Header Ads

KABLA SIJAFA, LAZIMA DUNIA INISAMEHE - 01

Mwaka 1985, Afrika Mashariki.
Hali ilikuwa mbaya duniani, watu wengi walikuwa wakifa sana nchini Uganda na sehemu fulanifulani za Tanzania hasa mkoa wa Kagera katika sehemu za Kanyigo! Watu waliugua ugonjwa usiojulikana na kukonda sana, miili yao iliota majipu na mapele, homa za mara kwa mara ziliwaandama na hatimaye walikufa wakiwa na uzito mdogo sana.
Watu walizidi kuchanganyikiwa juu ya kilichokuwa kikiwaua wananchi wa Tanzania na Uganda lakini hakuna aliyekuwa na jibu zaidi ya watu kuendelea kuteketea.
Waliokufa zaidi kutokana na ugonjwa huo walikuwa ni vijana tena ambao walianza kupata mafanikio katika maisha yao, vijana wengi walikufa na kuacha magari, pikipiki na majumba ambayo yalikuwa hayajamalizika kujengwa au kama yalimalizika basi waliobaki kuishi walikuwa ni watoto na bibi vizee, mbele ya nyumba nyingi kulijaa makaburi.
Lilikuwa si jambo la ajabu kukuta makaburi kumi hadi ishirini kwenye familia moja! Na watoto yatima walizidi kuongezeka kila siku.
Lilikuwa ni tishio kwa maendeleo ya nchi nyingi za Afrika, haikujulikana huku Ulaya ilikuwaje lakini viongozi wa nchi za Afrika hasa Zimbambwe, Afrika ya kusini, Zambia, Malawi, Tanzania, Uganda, Kenya na nchi nyingine zilizo kusini mwa jangwa la sahara walizidi kuchanganyikiwa sababu vijana ambao ndio nguzo ya uchumi wa nchi zao walizidi kuteketea!
Hiyo ndiyo ilikuwa hali halisi na hakuna aliyejua ni ugonjwa gani uliowateketeza binadamu hao!
Madaktari walizidi kuumiza vichwa vyao usiku na mchana kuchunguza chanzo cha ugonjwa huo hatari lakini hakuna aliyekuja na jibu la kugundua wadudu waliosababisha ugonjwa huo, kitu pekee walichofanikiwa kukigundua katika vipimo vya damu ni wagonjwa wote waliokufa kwa ugonjwa huo walikuwa na upungufu mkubwa wa chembechembe nyeupe za damu za damu zilizoitwa T-Lymphocytes! Chembechembe hizo ndizo zilikuwa na wajibu wa kuulinda mwili.
Baadaye wataalam walifanikiwa kumgundua mdudu aliyefanana sana na wadudu wa mafua na Surua katika damu ya mgonjwa mmoja nchini Uganda, mdudu huyo alikuwa ni aina ya virusi lakini wataalam walishindwa kuelewa aliitwaje, hakuwa na sifa za virusi wa kawaida na alishambulia sana chembechembe nyeupe na kumfanya binadamu kukosa kinga hivyo kushambulia ipasavyo na kila ugonjwa aliokutana nao.
Madaktari walishindwa kugundua ugonjwa huo iliitwaje ikabidi waubandike jina kufuatana na jinsi ulivyoathiri afya ya mgonjwa, wakauitwa ugonjwa huo UKIMWI, ingawa wananchi tayari walishaupachika majina tofauti tofauti kama Slimu wakielezea jinsi watu walivyokonda au Juliana kwa sababu uliingia nchini Tanzania wakati watu wengi wakivaa mashati ya vitambaa vyenye maua mengi vilivyoitwa Juliana.
Mwanzoni watu hawakuelewa ugonjwa huo uliambukizwa vipi wengine walihisi labda ni katika chakula au hewa na kuogopa kula au kulala chumba kimoja na wagonjwa wa ukimwi, wagonjwa wengi walitupwa porini na kufa peke yao mara baada ya kugundulika wana ugonjwa huo au familia zilikimbia nyumba na kuwaacha wakifa peke yao hali hiyo ilisikitisha sana.
Waumini wa dini walikesha makanisani wakimwomba Mungu aiokoe duniani na janga hilo ambalo wao waliamini ilikuwa ni adhabu kwa dunia sababu Mungu alisema asingeiangamiza dunia kwa maji kama alivyofanya kwa Nuhu! Lakini pamoja na maombi hayo bado ukweli haukubadilika uliendelea kubaki hapohapo tu na watu walizidi kuteketea.
Jamii ilikumbwa na woga ikafikia wakati watu wakawa hawawezi kupeana mikono wakati wa kusalimiana, wengine wakawa wanaogopa hata kupanda mabasi wakiogopa kupumua hewa sawa na wagonjwa wa Ukimwi! Kifupi hali ilitisha.
Shirika la afya duniani (WHO) lilituma wataalam kuja kufanya uchunguzi wake nchini Uganda na Tanzania katika mkoa wa Kagera, majibu yaliyotokana na utafiti wao yalionyesha kuwa ugonjwa huo ulisababishwa na mdudu aliyeitwa HTLV yaani Human T Lymphocytes virus na walizitaja njia zote zilizotumika kuambukiza ugonjwa huo ikiwemo ya watu kujamiiana na kuongezwa damu.
Tangu siku ya tangazo hilo watu waliogopa kujamiiana na waliotaka kufanya hivyo ilibidi watumie mipira maalum iliyoitwa kwa jina la kondomu ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo zaidi.
Pamoja na hayo ugonjwa wa ukimwi bado ulizidi kusambaa kwa kasi ya ajabu na kuua watu wengi jambo lililoonyesha kuwa watu walikuwa hawazingatii kabisa elimu ya afya waliyokuwa wakipewa.
Lakini ugonjwa huo haukuwa Afrika peke yake huko ulaya nako uliendelea kuwashambulia watu ingawa si kwa kasi kubwa kama Afrika, huko uliwaua sana mashoga na watumiaji wa madawa ya kulevya kwa njia ya kujichoma sindano, ni hapo ndipo ilipogundulika kuwa virusi vya ugonjwa huo vilisambazwa kwa njia ya sindano!
Likatolewa agizo kuwa sindano zote ni lazima zichemshwe au zitumike mara moja kwa mgonjwa mmoja.
Hivyo ndiyo ilivyokuwa na watu waliendelea kuteketea kila siku iliyokwenda kwa Mungu.

****
Mfanyabiashara maarufu mwanamke nchini Marekani, Suzzane Leon aliyeishi katika jiji la New York alimiliki kiwanda kikubwa cha utafiti wa madawa ya Ukimwi, ni kiwanda chake ndicho kiliigundua dawa iliyoitwa ZAT ambayo iliaminika kuongeza siku za kuishi duniani kwa mgonjwa wa Ukimwi. Dawa hiyo ilinunuliwa na karibu kila mgonjwa wa Ukimwi duniani.
Kiwanda hicho hakukimiliki yeye peke yake bali pamoja na Mfanyabiashara mwingine David Syndrome ambaye alimiliki hisa asilimia thelathini katika kiwanda hicho.
Pamoja na utajiri waliokuwa nao na kuwa na kiwanda cha kutengeneza madawa ya Ukimwi, wafanyabiashara hao walikuwa katika hali mbaya ya kifo wote walikuwa wamekondeana vitandani mwao wakifa taratibu kwa ugonjwa hatari wa Ukimwi! Suzzane hakuwa hata na uwezo wa kufanya kazi, David alijitahidi kwenda kazini mara kwa mara ingawa kwa shida
Novemba 31, 2000 siku moja tu kabla ya siku ya ukimwi duniani, mfanyabiashara Suzanne alikuwa jukwaani huko Las Vegas akihutubia watu juu ya Ukimwi, watu wengi walijaa kumsikiliza alikuwa mfano na gumzo katika Marekani nzima, alijitolea kuielimisha jamii ya Wamarekani juu ya ugonjwa huu lakini kabla hajamaliza hotuba yake alianguka jukwaani na kufa.
Muda mchache kabla ya kuanguka alitoa kauli iliyowashangaza watu wengi alisema:
“NAIOMBA DUNIA NZIMA HASA AFRIKA INISAMEHE KWA NILIYOYAFANYA KWANI NIMEUA WATU WENGI WASIO NA HATIA!”
Watu walishindwa kuelewa ni kwanini tajiri huyo mwanamke aliyeaminika kuwa ni mwanamke pekee tajiri nchini Marekani aliyeutikisa hata tajiri wa Bill Gates, aliamua kutoa kauli hiyo! Wapo baadhi ya watu walihisi labda aliwaambukiza watu Ukimwi makusudi lakini hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa na jibu la swali hilo sababu aliyetoa kauli hiyo alikufa.
Miezi kumi tu baada ya kifo cha tajiri Suzanne, mshirika wake katika kiwanda David Syndrome nae alifariki dunia, alikuwa katika hali mbaya sana ya Ukimwi lakini aliificha aibu ya kufa na Ukimwi kwa kufa kifo tofauti na Suzzane! Alikuwa kwa kudungwa na sindano ya sumu.
****
Septemba kumi na moja Jengo la WTC lilipolipuka kutokana na ugaidi uliofanywa na Osama Bin Laden, David Syndrome alikuwa ndani ya gari lake aina ya Limmousine akitokea kiwandani kuangalia shughuli zake sababu baada ya kifo cha Suzzane kila kitu aliachiwa yeye.
Syndrome alikuwa katika hali mbaya mno na alijiuliza kwanini afe kifo cha kuteseka kiasi kama alichokufa Suzzane? Hakuwa tayari kushuhudia akiendelea kukonda kila siku hadi kuingia kaburini mwake.
Akiwa katika mawazo hayo ghafla alishtukia anaona ndege ikiruka angani kulielekea jengo la WTC, mwendo wa ndege ile haukuwa wa kawaida ilivyokwenda mrama sana ikiyumba kutoka upande mmoja kwenda mwingine, Davis Syndrome alishangaa na kuhisi kuna kitu kingetokea.
“My God it is United states flight number 175, what is happening?”( Mungu wangu ni ndege ya shirika la ndege la Marekani namba 175 sijui ni nini kimetokea?)
Aliwaza David Syndrome huku akiangalia juu angani kushuhudia jinsi ndege ile ilivyolifuata jengo la biashara duniani.
Ndege ile ilikwenda moja kwa moja na kuligonga jengo lile na palepale ulitokea mlipuko mkubwa sana na jengo lile lilishika moto na kuanza kuteketea! Kilio kilitanda kila sehemu na watu walianza kukimbia kutoka eneo hilo kuokoa maisha yao na waliokuwa ndani ghorofa ya chini walikimbia haraka kutoka ndani ya jengo wakiwaka moto, wengine waliokuwa juu walijirusha nakuanguka chini wakafa palepale.
“America on fire, American on fire!”(Marekani inawaka moto, Marekani imewaka moto!)
*****
Wakati watu wengi wakikimbia kutoka ndani ya jengo hilo huku wakiwa wameshika moto na kulia, David Syndrome alipata wazo la ajabu kichwani mwake.
“Huu ndio wakati wa kuiondoa roho yangu siwezi kufa kwa mateso makali kiasi hiki, siwezi kusubiri kifo cha Ukimwi!” Alisema David.
Baada kusema hayo alifungua droo katika kabati ya gari lake na kutoa kalamu na karatasi alianza kuandika maneno fulani katika karatasi hiyo.
“Nimeamua kufa lakini ni lazima niuombe ulimwengu msamaha kwa niliyoyatenda, nimemkosea karibu kila mtu nimeua watu wasio na hatia kwa sababu ya kutaka utajiri, nilifanya makosa ndio maana Mungu akanigeuzia mimi adhabu hiyo!” Aliwaza.
Baada ya kuandika kikaratasi hicho alikieweka ndani ya gari lake na kuteremka garini, alisimama nje kwa kama dakika tano hivi, akapiga magoti chini na kuanza kusali akimwomba Mungu msamaha kwa aliyoyafanya hapa duniani.
Alipomaliza kusali David Syndrome alinyanyuka na kusimama wima aliendelea kuwaangalia watu wakikimbia kutoka katika jengo la WTC wengi wao wakiwaka moto na jengo likizidi kuteketea, David alizidi kusimama eneo lile akiwa ameduwaa mtu mmoja alimfuata na kumgusa mgongoni.
“Hey sickman get out of this place!”(Wewe mgonjwa toka katika eneo hili)
Ni maneno ya msamaria ndiyo yaliyomfanya David Syndrome kuamua kutimiza azma yake ya kujiua kwa mtindo tofauti na Suzzane, badala ya kukimbia kujiokoa kama walivyofanya watu wengine yeye alianza kukimbia kuelekea ndani ya moto uliokuwa ukiwaka, njiani alipishana na watu wakitoka ndani yeye akiingia watu wote walimshangaa na wengi walimwona amechanganyikiwa.
Kabla hajaingia ndani zaidi jengo lile lilianza kuporomoka na kudondosha vipande vikubwa vya udongo! Pande moja kubwa lilimwangukia na kumgandamiza David Syndrome ardhini.
Muda mfupi tu baadaye magari ya idara ya uokoaji ya Marekani pamoja na zimamoto yalifika na shughuli ya uzimaji moto ilianza kufanyika, eneo la karibu na mlango ndilo lilikuwa na kwanza kuzimimwa na majeruhi wote waliokuwa wamegandamizwa vibaya na mapande makubwa ya vyuma na udongo waliondolewa, wengine walikuwa ni nyama tu! Ilikuwa si rahisi kuwatambua kwa jinsi walivyokuwa wameharibiwa.

Je nini kitaendelea?
Tukutane  mahali hapa.
Unaweza KULIKE na KUSHARE kwa ajili ya marafiki zako wengine.

  
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI

No comments