Header Ads

Fitna...! Ngoma, Kamusoko out Yanga, Pluijm atangaza vita


HII siyo fitna ya soka ila ndiyo uhalisia wenyewe, wiki moja kabla ya Yanga kuikaribisha Sagrada Esperança ya Angola katika Hatua ya Mtoano ya Kombe la Shirikisho, habari ambayo siyo nzuri kwa Wanajangwani ni kuwa watawakosa wachezaji wao wawili muhimu.

Yanga itakutana na timu hiyo wiki ya Mei 6-8 kisha kurudiana wiki ya Mei 17-18, ambapo mshindi wa hapo atafuzu hatua ya makundi.

Wachezaji ambao wanatarajiwa kuukosa mchezo wa kwanza utakaopigwa jijini Dar ni Donald Ngoma na Thabani Kamusoko wote ni raia wa Zimbabwe, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kadi mbili za njano walizozipata katika mechi dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Yanga iliangukia Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Al Ahly katika Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa jumla ya mabao 3-2, Ngoma na Kamusoko walikuwa wachezaji muhimu katika michezo yote miwili ambapo walikuwa na msaada mkubwa kikosini.

Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh, ndiye ambaye ameliambia gazeti hili juu ya suala hilo.

“Maandalizi yetu dhidi ya mchezo wetu unaokuja wa kimataifa dhidi ya Esperanca yapo vizuri, kila kitu kinakwenda sawa, lakini tunatarajia kuwakosa wachezaji wetu wawili katika mchezo huo ambao ni Ngoma na Kamusoko kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.

“Hakutakuwa na shida juu ya kutokuwepo kwao kwani kocha atawatumia wachezaji wengine waliopo katika kikosi kwa kuwa tuna wachezaji wengi, hivyo hakuna kitakachoharibika ili kuhakikisha tunashinda,” alisema Hafidhi.

Walipotafutwa wachezaji hao kuzungumzia juu ya wao kukosa mchezo huo, Kamusoko hakupatikana, Ngoma alisema mpaka apate ruhusa ya kocha au meneja wake. Gazeti hili lilipowasiliana na Hafidhi juu ya suala hilo aliomba muda azungumze na Ngoma kisha atatujulisha, lakini mpaka tunaenda mitamboni hakupatikana kutoa mrejesho.


No comments