Header Ads

DAMU, MABUSU NA MACHOZI - 38


MTUNZI: ERIC SHIGONGO
ILIPOTOKA
Baada ya kuteseka ziwani Nancy na Danny wanaokolewa na kurudishwa Kigoma ambako wanalazwa hospitali na baadaye kukutana na wazazi wao! Ni furaha kubwa kwa kila mmoja wao lakini furaha hiyo haijatimia mpaka watoto wengine Catherine na David walioko kisiwani Galu wapatikane.
Polisi waliokwenda kisiwani wanafanikiwa kuwakamata mzee Kiwembe na babu Ayoub na kuwaokoa watoto Catherine na David kisha kuondoka nao kwa helkopta ya jeshi waliyokwenda nayo, maaskari wote wanasema kazi imekuwa rahisi kuliko walivyotegemea lakini ghafla wakiwa angani mambo yanaanza kuwaharibikia baada ya wingu zito kutokea angani na kusababisha giza nene kiasi cha rubani kushindwa kuona alikokuwa akielekea! Hali hii inatisha kila mmoja wao anahisi ni nguvu za giza za wazee wawili hatari waliowakamata.
Je, nini kinaendelea? Fuatilia.............
Ilikuwa ni furaha kubwa kwa mzee Katobe na mke wake hatimaye kukutana tena na Nancy pamoja na mchumba wake Danny, watu waliokuwa wamepoteza matumaini ya kuwaona tena! Wakiamini walikufa kisiwani Galu, lakini kama walivyosema wazee hao furaha yao ilikuwa haijakamilika mpaka Catherine na David, watoto wao wengine wapatikane! Ingawa hawakuwa watoto wa kuwazaa yeye, mzee Katobe aliwapenda sana watoto hao, hakuwabagua kama ilivyokuwa kwa Nancy ndivyo ilivyokuwa kwa David na Catherine.
“Mama!” Nancy alimwita mama yake.
“Bee mwanangu!”
“Kama nikipona sitakwenda Bagamoyo, bado nitakuwa na sababu ya kurudi tena kisiwani Galu kuwafuatilia Catherine na David, sijakata tamaa!”
“Sawa lakini polisi ndio wanafuatilia kwa hivi sasa, kama nilivyokuambia Helkopta ipo kisiwani Galu, ni vyema ukawa mvumilivu!”
“Siwaamini polisi kabisa! Walishindwa kutusaidia mwanzo watawezaje leo?”
“Sawa, inawezeka walikuvunja moyo lakini wape nafasi nyingine!”
“Haiwezekani!”
Nancy hakuwa na imani kabisa na jeshi la Polisi na hiyo ilitokana na historia ya nyuma tangu walipotekwa wazazi wake pamoja na Danny na yeye kwenda kutoa taarifa polisi lakini bado hawakumsaidia chochote mpaka yeye mwenyewe kwa mikono yake akaamua kwenda mstari wa mbele na kupambana na mzee Katapila pamoja na kundi lake la majambazi hatimaye kumwokoa Danny na baadaye kuwaokoa wazazi wake shambani Tindiga walikokuwa wamefichwa, jambo hilo lilimfanya asiwe na imani na jeshi la polisi kabisa ndio maana aliongelea suala la yeye mwenyewe kwenda kisiwani Galu kuwakomboa wadogo zake, hawakuwa na imani kabisa kama askari waliodaiwa kwenda kisiwani kwa helkopta wangeweza kurudi Kigoma wakiwa na Catherine na David.
“Nancy!” Danny alimwita mchumba wake.
“Bee!”
“Sikiliza maneno ya mama kwanza, naelewa una uwezo wa kurudi hadi kisiwani Galu na kuwakomboa wadogo zetu na uelewe wazi ukienda wewe ujue wazi hata mimi nitakufuata, siwezi kukuacha uende peke yako lakini nakushauri tutulie kidogo tuendelea kuwaombea Catherine na David mpaka polisi watakaporejea kutoka Galu!”
“Sawa lakini...!” Alikubali Nancy ingawa kwa shingo upande.
Siku nzima walishinda vizuri huku wakiangalia hali za wagonjwa wao, Nancy alikuwa akiendelea vizuri zaidi kadri saa zilivyopita, alishaanza hata kutabasamu! Dripu aina ya Glucose alizowekewa katika mishipa yake zilimfanya apate nguvu harakaharaka, hakuwa na jeraha mahali popote mwilini mwake! Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Danny, yeye tayari alikuwa na uwezo wa kusimama, kutembea na kuzungukazunguka nje ya wodi! Kulikuwa na matumaini makubwa sana ya kupona na kurejea katika maisha yao ya kawaida, mapambano yalikuwa yamekaribia kufika mwisho, kitu pekee kilichokuwa bado kinasumbua akili zao ni wadogo zao lakini kama wao pia wangekuwa huru basi kitu pekee ambacho kingekuwa kimebaki mbele yao ni ndoa na baadaye kurudi tena chuo kikuu kuendelea na masomo mahali walipokomea, hata kama wangetakiwa kuanza mwaka wa kwanza walikuwa tayari.
Kila alipoyakumbuka maisha aliyopitia Danny, aliogopa! Alitishwa na historia yake, alikuwa ametoka mbali kimaisha mpaka kufika hapo alipokuwa, lilikuwa ni jambo ambalo hakuna mtu angeamini kama angemsimulia kuwa alihangaika kiasi hicho na mpaka kujikuta akiua watu kwa sababu ya msichana aliyempenda! Aliamini wengi wangeiona ni historia tu ama hadithi ya kubuni ambazo watu huziandika katika magazeti na vitabu.
“Historia ya maisha yangu inatosha kabisa kuandika kitabu, nikimsimulia mtu kama Chriss Magori anaweza kuandika hadithi kwenye magazeti yake ya Kasheshe na Komesha!”Aliwaza Danny.
Ni kweli kabisa, Danny alikuwa amepitia maisha magumu kupita kiasi, kila alipokumbuka siku ya kwanza aliyokutana na Nancy chuo kikuu alisikitika lakini hakujuta! Aliamini kila kilichotokea ulikuwa mpango wa Mungu, alimkumbuka pia Tonny, hata yeye hakumchukia, kilichomsikitisha tu ni kwamba alikuwa marehemu! Kichwa chake kilijaa mawazo mengi sana lakini yote hayo hayakuwa na maana tena katika kipindi hicho, ilikuwa ni historia cha muhimu ilikuwa ni kuwaokoa Catherine na David kisha maisha kusonga mbele kuanzia hapo.
Walisubiri taarifa za polisi kuwa wenzao waliokwenda kisiwani Galu walikuwa wamerejea na watoto lakini hazikuja, kila mkuu wa kituo alipokuja kuwaona Nancy na Danny alikuwa na jibu moja tu “Hatuna mawasiliano kabisa na helkopta! Hata sisi tunashindwa kuelewa ni kitu gani kimetokea!” Maneno hayo machache yalimchanganya akili karibu kila mtu, Nancy alilia akiamini wadogo zake wasingeonekana tena kwani aliuelewa uwezo wa mzee Kiwembe na Babu Ayoub katika mambo ya mazingara.
“Nina uhakika kabisa hao polisi waliokwenda na helkopta hawajafika kisiwani Galu! Lazima helkopta yao imezama na hata kama wamefika na kuwachukua watoto pamoja na hao wazee sidhani kama watafika salama hapa Kigoma, nawaelewa wale wazee ni wachawi sana!”
“Sasa wewe uliokokaje?” Aliuliza Mkuu wa Kituo.
“Hata mimi sielewi!”
“Basi hivyo hivyo ulivyookoka wewe ndivyo watakavyookoka wadogo zako!”
“Siamini! Kazi hii lazima niifanye mwenyewe na kama Danny atakubali kuongozana na mimi itakuwa vizuri zaidi natoa muda wa saa sabini na mbili kama hawajaonekana basi mimi nitarudi tena kisiwani Galu, nitapambana kwa namna yoyote mpaka niwaokoe wadogo zangu!” Aliongea Nancy kwa uchungu, alimaanisha alichokisema na hakuwa na utani hata kidogo, wazazi wake walilielewa jambo hilo, siku zote. Nancy alipoongea katika sura iliyoonekana usoni kwake hapakuwa na namna yoyote mtu angeweza kumzuia. Maneno ya Nancy hayakumfurahisha mkuu wa kituo na kulazimika kuondoka wodini kurudi kazini kwake, hata yeye alikuwa na mawazo mengi sana juu ya vijana wake na zaidi ya yote helkopta ya mkuu wake wa kazi, Inspekta Jenerali aliyekuwa mjini Kigoma kufuatilia suala hilo.
“Hivi saa sabini na mbili ni siku ngapi?” Mama yake Nancy aliuliza akiwa amemwangalia mume wake usoni.
“Siku tatu!”Danny alijibu kabla mzee Katobe hajasema lolote.
“Basi tusubiri!”
Siku ya kwanza ikapita hali ya Nancy ikazidi kuwa nzuri, ikaja ya pili na hatimaye ya tatu bila polisi kuwa na taarifa yoyote juu ya helkopta iliyokwenda kisiwani Galu, kila mtu katika jeshi hilo alikuwa amechanganyikiwa! Hisia kwamba ilikuwa imezama hawakuzipa kipaumbele katika fikra zao kwa sababu boti zilizunguka huku na kule katika ziwa Tanganyika bila kuona mabaki ye helkopta lakini baadhi ya polisi walihisi pengine ilizama hadi chini kabisa ya ziwa kama ilivyozama ndege iliyoua wacheza wa timu ya taifa ya Zambia.
“Kama ni hivyo basi haitapatikana kabisa maana ziwa Tanganyika kina chake ni kirefu kuliko ziwa lolote Afrika na sijui ni dunia nzima?”
“Mimi kwa kweli sielewi lakini kama hivyo ndivyo, hili ni pigo kubwa sana kwa jeshi la polisi na Tanzania kwa ujumla, hivi hawa wazee wana uwezo gani? Sijawahi katika maisha yangu kuona mtu anayeteketeza binadamu wenzake kiasi hiki!” Maaskari waliendelea kujadili, kila mtu alisema lake lakini hakuna aliyekuwa na jibu sahihi juu ya mahali walipokuwa maaskari na helkopta ya jeshi.
Tayari Nancy alishaanza kusisitiza safari yake ya kwenda Galu, hakuwa na maongezi mengine zaidi ya kuondoka kwenda kufanya ukombozi mwingine! Wazazi wake walimwona kama mtu aliyechanganyikiwa na akili kwani pamoja na ushauri wote waliompa bado hakukubaliana nao, hata Danny alishindwa kumhamisha Nancy kutoka kwenye msimamo wake.
Hawakuwa hospitali tena tayari walisharuhusiwa na kuhamia katika hoteli maarufu mjini Kigoma iitwayo, Lubumbashi ambako walipanga vyumba wakisubiri ujio wa Catherine na David, Danny na Nancy walilala chumba kimoja na mzee Katobe aliyewachukulia chumba cha kulala watu wawili, jambo lililoonyesha wazi kuwa mzee huyo alishahalalisha na kutangaza kuwa walikuwa mtu na mke kabla hata ya ndoa.
“Danny mimi kesho naondoka!”
“Kwenda wapi mpenzi?”
“Nimekwishasema kuwa narudi kisiwani kuwakomboa wadogo zangu!Siwezi kuwaacha wateseke peke yao Kisiwani kama ni maisha yangu ni bora yapotee wakati nikiwatafuta Catherine na David!”
“Lakini kwanini usivute subira kidogo?”
“Nimevumilia vya kutosha! Nilitoa saa sabini na mbili lakini bado polisi hawajawaleta na kila siku wanadai helkopta yao imepoteza mawasiliano, inawezekana hakuna lolote linalofanyika ni uongo tupu!” Aliongea Nancy kwa msisitizo usiku wa manane wakiwa chumbani kwao.
“Unaondoka lini?”
“Kesho asubuhi!”
“Huniachi hapa Kigoma!”
“Kama uko tayari twende sawa lakini kama unasikiliza maneno ya baba na mama baki!”Aliongea Nancy kwa kujiamini, hakuwa mwanamke wa kawaida kwa jinsi alivyokuwa na msimamo mkali, akili yake ilishabadilika kabisa kutoka na mambo aliyoyafanya.
*****
Asubuhi kulipokucha mambo yalikuwa tofauti kwa mzee Katobe na mke wake, siku zote walizoea kuzinduliwa usingizini na Nancy pamoja na Danny wakiwasalimia lakini siku hiyo mpaka saa moja na nusu hakuna mtu aliyegonga mlango wao, waliingiwa na wasiwasi mwingi na kujikuta wote kwa pamoja wakinyanyuka kwenda kugonga chumbani kwa watoto wao.
“Mh!” Mama yake Nancy aliguna kukuta mlango uko wazi, wakabisha hodi lakini hawakuitikiwa mwisho wakaamua kuingia ndani ya chumba, hawakuamini macho yao kukuta hakuna mtu.
Walikimbia hadi nje kuangalia wakifikiri labda walikuwa nje ya hoteli wakifanya mazoezi lakini hawakuwaona mahali popote! wakarudi mpaka mapokezi na kujaribu kuulizia kwa msichana aliyekuwe nyuma ya meza kubwa.
“Mbona wameondoka saa kumi na mbili asubuhi?”
“Kwenda wapi?”
“Walisema wanasafari kidogo na wamewaaga!”
Wazazi wa Nancy hawakutaka kuongea kitu kingine zaidi, tayari watoto wao walishatoroka kurudi tena kisiwani Galu, jambo ambalo wao waliamini lilikuwa ni hatari kubwa kufanyika kwa wakati huo ukizingatia hata helkopta ya polisi ilikuwa bado haijarejea.
“Yaani wameshindwa kutusikiliza?” Mzee Katobe aliuliza, mama yake Nancy hakuwa na uwezo wa kujibu swali hilo zaidi ya kumwaga machozi,walitoka mbio hadi nje tena na kukodisha teksi iliyowapeleka hadi Bandarini ambako baada ya kupeleleza walipewa taarifa kuwa, Nancy na Danny walikodisha boti iwapeleke kisiwani Galu! Ilikuwa habari ya kusikitisha zaidi.
****
Tayari Nancy na Danny walikuwa katikati ya ziwa Tanganyika ndani ya boti ambayo Nancy aliikodi kutokana na pesa alizopewa na baba yake mara tu baada ya kutoka hospitali, Nahodha wa boti alikuwa akiipeleka kwa kasi isiyo ya kawaida, hayo yakiwa ni maelekezo kutoka kwa Nancy aliyetaka wafike kisiwani Galu haraka iwezekanavyo, hakuna alichokifikiria zaidi ya ukombozi wa wadogo zake Catherine na David! Ndani ya boti kulikuwa na mapanga mawili yaliyonolewa kotekote, mikuki miwili pamoja na pinde na mishale yake! Hizo ndizo silaha walizoziandaa kwa ajili ya kupambana na wazee wawili hatari, Kiwembe na Babu Ayoub.
Hawakuwa na uhakika wa kupata ushindi walikokuwa wakielekea, hasa walipozifikiria nguvu za giza walizokuwa nazo mzee Kiwembe na babu Ayoub, mawazo hayo yaliwatisha wote wawili lakini hawakutaka kabisa yawakatishe tamaa! Walikuwa tayari kupambana mpaka wawakomboe wadogo zao na huo ndio ungekuwa mwisho wa vita, vichwani mwao hawakufikiria kabisa kuwa walikokuwa wakielekea hapakuwa na Catherine, mzee Kiwembe, babu Ayoub wala David, watu hao wote walishaondoka kisiwani Galu kuelekea Kigoma baada ya Polisi kuvamia kisiwa na helkopta kisha kuwaweka chini ya ulinzi wazee hatari na kuwakomboa watoto wawili wadogo. Nancy alikuwa akimwangalia Danny kwa jicho la upande, ukimya wake ulimfanya awe na wasiwasi! Alielewa wazi ni kiasi gani mchumba wake hakufurahishwa na safari hiyo lakini alilazimika kumfuata kwa sababu alimpenda.
“Unajisikiaje?” Nancy aliuliza.
“Safi tu!”
“Mbona unatetemeka?”
“Baridi!”
“Kweli au unaogopa?”
“Nini?”
“Wazee wawili tuowafuata!”
“Hawanitishi tena! Mambo tuliyoyapitia mimi na wewe ni makubwa, hata kama ningekuwa naogopa siwezi kukuacha uende peke yako! Mapanga, mikuki na hii mishale ni halali yao!” Danny aliongea kwa kujiamini.
Saa nzima na nusu baadaye tayari walikuwa wakiwasili kisiwani Galu, siku hiyo walishangazwa na hali ilivyokuwa shwari tofauti na mara ya kwanza wote wawili walipofika kisiwani hapo, ambapo dhoruba kali ilichukua roho za watu! Hawakuamini kama walikuwa wamefika katika hali ya utulivu namna hiyo, boti ilipogoa wote wawili walirukia majini wakachukua silaha zao na kuanza kutembea hadi nchi kavu ambako waligeuka na kumpungia nahodha wa boti mkono.
“Mtachukua muda gani?” Nahodha wa boti aliwauliza.
“Haitachukua muda mrefu sana ingawa kazi ya uwindaji ni ngumu! Tuvumilie, tukishaua hata mnyama mmoja tutarudi haraka iwezekanavyo tuondoke!” Danny alimwambia nahodha wa boti, hivyo ndivyo walivyomdanganya wakati wakimkodi, kwamba walikuwa wakienda Kisiwani Galu kuwinda wanyama wa porini ambao hawakupatikana Bara.
“Basi msichelewe nitawasubiri hapa!”
“Sawa!” Wote wawili waliitikia.
Safari ya kupandisha juu kutoka mwaloni ambako boti iligoeshwa ilianza, Danny na Nancy walikuwa wamedhamiria kufanya ukombozi na walitembea harakaharaka hadi eneo la karibu kabisa na vibanda vya mzee Kiwembe na babu Ayoub, kulikuwa na mita kama mia moja na hamsini tu mbele yao! Wakasimama na kuangaliana, saa ya kazi ilikuwa imewadia.
“Tupige magoti tumwombe Mungu atusaidie!”
“Ni vyema na haki maana hakuna anayeelewa kitakachotokea mbele yetu!”
Walipiga magoti chini na kusali wakiomba ulinzi na baada ya hapo walianza kunyata wakielekea mbele hadi nyuma ya kibanda cha babu Ayoub, walishangazwa na ukimya wa ajabu uliokuwepo! Hawakusikia sauti ya mtu yeyote, si Catherine wala David! Hofu ilianza kuwaingia kuwa huenda watoto hao walikwishauawa au wametoroshwa kwenda upande mwingine wa kisiwa. Walisonga hadi mbele ya kibanda hicho walishangaa kukuta kiko wazi, ikabidi waingie ndani ambako walikuta hakuna mtu lakini vyombo na mizigo mbalimbali ya babu Ayoub ikiwa mahali pake! Wakizidi kuingiwa na wasiwasi walitembea tena kuelekea kwenye kibanda cha mzee Kiwembe nako walikuta hali hiyo hiyo, wakapata uhakika kabisa kwamba watoto waliokuja kuwakomboa hawakuwepo.
“Kuna mawili tu hapa!” Nancy aliongea.
“Yapi?”Danny akauliza
“Aidha wametoroshwa au wameuawa!”
Nancy aliishiwa nguvu mwilini, hakutaka lolote kati ya mambo hayo mawili liwe limetokea! Aliwapenda wadogo zake na alitaka kuwa nao, alikaa chini na kuweka silaha zake chini huku akimwangalia Danny aliyekuwa akitembea huku na kule katika nyasi kuona kama kulikuwa na dalili yoyote ya watu kuwa wameondoka sehemu hiyo muda mfupi kabla, kwa sababu ilikuwa imenyesha mvua siku hiyo alitegemea kuona alama za miguu ardhini lakini haikuwa hivyo!
Walibaki sehemu hiyo kwa muda mrefu wakitafakari nini cha kufanya bila kupata jibu hatimaye wakawa wameamua kuzunguka huku na kule kisiwani kuona kama kulikuwa na dalili yoyote ya mahali mzee Kiwembe na babu Ayoub walikopita lakini bado hawakufanikiwa, jioni wakiwa wamekata tamaa kabisa waliamua kurejea kwenye boti iliyowaleta tayari kwa kurejea Kigoma wakiwa wamenyongíonyea kabisa.
“Vipi?”
“Hatukufanikiwa kuua mnyama yoyote!”
“Kwa hiyo?”
“Turudi zetu Kigoma!” Hilo ndilo lilikuwa jibu la Nancy ambaye mashavu yake yalilowa machozi sababu ya kuwalilia Catherine na David, alikuwa na uhakika kabisa hawakuwa hai! Lazima kwa hasira mzee Kiwembe na babu Ayoub waliamua kuwaua baada ya yeye na Danny kutoroka, ndani ya moyo wake alianza kujilaumu ni kwanini aliwaacha wadogo zake wakauawa lakini hakumwambia Danny juu ya jambo hilo na hakutaka litawale ubongo wake, yote alimwachia Mungu.
“Mh!” Danny aliguna.
“Nini tena?”
“Ule sio mtumbwi wao kweli?”
“Uko wapi?” Nancy akauliza.
“Pale kwenye nyasi!” Danny aliongea akiwa amenyoosha mkono wake wa kuume na kusonta kwenye nyasi zilizokuwa jirani na eneo hilo.
“Ndio! Ni wenyewe, sasa wameondoka na nini?”
“Hata mimi sijui!”
“Tufanye nini sasa?”
“Lazima wapo! Turudi tukawasubiri, hatuwezi kurudi Kigoma mikono mitupu, kama hatuendi na watoto basi twende na wao!”
“Akina nani?” Nahodha aliwauliza baada ya kuwa wameongea muda mrefu bila kumshirikisha lakini hakuna aliyemjibu badala yake Nancy alimuuliza gharama ya kuwasubiri kwa masaa mengine matatu zaidi.
“Shilingi elfu tano kwa saa!”
“Nitakulipa!” Aliongea Nancy na mara moja yeye na Danny walishuka na kuanza kukimbia hadi kwenye vibanda vya babu Ayoub na mzee Kiwembe ambako walijificha nyuma ya kichaka na kusubiri kama kweli wazee hao walikuwa wametoka kwenda mahali basi wangerudi na kuwakuta lakini hata baada ya kusubiri masaa matatu bado hawakuweza kuwaona, wakakata tamaa kabisa na kuamini hawakuwemo kisiwani! Wakiogopa kumuudhi mwenye boti walirejea na kupanda boti yao kurejea Kigoma wakiwa wamechoka hoi bin taaban.
Nancy alilia machozi njia nzima wakielekea Kigoma na ilikuwa kazi ya Danny kumbembeleza, nahodha wa boti hakujisumbua kuuliza swali juu ya kilichomfanya Nancy alie, alichukulia haikuwa shughuli yake, kitendo cha kutojibiwa alipouliza mara ya kwanza kilimuudhi kupita kiasi! Tangu wakati huo alichojali yeye ni kazi yake, kama saa nne na nusu hivi ya usiku waliwasili Kigoma na kunyoosha moja kwa moja hadi Lubumbashi hoteli na kupokelewa na wafanyakazi wa hoteli hiyo.
“Mlikuwa wapi? Wazazi wenu wamewatafuta sana!”
“Tulisafiri kidogo!”
“Bila kuwaaga?”
“Ilikuwa ghafla!”
“Wako wapi sasa?√≠ Nancy aliuliza kwa mshangao.
“Walikuwa hapa muda si mrefu ila wamefuatwa hapa na gari la polisi!”
“Kwenda wapi?”
“Nafikiri kituoni!”
“Kuna nini?”
“Hawakunieleza kitu chochote ila niliona mama yako analia sana, neno helkopta likitajwa mara mbili mbili kisha wakaondoka haraka ndani ya gari!”
Danny alimwangalia Nancy usoni, wakagonganisha macho, wote walikuwa wamepatwa na mshtuko juu ya habari hizo, kichwani mwa Nancy hisia huenda helkopta ilifika kisiwani na kuwakomboa Catherine na David lakini baadaye kupatwa na ajali zilianza kutawala, kitu hicho ndicho kiliendelea akilini mwa Nancy! Wote wawili wakaamua kuondoka mbio hadi kituo cha polisi ambako walikuta watu wengi wamejaa wakishangaa kitu ambacho Danny na Nancy hawakukielewa, hawakutaka kupoteza muda walichofanya ni kukimbia moja kwa moja hadi ndani ya kituo ambako waliomba kuonana na mkuu wa kituo, maaskari wote waliowakuta mapokezi walionyesha kuwashangaa.
“Nyie mlikuwa wapi?”
“Kwa nini?”
“Mmewahangaisha sana wazazi wenu!”
“Wako wapi hivi sasa?”
“Wamekwenda hospitali ya Maweni!”
“Kuna nini?”
“Wamekwenda kuwatambua......!” Hakuweza kuikamilisha sentensi yake baada ya askari aliyekuwa jirani yake kumkonyeza, kitendo hicho pia Nancy alikishuhudia na kuzidi kuingiwa na wasiwasi moyoni mwake na kuamini kulikuwa na tatizo limetokea, kwa sababu hata wao walipafahamu hospitali hawakutaka kupoteza muda wa kuuliza maswali zaidi ilibidi waondoke hadi stendi ambako walikodisha teksi iliyowapeleka moja kwa moja hadi hospitali ya mkoa wa Kigoma kushuhudia walichokwenda kutambua wazazi wao ambacho askari hakutaka wakielewe.
Nusu saa baadaye tayari walishafika hospitalini na kuanza kuzunguka huku na kule wakiwatafuta mzee Katobe na mkewe.
*******
Hali ya hewa angani ilikuwa mbaya kwa karibu masaa mawili, rubani wa helkopta ya jeshi akihangaika kusonga mbele lakini alishindwa kabisa kwa sababu ya giza lililokuwepo na uzito wa hewa! Alishindwa kuelewa nini kingetokea mbele yao na kulazimika kuwaomba watu wote waliokuwemo ndani ya helkopta hiyo wamwombe Mungu afanye muujiza ili kuokoa maisha yao!
Alikuwa amehangaika na helkopta hiyo kwa karibu masaa mawili bila mambo kubadilika mpaka taa ya mafuta ikaanza kuwaka jambo lililoashiria hatari kwani kama injini zingeishiwa mafuta kabisa zingezima na baadaye helkopta ingeanguka na kulipuka na wote wangekufa.
Hapo ndipo alipofikiria suala la kutafuta mahali pa kutua na kuanza kutupa macho yake chini lakini kila upande alioangalia kulionekana kuwa na maji hatimaye aliamua kukata kona kuelekea ufukweni ambako alitua kwa usalama bila kuelewa palikuwa ni mahali gani, muda mfupi baadaye walishangazwa kundi la watu wafupi kupita kiasi ambao kwa idadi hawakupungua hamsini waliofika eneo hilo na kuizunguka helkopta.
Maaskari waliweka silaha zao tayari kwa lolote ambalo lingetokea lakini hakuna vurugu yoyote iliyojitokeza! Hakuna aliyeshuka wala kudiriki kufungua mlango, muda wote walikuwa wakijaribu kuwasiliana na kwa njia ya simu ya upepo ili waje waokolewe au kuletewa msaada wowote lakini hapakuwa na mafanikio yoyote.
Walibaki eneo hilo kwa siku tatu bila chakula njaa ikizidi kuwasumbua na Mbilikimo hawakuondoka walisubiri kwa uchu, kwa sababu walishasikia habari za mbilikimo wala watu wa Kongo! Waliamini kabisa watu wafupi waliozunguka helkopta yao ndio wao, ndio maana hakuna mtu aliyediriki kuugusa mlango kwa kuogopa kuwa kitoweo.
Pamoja na njaa rubani hakuchoka kutafuta mawasiliano, katika hali ambayo hawakuitegemea kabisa siku ya tano wote wakiwemo babu Ayoub na mzee Kiwembe wakiwa wamelegea kabisa, mawimbi ya redio yalinasa wakawa wameinasa Kigoma na kuongea na Kamanda wa Polisi na kumweleza kila kitu juu ya mahali walipokuwa.
Lilikuwa ni suala lililohitaji haraka kwa jeshi la polisi ili kuokoa maisha ya maaskari wenzao waliokuwa wamekwama porini na helkopta, kikao cha haraka kiliitishwa na kupitishwa uamuzi wa kutafuta helkopta ya kukodi kutoka jijini Dar Es Salaam lakini kabla ya kufanya hivyo waliamua kujaribu kwanza kuulizia kwenye mashirika ya Wakimbizi.
Kama bahati walifanikiwa kupata helkopta kutoka shirika la kuhudumia wakimbizi, UNHCR! Muda huo huo ikaondoka kwenda eneo waliloelekezwa, kwa kutumia viona mbali haikuwachukua muda mrefu kugundua mahali helkopta ya jeshi la polisi ilipokuwa na wakatua!
Nao pia walishangazwa na umati wa mbilikimo waliokuwepo, hata hivyo risasi zilimiminika na kuwasambaza wote ndipo maaskari wakakimbia na kwenda kuvunja mlango wa helkopta ya jeshi na kuingia ndani, watu wote walikuwa hoi kwa njaa walichofanya ni kuanza kuwasomba mmoja baada ya mwingine mpaka kuwamaliza na helkopta ikaruka kurejea Kigoma ambako walikimbizwa hospitalini na kuanza kupewa matibabu.
Muda huo huo taarifa zilitumwa hoteli ya Lubumbashi kuwataarifu mzee Katobe na mkewe juu ya kupatikana kwa watoto wao na wakaondoka mbio kwenda hospitali usiku huo huo ambako waliwakuta Catherine na David katika hali mbaya, walikuwa chumba cha wagonjwa mahututi na matumaini ya kuokoa maisha yao yalikuwa kidogo sana, muda mfupi baadaye Nancy na Danny walifika wakikimbia.
“Jamani Nancy mlikuwa wapi?”
“Tuliwafuatilia Catherine na David kisiwani Galu!”
“Mbona tayari wako hapa!”
“Wako hapa?”
“Ndio, lakini hali zao ni mbaya!”
“Wamefikaje?”
Mzee Katobe alianza kuwasimulia taarifa aliyopewa na polisi juu ya namna watoto walivyookolewa na hatimaye kufika Kigoma! Ilikuwa ni kama hadithi lakini huo ndio ulikuwa ukweli, siku mbili baadaye baada ya matibabu ya kina hali za Catherine na David zilirejea katika hali ya kawaida, dripu za maji ya sukari walizopewa ziliwapa nguvu na kuwafanya wazima kabisa.
Ilikuwa furaha kubwa mno kwa familia hii kuungana tena, mzee Kiwembe na mwenzake babu Ayoub walifikishwa mbele ya sheria kwa kosa la utekaji na utesaji na wakahukumiwa kwenda jela miaka kumi na tano, pamoja na mzee Kiwembe kujitetea kuwa watoto Catherine na David walikuwa wake hakuna aliyejali! Sheria ilichukua mkondo wake, baada ya hukumu hiyo mzee Katobe, mke wake, Danny, Nancy, Catherine na David walirejea Bagamoyo! Kila mtu alishangaa kuwaona tena, familia iliyosambaratika ilikuwa imeungana upya na hakuna kilichosubiriwa isipokuwa ndoa ya Nancy na Danny!
Wazazi wa Danny walipelekewa taarifa juu ya kupatikana kwa mtoto wao jambo ambalo hawakuliamini, ilibidi wasafiri kurejea Tanzania kufurahi pamoja na mzee Katobe na familia yake, waliunga mkono ndoa na ikafungwa wiki mbili tu baadaye, hatimaye Danny na Nancy wakawa mtu na mke wake! Ilikuwa ni kama sinema ya Kihindi lakini ulikuwa ukweli mtupu na baada ya ndoa hiyo walishauriwa kurudi tena chuo kikuu kuendelea na masomo yao, hakuna aliyebisha! Mwaka uliofuata walijiunga tena na chuo kikuu kwa masomo ya sheria, yaliyotokea maishani mwao yalikuwa historia na hawakutaka kabisa kuyaongelea mauaji yote waliyofanya, walitubu dhambi zao na kurejea kanisani! Maisha yao yalikuwa ya raha mustarehe chuoni wakiishi chumba kimoja na kufanya kila kitu pamoja.
“Unamkumbuka Tonny?” Nancy alimuuliza Danny siku moja wakiangalia mchezo wa televisheni uitwao Days of our Lives ambao huonyeshwa na channel Ten.
“Sitaki kumkumbuka, yaliyopita si ndwele.....tugange?”
“Yajayo!” Nancy aliitikia na wote wakacheka.
“For sure we have been through Blood, Kisses and Tears!”(Kwa hakika tumepita katika vipindi vya damu, mabusu na machozi!) Alimaliza Danny akitabasamu.
Tumefikia mwisho wa hadithi yetu ndefu! Ahsanteni kwa uvumilivu wenu, penye mafundisho, naomba upachukue ili yaweze kukuongoza kwenye maisha yako
MWISHO

No comments