Header Ads

Huwezi kuamini Baba Diamond apata kibarua cha kumenya viazi!


DAR ES SALAAM: Inashangaza! Wakati wengi wanaamini mzazi hakosei, kwa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ hali ni ya tofauti kwani licha ya kuaminika ana ukwasi wa kutosha, analalamikiwa kutomsaidia baba yake waliyetofautiana, Abdul Juma kiasi cha kukutwa akifanya kibarua cha kumenya viazi vya chipsi ili apate senti za kujikimu, Risasi Jumamosi limeinyaka.

TUJIUNGE NA CHANZO
Aprili 27, mwaka huu, Risasi Jumamosi likiwa katika harakati za kukusanya matukio, lilipigiwa simu na chanzo kilichoomba hifadhi ya jina ambapo kilivujisha habari kwamba, baba Diamond anafanya kibarua cha kumenya viazi katika eneo maarufu la kuuza chipsi lililopo Mtaa wa Liwiti- Kariakoo jijini Dar.SIKIA UBUYU HUU
Chanzo: Hapo ni Risasi Jumamosi? Naongea na mhariri? Au nimekosea namba?
Risasi Jumamosi: Hujakosea, hapa ni Risasi Jumamosi, karibu sana, kuna mpya?
Chanzo: Yeah! Hivi mnajua kwamba baba Diamond anafanya kibarua cha kumenya viazi hapa Liwiti? Kuna  banda maarufu sana kwa chipsi. Huwezi amini, watu wanamshangaa maana nasikia ana nyumba Magomeni-Kagera (Dar) na wapangaji wanamlipa kodi.
Risasi Jumamosi: Tunashukuru sana, tunaanza kuifanyia kazi, lakini unaweza ukatuelekeza kibanda chenyewe kilipo?
Chanzo: Mtaa wa Liwiti, we ukifika ulizia banda maarufu la chipsi. Leo nimegeuka paparazi wenu wa kujitegemea, nilipomuona nikabana mahali na ‘kumfotoa’ picha kadhaa.
Risasi Jumamosi: Umetisha sana, enhe! Tunazipataje? Una mtandao wa WhatsApp?
Chanzo: Mimi sijajiunga na bando lakini dakika sifuri tu najiunga fasta, nawatumia au ikishindikana nitawaletea hapo mjengoni, si ni Bamaga-Sheli?
Risasi Jumamosi: Sawia! Tena hata kama vyote hivyo vikishindikana, tuelekeze ulipo tutakufuata kwa usafiri wa kasi.
Chanzo: Oke, ngoja nijiunge kwanza tuone. Lakini nimeuliza watu hapa wanasema yeye ni mtu wa vibarua hivyo akimaliza kumenya viazi anaondoka zake.

CHANZO CHATUMA FASTA
Kuonesha kwamba chanzo kipo makini na kazi yake, ndani ya dakika chache, tayari kilijiunga na bando na kutuma picha zinazomuonesha baba Diamond ‘baba D’ akiwa bize kibandani hapo akifanya shughuli mbalimbali ikiwemo kumenya viazi, kukaanga kuku na mambo mengine.

BABA DIAMOND APIGIWA SIMU
Ili kuishibisha habari hii, Risasi Jumamosi lilimpigia simu mzazi huyo ili kumsikia anazungumziaje kazi hiyo mpya aliyoianza hivi karibuni na kama amekosa kipato kiasi cha kuamua kufanya vibarua ambapo alianza kupangua hoja kwa kujikanyagakanyaga kama hivi:
“Wewe kwani nani amekupa hizo picha? Mimi sijawahi kufanya hiyo kazi bwana, acheni mambo yenu! Halafu mnapenda kunifuatilia, mimi sitaki bwana, niacheni na maisha yangu. Mnazidi kuchochea ugomvi na mwanangu (Diamond) kila siku.”
RISASI LAMPIGIA TENA
Ili kutaka kumhakikishia kuwa, Risasi Jumamosi lina ushahidi wa picha zinazomuonesha mzazi huyo akimenya viazi na kukatakata kuku, lilimpigia kwa mara nyingine ambapo safari hii alikuja na jibu lingine:
“Kama ni Kariakoo itakuwa ni pale kwa mshikaji wangu mmoja hivi anauza chipsi, nilikwenda pale hivyo nikaona nimsaidie kazi kidogo, lakini si kwamba amenipa kibarua.”
Diamond alipotafutwa kuhusu maoni yake baada ya baba yake kukutwa akimenya viazi vya chipsi, simu yake iliita bila kupokelewa. Hata hivyo, mara kadhaa nyota huyo amekuwa hapendi kuzungumzia umbali uliopo kati yake na mzazi wake huyo.
TUMEFIKAJE HAPA?
Mzee huyo na mwanaye wamefika walipo sasa baada ya mzazi huyo kudaiwa kuwaacha bila kuwajali kwa muda mrefu, Diamond na mama yake, Sanura Kasim ‘Sandra’ kitu ambacho kilimchochea Diamond asiwe na mapenzi ya dhati kwa mshua wake huyo.
Hata hivyo, Diamond anatajwa kumsaidia baba yake kwa ‘vijisenti’ tu ambavyo huishia kwa kununulia mboga.

USIKOSE KUSOMA GAZETI LA AMANI, ALHAMISI IJAYO UONE NAMNA DIAMOND ANAVYOKOSA PEPO YA MUNGU HUKU ANAJIONA.

 CHANZO: Risasi Jumamosi


No comments