifo cha Danny, hakuna aliyekuwa tayari kuamini kwamba Danny alikuwa marehemu pamoja na wema wote alioufanya! Lawama zote walimtupia mzee Katapila baada ya Nancy kuwasimulia namna mzee huyo alivyoshiriki katika mikakati ya utekaji!
Hakuna alichostahili mzee huyo zaidi ya kifungo cha maisha gerezani au kunyongwa kabisa kwani alisababisha vifo vya watu wengi. Agness na Tonny walikuwa marehemu, mtu pekee aliyekuwa amebaki hai alikuwa mzee Katapila aliyekuwa hospitali akiendelea kutibiwa jeraha la risasi alilokuwa nalo lakini akiwa amefungwa pingu kitandani kwake..
Kitu kingine kilichowasikitisha zaidi wazazi wa Nancy ni watoto Catherine na David, kitendo cha kuambiwa walitekwa na mzee Kiwembe pamo ja na babu Ayoub na kurudishwa kisiwani kiliwachanganya na walishindwa kuelewa nini kingefanyika kuwakomboa watoto hao, Nancy aliwaondoa wasiwasi na kuwaeleza kazi hiyo ingekuwa yake mpaka kuhakikisha watoto wote wanarudi katika himaya ya wazazi wake.
“Utaweza?”
“Nitaweza baba!”
“Angekuwepo Danny mngeweza kusaidiana!”
“Msiwe na shaka na ninafikiri nitapata msaada wa polisi kwa sababu wamekwishaelewa tatizo liko wapi!”
“Itakuwa ni vyema kama nao watakombolewa!”
Mzee Mwinyimkuu alikuwa mtu kwanza kuruhusiwa kutoka hospitali, hakutaka hata kuishi siku mbili mjini Kilosa, alichofanya ni kuaga na kuondoka hadi Morogoro ambako alipanda mabasi yaliyomrejesha hadi Dar Es Salaam, kwa pesa kidogo alizopewa na Nancy aliweza kusafiri hadi Kigoma ambako aliendelea na safari yake kupitia ziwa Tanganyika hadi Kongo. Aliapa kutoyasahau yaliyompata Tanzania, wiki moja baadaye baba na mama yake Nancy walikuwa na hali nzuri pia wakaruhusiwa na kurejea Dar Es Salaam na baadaye Bagamoyo, wakawa wamerejea katika maisha yao ya kawaida.
Watu waliowafahamu, majirani na marafiki wilayani Bagamoyo walipopata habari ya kurudi kwao walifurahi kupita kiasi, ilikuwa ni sherehe kubwa lakini walisikitika walipoambiwa Danny alifariki dunia! Taarifa hizo baadaye mzee Katobe alipopata nafuu alirejea tena Dar Es Salaam wizara ya Mambo ya nchi za nje na kutoa taarifa ili wazazi wa Danny waliokuwa nje ya nchi kwenye ubalozi wajulishwe juu ya kifo cha mtoto wao, hata wafanyakazi wa wizara hiyo waliomfahamu Danny walilia machozi ya uchungu, si hao tu bali pia wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam waliosoma naye darasa moja kabla hajakatisha masomo kwa ajili ya Nancy walisikitika na kuiomba serikali imchukulie mzee Katapila hatua kali kwa kitendo cha unyama alichokifanya.
Siku tatu baada ya mzee Katobe kutoa taarifa wizara ya Mambo ya nchi za nje, baba na mama yake Danny waliwasili nchini wakiwa na huzuni kubwa, Danny alikuwa mtoto wao wa pekee! Hivyo kifo chake kilimaanisha wasingekuwa na mtoto mwingine tena, ulikuwa msiba mkubwa sana kwao! Cha kushangaza hawakua na hamaki yoyote kwa mzee Katobe na familia yake, walichofanya wao ni kurudi tena shambani kwa mzee Katapila na kuendelea kuitafuta maiti ya mtoto wao, kwa wiki mbili walifanya kazi hiyo bila mafanikio hatimaye wakakata tamaa kabisa! Hapakuwa na mazishi ya Danny, lakini kila mtu aliamini mtoto huyo hakuwa hai.
“Kwa kweli tumeumia lakini hatuna la kufanya, ulikuwa mpango wa Mungu!”
“Poleni sana hata sisi pia tuna masikitiko makubwa sana! Matatizo yote yaliyotupata sisi tunayaona ni madogo sana kuliko kumpoteza Danny!”
“Hakuna shida! Lililopangwa na Mungu mwanadamu hawezi kulikwepa!” Mama yake Danny alisema.
Wote waliamini walikuwa wameumia lakini kama maumivu yao yangepimwa kwenye mzani, kuna mtu mmoja angewazidi wote! Kifo cha Danny kilikuwa pigo kubwa maishani mwake, hakika asingeweza kukutana na mtu mwingine kama yeye mpaka kaburini kwake! Huyo hakuwa mwingine bali Nancy, kwake kila siku kilikuwa ni kilio na majonzi pamoja na kufanikiwa kuwaokoa wazazi wake, haikutosha! Kutokuwepo kwa Danny maishani mwake lilikuwa pengo lisilozibika.
Hakula chakula kwa karibu wiki nzima, alikonda na kunyongĂ­onyea mpaka ikafikia wakati wazazi wake wakaanza kuwa na wasiwasi angekufa kwa njaa na kulazimika kumpeleka hospitali ambako alitundikiwa dripu ya sukari zilizomtia nguvu mwilini mwake, kilichofuata baada ya hapo ni ushauri Nasaha uliomwimarisha na kumfanya aukubali ukweli wa yote yaliyotokea! Nancy akasimama imara tena na mipango ya kwenda kisiwani Galu kuwaokoa wadogo zake ikaanza kuzunguka ubongoni mwake na alitaka kuondoka wakati wowote lakini polisi walimzuia mpaka atoe ushahidi mahakamani.
“Kwani kesi hiyo haiwezi kuendelea bila mimi kuwepo?” Alimuuliza Mkuu wa kituo cha polisi Bagamoyo wakati akijiandaa na safari yake kwenda Kigoma.
“Haiwezekani! Ushahidi wako ni wa muhimu sana!”
“Nina kazi nyingine ya kufanya!”
“Kazi gani?”
“Nahitaji kuwafuatilia wadogo zangu!”
“Wadogo zako wapi?”
“Kwenye maelezo yangu nilishasema kuwa wadogo zangu nao walitekwa!”
“Na mzee Katapila?”Mkuu wa Kituo aliuliza.
“Hapana!”
“Na nani tena?”
“Wako wazee wawili waliowahi kuniteka mimi na mama yangu!”
“Lini tena? Mbona maisha yenu yamejaa historia za kutekwa?”
Ilibidi Nancy asimulie tena kilichotokea mpaka yeye na mama yake wakajikuta wapo katika kisiwa cha Galu ambako walipata mateso yaliyomfanya alie machozi wakati akisimulia, mkuu wa kituo alibaki mdomo wazi! Hakuwa tayari kuamini kama mambo yote hayo yalimpata msichana aliyekuwa mbele ya meza yake, ilionyesha kama Tanzania haikuwa na Serikali, isingewezekana mtu afanye ukatili wa aina hiyo na asichukuliewe hatua.
“Kwa hiyo huko Kisiwani ndio unakotaka kwenda?”
“Ndiyo!”
“Huhitaji kwenda! Jeshi la polisi litaifanya kazi hiyo!”
“:Siwaamini polisi! Si unakumbuka niliwahi kuwataarifu juu ya kutekwa kwa Danny pamoja na wazazi wangu lakini hamkutilia maanani!”
“Tuyasahau ya zamani, nitawasiliana na Kigoma na jeshi la polisi ndilo litakayokwenda hadi Kisiwani na kufanya ukombozi, hao wazee ni lazima wafikishwe mbele ya sheria, nakushauri utulie Nancy ili uwepo wakati kesi ikiendelea!”
“Kwa hiyo unanieleza kwamba niwaamini polisi?”
“Wala usiwe na shaka, utawala uliopo hapa Bagamoyo kwa sasa ni tofauti na zamani, mkuu wa kituo aliyekuwepo alihamishwa kwenda Makao makuu baada ya kufanya makosa fulani, likiwemo hilo la kutofuatilia mambo!”
“Ina maana wewe nikuamini?”
“Asilimia mia moja nitalifanyia suala lako kazi hadi wadogo zako wapatikane!”
“Acha nione!”
Akiwa bado yupo ofisini, mkuu wa kituo alinyanyua simu na kumpigia Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani na akimtaarifu juu ya tukio alilolisikia toka kwa Nancy, kwa kumwangalia machoni wakati akiongea, Nancy alielewa ni kiasi gani hata Kamanda wa Polisi wa Mkoa alikuwa ameshtuka, kwa maneno aliyoyasikia kutoka mdomoni kwa mkuu wa kituo, aliamini hatua za haraka zingechukuliwa! Mpaka anaondoka hicho ndicho kitu kikubwa alichokiamini, alipofika nyumbani aliwasimulia wazazi wake mambo yote yaliyojitokeza polisi nao wakamshauri jambo hilo hilo.
“David na Catherine ni watoto wetu lakini nina uhakika huko waliko, maisha yao hayako hatarini sana!Bado polisi wanaweza kuifanya kazi uliyotaka kuifanya wewe na kuikamilisha, waache waendelee! Wape mwezi mmoja kabla hujafikiria jambo jingine!” Mama yake Nancy aliongea.
Taarifa juu ya kuwepo kwa watoto waliotekwa na kufichwa katika kisiwa cha Galu kilichopo katikati ya Ziwa Tanganyika zilifika hadi makao makuu ya jeshi la polisi ambako amri ilitolewa kwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Kigoma kuwa, kiundwe kikosi maalum kwa ajili ya ukombozi wa watoto hao! Jumla ya askari ishirini walikusanywa, wakakabidhiwa silaha na kuondoka ndani ya boti mbili ziendazo kwa kasi kuelekea kisiwani Galu, hakikuwa kisiwa kigeni kwao kwani mara kwa mara walikiona wakiwa katika doria za kusaka magendo na wavuvi haramu, lakini hata siku moja hawakuwahi kufikiri kuwa binadamu waliishi ndani ya kisiwa hicho.
Walikuwa na matumaini makubwa ya kurudi na ushindi, wakiwa na watoto pamoja na watekaji ambao wangefikishwa mbele ya sheria mara moja! Hiyo ndiyo kazi waliyokuwa wamepewa na Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kigoma. Isingewezekana watu wawili washindane na askari ishirini wenye silaha waliokuwa tayari kuua ili mradi watoto David na Catherine wakombolewe.
“Jamani sikilizeni!” Mmoja wa maaskari alisema
“Vipi?”
“Tunakwenda kupambana na watu tusiowafahamu!”
“Kwa hiyo?”
“Mimi hawa wazee wa Kiha huwa siwaamini, wanaweza kuwa na ndumba halafu tusifanikiwe kufanya lolote!”
“Wewe acha bwana, umeshaanza imani za kishirikina, wewe twende kazini, acha kutuvunja moyo!”
Yalikuwa maongezi ndani ya boti moja ya polisi wakizidi kusonga mbele, kisiwa cha Galu kilishaanza kuonekana mbele yao! Walikuwa na uhakika katika muda wa dakika thelathini wangekuwa wanagoa kwenye ufukwe wa kisiwa hicho, kila mmoja wao aliweka bunduki yake tayari kwa kazi iliyokuwa mbele. ilikuwa ni lazima warejee na watoto hata kama watekaji wangeuawa, hilo ndilo lilikuwa lengo lao na walijua ingekuwa ni kazi ndogo sana kwao.
Ghafla wakiwa wamebakiza kama mita mia mbili hivi ili wagoe kisiwani, kitu kama kimbunga cha ajabu kiliibuka kutokea nyuma yao kikiyazungusha maji kwa nguvu isiyo ya kawaida! Pamoja na kusafiri siku zote katika ziwa Tanganyika, kila mmoja wao alikiri kimbunga hicho hakikuwa cha kawaida, bila kutegemea hofu ya kifo ilitanda! Hakikuwazungusha watu waliokuwa kwenye boti moja tu, bali ilikuwa hekaheka hata kwa boti ya pili! Walipiga kelele wakiitana na kuombana msaada lakini hapakuwa na mtu wa kumsaidia mwenzake, hali ilikuwa mbaya na muda mfupi baadaye boti zote mbili zilibinuliwa na kuwamwaga maaskari majini! Walishindiwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kimetokea kwani hata maji waliyodumbukia ndani yake yalikuwa na joto kali kama yaliyokuwa yakichemshwa jikoni, wote walilia kwa jinsi walivyoungua.
“Naungua!Naungua!Naungua!” Maaskari walisikika wakilia.
********
Kesi ya mzee Katapila ilivuta usikivu wa watu wengi jijini Dar Es Salaam, mahakama ilifurika kila ilipotajwa! Watu walichukizwa na kitendo alichokifanya, ingawa ujambazi ilikuwa ni sifa yake kwa muda mrefu lakini walishtuka, haikuwa rahisi mtu aliyesaidia jamii kama yeye kuwa bado aliendelea na tabia ya kikatili namna hiyo! Vyombo vya habari viliripoti maendeleo yote ya kesi, kwa sababu hiyo hapakuwa na njia yoyote ambayo mzee Katapila angeitumia kucheza na mfumo wa sheria, hakuna Hakimu aliyekuwa tayari kupokea rushwa ili kupindisha sheria kwani viongozi wote wa serikali waliifuatilia kesi hiyo kwa macho na masikio yao yote.
Hakuwa na namna ya kujitetea, ushahidi ulikuwa umembana kila upande! Hakuwa yeye peke yake katika keshi hiyo bali pia baba yake mdogo Agness mzee Shao, aliyekwenda kwake na kumlipa fedha ili afanye utekaji! Wote walikuwa na kesi ya kujibu na pamoja na kuwa na mawakili wazuri bado haikusaidia, walijikuta wakihukumiwa kwenda jela miaka thelathini kwa mzee Shao na Katapila alihukumiwa kifungo cha maisha! Badala ya kusikitika wakazi wa jiji la Dar Es Salaam waliruka juu na kushangilia.
Hata Nancy pamoja na wazazi wake pia walifurahi kupita kiasi lakini furaha hiyo haikutosha, kwani David na Catherine walikuwa bado hawajapatikana na taarifa zilizopatikana kutoka Kigoma ni kwamba maaskari waliotumwa walishindwa kukifikia kisiwa kwa sababu ya dhoruba kali iliyojitokeza kila walipokikaribia! Jumla ya askari sabini na sita walishapoteza maisha kiasi cha jeshi la polisi kuanza kukata tamaa hasa walipofikia roho zilizopotea wakilinganisha na walizokuwa wakijaribu kuziokoa. Maneno kuwa wazee waliokalia kisiwa hicho walikuwa wachawi yalitawala lakini jeshi la polisi halikuwa tayari kwenda kwa mganga wa Kienyeji ili lifanikiwe kufika kisiwani Galu, walidai hiyo haikuwemo katika PGO, yaani Police General Order, au maagizo ya namna polisi wanavyotakiwa kufanya kazi.
“Nafurahi mzee Katapila amehukumiwa kifungo cha maisha, lakini moyo wangu haujatulia mpaka David na Catherine wapatikane! Kama polisi wameshindwa basi nitakwenda mwenyewe!” Nancy aliwaambia wazazi wake.
Je nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu mahali hapa.
Unaweza kushare uwezavyo.

No comments