Header Ads

KABLA SIJAFA LAZIMA DUNIA INISAMEHE- 3


The Nigeria Institute of Medical Research ndicho kilikuwa kituo kikubwa zaidi cha kufanya utafiti wa magonjwa mbalimbali nchini Nigeria,kikiwa katika jiji la Lagos! Kila mtu mwenye matatizo yaliyoshindikana kugunduliwa na hospitali nyingine nchini Nigeria alipimwa katika kituo hicho.
Kituo hicho kilichokuwa na matawi kote nchini Nigeria kiliingiza pesa nyingi sana kwa siku moja kutokana na wagonjwa waliokwenda kupimwa pale na pia kilipata tenda mbalimbali za mashirika ya kimataifa kufanya utafiti wa magonjwa mbalimbali kama Malaria, matende, malale n.k katika nchi ya Nigeria na hata nchi jirani za Ghana na Ivory cost na kililipwa mamilio ya dola kila mwaka.
Kwa pesa nyingi kilichoingiza kituo hicho cha NIMR kiliweza kuanzisha hospitali karibu kila mkoa wa nchini Nigeria, kikaajiri madaktari wazungu kutoka Uingereza na Marekani! Watu walifurika kutibiwa katika hospitali hizo na pesa zilizipatikana zilizitumika kuanzisha benki iliyoitwa Nigeria bank of Commerce! Iliyomilikiwa na kituo hicho.
Benki hiyo kwa muda wa miaka miwili tu ilijipatia kiasi kikubwa cha wateja na kuwa miongoni mwa benki kubwa nchini Nigeria na kutengeneza mamilio ya faida.
Mafanikio hayo yalikuja kwa sababu ya huduma nzuri zilizotolewa na benki hiyo kwa wananchi wa Nigeria, benki ya Nigeria Bank of Commerce iliendeshwa kwa mtindo wa kiingereza wa the first in the first out, yaani wa kwanza kuingia ndiye alikuwa wa kwanza kutoka.
Mtindo huo wa kuendesha benki haukuwepo nchini Nigeria, mmiliki wa benki na vituo hivyo aliuiga mtindo huo kutoka Uingereza alikoishi kwa miaka mingi kabla ya kurudi nyumbani kwao Nigeria.
Maendeleo hayo yaliwashangaza watu wengi sana na hawakujua mwenye benki, hospitali na vituo vingi vya utafiti alipata wapi pesa nyingi za kuanzisha miradi hiyo! Watu walibaki midomo wazi kwa jinsi maendeleo yake yalivyokwenda kwa kasi, alijikuta ni miongoni mwa matajiri wakubwa sana nchini Nigeria.
Pesa nyingi alizozipata tajiri huyo alizitumia kununua hisa katika makampuni mengine huko ulaya na Marekani, mfano alinunua hisa za asilimia 10 katika kiwanda cha kutengeneza vifaa vya michezo ya Adidas.
Utajiri wa mtu huyo ulitisha katika Nigeria, iliaminika hapakuwa na mtu tajiri kama yeye katika Nigeria hasa pale aliponunua eneo kubwa la visima vya mafuta huko Kaskazini mwa Nigeria, hilo ndilo liliwafanya wananchi na hata serikali kuamini kuwa kweli mfanyabiashara huyo alikuwa ni tajiri kupita mtu yoyote katika nchi hiyo.
Serikali ilimfuatafuata ilishindwa kumpata kwa sababu alilipa kodi zake kama kawaida, na hesabu zake zilikuwa wazi bila ujanja ujanja.
Huo ndio ulikuwa utajiri wa mtu huyo kutoka kabila la Dogo na lenye kudharaulika nchini Nigeria la Waagoni, yeye na mwandishi maarufu na mtetezi wa haki za Waagoni Ken Sarowiwa walikuwa marafiki wakubwa na ni yeye aliyefadhili shughuli zote za mtetezi huyo katika kuwatetea Waagoni. Alipohukumiwa kifo na rais Sani Abacha wa Nigeria tajiri huyo alilia machozi na aliamuru shughuli zake zisimame kwa wiki nzima katika kumuomboleza Ken Sarowiwa.
Kwa kusimama huko kwa kazi zake nchi ya Nigeria ilijikuta ikikumbwa na uhaba mkubwa wa mafuta, kwa sababu ni visima vyake vilivyoihudumia Nigeria kwa mafuta.
Tajiri huyu hakuwa mwingine bali chifu Onuku, tajiri aliyeheshimika nchini Nigeria kutokana na utajiti wake, watu wengi walimsalimia kwa kumpigia magoti, kila mtu nchini humo alimwita kwa jina la Chifu sababu ya pesa zake.
Iliaminiwa na wengi kuwa si ajabu aliheshimika kuliko hata Rais wa nchi hiyo, alitembea na msafara mrefu wa magari yasiyopungua kumi wakati mawaziri walitembea na misafara wa magari matatu tu!
Alikuwa ni jeshi lake la kumlinda nyumbani kwake, kazini na kwenye shughuli zake, jeshi ambalo halikutegemea kabisa msaada wowote wa polisi wala serikali, lilikuwa jeshi lenye kujitosheleza.
Alikuwa tajiri mno ni yeye aliyeipa serikali ya Nigeria pesa nyingi katika kampeni zake za uchaguzi kumwezesha Rais kushinda uchaguzi na kuingia madarakani! Rais yoyote aliyepigiwa debe na chifu Onuku ilikuwa ni lazima ashinde uchaguzi na kuwa rais! Kwa sababu hiyo chifu Onuku aliheshimiwa na kila mtu nchini humo.
Pamoja na heshima yote hiyo hakuna mtu aliyejua historia ya utajiri wake! Watu walishindwa kuelewa chifu Onuku alitajirika vipi, wapo waliosema alikuja na mamilioni ya paundi kutoka Uingereza na wapo pia waliosema mali ile haikuwa yake bali alikuwa msimamizi matajiri wakiwa Uingereza wakitesa na familia zao.
Maneno yote hayo hayakuwa kweli kuhusiana na utajiri wa chifu Onuku! Mali yote ilikuwa yake na aliipata nchini Uingereza tena kwa muda mfupi na kuamua kurudi nyumbani kwao Nigeria kuanzisha miradi yake iliyomwingizia pesa nyingi na kumfanya tajiri.
Huo ndio ulikuwa ukweli kuhusu chifu Onuku na hivyo ndivyo alivyoipata mali yote aliyokuwa nayo, lakini jina lake halisi hakuwa chifu Onuku aliitwa Profesa Daniel Owo.
*****
Miaka thelathini kabla:
Kijana mdogo na mzuri Daniel Kwanu Owo kutoka Nigeria alikwenda nchini Uingereza kusoma digrii ya kwanza ya elimu ya viumbe au Microbiology iitwavyo kitaalam, katika chuo kikuu cha Oxford.
Yalikuwa ni masomo ya miaka minne, baada ya kumaliza digrii yake ya kwanza katika chuo hicho Daniel hakutaka kurudi tena Nigeria alitamani aendelee kuishi nchini Uingereza na kuendesha maisha yake huko huko kwani hakuwa na kitu cha kufanya nchini mwake.
Kwa sababu ya kutokuwa na hati ya kumruhusu kuishi nchini Uingereza alilazimika kumuoa mwanamke wa Kiingereza mwenye umri mara mbili ya umri wake aliyekuwa amefiwa na mume wake! Alifanya hivyo ili apate tu kibali cha kuishi nchini humo.
Miaka mitatu baada ya kumuoa mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Linda Taylor, Daniel alipewa uraia wa Uingereza na akatafuta kazi katika kampuni moja ya utafiti wa magonjwa ya binadamu iliyoitwa British Microbiology Institute, ndoto yake ya kuishi Uingereza ikawa imetimia!
Alifanya kazi katika kituo hicho kwa muda wa miaka mitatu mfululizo na mwaka 1972 aliacha kazi na kujiunga tena na chuo kikuu cha Edinburgh ambako alichukua shahada yake ya pili ya Elimu ya viumbe.
Aliishangaza Uingereza kwa uwezo wake mkubwa na ugunduzi ni yeye ndiye aligundua kuwa mdomoni kwa binadamu kulikuwa na wadudu wasio na madhara lakini waliweza kusababisha matatizo tu pale kinga ya mwili wa mwanadamu ilipopungua!
Waingereza walishangazwa na ugunduzi huo kamwe hawakuwahi kufikiria kuwa Mwafrika tena mwenye asili ya Nigeria angeweza kufanya muujiza huo katika historia ya Microbiologia.
Alipomaliza digrii yake ya pili kabla hata ya kufanya kazi aliandika kuhusu elimu ya viumbe kilichoitwa Microbiology in the modern world, kitabu hicho kilipokubaliwa na bodi ya maprofesa jina lake la Daniel ambaye wakati huo aliitwa Dr. Daniel Kwanu Owo lilibadilika akawa anaitwa Profesa Daniel Owo.
Profesa Daniel Owo aliyeheshimiwa na kila mtu nchini Uingereza kwa utafiti aliofanya kuhusu wadudu! Majina yote ya wadudu yalikuwa kichwani mwake kama vile mtoto alivyokariri herufi za A mpaka Z! Hata kama ungemuamsha usingizini angekutajia kila kitu.
Hakutaka tena kufanya kazi za utafiti Profesa Owo aliamua kurudi tena Oxford, safari hiyo haikuwa kusoma tena bali akawa mhadhiri akifundisha somo la elimu ya viumbe wadogowadogo!
Alifundisha vizuri mno kiasi kwamba mwanafunzi yeyote aliyefundishwa na profesa Daniel Owo alielewa vizuri na baada ya kumaliza chuo wanafunzi aliowafundisha hawakupata taabu kupata ajira nchini Uingereza kwa sababu sifa za profesa Owo zilitanda kila mahali.
Katika muda wote alioishi Uingereza Profesa hakuwahi hata siku moja kurudi Nigeria, kwa sababu aliogopa kulogwa! Alikaa Uingereza yeye na mkewe na hawakufanikiwa kupata hata mtoto mmoja na mkewe kwa sababu mkewe alikuwa mzee sana!
Umaarufu na sifa alizopata profesa Owo nchini Uingereza zilimvimbisha kichwa sana na kujikuta anaanza kujisahau akajiingiza katika masuala ya ulevi wa pombe kali tabia aliyojifunza kutoka kwa mkewe, aliizoea pombe na yeye ikamzoea.
Ulevi ulizidi, ulevi ulipindukia na kujikuta ameanza tabia ya kulewa na kulala kwenye baa! Kiasi kwamba akawa anajisahau hata kufanya kazi yake akawa anakunywa pombe mpaka kujikojolea katika nguo zake! Akawa mchafu kupita kiasi, marafiki aliokuwa nao nchini Uingereza walijaribu kumbadilisha bila mafanikio yoyote.
Ulevi ukawa sehemu ya maisha yao yeye na mkewe aliyempenda wakawa wanakunywa pombe asubuhi hadi jioni wakati mwingine kulala huko huko.
Tabia hiyo haikuvumiliwa sana na uongozi wa chuo cha Oxford pamoja na kuwa uwezo wake wa kufundisha na kufanya utafiti ulihitajika sana! Uongozi wa chuo ulimfukuza kazi mara moja!
Profesa Owo akajikuta yupo kijiweni yeye na mke wake wakitumia akiba yote waliyokuwa nayo benki kunywa pombe na kufanya starehe! Afya zao ziliharibika na maisha yakawa magumu kupita kiasi, kero mbalimbali ziliwaandama na walifukuzwa katika nyumba waliyokuwa wakiishi sababu ya kukosa pesa ya kulipia pango! Profesa Owo na mkewe wakaanza kuzagaa mitaani.
Watu walishangaa iweje mtu mwenye elimu ya juu na uwezo mkubwa kama profesa Owo ahangaike kiasi kile mitaani! Ubalozi wa Nigeria nchini Uingereza ulipanga mpango wa kumrudisha nyumbani lakini mkewe alikataa na aligoma kula kwa wiki nzima mpaka mpango ukasitishwa.
*****
Utajiri wa David Syndrome, Suzanne Leone na Bill Gate:
Utajiri wa David Syndrome na mwanamke Suzanne Leone uliitishia nchini Uingereza na si Uingereza peke yake bali hata Marekani! Iliaminika hapakuwa na tajiri mkubwa kama wao katika nchi hizo mbili sifa zao zilienea Uingereza na Marekani nzima!
Walikuwa matajiri walioiletea sifa kubwa sana Uingereza kwa utajiri waliokuwa nao, ni wao walioifanya Uingereza ionekane ni taifa kubwa na lenye utajiri mkubwa.
Suzanne na David walifahamiana na utajiri wao ulikuwa karibu sana kama walizidiana sana basi ni kwa paundi chache sana! Na kila mara walipowasiliana walielezana umuhimu wa kufanya biashara ili kusiwepo na mtu mwingine tajiri kuliko wao duniani na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa David Syndrome na Suzanne Leone..
Lakini huko Marekani mtu mmoja aliudhiwa sana na kitendo cha matajiri wakubwa duniani kutoka Uingereza, yeye alitaka mtu tajiri kuliko wote duniani atoke Marekani huyo hakuwa mwingine bali kijana mdogo Bill Gate! Alichukizwa sana na utajiri wa David Syndrome na Suzzane Leone na alijiwekea ahadi ya siku moja kuwa tajiri kuwazidi wao na alifanya kila alichoweza kuhakikisha kuwa ndoto hiyo inatimia.
“Dady I want to be richer as compared to David Syndrome and Suzanne Leone!”(Baba nataka niwe tajiri kuliko David Syndrome na Suzanne Leone!) Hivyo ndivyo kijana Bill Gate alivyokuwa akimweleza baba yake kila mara na baba yake alimwona kama anachanganyikiwa kwa sababu ilikuwa si rahisi mtu kutajirika kuwazidi watu aliowaongelea.
Usiku na mchana Bill alishinda katika chumba maalum akifanya utafiti wa kitu ambacho kingerahisisha kazi za mwanadamu, alitaka aunde kitu kimoja ambacho kingefanya kazi zote za binadamu isipokuwa kuongezea uhai wa mwanadamu.
Kwa miaka kadhaa baada ya kumaliza chuo kikuu alikaa ndani akifanya utafiti wake, alitumia muda mdogo sana nje kupumzisha akili! Alipotoka huko alikuwa amegundua kifaa kilichoitwa kompyuta!
Dunia nzima ilikipokea kifaa hicho kwa shangwe na kilipofanyiwa majaribio kilileta mafanikio makubwa sana, dunia nzima ilianza kununua kifaa hicho, Ulaya, Marekani, Australia na nchini nyingine nyingi za Afrika ziliagiza makontena kwa makontena ya kifaa hicho!
Katika muda wa miaka michache tu dunia nzima ilikuwa ikitumia kompyuta na tayari Bill Gates alikuwa tajiri kuliko mtu mwingine yoyote duniani! Akaitimiza ndoto yake ya kuwazidi David Syndrome na Suzzane utajiri na kuileta sifa hiyo Marekani! Ilikuwa furaha mno kwake na baba yake hakuamini.
“I never believed when you said you were going to be richer than David and Suzanne!”(Sikukuamini mwanangu uliposema utakuwa tajiri kuliko David na Suzanne)
“GOD IS GREAT DAD!!”(Mungu ni mkubwa baba!)
*****
Ushindi huo wa Bill Gate uliwaudhi sana David Syndrome na Suzzane na waliamua kuziunganisha mali zao zote na kufanya kampuni moja lakini bado hawakumfikia Bill Gate kwa utajiri aliokuwa nao! Kwani utajiri uliendelea kukua kila siku iliyokwenda kwa Mungu!
David Syndrome na Suzzane walichanganyikiwa! Walishindwa wafanya nini kuibakiza sifa waliyokuwa nayo, walikuwa ni wenye mawazo mengi kila siku iliyokwenda kwa Mungu wakifirikia wangefanya nini kuibakiza sifa hiyo Uingereza, walisahau hata kufanya kazi vizuri walimfikiria Bill Gate.
Katika mwaka mmoja tu wa mawazo hayo walijikuta utajiri wao ukianza kuporomoka taratibu na waliandamwa na madeni, lakini utajiri wa Bill Gate uliendelea kukua tena kwa kasi ya ajabu.
“Ni lazima tumshinde tu! Mmarekani hawezi kumshinda Mwingereza!”
“Lakini tutamshinda kwa njia gani?”
“Subiri nitakueleza baada ya siku mbili, ninahitaji kuwaza vizuri!”
“Tafuta njia yoyote ile ili tuibakize heshima mikononi mwetu! Sawa?”
“Wewe usiwe na wasiwasi!”
****
Siku mbili baadaye kweli David Syndrome alikuwa amefikiria kitu ambacho kingewafanya matajiri tena, ndiyo ulikuwa ni mpango wa muda mrefu lakini matunda yake aliamini yangekuwa mazuri kupita kiasi na utajiri wao ungemzidi tena Bill kwa sababu dunia nzima ingewategemea wao na watu wengenunua kitu ambacho wangetengeneza kuliko hata kompyuta kwa sababu kingekusa uhai wa mwanadamu.
Siku hiyo hiyo David alimpiga simu Suzanne na kumwomba waonane.
“I have thought of something great which will make the entire world worship us!”(Nimefikiria kitu fulani kikubwa sana kitakachofanya ulimwengu wote utuabudu!)
“What is that sir?”(Umegundua nini bwana?) Aliuliza Suzanne.
“Meet me at Dracula hotel this evening! I will tell you everything about the vission I have!”(Tukutane Dracula hoteli nitakuambia kila kitu katika maono yangu!)
“What time?”(Muda gani?)
“7:30pm!”
****
Suzanne na David walikaa ndani ya hoteli ya Dracula kwenye meza iliyokuwa pembeni kabisa mwa ukumbi wa hoteli hiyo na walikuwa wakiongea kwa sauti ya chini sana ili mtu asisikie walichokiongea, kilikuwa ni kitu hatari mno.
“Nimefikiria juu ya suala la kutengeneza mdudu ambaye atawafanya watu waugue sana na kukondeana na kutakuwa hakuna tiba sisi tutatengeneza dawa za kuongeza nguvu na kuongeza siku kwa wagonjwa wa ugonjwa huo! Je tutakuwa hatujatajirika na kubaki na sifa yetu? Ndiyo itachukua muda mrefu lakini mwisho wa yote tutakuwa matajiri kumshinda Bill Gate?” Alisema David Syndrome huku Suzanne akisikiliza kwa makini.
“Jambo hilo linawezekana kweli, au wewe ni una utaalamu wa wadudu?’ Suzanne aliuliza.
“Hii ni kazi ndogo yupo mtaalamu mmoja anahangaika mitaani sasa hivi anaitwa profesa Owo, alikuwa mhadhiri katika chuo cha Oxford wakamfukuza nafikiri huyo atatusaidia sana!”
“Basi ni vyema tumwone kwanza huyo profesa!”
Dakika chache baadaye walimkuta profesa Owo ndani ya baa akinywa pombe na mkewe, waliomba wamuone pembeni naye akanyanyuka na kuwafuata na walimweleza kila kitu walichotaka afanye.
“How much are you going to pay me?” (Mtanilipa shilingi ngapi?)
“We shall pay you two million pounds, one million on the signing date and balance of one million shall be paid when the job is complete”(Tutakulipa paundi milioni mbili, moja siku ya kusaini mkataba na nyingine utakapomaliza kazi)
Paundi milioni mbili kwa wakati ule zilikuwa sawa na shilingi za kitanzania bilioni moja na milioni mianane! Profesa Owo hakuamini kama alichokuwa anaambiwa ni kweli.
“When are we signing the contract?”(Mkataba tutausaini lini?)
“Can you do the job?”(Lakini unaiweza kazi hiyo?)
“Aaahgh! Thats a tiny job to me! All the patient will suffer from Diarrhoea, TB, Abscesses, on and off fevers and Eventually they will die”(Aaahgah! Hiyo ni kazi ndogo sana kwangu, wagonjwa wote wataugua kuharisha, kifua kikuu, majipu, homa za mara kwa mara na baadaye watakufa!)
“But he will show us the formular to make a certain drug to lenghen the a lives, ok?”(Lakini utatuonyesha njia ya kutengeneza dawa ya kuongeza siku zao za kuishi, sawa?)
Je nini kitaendelea?
Je profesa Owo atalipwa pesa hizo? Je, atamtengenezaje mdudu huyo? Na je nini kitawapata David Syndrome na Suzanne Leone? Je ukweli utajiri wao utalingana na wa Bill Gate?

No comments