Header Ads

Magufuli: Wanaotetea majipu tutawatumbua

 Rais Dk. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi, Mzee Ally Mtopa wakati alipokutana na Wenyeviti na Makatibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa mikoa na Wilaya za Tanzania Bara na Visiwani, Ikulu jijini Dar es Salaam jana. PICHA: IKULU

WAKATI baadhi ya taasisi za haki za binadamu, wasomi na wanasiasa wakikosoa mfumo wa Rais John Magufuli, wa kuwawajibisha watendaji wa umma, kiongozi huyo wa nchi amesema wanaowatetea watendaji wanaowajibishwa, nao ni majipu na ataanza kuwafuatilia.
Baadhi ya wanasiasa ambao wamejitokeza hadharani na kumkosoa Rais Magufuli kwa mfumo wake huo ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na aliyekuwa mgombea wa chama hicho kwa mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam na Wenyeviti na Makatibu wa CCM wilaya na mikoa yote nchini wakati akiwashukuru kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka jana, alisema anashangaa watu hao kuwatetea watendaji hao aliosema ni matajiri waliokuwa wakiiba huku wakiacha maskini waliokuwa wakiibiwa.

Kama ni haki za binadamu ziko kwa matajiri waliokuwa wanaiba, haki za binadamu hawa waliokuwa wanaibiwa hazipo? Kwa hiyo unaweza kuona hao waliokuwa wanawatetea nao ni majipu, nao tutaanza kuwafuatilia," alisema na kuongeza:

Hata ukimtoa huyo, hata nikimtoa hadharani, wanasema eti nimefanya kosa, waliwaibia Watanzania hadharani, lazima tutawatangaza hadharani, mateso waliyoyapata Watanzania mamilioni kwa kuibiwa na hawa wachache, lazima na wao waanze kuyapata hayo hayo." Alisema:

Aliyewateua ni mimi na niliwataja hadharani, sasa kwa nini wafurahi kutajwa hadharani siku ya kuteuliwa na wasitajwe hadharani siku ya kutumbuliwa? ...Kwa sababu hao ndiyo saizi yangu kuwatumbua, kama ni mkurugenzi wa manispaa au wa wapi, nimemteua mimi, wanasema eti apewe muda wa kujieleza,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hatua zinazochukuliwa na serikali yake kwa kuwawajibisha baadhi ya watendaji wabadhirifu, imesaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha. Alitoa mfano wa fedha zilizookolewa kwenye wafanyakazi hewa ambao alisema mpaka sasa wamefikia 7,700.

Alisema upembuzi juu ya watumishi hewa bado unaendelea na kwamba fedha walizokuwa wakilipwa zingetumika kujenga barabara, shule na hospitali.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewataka viongozi wa CCM kusameheana kwa yale yote yaliyotokea wakati wa uchaguzi na kutaka wawe na mshikamano ili wawasaidie wananchi kupata maendeleo. “Kwa hiyo nataka kuwahakikishia wana-CCM kuwa sisi tutaendelea kusimamai imara, tunataka Tanzania iwe yenye neema, Tanzania tajiri, ila kuna watu wachache ambao wametumia vibaya nafasi zao, alisema.

Utumbuaji wa karibuni ambao umelalamikiwa ni ule wa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa wakati wa uzinduzi wa Daraja la Nyerere.

Hatua yake ya kumsimamisha Kabwe ilifananishwa na ile ya udunguaji wa ndege kutokana na kuchukua uamuzi huo akiwa jukwaani, tena baada ya kuwahoji wananchi.

Kabla ya kufanya hivyo, Rais Magufuli alikuwa akisimamisha watumishi hao kwa kuchukua uamuzi akiwa ofisini, kisha Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu kutoa taarifa kwa umma.

Uamuzi wa kumsimamisha Kabwe ulichukuliwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kueleza mikataba tata mitatu iliyoingiwa na mkurugenzi huyo.

Katika mikataba hiyo, mmoja umelisababishia Jiji la Dar es Salaam hasara ya karibu Sh. bilioni tatu.

Baada ya Makonda kuitwa jukwaani na kueleza yale aliyodai yametendwa na Kabwe, Rais Magufuli alisema:

Jamani sasa mnataka nifanyaje? Mnataka nitumbue jipu hapa hapa? Wangapi wanataka nitumbue jipu?,alihoji huku mamia ya wananchi wakinyoosha mikono kuashiria wanamuunga mkono.

Baada ya hatua hiyo, Rais Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi Kabwe kupisha uchunguzi huku akisema apelekewe salamu za kusimamishwa kwake huko huko aliko.

Uamuzi wa kumsimamisha Kabwe ulitolewa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Daraja la Kigamboni ambalo litajulikana kama Daraja la Nyerere.

Daraja hilo linaunganisha Kigamboni na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam. Kabwe ambaye hakuwapo eneo la tukio wakati akisimamishwa, alipotafutwa na Nipashe muda mfupi baadaye kuzungumzia agizo la Rais, alisema kama Rais Magufuli ameamua kumsimamisha kazi, hajakosea.


CHANZO; NIPASHE

No comments