Header Ads

Mama Lulu awa Kituko Kaburini kwa Kanumba, Mastaa wamshangaa, Lulu azua maswali


DAR ES SALAAM: Katika hali ya kushangaza, mama wa mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’, Lucresia Karugila, amegeuka kituko kwa kufanya mambo yasiyo ya kawaida katika kumbukumbu ya miaka minne ya kifo cha Steven Kanumba, aliyekuwa mpenzi wa mwanaye.

NI KINONDONI
Tukio hilo lililoushangaza umati uliohudhuria shughuli hiyo, lilijiri wikiendi iliyopita katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambako pia kulifanyika misa maalum ya kumuombea marehemu katika kaburi la Kanumba.
MAMBO YALIANZA HIVI
Tofauti na walivyovalia watu wengi nguo nyeusi kama ishara ya majonzi, mama huyo aliingia makaburini hapo akiwa amevaa ‘t-shirt’ ya kumpongeza mwanaye Lulu kwa ushindi wa tuzo aliyoipata hivi karibuni nchini Nigeria huku akiwa na shada kisha akaenda kuliweka kwenye kaburi la Kanumba huku akionekana kuyumbayumba.

IMG_3424 “Mh! Mwenzangu mbona kama mama Lulu ameshtukizwa kuja, anaonekana kachangamka mno, halafu hata t-shirt aliyoivaa haiendani na msiba, atavaaje t-shirt ya kumpongeza mwanaye wakati hapa ni makaburini na isitoshe huyo mwanaye mwenyewe hata hakuja hapa, cheki anavyotembea,” alisikika msanii mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
AMKUMBATIA KILA MTU
Kama hiyo haitoshi, mama Lulu alionesha kuchangamka zaidi na kuwavunja mbavu watu kwa jinsi alivyokuwa akimkumbatia kila mtu aliyekuwa eneo hilo ambapo alianza kwa kumkumbatia Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff), Simon Mwakifwamba kisha kupiga naye picha na baadaye akahamia kwa mastaa wengine ambao alikuwa hajawaona siku nyingi.
AJISHTUKIA
Kuna wakati mama Lulu alionekana kujishtukia kwa kusema kuwa yeye amevaa t-shirt ya Lulu kwani ni vazi tu lakini kilichowashangaza wengi ni namna ambavyo alikuwa akionekana kuchangamka kwa kucheka na kuongea kwa sauti ya juu.
Lulu-michael1MASTAA WAMSHANGAA
Mastaa waliofika makaburini hapo ambapo mbali na kumbukumbu ya Kanumba kulikuwa na mazishi mengine yakiendelea, walionekana kumshangaa huku wengine wakisema huenda anaongea sana na kupiga ‘selfie’ kwa sababu ‘ameshtua’ mvinyo kidogo.
“Duh! Mama Lulu kaja makaburini amechangamka mno, halafu bora basi angejifunika kanga kuziba tu ile nguo inayomshabikia mwanaye wakati Lulu mwenyewe ameshindwa kuja,” alisema msanii mwingine.
AMSHOBOKEA STEVE NYERERE
Baada ya watu kupungua na wengine kuwa wametawanyika mama Lulu alimuona Steve Nyerere na kumkimbilia kisha kumkumbatia na kuulizana hali, hali hiyo haikufurahiwa na watu waliokuwa makaburini kwani wapo waliosema kuwa mama Lulu habadiliki.
“Mama Lulu yuko kama jana jamani, embu muone hajui kama hapa ni makaburini kwanza amekuja amechelewa lakini bado anaongea sana, angetakiwa kuwa mstaarabu kidogo kuliko kuwa kituko maana kila analolifanya watu wanamshangaa na wengine wakimcheka,” alisikika msanii mwingine.
LULU AZUA MASWALI
Mama Lulu alipata wakati mgumu kwani kila msanii aliyekuwa akikutana naye alikuwa akimuuliza kuhusiana na kutokuwepo kwa mwanaye Lulu eneo hilo ambapo alikuwa akiwajibu kuwa hakufahamu alikokuwa kwani hakumshirikisha katika safari hiyo.
“Mimi sijui alipo Lulu sijamshirikisha lolote kwenye maamuzi yangu, nimetoka kwangu nikapita Namanga, nikanunua shada kisha nikaja kuadhimisha miaka minne ya kifo cha Kanumba,” alisema Mama Lulu.
Kanumba-612MAPAPARAZI WAMSAKA LULU
Baada ya mama Lulu kushindwa kujua alipo mwanaye huku kila mtu akihoji kivyake juu ya kukosekana kwa mrembo huyo katika shughuli hiyo, mapaparazi walimtwangia simu Lulu bila mafanikio kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa.
ATUPIA POSTI INSTA
Hata hivyo, baadaye Lulu aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kuwa yeye kila siku kwake ni kumbukumbu ya Kanumba kwani hana siku maalum.
“Mimi sina siku maalum ya kumkumbuka Kanumba kwani namkumbuka kila siku,” aliandika Lulu.
MAMA KANUMBA AFUNGUKA
Hata hivyo, pamoja na vituko vyote alivyoonesha mama Lulu, mama Kanumba alimshukuru kwa uwepo wake lakini hakufurahishwa na kitendo cha Lulu kutofika.
“Mimi sihitaji anipe fedha au nini, suala la msingi ni faraja tu. Kama hivi mama yake alivyokuja, na yeye angefika ingekuwa ni jambo jema,” alisema mama huyo.
KUMBUKUMBU
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 nyumbani kwake Sinza-Vatcan jijini Dar akiwa na Lulu aliyekuwa mchumba wake. Lulu alishtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia kutokana na kudaiwa kugombana na marehemu siku ya tukio.
CHANZO: IJUMAA WIKIENDA

No comments