Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 36


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
ILIPOTOKA...
Nancy amefanikiwa kuwakomboa wazazi wake ingawa ameshindwa kuokoa maisha ya Danny! Mzee Katapila anahukumiwa kifungo cha maisha gerezani na baba yake mdogo na Agness, mzee Shao amehukumiwa kifungo cha miaka thelathini jela kwa kushirikiana na mzee Katapila katika utekaji.
Kwa mtu mwingine yeyote kazi ingeonekana kuwa imekwisha lakini kwa Nancy, kazi bado! Hivi sasa anafikiria kwenda kuwakomboa wadogo zake waliotekwa kwenye kisiwa cha Galu katikati ya ziwa Tanganyika, kazi inayoonekana kulishinda jeshi la polisi sababu ya miujiza inayowapata maaskari wanaojaribu kwenda kisiwani humo, tayari maaskari sabini na sita wamekwishapoteza maisha.
Je, Nancy atakwenda kisiwani? Endelea........
Habari za kisiwa cha Galu na maajabu yaliyokuwa yakitokea, vilivuta usikivu wa kila mtu mjini Kigoma na Tanzania nzima kwa ujumla! Idadi ya polisi waliopoteza maisha ilipofikia mia moja na ishirini ilibidi jeshi la polisi nchini liamue kusitisha operesheni hiyo, baadhi walianza kutoamini kuwa kweli kulikuwa na watoto wawili katika kisiwa hicho waliotekwa! Kulikuwa na kila dalili kuwa uchawi ulitumika, miujiza iliyotokea ilimshangaza karibu kila mtu.
“Kisiwa gani hiki kisichoingilika?” Ndilo swali walilojiuliza wakuu wa Polisi, karibu wakuu wote wa jeshi la polisi walikuwa mjini Kigoma.
“Hata sisi tunashangaa, visiwa vyote katika ziwa Tanganyika vinaingilika lakini hiki kimetushinda kabisa!”
“Au mzizi?”Mkuu wa ufuatiliaji wa majanga katika jeshi la polisi, Kamshina Aziz aliuliza
“Hivyo ndivyo inavyoaminika na mimi nalazimika kukubaliana na jambo hilo kwani ukikikaribia kisiwa cha Galu hali hubadilika ghafla, mawimbi makubwa hujitokeza na hata mkifanikiwa kufika kila atakayekanyaga ardhi ya kisiwa huanza kusikia moto unamuunguza mwili mzima!”
“Jeshi la Polisi haliwezi kujiingiza katika mambo ya kishirikina, mfano kwenda kwa waganga kuagulia ili kuelewa nini cha kufanya hata hivyo lazima tutafute mbinu ya kuingia katika kisiwa hicho na kuwakomboa watoto waliotekwa!”Mkuu wa jeshi la Polisi nchini alisema.
“Lakini Kamanda, huoni kama tumepoteza idadi kubwa ya maaskari kwa sababu ya watu wawili?”
“Hatuwezi kuacha ni lazima tuendelee ila simamisheni kwanza zoezi, turudi Dar Es Salaam tukajipange upya!”
Hayo ndiyo yalikuwa maamuzi ya jeshi la polisi nchini, jitahada zote zilizokuwa zikifanyika kwa lengo la kuwakomboa watoto David na Catherine, zilisimama! Hivyo ndivyo vyombo vya habari vilivyoripoti na Nancy pamoja na wazazi wake kuzipata habari hizo, haikumwingia Nancy akilini ni hapo ndipo alipoona kulikuwa na kazi ya ziada ya kufanya, hakuwa tayari kuwapoteza wadogo zake kama alivyompoteza Danny kwa kuliwa na Simba.
“Baba!” Alimwita baba yake.
“Naam mwanangu!”
“Haiwezekani!”
“Kwanini?”
“Siwezi kupoteza watu watatu kama nimefanikiwa kuwakomboa wewe na mama, vivyo hivyo ningependa kuwakomboa Catherine na David!”
“Ni sawa lakini...”
“Lakini nini baba?”
“Kwa jinsi tunavyosikia, kisiwa cha Galu kina mambo mengi mabaya, tusingependa kukupoteza wewe pia! Tutakuwa hatuna mtoto kabisa, maisha yetu yameharibika sana tunakuhitaji sana Nancy!”Mzee Katobe alimwambia binti yake.
“Nakuelewa baba lakini hatuwezi kuwaacha David na Catherine wakae kisiwani Galu katika mateso! Mimi nawapenda na bila shaka nyinyi pia, au sio mama?”
“Ni kweli lakini inabidi tukubaliane na ukweli uliopo!” Mama yake alijibu.
Wazazi wake wote walikuwa na huzuni na walionyesha ni kiasi gani mioyo yao ilikuwa na wasiwasi, walimpenda sana Nancy na hawakutaka kumpoteza! Walijaribu kadri ya uwezo wao wote kumshawishi Nancy abadili msimamo wake lakini haikuwezekana, aliendelea kusisitiza ni lazima aende ziwa Tanganyika hadi kisiwani Galu na kuwakomboa wadogo zake, aliamini jambo hilo liliwezekana ingawa si kwa asilimia mia moja, alielewa ilikuwa ni kazi ngumu sana kwani idadi ya maaskari walipoteza maisha ilimtisha! Lakini haikumvunja moyo na kumfanya ahofie kwenda kisiwani.
Kwa wiki nzima waliongea na Nancy lakini haikuwezekana kabisa kumbadili mwisho wakamruhusu aende, mzee Katobe alikwenda benki na kuchukua sehemu ya akiba iliyokuwa imebaki na kumkabidhi Nancy milioni mbili zimsaidie katika kazi yake! Hawakutaka kumwacha aondoke hivyo hivyo ilibidi tambiko la kijadi lifanyike, mzee Katobe na mke wake walitafuta maziwa yaliyokamuliwa katika ng’ombe asubuhi, wakayaleta nyumbani na kumwosha mtoto wao kwa maji ya mtungini wakimsugua kwa mtama uliosagwa kwenye jiwe na walipomaliza walimkalisha mlangoni wakawa wanabugia maziwa mdomoni na kumpulizia mtoto wao mwili mzima huku wakiomba baraka zimwogoze na kumlinda aendako!
Kazi ilipomalizika Nancy alifungiwa ndani ya nyumba bila kuruhusiwa kutoka na jioni ya siku hiyo ilifanyika sherehe iliyohudhuriwa na watu watatu tu, Nancy, mama na baba yake! Ilikuwa ni kama pasaka, siku ya kuagana na wazazi wake! Hakuwa na uhakika wa kurudi salama katika operesheni aliyokuwa anakwenda kuitekeleza, yeye mwenyewe aliita Operesheni kata roho! Hakuogopa wala kuwa na wasiwasi moyoni mwake, hakuona sababu ya kuendelea kuishi kama maisha yake yalishaharibika na mwanaume aliyempenda alikuwa ni marehemu! Hivyo kwa Nancy kifo kilikuwa kitu sahihi kwa wakati huo, isitoshe alielewa mwisho wa maisha ya kila mwanadamu ni kifo.
“Sasa kwanini nisife wakati najaribu kuokoa maisha ya wadogo zangu? Sina sababu ya kuishi kama Danny alishafariki dunia, watu wakuwaonea huruma ni baba na mama yangu lakini sina jinsi kwa sababu pia jukumu la kuwaokoa Catherine na David ni langu!” Aliwaza
Siku iliyofuata Nancy aliondoka Bagamoyo na kusafiri hadi Dar Es Salaam ambako alipanda treni lililomsafirisha hadi Kigoma na kufika baada ya siku tatu akiwa amechoka hoi bin taaban, ingawa Polisi walishasitisha zoezi la kuwakomboa Catherine na David bado siku iliyofuata Nancy alipoamka na kutoka katika hoteli ya Lubumbashi aliyofikia alikwenda moja kwa moja Makao makuu ya polisi ya mkoa wa Kigoma ambako aliomba kuonana na Kamanda wa Polisi wa mkoa, haikuwa kazi ngumu sana kumpata hasa alipojitambulisha kwa kutaja jina lake na uhusiano aliokuwa nao na watoto waliokuwa kisiwani! Jina lake lilishakuwa maarufu masikioni mwa polisi kutokana na kitendo cha kijasiri alichokifanya wilayani Kilosa na kuwakomboa wazazi wake.
“Unataka kumwona Kamanda?”Msichana wa mapokezi alimuuliza.
“Ndio!”
“Subiri kidogo nimuulize kama ana nafasi ya kukuona!” Alijibu msichana huyo na baadaye kupiga namba ya bosi wake, yeye pia hakuwa na kizuizi Nancy akaruhusiwa na kupandisha ngazi hadi ofisini kwa Kamanda ambako Nancy alieleza nia yake ya kujaribu kwenda Kisiwani Galu kuwakomboa ndugu zake, Kamanda wa polisi alimwangalia kwa macho ya huruma yaliyoonyesha wazi ilikuwa kazi ngumu kiasi gani kwa mtoto wa kike kama yeye kuweza kufanya kazi iliyowashinda wanaume tena askari wa Jeshi la Polisi..
“Utaweza binti?”
“Sina uhakika lakini nataka kujaribu!”
“Bahati nzuri nimepokea ujumbe wa polisi kutoka Dar Es Salaam kuwa kuna kikosi maalumu kinatumwa kwa ndege leo na kitafika hapa mchana, labda ungewasubiri askari wetu uongozane nao!”
“Nipo tayari kufanya hivyo!”
“Basi hakuna tatizo!” Kamanda alijibu na kumruhusu Nancy aondoke, kabla hajatoka alikumbuka kitu akageuka na kumwangalia Kamanda.
“Vipi?”
“Nitajuaje kama wamefika?”
“Aha! Nakushauri uje hapa saa sita mchana!”
“Ahsante!”
Habari aliyopewa na Kamanda ilimpa matumaini zaidi na kumtia nguvu zaidi ya alizokuwa nazo, alirudi hotelini ambako alijifungia chumbani kwake na kuendelea kuvuta fikra juu ya kazi iliyokuwa mbele yake, alikuwa ameamua kuwakomboa wadogo zake hata kama ingegharimu maisha yake mwenyewe, alipenda kusinzia mpaka muda aliopewa ufike lakini haikuwa hivyo, alikuwa macho mpaka saa tano na nusu alipoondoka kurejea kituoni, hali aliyoikuta kituoni mchana huo ilimshangaza! Ilikuwa tofauti na asubuhi alipofika kituoni kuonana na Kamanda, kulikuwa na idadi kuwa ya maaskari waliovaa tofauti na askari wa kawaida! Walionekana wazi ni wazamiaji wa majini, bila kuuliza alielewa ndio waliokuwa wakitegemewa kutoka Dar Es Salaam, alichofanya ni kupandisha moja kwa moja hadi ofisini kwa Kamanda wa Polisi.
“Wamekwishafika na nusu saa ijayo mtakuwa safarini kwenda Kisiwani Galu, una silaha?”
“Hapana!”
“Unategemea kupambana na nini?”
“Silaha itapatikana hukohuko!”
“Basi jiandae!” Kamanda aliongea akionyesha wasiwasi mwingi na mwisho wa maongezi yake alijaribu kumshawishi Nancy abaki Kigoma ili polisi waende peke yao na kumletea taarifa au kuja na watoto kama wangefanikiwa kuwakomboa lakini Nancy alikataa katakata na kusisitiza aruhusiwe kuambatana na Polisi.
“Lakini una uhakika watoto wako Kisiwani?”
“Asilimia mia moja kwa sababu waliowateka ninawafahamu!”
“Kivipi?”
Ilibidi Nancy amsimulie Kamanda kila kitu kilichotokea maishani mwake mpaka akajikuta yupo kisiwani Galu, ni maneno hayo ndiyo yalimfanya Kamanda aone umuhimu wa Maaskari kuongozana na Nancy kwa sababu alikielewa vizuri kisiwa hicho! Nusu saa baadaye kweli waliondoka hadi ziwani kulikokuwa na boti zilizoandaliwa tayari, wote walipanda na safari ya kwenda Galu ilianza!Maaskari wote waliokuwa ndani ya boti walivaa kizamiaji wakiwa na mitungi ya hewa ya oksijeni migongoni mwao na mpira uliofungwa moja kwa moja kwenye pua zao, Nancy pia alifungiwa mtungi mmoja mgongoni pia akavishwa boya moja kifuani kwake ili limsaidie kama ingetokea boti ikazama.
Safari yao hadi Kisiwani Galu ilitegemewa kuwa ya saa mbili na ndivyo ilivyokuwa, hali ya ziwa ilikuwa shwari lakini kisiwa kilipoanza kuonekana mbele yao kikiwa kama kilometa mbili kutoka mahali walipokuwa mambo yalianza kubadilika, hali ya hewa ikaanza kuchafuka! Uliiubuka upepo mkali kama kimbunga uliyoyazungusha maji na hata boti zao, maaskari walianza kuingiwa na hofu wakijua mambo waliyoyasikia ndiyo yalikuwa yanatokea lakini walijipa moyo kwa sababu wote walivaa vifaa maalum vya kuzamia. Hali ilizidi kuwa mbaya kadri dakika zilivyosonga, kilometa mbili zilikuwa mbele yao zilionekana kama kilometa mia moja, hawakuweza kusonga mbele hata hatua kumi! Boti zao zikabinuka na kuwamwaga majini.
Kelele zilizikika kila mahali, boya alilovaa Nancy lilimsaidia akajikuta akielea majini, lakini kitu kimoja kilimshangaza alikiona kiumbe kisicho cha kawaida kikiogelea katikati yake na maaskari wengine, kilikuwa ni kama binadamu lakini si binadamu wa kawaida! Kilimwogopesha, kila kilipowafikia maaskari kiliwavua mtungi wa hewa na kuwaacha wakitapatapa majini! Wote walifanyiwa hivyo na kilipomfuata Nancy alipoteza fahamu hamu hapo kwa sababu ya woga na kuzinduka akiwa ufukweni katika kisiwa cha Galu saa tano baadaye, alipofungua macho yake alimkuta mzee mmoja amekaa pembeni mwake! Haikumchukua hata sekunde mbili kumtambua, alikuwa Babu Ayoub!
“Umejileta! Nilikumisi sana!” Aliongea mzee huyo akitabasamu.
Mwili wa Nancy ulitetemeka, hakuamini kama alikuwa ameingia mikononi mwa mzee huyo aliyemtesa kwa kipindi kirefu kisiwani, machozi yalimtoka hakuwa na uhakika wa kurudi alikotoka tena! Maaskari wote aliokuwa nao katika safari ya kwenda kisiwani walikuwa wamekufa maji baada ya mitungi yao ya hewa kung’olewa, muda mfupi baadaye akilia mzee Kiwembe aliwasili akiwa na Catherine pamoja na David! Afya zao zilikuwa mbaya na za kusikitisha.
“Karibu kisiwani Nancy, hakuna mtu atakayefanikiwa kuja kukutoa hapa tena!Tumejizatiti vya kutosha!” Aliongea mzee Kiwembe akitabasamu.
Ingawa alikuwa akilia Nancy alishindwa kuvumilia, akanyanyuka mahali alipokuwa amekaa na kwenda kuwakumbatia wadogo zake! Alikuwa katika himaya nyingine alikotegemea mateso makali na pengine maisha yake yote yaliyobaki kuishia katika kisiwa hicho! Hakuwa na uwezo wa kupambana na nguvu za uchawi walizokuwa nazo wazee hao wawili.
*******
Danny hakufa. Wakati akihangaika barabarani usiku alipopigwa mshale na kuachwa shambani kwa mzee Katapila, alitokea mwindaji akitoka porini kutega mitego yake! Alipomwona alishtuka, akasimama na kuanza kumulika na tochi, Danny aliuona huo ndio msaada pekee na kuanza kupiga kelele akiomba msaada. Mwindaji alimsogelea na kumuuliza nini kilichompata, Danny alisimulia kila kitu kwa taabu kubwa akimwonyesha mwindaji huyo mshale uliokuwa mbavuni mwake.Cha kushangaza Mwindaji hakuonyesha mshtuko wowote, alichofanya ni kusimama ubavuni kwa Danny kwa miguu yake yote miwili mshale ukiwa katikati na kuukamata kwa mikono yake yote miwili akaanza kuuvuta kwa nguvu zake zote, Danny alilia kwa maumivu mpaka akapoteza fahamu.
Mshale ulipochomoka damu nyingi ilivuja, mzee huyo mfupi mwenye misuli ambaye pia alibeba upinde na mishale, alikifungua kibuyu kilichokuwa kiunoni mwake, akakifungua na kumwaga dawa nyeusi kwenye mkono wake wa kushoto na yote akaiweka kwenye kidonda kilichokuwa kinamwaga damu! Danny akiwa amepoteza fahamu alibebwa begani hadi kwenye kibanda alichoishi mzee huyo katikati ya pori la Tindiga ambako alilazwa chini na mzee kuchukua pembe ya Mbuzi iliyochomekwa kwenye paa la nyumba. Sehemu pana iliyokuwa wazi aliifunika kwenye jeraha na nchani kulikokuwa na tundu dogo alifunika na mdomo wake kisha kuanza kunyonya hewa iliyokuwemo ndani ya pembe na kuifanya pembe iung’ang’anie mwili wa Danny! Kisha akachukua kitu kama Nta na kuliziba tundu, pembe ikabaki wima! Wakati yote hayo yanafanyika bado Danny alikuwa hajarejewa na fahamu zake.
****
Mzee huyo aliendelea kunyonya damu chafu na nyeusi kutoka kwenye kidonda cha mshale, alifanya hivyo kwa muda mrefu mpaka Danny akaanza kujitingisha na baadaye kufungua macho yake na kuangalia huku na kule! Alishangaa kujikuta yu mahali asipopafahamu, aliyemshangaza zaidi ni mzee aliyekuwa pembeni mwake! Hakumtambua na alishangazwa na shughuli aliyokuwa akifanya kwa kutumia pembe iliyofanana na ya mbuzi. Kwa muda aliendelea kujiuliza maswali mengi kichwani mwake fahamu zikiendelea kumrejea taratibu hatimaye akawa mtu kamili lakini hakuelewa kilichotokea mpaka akawa mahali hapo.
“Shikamoo!” Aliamkia
“Marahaba hujambo? Kama umeweza kuniamkia basi utapona, sikuwa na matumaini! Naitwa mzee Ibrahim, wewe?”
“Danny, kimetokea nini?” Danny aliuliza
“Sumu!”
“Sumu ya nini?”
“Ya mshale! Ilitaka kukuua kabisa, nani alikuchoma?” Swali hilo lilirejesha kumbukumbu zote kichwani mwa Danny, kitu kama mkanda wa sinema kikaanza kuonekana akili mwake, aliona namna alivyosafiri na Nancy kutoka Dar Es Salaam hadi Tindiga shambani kwa mzee Katapila, alivyoruka ukuta na baadaye kuchomwa mshale! Kufikia hapo hakukumbuka kitu zaidi ya giza lililotanda usoni mwake, alilia kwa sauti ya juu akiita jina la Nancy kiasi cha kumfanya babu atake kujua mtu huyo alikuwa nani.
“Ndiye aliyekuchoma mshale?”
“Hapana!”
“Ni nani?”
“Mchumba wangu!”
“Ilikuwaje?” Babu aliuliza.
Kufikia hapo ingawa kwa taabu, mzee Ibrahim akiwa amesimamisha zoezi zima la kunyonya sumu kwa kutumia pembe ya Mbuzi, Danny alilazimika kusimulia kisanga chote hadi kufika shambani kwa mzee Katapila, mzee Ibrahim alishangaa sana! Hakuamini hata kidogo kama mzee Katapila angeweza kuwa amefanya kitendo hicho kwani alikuwa mtu mwenye moyo wa kusaidia sana watu wa vijiji vilivyozunguka shamba lake, Danny alipozidi kumsisitizia ilibidi akubali na kuamua kumsaidia tiba za jadi mpaka apone.
“Nitakutibu kwa tiba za jadi, ukienda hospitali hawan uwezo wa kuiondoa sumu ya mshale mwilini! Utakufa!”
“Lakini nataka kuonana na mchumba wangu!”
“Usiwe na wasiwasi hayo yatafanyika baadaye, kitu cha muhimu kwako hivi sasa ni afya kwanza!”
“Sasa atajuaje kwamba niko hapa?”
“Hilo haliwezekani mpaka utakapopona ndipo utakwenda!”
Baada ya maongezi hayo mzee Ibrahim aliendelea kunyonya sumu kutoka kwenye kidonda, damu nyingi nyeusi ilizidi kutoka na kumhakikishia Danny kuwa hiyo ndiyo ilikuwa sumu ikitoka, mpaka asubuhi alikuwa bado akimfanyia tiba za jadi na kumkanda kwa maji ya moto baadaye alitoka nje na kurudi na majani aliyoyapikicha mikononi mwake kisha kuyabandika kwenye kidonda, maumivu aliyoyapata Danny yalikuwa ni afadhali yale ya mshale, mzee Ibrahim alicheka akimwambia hiyo ndiyo ilikuwa tiba yenyewe.
Matibabu hayo ya jadi yaliendelea kwa wiki mbili mfululizo kidonda kikawa kinazidi kupungua na mwili wa Danny kurejewa na nguvu, aliishi na mzee kwenye kibanda chake wakila nyama za porini pamoja, mawazo yake kila siku yalikuwa kwa Nancy, altamani siku moja apone arejee Dar Es Salaam na baadaye Bagamoyo ambako yeye na mchumba wake wangefunga ndoa! Ilipogota wiki ya tatu kidonda kilishafunga lakini tatizo liliendelea kuwa kifua, kulikuwa na maumivu makali mno ndani ya kifua cha Danny. Alikandwa na maji ya moto kila siku lakini haikusaidia.
“Hiki kifua naona kitanishinda, kidonda kimepona lakini dawa zangu naona hazina uwezo wa kutibu ndani!”
“Sasa?”
“Itabidi uende hospitali! Sina ujanja tena, hata hivyo nimejitahidi na Mungu ametusaidia!” Alisema mzee Ibrahim.
Kwa Danny habari hiyo ilikuwa njema pamoja na kwamba alikuwa bado na maumivu makali kifuani, aliamini hospitali angepona upesi zaidi baada ya kupigwa picha ya kifua kuona mshale ulimuumiza kiasi gani, bado aliamini ndani kulikuwa na matatizo tena makubwa! Alikuwa ameishi na mzee Ibrahim kwa muda mrefu lakini muda wa kuondoka ulikuwa umefika, alimshukuru kwa wema wake na kwa ndani kidogo alisikia huzuni kutengana na mtu aliyeokoa maisha yake bila kufahamu angekutana naye tena lini.
“Sijui kama tutaonana tena mzee Ibrahim!” Danny alisema kwa huzuni.
“Usihuzunike sana Danny, wewe nenda na kama tulivyokutana basi tutakutana tena hivyohivyo, Mungu anafahamu!”
Walikumbatiana na mzee Ibrahim alimsindikiza Danny hadi barabarani karibu kabisa na lango la kuingia shambani kwa mzee Katapila, alimwonyesha mahali alipomkuta akiwa amelala hoi bin taaban! Danny alikumbuka kila kitu baada tu ya kuiona ngome ya shamba hilo, alimkumbuka Nancy pia na alishindwa kuelewa kama alikuwa hai ama alikufa katika mapambano ya siku hiyo. Muda mfupi wakiwa barabarani lilitokea lori lililobeba mbao, ni mzee Ibrahim aliyepunga mkono likasimama na kumwombea Danny msaada wa usafiri! Bahati nzuri lilikuwa likielekea Kilosa, aliruhusiwa kupanda nyuma na kusafiri hadi Kilosa.
Hakuwa na kitu kingine cha kufanya baada ya kufika mjini Kilosa zaidi ya kutembea hadi hospitalini umbali wa kama kilometa tano kutoka mahali aliposhushiwa, ilikuwa saa tatu na nusu wakati anafika mapokezi na kuandikisha jina lake, mfukoni hakuwa hata na senti tano, alishukuru Mungu hospitali ilikuwa ya serikali, baada ya kujiandikisha aliingia chumba cha daktari na kutoa maelezo yake, yaliyomshtua daktari hasa baada ya kuliona jereha lililokuwa ubavuni mwa Danny.
“Kwa hiyo ulichomwa mshale?” Daktari aliuliza kwa mshangao.
“Ndio!”
“Kwenye mapambano ya wakulima na wafugaji wa Kimasai au?”
“Hapana!” Alikataa Danny na kumsimulia daktari juu ya tukio lilitokea shambani kwa mzee Katapila, bahati nzuri daktari huyo alishasoma kila kitu kama magazeti na hakuona sababu ya kuendelea na matibabu bila kuitaarifu polisi, muda mfupi baadaye maaskari walifika lakini hawakuchukua maelezo ya Danny mpaka alipotoka chumba cha kupigwa picha ya kifua! Maaskari hawakuamini kama Danny waliyekuwa wakiongea naye ndiye ambaye habari zake ziliandikwa katika magazeti kwamba aliliwa na Simba.
“Wewe ndio Danny?” Mmoja wa maaskari aliuliza.
“Ndio afande!”
“Ulikuwa wapi?”
“Porini!”
“Hukuliwa na Simba?”
“Afande ningeliwa na Simba ungeniona hapa?”
“Basi tueleze kilichotokea!”
Danny alitoa maelezo yake kwa mara nyingine, wakati anamaliza tayari picha ya X-ray ilishakuja na daktari alimtaarifu kwamba kulikuwa na damu iliyokuwa imevuja kifuani na ilikuwa inagandamiza dayaframu hivyo kumsababishia maumivu makali kifuani, Daktari alimthibitishia kuwa hapakuwa na tiba nyingine zaidi ya operesheni ya kifua ambayo hata hivyo isingeweza kufanyika katika hospitali ya wilaya, isipokuwa hospitali ya mkoa wa Morogoro! Siku hiyo hiyo alisafirishwa hadi Morogoro ambako alifanyiwa upasuaji na damu iliyoganda kifuani kwake kuondolewa, alizinduka masaa kumi na sita baadaye na kujikuta kitanda chake kimezungukwa na watu aliowafahamu, tena wakilia machozi.
“Danny!” Ilikuwa sauti ya mzee Katobe!
“Naam baba!”
“Upo hai?”
“Kabisa! Mungu ni mwema, ameokoa maisha yangu!”
“Kila mtu anaamini uliliwa na Simba, tuliposikia taarifa ya habari kuwa umepatikana hatukuamini, tuliondoka Bagamoyo saa hiyohiyo na tumefika masaa mawili yaliyopita! Unajisikiaje sasa?”Mama yake Nancy alimuuliza Danny.
“Nafuu kidogo ingawa bado kuna maumivu, kuna jambo moja tu nataka kuuliza! Nilikosa kabisa mtu wa kumuuliza, hata polisi sikudiriki kuwauliza, nilikuwa naliogopa jibu ambalo ningepewa lakini bora mnieleze ukweli!”
“Nini mwanangu?” Mzee Katobe aliuliza.
“Mchumba wangu Nancy! Yupo hai au ni marehemu?” Jibu la Danny liliishia na swali.
Mzee Katobe na mke wake waliangaliana, Danny akaishuhudia ishara fulani kwenye jicho la mama yake Nancy! Alielewa kilichoendelea, kuna siri iliyokuwa ikifichwa bila hata kuelezwa alihisi Nancy alikuwa marehemu, alilia hadi mwisho wa uwezo wake na kusababisha kidonda chake cha upasuaji kuuma kupita kiasi na hata damu kuanza kuvuja! Daktari alipoitwa aliamuru Danny apewe dawa za usingizi, akalala na kuzinduka siku iliyofuata asubuhi! Mzee Katobe na mkewe wakiwa pembeni mwa kitanda chake, waliyaelewa madhara ya kumweleza ukweli, hawakuwa na njia zaidi ya kumdanganya alipohitaji kuelezwa wapi Nancy alikokuwa, hata wao walichofahamu ni kwamba Nancy hakuwa hai! Taarifa walizosoma katika vyombo vya habari kuwa askari wote alioongozana nao walikufa, ziliwafanya waamini hata mtoto wao hakuwa hai..
“Ni mzima tu!”
“Sasa kwanini yeye hakuja?”
“Alisafiri kwenda Kigoma kumsindikiza mzee Mwinyimkuu!”
“Naye alinusurika?”
“Tulinusurika pamoja naye, Nancy alituokoa!”
“Ni msichana jasiri sana, ninafurahi kuwa na mchumba kama yeye!” Alisema Danny uso wake ukionyesha tabasamu kidogo.
Wiki tatu baadaye aliruhusiwa kutoka hospitali akaondoka na wazazi wa Nancy hadi Bagamoyo ambako watu walishikwa na mshangao kumwona akiwa hai karibu wakazi wote wa mji wa Bagamoyo waliamini Danny alishaaga dunia, kwani ndivyo ilivyotangazwa! Kuonekana kwake akiwa hai kuliibua furaha ya ajabu na kufanya nyumbani kwa mzee Katobe kuwa na kitu kama sherehe kubwa ya mtoto kurudi nyumbani, Mbuzi alichinjwa na damu yake kunyweka kwenye sherehe hiyo ili kuondoa nuksi mwilini kwa Danny! Wakati watu wakisherehekea mawazo ya Danny yalikuwa kwa Nancy, hakulala wala hakuwa na kitu kingine kilichoendelea kichwani mwake! Alimhitaji Nancy si kwa jambo jingine ila wafunge ndoa baada ya mateso na kusubiri kwa muda mrefu.
“Atakuja tu!”
“Lini?”
“Tutajaribu kufanya naye mawasiliano!”
Hayo ndiyo yalikuwa majibu ya wazazi wa Nancy, Danny alipojaribu kudadisi juu ya Nancy lakini minongono ilisikika katika watu waliokuwa katika sherehe hiyo na kumfikia Danny kuwa mchumba wake alifariki dunia pamoja na maaskari wengine waliokuwa wakisafiri pamoja kwenda kisiwani Galu kuwakomboa wadogo zake Catherine na David! Danny alilia tena, ilibidi mzee Katobe na mkewe wamweleze ukweli! Hakuwa tayari kuukubali ukweli huo.
“Haiwezekani! Hawezi kuwa amekufa, siwezi kuamini mimi ni kama Thomaso mpaka nikuguse kwa mikono yangu, nitasafiri mwenyewe mpaka huko Kigoma na baadaye kwenda Kisiwani Galu hata kama nikifa ni sawa tu! Lakini sauti ninayoisikia moyoni mwangu ni kwamba, Nancy yupo hai na yupo katika mateso makali!” Aliongea Danny akilia na kuwafanya mzee Katobe na mke wake pia wabubujikwe na machozi, walimweleza hatari zilizokuwepo kisiwani Galu na idadi kubwa ya maaskari waliopoteza maisha lakini bado Danny hakukubali alitaka kwenda kujaribu na kujionea mwenyewe.
“Acha tu mwanangu! Sisi tulishapoteza na tumezoea!”
“Haiwezekani wazazi wangu, nawaombeni sana mniwezeshe kusafiri hadi Kigoma ili nimfuatilie Nancy, hajafa yupo hai! Hivyo ndivyo moyo wangu unavyonieleza!” Aliendelea kusisitiza Danny lakini mzee Katobe na mkewe waliendelea kumkatalia katakata, siku iliyofuata asubuhi walishangaa kukuta Danny hayupo chumbani akiwa ameacha ujumbe kuwa alikuwa amesafiri kwenda Kigoma na baadaye Galu kumfuatilai Nancy na wadogo zake..
“.......Lolote litakalonipata ni halali yangu sitakuwa na mtu wa kumlaumu, maisha yangu yamejaa mateso ni bora nikayamalizie huko huko Galu!” Ndivyo ulivyomalizia ujumbe huo.
*****
Tayari Nancy alikuwa kisiwani Galu tena, mikononi mwa mzee Kiwembe na babu Ayoub! Hakuwa na matumaini ya yeye kurejea nyumbani tena, safari yake ya kwenda kuwaokoa wadogo zake ilikuwa imemrudisha utumwani! Hakuwa na la kufanya, aliyarudia mateso aliyoyakimbia! Babu Ayoub alifurahi sana kumwona na alitaka mambo yale yale ya zamani yaendelee, amgeuze Nancy mke wake jambo ambalo Nancy hakukubaliana nalo kabisa, kila siku ulikuwa ni ugomvi tena mkubwa, hakuwa tayari kufanya tendo la ndoa na mzee huyo! Kitendo hicho kilimkera babu Ayoub akalazimika kufungua kisanduku chake na kutoa dawa fulani ambayo kila alipompulizia nayo Nancy puani alilala usingizi na kilichofuata baada ya hapo hakikuwa kingine zaidi ya ngono! Yalikuwa mateso makubwa tena makali, kwa mara nyingine alifanywa mtumwa wa ngono.
Ilikuwa siku moja ikawa wiki, hatimaye mwezi ukaisha akiwa kisiwani! Mwisho akalazimika kuyazoea mazingira, hapakuwa na njia ya kutoroka kuondoka kisiwani hivyo alihamishia nguvu zake katika kuwatunza wadogo zake ambao afya zao zilikuwa mbaya kwa wakati huo! Akazoea na kukubali kuwa mke wa babu Ayoub, aliamua kujifanya mjinga lakini akiwa na moja kichwani! Alitaka kuelewa siri iliyokuwepo katikati nguvu za giza za wazee hao zilizowaua maaskari kila walipojaribu kuingia kisiwani hapo na hakuwa na njia nyingine zaidi ya kujifanya yu katika mapenzi mazito na babu Ayoub.
“Nitafahamu tu! Kama Delila aliweza kufahamu siri ya nguvu za Samson, mimi nitashindwaje wakati mimi ni mwanamke kama yeye?” Aliwaza Nancy akiamini lazima siku moja afahamu siri ya nguvu walizokuwa nazo wazee hao wawili, ingawa hakuelewa ni lini lakini alikuwa na uhakika siku moja angefahamu na hiyo ndiyo ingekuwa siku ya ukumbozi wake.
Akawa mama wa nyumbani, akiwatunza na kuwajali wazee hao wawili pamoja na ndugu zake! Lakini kumbukumbu za nyumbani hazikumpotea, kitu kikubwa alichokiomba ni Mungu kumsaidia asipate ujauzito, hakulipenda kabisa jambo hilo! Hakutaka kuzaa na babu Ayoub, hakutaka makosa yaliyojitokeza kwa mama yake mpaka kuwazaa wadogo zake Catherine na David yatokee kwake.
“Laiti nigekuwa na vidonge vya majira ningekunywa lakini kwa hivi sasa sina, namwomba Mungu anisaidie mpaka nitakapoondoka hapa kisiwani!” Hayo ndiyo yalikuwa mawazo yake kila siku.
Mateso yaliendelea kila siku Nancy alitamani kuondoka lakini hapakuwa na njia ya kufanya hivyo, alikuwa chini ya ulinzi mkali akila samaki kila siku mchana na jioni, hakuna siku aliyofurahia maisha, kila siku ilikuwa huzuni lakini akiwa mbele ya mzee Kiwembe na babu Ayoub alijifanya hana kitu kilichomsumbua mpaka wakajikuta wamemzoea kabisa na kumwona ni sehemu ya maisha! Kila siku usiku ilikuwa ni ngono babu Ayoub naye akitafuta mtoto kutoka kwa Nancy lakini hakufanikiwa. Ni fikra juu ya Danny ndizo zilizomuumiza zaidi Nancy, alisikitika kwamba alikuwa marehemu, aliamini ni mwanamume pekee aliyempenda chini ya jua la Mungu! Alipokifikiria kifo chake kwa kuliwa na Simba aliumia zaidi na kuna wakati alijitupia lawama yeye mwenyewe kwa kusahau kumchukua wakati wanaondoka shambani kwa mzee Katapila, Tindiga.
Pamoja na shida zote zilizokuwepo kisiwani Galu, Nancy aliwapenda wadogo zake kupita kiasi na aliwalinda, kuwepo kwake kisiwani humo kulibadilisha hata afya zao! Ghafla wakawa ni watoto wenye afya njema ambao pia walilia kila walipowafikiria wazazi wao! Jambo hilo lilimtia huzuni sana Nancy na kufanya aumize kichwa ni kwa njia gani angeweza kuondoka na wadogo zake na kurudi Kigoma na baadaye Dar kisha Bagamoyo, hakuna siku angefurahi maishani mwake kama siku ambayo angerudi hadi Bagamoyo, hakika ingekuwa sherehe kubwa! Alitamani kuokolewa lakini alijua mpaka wakati huo hakuna mtu angeweza kumwondoa kisiwani, nguvu za giza za wazee hao wawili zilikuwa za kutisha.
“Mpaka nitakapozielewa mimi mwenyewe namna nguvu hizo zinavyotumika ndipo nitaweza kuondoka kisiwani hapa na wadogo zangu na kazi hii inaanza leo, maana babu Ayoub amekwishaanza kuniamini!”
Usiku wa siku hiyo Nancy alifanya kila alichokiweza kumburudisha babu Ayoub, alimfanyia mambo ambayo mzee huyo hakuwahi kufanyiwa na wakiwa katikati ya starehe alianza kumuuliza maswali juu ya nguvu alizozitumia! Badala ya kupata jipu zuri alishangaa kuona mzee huyo akinyanyuka kitandani na kusimama wima uso wake ukiwa umekunjwa kuonyesha hamaki aliyokuwa nayo.
“Unafikiri unaweza kunilaghai kwa njia hiyo? Huwezi! Hutaelewa nguvu hii milele, kama unataka kuelewa ili utoroke basi umekwama!” Aliongea babu Ayoub na kuendelea kufoka hadi asubuhi, siku hiyo hawakuongea kitu kabisa walishinda wamenuniana, Nancy alishindwa kuelewa ni kwa njia gani angeondoka kisiwani! Mpaka wakati huo aliamini ni lazima Jeshi la Polisi lilikuwa likijitahidi kuingia kisiwani lakini lilishindwa kwa sababu ya uchawi ambao wazee hao walikuwa nao.
*********
Danny alisafiri kwa treni hadi Kigoma na kuingia siku tatu baadaye akiwa amechoka kupita kiasi, jambo la kwanza aliloamua kulifanya ni kwenda kituo cha polisi cha kati mjini Kigoma na kuulizia mahali ambako jeshi la polisi lilikuwa limefikia katika juhudi zake za kwenda kuwakomboa watoto Catherine na David kisiwani Galu, jibu alilolipata kituo cha polisi lilimsikitisha sana, kwamba hapakuwa na uhakika kama kweli kulikuwa na watu katika kisiwa hicho! Hivyo polisi walikuwa wameamua kusitisha zoezi kwani wasingeendelea kufanya kazi kufuata maneno ya kusemwa tu ukizingatia kulikuwa na upepo mkali sana uliosababisha vyombo kuzama na askari wengi kupoteza maisha.
“Kwahiyo mmeamua kuacha mambo hivyo hivyo?” Danny alimuuliza Mkuu wa upelelezi wa Mkoa alipopata nafasi ya kuonana naye.
“Ndio!”
“Haiwezekani! Hata siku moja, yaani jeshi la polisi lishindwe kukomboa watu walioko kisiwani?”
“Ungekuwa wewe ungefanya nini kijana?”
“Ningefanya lolote linalowezekana mpaka nifike kisiwani!”
“Basi wewe fanya kama unaweza!”
“Na hilo ndilo lililonifanya nisafiri kuja Kigoma, siamini kama mchumba wangu Nancy alikufa, lazima nifuatilie kama nyie mmeshindwa basi juu yenu!” Alisema Danny na hapohapo alinyanyuka na kuanza kuondoka, alitembea hadi nje ambako pia hakusimama! Alitamani kusafari siku hiyo hiyo kwenda kisiwani Galu lakini hakuwa na fedha za kukodisha boti ambayo ingemfikisha katika kisiwan hicho hatari, hakuogopa kupoteza maisha yake ilimradi alikuwa akimfuatilia Nancy! Kwake kufa ilikuwa ni sawa na kuungana na mchumba wake ahera kama kweli alikuwa marehemu! Alishanusurika kufa mara ya kwanza hakuogopa kifo hata kidogo.
Alishuka moja kwa moja hadi ziwani ambako aliona mitumbwi mingi ya wavuvi, kichwani mwake kulikuwa na wazo moja tu! Kutafuta kibarua ambacho kingemwezesha kupata fedha ya kufanyia jambo moja, kukodisha boti ambayo ingemfikisha kisiwani! Siku hiyo hakubahatisha kupata kibarua lakini siku iliyofuata alipata kazi ya kuvuta, kokoro lililotumika kutega samaki wadogowadogo, siku hiyo peke yake alipata shilingi elfu tano! Kwa wiki nzima alifanya kazi hiyo na kupata shilingi elfu ishirini, pesa hiyo aliingiza katika biashara ya samaki na kuwa anapata faida ya shilingi elfu kumi kila siku aliponunua na kwenda kutembeza katika nyumba za watu sehemu iliyoitwa Mwanga. Alikuwa na hamu ya kutimiza shilingi laki moja na elfu ishirini, kwani alishapeleleza na kuambiwa gharama ya kukodisha boti yenye injini kwenda hadi Kisiwani Galu ilikuwa ni shilingi elfu themanini, alihitaji shilingi elfu ishirini zaidi kwa ajili ya kununulia panga, mkuki, upinde na mishale, hakuwa na uhakika wa kupata bunduki hivyo alilazimika kutafuta silaha za jadi.
Wiki tatu baadaye pesa ilishatimia, akanunua silaha alizozihitaji na kukodisha boti yenye injini mbili kumpeleka Kisiwani Galu! Alielewa ugumu wa safari yake kwa sifa alizokwishakuzisikia lakini hakuogopa, alishaamua kuyatoa maisha yake kwa ajili ya Nancy! Waliondoka Kigoma saa tisa na nusu za alasiri, masaa manne baadaye giza likianza kuingia walianza kukiona kisiwa cha Galu mbele yao, Danny akaanza kuwa na matumaini.
“Si ndio kile?”
“Haswa!” Alijibu Nahodha aliyeendesha boti ambayo Danny alikodi.
“Kumbe sio mbali?”
“Ni kwa sababu boti yangu inakwenda kwa kasi sana!”
“Kweli kabisa!”
“Unakwenda kisiwani kufanya nini?”
“Mimi ni mwindaji wa wanyama, huwa nasafirisha kwenda nje!”
“Kazi hiyo itakuchukua siku ngapi?”
“Mbili hivi!”
“Kwa hiyo tutakuwa kisiwani kwa siku mbili?”
“Hivyo ndivyo!”
“Itabidi uongeze pesa kidogo!”
“Hakuna shaka!” Danny alimdanganya Nahodha huyo kila kitu alichosema, asingeweza kumwambia ukweli juu ya sifa za kisiwa walichokuwa wakienda lakini baada ya kuwakomboa Nancy na wadogo zake ndio angeweza kusema ukweli wake
Walizidi kusonga mbele wakikaribia kisiwa na giza lilizidi kuongezeka, wakati huo kisiwa kilionekana kuwa kama mita mia moja kutoka mahali walipokuwa, moyo wa Danny ulikuwa ukipiga kwa nguvu ukijua sasa kazi ya ukombozi ilikuwa imewadia! Alikuwa na uhakika ndani ya moyo wake kwamba Nancy alikuwa hai na ilikuwa ni lazima amwokoe na kama hakuwa hai basi bado alikuwa na wajibu wa kuwaokoa Catherine na David na kurudi nao hadi Kigoma na baadaye kwenda nao Bagamoyo.
“Mh!” Nahodha aliguna ghafla.
“Vipi?”
“Sikioni!”
“Nini?”
“Kisiwa!”
“Kweli eh? Si kilikuwa hapa mbele yetu?”
“Yaani nashangaa! Kimepotea ghafla, ni kitu gani kinatokea?” Nahodha aliuliza na kabla Danny hajajibu chochote kilitokea kimbunga cha ajabu na kuanza kuyazungusha maji kama ilivyotokea kwa maaskari waliopoteza maisha yao majini, Nahodha alianza kupiga kelele na muda mfupi baadaye boti yao ilibinuliwa wakamwagwa majini, Danny alijaribu kuogelea lakini hakuwa na uwezo huo, maishani mwake hakuwahi kufanya mazoezi ya kazi hiyo! Alianza kunywa maji kisha kuzama, akaibuka juu na kuzama tena, alifanya hivyo kama mara tatu akinywa maji alipoibuka mara ya nne hakuwa na fahamu kabisa.
*****
Nancy alikuwa nje ya kibanda cha babu Ayoub akiwa mwenye mawazo mengi kichwani mwake, alijaribu kufikiria mambo yaliyokuwa yakijitokeza maishani mwake, tabu alizokuwa akizipata akiwa kisiwani Galu na kujiona ni mtu mwenye mkosi!
Alitamani kuwa huru na kuishi maisha yasiyo na maumivu kama aliyokuwa akiishi kisiwani humo akifanywa mtumwa wa ngono na babu Ayoub jambo ambalo hakulifurahia hata kidogo! Wadogo zake Catherine na David walikaa pembeni mwake nje ya kibanda chao.
Kulikuwa na giza kila mahali lakini hawakuogopa kwani walishazoea maisha ya kisiwani, ghafla aliwaona mzee Kiwembe na Babu Ayoub wakitokea ufukweni wakiwa wamebeba kitu kizito mikononi mwao, hakutaka kujiuliza maswali mengi, aliamini labda alikuwa ni samaki mkubwa waliyemnasa siku hiyo. Wazee hao wawili hawakusimama walinyoosha moja kwa moja hadi nyuma ya kibanda kulikokuwa na kibanda kingine kidogo walichokitumia kuhifadhi samaki waliowakausha.
Nancy hakuwajali, aliendelea kukaa kimya akiwa amewakumbatia wadogo zake waliokuwa wakiwindwa na usingizi, ilikuwa ni kawaida yake kuwasimulia hadithi kila siku jioni kabla ya kulala na kuwakumbusha historia ya mahali walipotokea na kwamba siku moja wangerejea tena nyumbani kwao ambako wangeishi kwa raha mustarehe!
Muda mfupi baadaye aliwashuhudia tena babu Ayoub na mzee Kiwembe wakitokeza kutoka nyuma ya kibanda, wote wawili wakicheka! Haikuwa kawaida yao kuwa na sura hizo kila walipotoka ziwani kwa shughuli za uvuvi, Nancy alijikuta akitaka kufahamu ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
“Vipi jamani mbona meno nje?”
“Tumemleta!”
“Nani?”
“Aliyejifanya bingwa kuliko wenzake!”
“Nani?”
“Mumeo mtarajiwa!” Alisema babu Ayoub, mara nyingi Nancy alishamsimulia juu ya Danny na namna alivyokufa na ni kiasi gani alimpenda.
“Mume wangu mtarajiwa nani?”
“Danny!”
“Danny?”
“Ndio!”
“Mmemtoa wapi?”
“Ziwani! Tulipata taarifa kwa njai tunazozifahamu kuwa anakuja na tukaenda kumpokea!”
“Yuko wapi?”
“Nyuma kwenye kibanda cha samaki!”
“Mnanitania!”
“Nenda kaangalie mwenyewe!”
Nancy akiwa amepigwa na butwaa bila kuamini alichokisikia kwa masikio yake alinyanyuka na kukimbia moja kwa moja hadi nyuma ya kibanda kulikokuwa na kibanda kingine kidogo, kwa jinsi kilivyokuwa kifupi alipiga magoti chini na kukifungua!
Kweli binadamu alikuwa ndani yake kwa sababu ya giza lililokuwepo hakuweza kuelewa mara moja kama kweli alikuwa Danny! Alinyanyuka na kukimbia hadi ndani ambako alichomoa nyasi kwenye paa la kibanda chao na kuziwasha na moto kisha kukimbia hadi nyuma ambako alimulika ndani ya kibanda na kumwona vizuri mtu aliyekuwa amelala ndani yake!
Haikuwa rahisi kuamini kuwa kweli mtu huyo alikuwa ni Danny ingawa ndicho kitu macho yake yalichoshuhudia, alihisi ni ndoto hata hivyo alijikuta akiutupa moto pembeni na kwa mikono yake miwili akaanza kumvuta Danny kumtoa ndani ya kibanda, aliyafanya yote hayo huku babu Ayoub na mzee Kiwembe wakishuhudia.
“Danny!Danny!Danny!” Aliendelea kuita Nancy lakini Danny hakuitika.
Alikuwa kimya kabisa kiasi cha Nancy kushindwa kuelewa kama alikuwa hai au mfu, kwa mara nyingine alipiga magoti chini akainamisha kichwa na kuweka sikio lake kifuani sehemu ya moyo na kuanza kusikiliza, aligundua moyo wake ulikuwa bado ukidunda.
Hakupata jibu ni namna gani Danny aliweza kusafiri hadi kisiwani hapo, wakati alichoamini kabla ya kuondoka Bagamoyo ni kwamba alikufa kwa kuliwa na Simba! Pamoja na hayo yote bado kichwani mwake alihisi ni ndoto na kufikiri muda si mrefu angezinduka na kujikuta yuko peke yake katika mateso kisiwani Galu.
Alichokiona kwa macho yake kiliendelea kuwa ukweli na hakuchoka kumtingisha huku akilia na kumwita kwa jina, picha iliyoonekana iliwaonyesha babu Ayoub na mzee Kiwembe ni kiasi gani Nancy alimpenda Danny.
“Unampenda sana sio?”
“Siwezi kusema uongo, ni kweli na mimi na yeye tulipanga kuoana muda mrefu uliopita, bila matatizo yaliyojitokeza hivi sasa mimi ningekuwa mke wake!” Nancy alijaribu kuwa mkweli kadri alivyoweza ili kuwaelewesha wazee hao ni namna gani alimpenda Danny, mwisho kabisa aliwashukuru kwa kumwokoa.
“Tumemwokoa kwa makusudi! Ili tuje tumuue mbele yako!”
“Jamani nawasihi msifanye hivyo!”
“Kwanini?”
“Nampenda!”
“Kwahiyo unataka kuondoka naye?”
“Si hivyo lakini nawaomba msimuue kwa mara nyingi nawashukuru sana mmemwokoa!”
“Tunasema tumemleta hapa kumuua mbele ya macho yako na wewe ukileta ubishi pia utauawa! Sisi si watu wa kuchezea hata kidogo!”
“Naelewa!”
“Mzee Kiwembe hebu mwonyeshe mfano!” Babu Ayoub alisema na mzee mwenzake akakimbia kwenda kwenye kibanda chake kilichokuwa jirani tu ambako alichukua fimbo ya Kiboko na kutoka nayo kisha kutembea nayo hadi mahali alipolala Danny akiwa hajitambui.
Kwa fimbo aliyokuwa nayo mzee huyo alianza kumchapa Danny mbavuni na sehemu nyingine za mwili baada ya kuwa amemvua nguo zote! Ngozi ya Danny ilichanikachanika na damu nyingi kumtoka! Nancy alijaribu kutaka kumzuia mzee Kiwembe asiendelee na zoezi alilokuwa nalo lakini haikuwezekana, babu Ayoub alimshika na kumzuia hata kusogea karibu.
Nancy alilia akiwaomba wasiendelee kumchapa lakini hawakusikia na mzee Kiwembe alipochoka alimkabidhi babu Ayoub fimbo na yeye kuendelea kumchakaza Danny kwa fimbo, walikuwa wamedhamiria kumuua kwa kumchapa na fimbo! Hata watoto Catherine na David pia walilia kushuhudia Danny akichapwa kiasi hicho.
Saa nzima baadaye zoezi lilisitishwa mzee Kiwembe akawachukua Catherine na David kwenda nao kwenye kibanda chake na Nancy alivutwa na babu Ayoub kwenda chumbani kwao. Kwa nguvu zake za kike alijaribu kuzuia asipelekwe lakini alishindwa, hakuwa na ubavu wa kupambana na mzee huyo, wakiwa ndani alilazimishwa kulala kitandani, huku akilia alitii amri hiyo na kujitupa kitandani. Mpaka wakati analala kitandani bado Nancy aliamini kilichokuwa kikiendelea kilikuwa ni ndoto ndefu! Isingewezekana hata kidogo Danny awe hai wakati aliliwa na Simba huko Kilosa mkoani Morogoro, isingewezekana tena awe Kisiwani Galu maelfu ya kilometa kutoka Bagamoyo.
Nancy aliendelea kuwaza na kuyalinganisha mambo yaliyokuwa yakitokea na ukweli! Usiku huo tofauti na siku nyingine zote hakuna kilichofanyika kati yake na babu Ayoub lakini kitu cha kwanza alichokifanya asubuhi ni kunyanyuka kitandani na kutembea hadi nje kwenda kuhakikisha kama kweli alichokiona jana yake kilikuwa ni kweli au ndoto, alishindwa kufanya hivyo usiku kwa sababu mlango ulifungwa na babu Ayoub na ufunguo kufichwa lakini kulipokucha aliufungua mlango.
********
Nancy aliamini alichokiona jana yake kilikuwa si ndoto baada ya kumwona Danny akiwa ameketi kitako ardhini na kunyoosha miguu yake huku akilia, ni kweli alikuwa yeye, macho yake hayakumdanganya! Alikaa pembeni mwake na kuanza kumwita kama alivyofanya jana yake,Danny alimwangalia kwa macho ya huruma bila kuitika wala kusema chochote pia alionekana kutoamini alichokuwa akikiona mbele ya macho yake. Wote wawili walikuwa wakilia na Nancy hakukata tamaa, aliendelea kumwita mpaka alipoitika.
“Nili..jua hu....jafa Nancy, hatimaye nimekuona, siyaamini macho yan...gu hivi sasa nipo tay...ari kufa ili mradi nime...kuona kwa mara nyingine!” Aliongea Danny kwa taabu.
“Siamini macho yangu, kama nimekuona tena! Nilikuwa naamini ulikufa kwa kuliwa na Simba, umefikaje hapa kisiwani Galu?!”
Danny alianza kumsimulia Nancy kila kitu kilichotokea ingawa kwa taabu kubwa, alielezea mateso aliyoyapata tangu shambani kwa mzee Katapila, nyumbani kwa mwindaji alikoishi akitibiwa kwa tiba za jadi! Operesheni aliyofanyiwa hospitalini Kilosa, hatimaye kuruhusiwa kutoka hospitali na wazazi kumweleza kila kitu kilichompata mchumba wake na kuamua kuwatoroka wazazi wa Nancy kwenda Kigoma, alieleza namna alivyopata pesa na kukodisha boti iliyomleta hadi karibu na Kisiwa cha Galu ambacho hata hivyo kilipotea machoni pao na baadaye dhoruba kubwa kutokea.
“Kwa hiyo baba na mama wanaamini mimi nilikufa?”
“Kweli kabisa na si hao tu, kila mtu ana....amini wewe ni ma....rehemu hata mimi nilitu....mia uja....siri tu!” Aliongea Danny kwa shida.
“Hawa wazee ni wachawi sana Danny, hata siku nilipokuja mimi yalinikuta mambo kama yaliyokukuta wewe! Dhoruba kali ilijitokeza na maaskari wote niliosafiri nao walikufa maji, mimi peke yangu nafikiri ndiye niliyenusurika ni wao waliofanya ninusurike na wameniambia walipata taarifa za kuja kwako wakaja kukupokea, kwa hiyo uliyekuwa umemkodisha lazima atakuwa amekufa maji!” aliongea Nancy.
“Sasa tufanyaje kuondoka hapa kisiwani kwani ni lazima tuondoke!”Alisema Danny
“Kweli kabisa Danny, lazima tuondoke hapa twende tukafunge ndoa yetu, mambo ninayofanyiwa hapa sijui kama utaweza kuyavumilia lakini mpaka sasa sielewi tutatumia njia ga..!” Kabla Nancy hajamaliza sentensi yake mlango wa banda la babu Ayoub ulianza kufunguliwa, alishtuka akijua mateso kwa Danny yalikuwa yanaanza upya.
“Rudi chini, lala chini haraka Danny! Jifanye huna fahamu au umekufa, huyu mzee anayekuja ni hatari!” Alisema Nancy harakaharaka na Danny alitii na kujitupa chini akatulia tuli!
Babu Ayoub alitembea taratibu kuelekea mahali Nancy alikokuwa ameketi pembeni mwa Danny aliyelala chali akijifanya hana fahamu, mkononi mzee huyo alibeba panga lenye makali kotekote, uso wake ulionekana kujawa na hasira! Nancy alielewa jambo lililokuwa mbioni kutokea.
*****
Nancy akielewa kilichokuwa kikitaka kutokea alinyanyuka mara moja na kumfuata babu Ayoub na kuanza kumbembeleza asimtendee Danny kitendo chochote cha kikatili, aliongea akilia machozi huku akimwambia mzee huyo hapakuwa na sababu yoyote ya kumuua Danny kama yeye Nancy alikuwa tayari ni mke wake!Babu Ayoub alionekana kutoyajali maneno yaliyotoka mdomoni mwa Nancy, alizidi kusonga mbele kumfuata Danny! Alikuwa amedhamiria kumuua mbele ya Nancy ili aweze kummiliki mwanamke huyo moja kwa moja, Nancy hakuchoka alizidi kumbembeleza mwisho alipiga magoti chini na kumshika miguu akimwomba arudishe moyo wake nyuma na kumhurumia Danny.
“Hana makosa! Kama ni mimi na yeye kupendana ilikuwa ni zamani babu Ayoub, tafadhali usimdhuru ni bora umwache hai hata kama utakuwa unamfungia kwenye kile kibanda kidogo, inatosha kuliko kuitoa roho yake!” Aliendelea kuongea Nancy na katika hali ambayo hakuitegemea kabisa alishangaa kumwona babu Ayoub akinyoosha mkono wake na kumkabidhi Nancy Panga, kwa fikra zake Nancy alifikiri labda angeelezwa alirudishe panga hilo ndani lakini alishangaa alipoyasikia maneno yaliyotoka mdomoni mwa babu Ayoub.
“Mcharange!”
“Unasema?”
“Nasema umkatekate wewe mwenyewe mpaka afe!”
“Jamani babu Ayoub! Kwanini unanipa mtihani mgumu kiasi hiki? Unajua kabisa siwezi kumuua Danny ingawa simpendi tena, nakupenda wewe!”
“Achana na hayo ninachosema mimi ni kwamba nataka umkatekate kwa panga akatike vipandevipande!”
“Siwezi! Labda ufanye mwenyewe!”Aliongea Nancy akilia.
Danny alikuwa kimya akijifanya mfu wakati alielewa kila kitu kilichoendelea, moyoni mwake hakuwa na uhakika na kitu ambacho kingetokea dakika kumi baadaye! Alifahamu Nancy asingeweza kumkatakata kwa panga kama alivyokuwa akiamriwa lakini alielewa babu Ayoub alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo, muda wote akiwa amefumba macho alimwomba Mungu muujiza utokee ili asiweze kuuawa, hakuwa na msaada mwingine wowote isipokuwa kwa Mungu!
Babu Ayoub alilinyakua panga toka mikononi mwa Nancy na kuunyanyua mkono wake juu tayari kwa kushusha na kumkatakata Danny, Nancy alikuwa akilia na kumbembeleza mzee huyo asifanye kitendo alichotaka kufanya, alimhakikishia yeye na Danny kusingekuwa na kitu tena! Alitumia kila aina ya maneno kubadilisha msimamo wa mzee huyo aliyeonekana wazi kumchukia Danny! Katika mshangao ambao Nancy hakuutegemea babu Ayoub alishusha panga lake chini huku akihema kwa nguvu, huruma ilikuwa imemwingia! Aliyaamini maneno ya Nancy na kuamua kuahirisha mauaji aliyotaka kuyafanya, mwili wa Danny ulikuwa umekufa ganzi akisubiri panga lishuke mwilini mwake hapo ndipo angeanza kupambana.
“Huyu hajafa!”
“Bado amezimia!”
“Nancy!”
“Bee!”
“Namwacha hai kwa sababu yako, nakupenda sana na sitaki kukuumiza lakini sitaki kuona uhusiano wa karibu kati yako na yeye na siku yoyote nitakapogundua kuna jambo linaendelea mtakiona cha mtema kuni, nitamuua yeye na wewe!”
“Sawa! Ahsante sana mpenzi, hautaona chochote kibaya! Kumbuka mimi ninakupenda na simpendi Danny tena, ilikuwa zamani wa sasa hivi ni wewe!” Aliongea Nancy akitetemeka bila kuamini kilichokuwa kimetokea, maneno yake ya kubembeleza yalikuwa yamefanya babu Ayoub aahirishe mauaji.
Si kwamba hakumpenda Danny, alimpenda kuliko kitu kingine chochote! Yote aliyoyafanya yalikuwa ni kumdanganya babu Ayoub, fikra zake zilikuwa kutoroka yeye na mchumba wake pamoja na wadogo zake! Ili hilo liwezekane ilikuwa ni lazima ajenge uhusiano wa karibu zaidi na babu Ayoub ili kumpumbaza na baada ya hapo ndio mipango ya kutoroka ingeendelea, alishuhudia babu Ayoub akimbeba Danny na kwenda kumfungia kwenye kibanda kidogo kilichokuwa nyuma ya nyumba, kilikuwa kidogo mno kiasi cha kushindwa hata kujigeuza lakini humo ndimo alimotakiwa kuishi siku zote akiwa kisiwani.
Muda mfupi baadaye mzee Kiwembe aliwasili akiwa na nyavu zake mkononi na kumtaka babu Ayoub waondoke kuelekea kazini, aliondoka akifuatana na Nancy hadi ndani ya kibanda chao, bado Nancy aliendelea kumpa shukrani kwa wema aliuofanya, yote hiyo ikiwa ni kumpumbaza mzee huyo! Hakuwa na kitu cha kuchukua ndani zaidi ya nyavu na kutoka hadi nje ambako aliungana na mwenzake na wakashuka kuelekea mwaloni ambako walipanda mitumbwi yao na kuelekea ziwani kwa shughuli zao za uvuvi, nyuma Nancy hakuwa na kitu kingine zaidi ya kwenda kwenye kibanda akiwa na wadogo zake na kuanza kuongea na Danny! Alimpa matumaini makubwa ya kuondoka kisiwani wakiwa salama na alimwomba awe mvumilivu, alimtayarishia chakula asubuhi hiyo hiyo akala lakini akiwa ndani ya kibanda! Nancy aliogopa kumtoa ingawa alikuwa na uwezo huo, hofu yake kubwa ilikuwa kurudi kwa babu Ayoub ghafla..
“Tutaondokaje?
“Hiyo itakuwa ni kazi yangu! Lazima tuondoke kisiwani, niachie mimi Danny! Haiwezi kuwa ghafla lazima nimlainishe kwanza huyu mzee!”
“Nitavumilia Nancy! Kumbuka mimi na wewe tuna ahadi ya kufunga ndoa na tumepoteza mambo mengi sana maishani mwetu ikiwemo elimu sababu ya uhusiano wetu, nakusihi tusiache jambo hili lipotee hivi hivi!”
“Halitapotea Danny! Wewe vumilia tu, kila siku natafuta mbinu ya kutuondoa hapa kisiwani!”
Ilikuwa siku moja mwisho ikatimia wiki, hatimaye mbili mwisho mwezi! Danny akiwa ndani ya kibanda, kitu pekee ambacho Nancy alikuwa amefanikiwa kukifahamu mpaka wakati huo ni mahali mtumbwi wa wazee hao wawili ulipofichwa, hilo peke yake lilimpa matumaini ya kuondoka kisiwani! Alipomwambia Danny juu ya jambo hilo pia alimpongeza, kilichobaki kikawa ni lini waondoke tena bila kumwacha mtu kisiwani zaidi ya mzee Kiwembe na babu Ayoub.
“Hilo linahitaji uvumilivu kidogo!”
“Lakini angalau umekwishajua nini cha kufanya!”
“Ndio!”
“Babu Ayoub anasemaje kuhusu mimi?”
“ ila siku anasema utakaa ndani ya kibanda hiki mpaka mwisho wa maisha yako, anadai uko katika kifungo cha maisha!”
“Wewe huwa unamwambiaje?”
“Sina cha kumwambia zaidi ya kumkubalia lakini nikiwa na moja kichwani!”
“Jitahidi Nancy, jambo hili lifanyike mapema nateseka sana kuishi katika kibanda kidogo kama hiki!”
“Naelewa mpenzi lakini hawa wazee si wakuwaendea haraka, inabidi tuwe makini sana katika zoezi tunalota

No comments