Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 37


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
ILIPOTOKA...
“Naelewa mpenzi lakini hawa wazee si wakuwaendea haraka, inabidi tuwe makini sana katika zoezi tunalotaka kulifanya, vumilia tu Danny, hatutamaliza wiki mbili hapa lazima tutakuwa tumeshaondoka kwa kutumia mtumbwi wao, kinachonisumbua ni namna gani tutaweza kuondoka wote!”
“Kwanini?”
“Nilikuwa nafikiri kuondoka usiku wakati babu Ayoub akiwa usingizini lakini nashindwa kuelewa tutawachukuaje Catherine na David ambao wanalala na mzee Kiwembe!”
“Hapo kweli ni kazi ngumu!”
“Sitaki kuwaacha Catherine na David hapa kisiwani, hiyo ndiyo kazi iliyonileta na wewe ulikuja kunifuata mimi!”
“Sasa tutafanyaje?” Danny aliuliza.
“Subiri nitafikiria!”
Siku mbili baadaye katikati ya usiku Danny alishtukia mlango wa kibanda alichofungiwa ndani mwake ukifunguliwa, ni kitendo hicho ndicho kilimuamsha usingizini, alishindwa kuelewa ni nani alikuwa akifungua mlango kwa harakaharaka aliamini ni babu Ayoub amekuja kumuua bila Nancy kuwepo lakini sauti iliyofuata ikinong’ona haikuwa ya babu Ayoub, alikuwa ni Nancy.
“Danny! Danny!” Iliita.
“Naam!”
“Toka twende!”
“Wapi?”
“Tutoroke!”
Danny alichomoka haraka kutoka kibandani na kusimama wima, swali lake la kwanza lilikuwa watoto, alitaka kujua ni wapi walikokuwa Catherine na David! Nancy hakutaka kumjibu, alimshika mkono na kuanza kukimbia naye wakipita katika ya vichaka kuelekea ufukweni ambako hisia za Danny zilimfanya afikiri Catherine na David walikuwa wakiwasubiri, ufukweni hapakuwa na watoto lakini mtumbwi ulikuwa tayari.
“Panda!”
“Watoto?”
“Wewe panda!” Nancy alisisitiza na Danny akapanda bila kuuliza maswali zaidi, Nancy alianza kupiga kasia na mtumbwi ukaanza kusogea mbele taratibu, hali ya ziwa ilikuwa shwari kabisa na kulikuwa na dalili za mvua! Ingawa walielewa uchawi na miujiza ya babu Ayoub na mzee Kiwembe hawakuogopa walikuwa tayari kupoteza maisha yao wakijaribu kujiokoa kuliko kuendelea kuteseka, mpaka wakati huo Danny hakuelewa ni wapi walikokuwa Catherine na David na hakuuliza tena! Kilometa kama kumi katikati ya maji, kukiwa na giza kila upande Nancy alichoka na kumkabidhi Danny kasia, akaiendeleza kazi na kusonga mbele kilometa ishirini zaidi! Alipochoka naye alimkabidhi Nancy kasia wakaendelea kubadilishana kwa mtindo huo mpaka kufika mbali kabisa mahali walikoelewa si babu Ayoub wala mzee Kiwembe ambaye angeweza kuwapata tena.
******
Saa kumi na nusu ya usiku, babu Ayoub alizinduka usingizini kitu cha kwanza ilikuwa ni kupapasa upande wake wa kushoto ambako mke wake siku zote alilala! Hakukuta kitu akafikiri labda alikuwa amekwenda kujisaidia kwa sababu mlango ulikuwa wazi lakini aliposubiri kwa saa nzima alishtuka, ikabidi atoke nje harakaharaka na kuanza kuangaza huku na kule lakini hakumwona Nancy mahali popote. Kilichomwijia kichwani harakaharaka ni Nancy alikuwa ametoroka pamoja na Danny, ili kuhakikisha jambo hilo alizunguka nyuma kwenye kibanda na kukuta kibanda kiko wazi na Danny hayupo ndani yake.
Alikimbia moja kwa moja hadi kibandani kwa mzee Kiwembe akagonga mlango na kufunguliwa kisha kumkalisha chini na kumweleza kila kitu kilichotokea usiku huo, mzee Kiwembe hakuamini kwa sababu Catherine na David walikuwepo, aliamini Nancy asingeweza kuondoka kisiwani na kuwaacha wadogo zake aliowapenda kiasi hicho.
“Sasa wako wapi?”
“Twende ufukweni tukaangalie!”
“Sawa!”
Waliondoka mbio kuelekea ufukweni mwa ziwa kuangalia kama Nancy na Danny walikuwepo, walishangaa kukuta mtumbwi wao haupo jambo lililoashiria kuwa kweli walikuwa wametoroka! Roho ilimuua babu Ayoub, alisonya na kuapa wasingefika mbali! Wote wawili waliondoka mbio kurudi vibandani mwao ambako walichukua zana zao zote za uchawi ili wavuruge hali ya hewa ziwani, Danny na Nancy wazame na baadaye watume mashetani yao kwenda kuwakamata na kuwarudisha kisiwani.
“Wakirudi hapa hakuna kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuwachinja, wanacheza na mimi ngedere hawa!”
Moto uliwashwa, dawa nyeusi kutoka kwenye kibuyu zikamwagwa ndani yake na moshi ukaanza kupanda kwenda juu na kimbunga kikubwa kikajitokeza, wote wakasimama na kuanza kusema maneno kwa kabila yao wakiamuru kibunga hicho kiende kikawalete Nancy na Danny!
******
Pamoja na kuwa wamekwenda umbali mrefu majini kwa kupiga kasia na kuwa na uhakika walikuwa wamefanikiwa kuwatoroka babu Ayoub na mzee Kiwembe, ghafla hali ya ziwa lililokuwa limetulia ilibadilika! Upepo mkali ulijitokeza ukivuma kutoka Kaskazini kwenda Kusini na kusababisha mawimbi makubwa pamoja na dhoruba isiyo na maelezo, mara moja Nancy alielewa kilichokuwa kikiendelea, babu Ayoub na mzee Kiwembe walikuwa wamefanya mambo yao! Matumaini ya kunusurika yalianza kupotea, picha ya ndoa yao iliyokuwa imeanza kujijenga kichwani ilianza kufutika, hali ilizidi kuwa mbaya na wote wawili waliamini kifo kilikuwa haki yao! Walikumbatiana wakiwa hawana matumaini kabisa na kulia machozi kwa pamoja.
“Tufanye nini darling?” Danny aliuliza.
“Kwa kweli sielewi!”
“Unafikiri huu ni upepo wa kawaida?”
“Hapana!”
“Sasa ni nini?”
“Hii ni kama ile siku ya ulipozama wewe na niliyozama mimi, hawa ni wale wale wazee na uchawi wao!”
“Ndio nakuuliza tufanyeje?”
“Kwa kweli sielewi! Kuna uwezekano tukajikuta tuko huko huko kisiwani!”
Kwa muda wa saa mbili hali iliendelea kuchafuka, mawimbi yalikuja makubwa kama nyumba na kuujaza mtumbwi wao maji! Hali ilikuwa mbaya, katika maisha yao hawakuwahi kukumbana na dhoruba kali kiasi hicho, machozi waliyolia yote yalikwenda na maji! Haukupita muda mrefu mtumbwi wao ukawa umepinduka na kujifunika chini juu, wote wakamwagwa majini! Danny alifanikiwa kujivuta na kupanda juu ya mtumbwi na kuketi akishuhudia Nancy akihangaika majini, hakuwa na uwezo hata mdogo wa kuogelea! Roho ilimuuma kwani hakuwa tayari kushuhudia kifo cha Nancy, ingawa yeye pia hakuwa na uwezo wa kuogelea, alichofanya ni kujitupa tena majini na kukamata gauni la Nancy kwa mkono wa kulia huku mkono wa kushoto ukiwa umeushika mtumbwi na kumfanya aelee.
Alimvuta Nancy na kumsogeza karibu yake na kuzuia asizame tena kwenda chini huku akiendelea kunywa maji, Danny alifurahi kuona amefanikiwa kulifanya jambo hilo aliloamini lilizuia kifo cha mwanamke aliyempenda kuliko wote, kwa nguvu zake zote alijivuta na kufanikiwa kupanda tena juu ya mtumbwi na kulala juu yake huku mkono wake wa kulia ukiwa umeshikilia gauni la Nancy aliyekuwa majini, kichwa peke yake ndio kikionekana juu ya maji! Hakuwa na uwezo wa kuongea chochote, alikuwa kimya kiasi cha kumfanya Danny ahisi labda alishakufa tayari na moyo wake kuuma kuliko kawaida, hakuwa tayari kabisa kukubaliana na ukweli huo kwani alikuwa amehangaika sana na mwanamke huyo, fikra zake zilipomrudisha chuo kikuu walikosoma pamoja, matatizo waliyoyapata katika mapenzi yao na mahali walipokuwa wakati huo Danny alijikuta akipita kelele na kukataa kabisa kuwa Nancy alikuwa bado hajafa..
“Nancy!Nancy!Nancy!” Alimwita mara tatu mfululizo bila kuitikiwa! Jambo hilo lilimfanya azidi kuamini mchumba wake hakuwa hai pamoja na kuukata ukweli huo, maji aliyokuwa amemeza yalikuwa yamemdhuru, pengine yalijaa kwenye mapafu na kumfanya ashindwe kupumua, Danny alitamani wawe nchi kavu ili aweze kumkamua maji yatoke tumboni lakini hapakuwa na uwezekano huo, pamoja na hali hiyo bado hakukata tamaa, hakuwa tayari kumwachia kwa mkono wake wa kulia uliendelea kushikilia gauni la Nancy akiwa amelala juu ya mtumbwi.
Mara kadhaa alijaribu kumvuta ili ampandishe juu ya mtumbwi lakini haikuwezekana, Nancy alikuwa mzito kupita kiasi na hali ya hewa ilikuwa ikiendelea kuwa mbaya kadri saa zilivyozidi kupita, mtumbwi ulikosa muelekeo na kuanza kupelekwa na maji kufuata mkondo na upepo! Hakuelewa tena walikuwa wakielekea wapi lakini bado hakumwachia Nancy aliyekuwa kimya kabisa! Hatimaye ikawa jioni na usiku ukaingia haliya hewa ilikuwa bado ni mbaya, majira kama ya saa saba na nusu ya usiku alimsikia Nancy akijitingisha na alipomwita aliitika, Danny akafurahi kupita kiasi, lilionekana kuwa jambo ambalo hakulitegemea kabisa.
“Tuko wapi?”
“Majini!”
“Nini kimetokea?”
“Tumezama!”
Jibu hilo la Danny lilimfanya Nancy akumbuke kila kitu na kuelewa kumbe alipoteza fahamu muda mfupi baada ya mtumbwi wao kuzama, kumbukumbu zilizidi kumiminika hasa alipouona mtumbwi wao na Danny akiwa juu yake na aliamini kila kitu kilichokuwa kikitokea ilikuwa kazi ya wazee wawili hatari, mzee Kiwembe na babu Ayoub! Lakini kwa sababu walikuwa hai mpaka wakati huo aliamini wasingekufa na alimwomba Danny aendelee kumshikilia kwani mwili wake haukuwa na nguvu, alikuwa amelegea na alikuwa na na ganzi kali mwilini iliyosababishwa na ubaridi wa maji, hicho ndicho kilifanya ashindwe hata kupanda juu ya mtumbwi pamoja na msaada wote aliopewa na Danny.
Ikawa asubuhi, ikawa jioni siku ya pili! Na ikawa tena asubuhi, ikawa jioni siku ya tatu na hatimaye siku ya nne na ya tano bado wakielea majini, Danny akibadilisha mikono kutoka kushoto kwenda kulia kumshikilia Nancy aliyekuwa bado yupo ndani ya maji, kama ilivyokuwa mwanzo alikuwa haongei kitu tena na si yeye tu bali pia Danny hakuwa na kauli! Baridi kali iliyokuwepo ziwani, dhoruba iliyosababishwa na mvurugiko wa ziwa pamoja na njaa ya siku tano bila kula chakula iliwamaliza nguvu kabisa, walikuwa ni kama maiti, ingawa walihema hawakuwa na matumaini ya kupona! Walijihesabu ni wafu, matumaini ya kunusurika yalishafutika..
“N...an....cy!” Aliita Danny akitetemeka.
“B..e..e!” Nancy naye aliitika meno yake yakigongana, huku kitu kama moshi kikimtoka mdomoni sababu ya baridi, nguzo yake wakati huo ilikuwa Danny kama mkono wake ungemwachia basi angezama majini na kufa mara moja!
“Na....kup..enda!”
“Nak...pe.....nda..pia!”
“Na ni...natamani tuo....kolewe ili tuka....funge nd..oa ye..tu!” Aliendelea kuongea kwa taabu Nancy.
“Ha..ta mi...mi pia nat...am...ani!”
“Lakini mikono yangu ime...choka kukushikilia Nancy! Nashi.......ndwa kue.....ndelea, nalazi....mika kuku....achia! Sio kwa.....mba siku....pendi lakini kwa sa....babu siwezi tena mpenzi, misuli yote inaniuma na mikono imekufa ganzi! Naomba usinielewe vibaya, tangulia na mimi nakufuata, tutafunga ndoa yetu pep....oni ka...ma tukifa...nikiwa ku...fika huko! Kumbuka kutubu dhambi zako zote, mimi na we...we tuli....ua watu wengi sana!” Aliongea Danny mkono wake ukilegea na kuanza kumwachia Nancy.
“Danny! Danny! Tafa..dhali usini...achie! Jika...ze kidogo, sita...ki kufa!” Aliongea akilia Nancy na machozi yakimtiririka na kujichanganya na maji ya ziwa.
Pamoja na kulia akiomba asiachiwe haikuwezekana tena, vidole vya Danny vilimwachia taratibu, Nancy akaanza kuzama macho ya Danny yakishuhudia hatimaye kichwa kikamezwa na maji.
********
Kikao kilikuwa kikiendelea ndani ya ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, karibu uongozi wote wa jeshi la polisi nchini ulikuwa ndani ya ofisi hiyo, mpaka Inspekta Jenerali aliyewasili asubuhi ya siku hiyo kwa helkopta kutokea Dar Es Salaam! Suala la Kisiwa cha Galu na watoto waliodaiwa kutekwa na kufichwa pamoja na idadi ya maaskari waliopoteza maisha lilishakuwa la Kitaifa, ilikuwa ni aibu kwa jeshi kushindwa kuingia katika kisiwa hicho na kuwakomboa watoto waliokuwepo.
“Mnafikiri tufanye nini?” Inspekta Jenerali aliuliza akitaka kufahamu kama kulikuwa na mawazo yoyote tofauti baada ya operesheni hiyo kusitishwa kwa kipindi.
“Labda twende Kasulu, yupo mzee mmoja anaitwa Kazaroho!” Kamanda wa Polisi alisema.
“Wa nini?”
“Ni Mganga maarufu sana wa jadi!”
“Atusaidie nini?” Inspekta Jenerali aliuliza
“Ninachoamini mimi ni kwamba kisiwa cha Galu kina mambo ya kishirikina ndio maana vijana wetu wanapoteza maisha, mzee ninayemwongelea anaweza kutupa ndumba angalau za kuzuia upepo ili tuweze kufika kisiwani, vinginevyo tutaendelea kufa Kamanda!”
“Yaani wewe katika Karne ya ishirini na moja unataka kuliingiza jeshi la polisi katika mambo ya uchawi na ushirikina? Hufai! Mara ishirini ungeniambia tutafute mchungaji twende naye akafanye maombi ili nguvu za giza zipambane na nguvu za Mungu hapo ningekuelewa” Inspekta Jenerali alifoka na Kamanda wa polisi alibaki kimya kabisa.
Watu wote waliokuwemo katika kikao hicho walitoa mawazo yao lakini wazo lililoonekana kukubalika zaidi ni la Mkuu wa Kituo cha Kati mjini Kigoma Inspekta Ibrahim Katole, yeye alishauri helkopta aliyokwenda nayo Inspekta Jenerali ndiyo itumike kuwasafirisha askari mpaka kisiwani, kila mtu alipiga makofi kulishangilia wazo hilo hata Inspekta Jenerali alikubali akiamini kama njia ya maji ilikuwa haiwezekani basi njia ya anga ndiyo iliyotakiwa kutumika.
“Labda hao wazee na hali ya hewa wanaweza kuichafua halafu helkopta yetu ikaanguka?”
“Sidhani!”
“Potelea mbali lolote litakalojitokeza niko tayari! Suala hili limenifanya nionekane siwezi kazi, Kamanda andaa vijana ili waondoke sasa hivi kwenda kisiwani Galu, wape silaha za kutosha! Nataka watakaporudi hapa wawe na hao wazee wawili pamoja na hao watoto!”
“Sawa afande!” Aliongea Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma akipiga saluti kuonyesha heshima kwa mkubwa wake wa kazi na huo ndio ukawa mwisho wa kikao.
Kilichofuata baada ya hapo yalikuwa ni maandalizi ya safari ya kwenda Galu,maaskari kumi na tano wenye uwezo wa kupambana walipangwa kwa ajili ya operesheni hiyo na kupewa zana zote za kazi, majira ya saa saba ya mchana helkopta iliondoka kuelekea kisiwani Galu, maaskari wote wakiwa wamapania kupambana kwa nguvu zao zote hata kama ingebidi wapoteze maisha lakini wawaokoe watoto waliokuwa kisiwani! Wasiwasi wao ulikuwa mmoja tu, NGUVU ZA GIZA! Hawakuwa na uhakika kama wazee wachawi waliokuwa kisiwani wasingeweza kuitungua helkopta yao kwa makombora ya kichawi na kuwateketeza.
“Tutafika?” Waliulizana.
“Lolote litakalokuwepo mbele ni halali yetu ili mradi tuliamua kwa hiari yetu kuingia jeshini! Au kuna mtu alilazimishwa?”
“Hapana!”
“Basi kazi ni moja tu!” Mkuu wa msafara huo Inspekta Ibrahim Katole aliwaambia vijana wake, pamoja na maneno hayo hakuna aliyekuwa na uhakika wa kufika kisiwani salama, sifa za wazee wawili hatari walioishi katika kisiwa hicho ziliwatisha..
*****
Helkopta ya jeshi la polisi ilikuwa ikipita juu ya maji katikati ya ziwa Tanganyika kuelekea kisiwani Galu, ndani yake kulikuwa na maaskari waliokuwa na hamu kubwa ya kufika katika kisiwa hicho ili kukabiliana na wazee wawili wachawi, tayari walikuwa wakiona kisiwa hicho kwa mbali na walitegemea katika muda wa dakika tano wangekuwa wakitua kisiwani humo! Ghafla mmoja kati ya maaskari alipiga kelele akiwaita maaskari wenzake ambao wote macho yao yaliangalia mbele.
“Vipi afande?”
“Jamani hebu angalieni pale!”
“Kuna nini?”
“Kuna watu wamezama na mtumbwi!”
“Yaani wewe umewaona kwa macho yako?”
“Hapana nimetumia hiki kiona mbali!”
“Hebu!”Mkuu wa kikosi hicho aliomba kiona mbali na kuanza kuangalia chini majini, kweli aliwaona watu wawili mmoja akiwa juu ya mtumbwi na mwingine akiwa amezama kichwa peke yake kikiwa juu ya maji!
“Umewaona?”
“Kweli kabisa!”
“Sasa tufanye nini? Tunyooshe Galu au tuwaokoe kwanza?”
Wawili kati yao waliamua safari iendelee ili watimize kazi waliyotumwa na jeshi lakini wengi walisema wafanye kila kilichowezekana kuokoa roho za watu hao, kauli ya wengi wape ilipita na helkopta ikaanza kushushwa taratibu kuelekea majini eneo ambalo watu hao walionekana, huku kamba zikitayarishwa kwa ajili ya mmoja wa maaskari kushuka hadi majini na kutoa msaada! Lakini kabla hawajafikachini karibu zaidi askari aliyekuwa na kiona mbali alipiga kelele kuwaeleza wenzake kuwa tayari aliyekuwa majini amezama kabisa!
Kamba ilishushwa haraka na mmoja wa maaskari akapita katika moja ya milango na kushuka moja kwa moja kwa kutumia kamba hadi majini, wakati anafika ndio Nancy alikuwa akiibuka kwa mara ya kwanza huku akinywa maji mengi, askari alimdaka na kumfunga kamba mkononi kisha kuwaonyesha ishara wenzake na mashine maalumu ya kuvuta kamba iliyokuwemo ndani ya helkopta ilianza kufanya kazi yake na wote wawili wakavutwa hadi juu na kusadiiwa kuingia ndani.
Kamba nyingine ilitupwa tena majini ikiwa imemfunga askari mwingine ambaye alikwenda moja kwa moja hadi chini karibu na mtumbwi ambao Danny alilala juu yake, aliipitisha kamba shingoni na kumfunga kifuani kisha kuonyesha ishara kama alivyofanya mwenzake na hapohapo akaanza kuvutwa kuelekea juu! Ilikuwa operesheni ya dakika zisizozidi tano, wote wawili wakawa wameokolewa!
“Mh! Huyu msichana nimemkumbuka! Ndiye aliyeondoka na maaskari wetu mara ya kwanza kabisa, na tukaamini kwamba amekufa! Nashangaa sana kumwona yuko hai!”Alisema mmoja wa maaskari wakati wakijitahidi kumkamua Nancy maji aliyokuwa ameyameza katika wakati wa kuzama.
“Aisee ni kweli kabisa!”
“Lakini taarifa tulizozipata ni kwamba alikufa pamoja na maaskari wetu?”
“Hivyo ndivyo ilivyosemekana!”
“Na huyu kijana?”
“Huyu simkumbuki!”
“Au ni mmoja wa watekaji?” Waliulizana na Danny alisikia kila kitu kilichoongelewa.
“Hap....ana jamani mimi sio mte.....kaji na mimi pia nilit....ekwa na wazee wa.....wili wana....oitwa Kiwembe na Ayoub!” Aliongea kwa taabu Danny, mashavu yake yalikuwa bado yameng’ang’aniana kwa sababu ya baridi..
“Wewe ni nani?”
“Naitwa Danny! Mchu.....mba wa.....ke na Na...ncy! Nawa...shukuru sana kwa kut....uokoa, nani amewa....eleza kwa...mba tuko hapa?”
“Hatujaelezwa na mtu ila tulikuwa safarini kwenda kisiwani Galu kuwakomboa watoto wawili waliotekwa muda mrefu na wazee uliowataja!” Mmoja wa maaskari alisema, hapo Danny aliwaeleza kila kitu kilichotokea ingawa kwa taabu, Nancy akiwa kimya akiendelea kukamuliwa maji tumboni., ilikuwa ni bahati kubwa sana kwao kuokolewa kwani walishakata tamaa kabisa ya maisha.
Uamuzi uliochukuliwa ni kuwarejesha Nancy na Danny Kigoma haraka iwezekanavyo kabla safari ya kwenda Galu haijafanyika, hali zao zilikuwa mbaya na ziliwatisha maaskari wote waliokuwemo ndani ya helkopta hiyo ya polisi, waliwasiliana haraka na Kamanda wa Polisi wa Mkoa kumtaarifu juu ya kilichokuwa kikiendelea, tayari ilishakata kona kuelekea Kigoma ambako walifika dakika ishirini baadaye na kutua na Danny na Nancy wakashushwa na kupakiwa katika magari ya wagonjwa yaliyokuwa yameandaliwa tayari na kuondoka muda huo huo kuelekea hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Mlugwanza.
Askari nao hawakutaka kupoteza muda bado walikuwa na safari ya kwenda kisiwani Galu, ilikuwa ni lazima siku hiyo wafike na kuwatia nguvuni mzee Kiwembe na babu Ayoub waliotisha kwa uchawi! Hiyo haikuwa kazi pekee bali pia kuwaokoa watoto David na Catherine ambao tayari walikuwa na uhakika kwa maelezo waliyopewa na Danny kwamba kuwa walikuwepo kisiwani! Dakika thelathini baadaye helkopta yao ilitua Kaskazini mwa kisiwa cha Galu kilometa ishirini kutoka mahali makao ya wazee hao wawili yalipokuwa.
“Twendeni!” Kiongozi wa maaskari aliamuru.
“Sawa afande!”
“Tuko tayari afande!” Maaskari waliitikia mfululizo na wote walianza kutembea silaha zikiwa mikononi mwao kuelekea sehemu walikoviona vibanda ambavyo waliamini vilikuwa vya watu waliokuwa wakiwatafuta, walikuwa na uhakika hakuna aliyegundua kwamba walikuwa wametua kisiwani hapo.
Nusu saa baadaye wakipita chini ya miti walitokeza eneo hilo, kitu cha kwanza walichokiona ni watoto wawili wakiwa wamekaa nje wakiota jua, afya zao zilikuwa mbaya na waliamini ni watoto hao waliokuwa wamewafuata! Hawakuwaona wazee waliokuwa wakiwatafuta mahali popote, pamoja na maaskari wengine kudai wawachukue watoto kiongozi wa kikosi alikataa na kusema inabidi wavumilie mpaka watakapotokeza ili wawakamate na kuondoka nao!
“Lakini afande tungechukua kwanza watoto!”
“Hapana!”
“Basi tukaangalie inawezakana wapo ndani!”
“Tulieni kwanza kama wapo ndani tutawaona wakijitokeza!”
Maaskari wote walitii amri ya kiongozi wao na kubana katika nyasi, eneo ambalo waliona kila kitu kilichoendelea katika vibanda vya wazee hao, watoto waliendelea kukaa nje na muda mfupi baadaye mzee Kiwembe na babu Ayoub walifika wakikimbia kutoka eneo la chini na kuingia ndani ya vibanda vyao na walipotoka waliowanyakua watoto na kuanza kukimbia kuelekea walikotokea! Ni hapo ndipo maaskari walipojitokeza na kuwaweka chini ya ulinzi.
“Mpo chini ya ulinzi hamtakiwi kufanya lolote tafadhali wekeni hao watoto chini!”
Mzee Kiwembe na babu Ayoub waliwaweka David na Catherine chini na kunyanyua mikono yao juu, hawakuwa na ujanja tena! Uchawi wao haukuwa na uwezo nchi kavu zaidi ya majini, maaskari wawili wenye pingu walitembea kwenda mbele na kuwafunga mikono yao pamoja na kuwabeba David na Catherine, safari ya kuelekea mahali ilipokuwa helkopta ilianza, maaskari walishangaa jinsi ambavyo kazi ya kuwakamata wazee hao ilivyokuwa rahisi tofauti kabisa na walivyofikiria.
“Ah! kumbe tulikuwa tunaogopa bure!” Mmoja wa maaskari alisema wakati helkopta inaiacha ardhi ya kisiwa cha Galu.
“Usiseme hivyo! Hawa wazee wanatisha majini, wenzetu wengi sana wamepoteza maisha! Shukuru Mungu tumetumia helkopta hata sisi tusingepona kama tu tungejaribu kutumia boti!”
Dakika tano baadaye wakiwa angani, lilijitokeza wingu zito tena kwa ghafla ambalo lililowashangaza wote na kusababisha giza lililomfanya rubani ashindwe kuona mbele, wote walianza kuingiwa na hofu kuwa huenda nguvu za giza za wazee hao hatari zilikuwa zimeanza kufanya kazi.
*****
Taarifa za kuokolewa kwa Danny na Nancy zilitangazwa katika taarifa ya habari ya siku hiyo mchana ambayo pia mzee Katobe na mkewe waliisikia, hawakuamini! Walifikiri labda masikio yao yamesikia kitu kingine hasa mtangazaji aliposema kwamba, jeshi la polisi lilikuwa limekwenda kwa helkopta kisiwani Galu kuwakomboa watoto wengine waliobaki na kuwatia nguvuni wazee waliowateka ili wafikishwe mbele ya sheria.
Hawakutaka kupoteza muda walichofanya ni kwenda benki kuchukua fedha na kusafiri hadi Dar Es Salaam ambako walipanda ndege iliyowasafirisha moja kwa moja hadi Kigoma, safari nzima mama yake Nancy alikuwa akilia na alishindwa kuelewa machozi yalimtoka kwa sababu ya furaha au huzuni alitamani kuwaona watoto wake alioamini walikuwa wafu tayari! Mpaka anafika hospitali ya Murugwanza kutoka uwanja wa ndege wa Kigoma alikuwa bado hajaamini kama kweli waliookolewa walikuwa ni Nancy na Danny, alihisi labda ni watu wengine lakini walipofika wodini na kuwaona, machozi zaidi yalimtoka, hayakuwa machozi ya huzuni isipokuwa furaha! Aliinama na kumbusu Danny kisha kwenda kwa Nancy na kumbusu pia, vivyo hivyo ndivyo alivyofanya mzee Katobe..
“Poleni wanangu!”
“Ahsante mama!” Alijibu Danny.
Nancy hakuwa na uwezo wa kuongea, yaliyokuwa yakitokea kwake yalikuwa ni kama ndoto, hakuamini kama kweli alikuwa amewaona wazazi wake baada ya mateso ya muda mrefu! Machozi yalikuwa yakimbubujika mfululizo, kwake pia yalikuwa ni machozi ya furaha si huzuni, lakini furaha yake ilikuwa haijakamilika mpaka David na Catherine pia waokolewe.
“Taarifa ya habari imesema kwamba polisi kwa kutumia helkopta iliyowaokoa ninyi wamerudi tena kisiwani kuwafuatilia Catherine na David ikiwa ni pamoja na kuwatia nguvuni wazee waliowateka!”
“Baba wazee hao ni wakatili na ni wachawi sina uhakika kama kweli watafanikiwa kukamatwa!”
“Wacha tusubiri matokeo! Namshukuru Mungu ameokoa maisha yenu na kama alivyowaokoa ninyi ndivyo atakavyookoa maisha ya wadogo zenu! Hivi sasa tuendeleze maombi, kila siku tulikuwa tukiwaombea na hatutachoka mpaka watoto wetu wengine wameokolewa!” Aliongea mzee Katobe akiwa amemshika Nancy kichwani hakika ilikuwa ni siku ya furaha lakini isingetimia mpaka Catherine na David nao waokolewe.
Je nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa mahali hapa.

No comments