Header Ads

Mambo matano ambayo huyafahamu kwa Mo Music


Moshi Katemi ‘Mo Music’

Rock City ni miongoni mwa miji mikubwa Bongo. Inasifa kemkemu ambapo kwenye ‘code’ ya burudani inashika namba kwa kutoa wasanii wenye majina makubwa, ambapo mbali na Fid Q, PNC, Young Killer, Rado, Barakah Da Prince na wengine wengi katika ardhi hiyo amekulia msanii wa Bongo Fleva anayefanya vizuri kwa sasa Moshi Katemi ‘Mo Music’.
Huyu ni staa wa Wimbo wa Basi Nenda, hapa anafunguka mambo matano (5) ambayo anasema huyafahamu.

Atendwa, atusua kimuziki
Mo Music anasema sababu hasa ya yeye kutusua kimuziki ilikuwa baada ya kutendwa kimapenzi na msichana aliyempenda wakati akiwa sekondari huko Rock City.

Anasema alianza uhusiano na msichana huyo wakiwa kidato cha pili lakini baada ya kumaliza kidato cha nne na msichana huyo kufaulu kuendelea na masomo mkoani Kilimanjaro mambo yalibadilika jambo lililomuumiza mno moyo kiasi cha kupata ‘feeling’ za kutunga Wimbo wa Basi Nenda uliomtambulisha. Hata hivyo, yeye na msichana huyo ni marafiki, kwa sasa yupo jijini Dar anajiendeleza kimasomo katika Chuo cha Ardhi.

Aruhusiwa kuimba kanisani pekee
Mo Music anasema alipokuwa anaanza kufanya harakati za muziki mama yake alikuwa hapendi lakini hata hivyo, baada ya kuona anaipenda sana kazi hiyo alimruhusu kuimba tu kanisani.
“Nilikiuka agizo hilo la bi mkubwa lakini haikuwa ishu sana maana baada ya kutoka pia anayafurahia mafanikio yangu hata kama si makubwa kiivyo!”

Alikuwa rapa
“Nilianza gemu nikiwa rapa, nilirekodi wimbo wa kwanza mwaka 2010 uitwao Nakudanganya baadaye nilibadilika baada ya kukutana na prodyuza wangu Lol Pop na kugundua kuwa nina kipaji cha kuimba.”

Menejimenti yake inamkwamisha
Mo Music anasema kati ya vitu ambavyo vinamuumiza kichwa kwa sasa ni menejimenti aliyomo iitwayo Aljazeera ambayo iko chini ya MacDenis. Anadai menejimenti hiyo haimsaidii kwa lolote na imegeuka kuwa ‘business partner’ wake maana anachangia kwa asilimia kubwa ili kazi zake ziende japo mkataba wake hauko hivyo.

“Kiukweli menejimenti yangu inaniumiza sana, nimevumilia mpaka nimechoka maana badala ya mambo yangu kusonga mbele yanarudi nyuma. Ninapohisi ni wakati muafaka wa kuachia ngoma au kufanya skendo wao wananiambia subiri, kila mara nimekuwa mtu wa kusubiri, siyo siri nimechoka na sasa ninafanya jitihada za kuvunja mkataba.”
Hayuko kwenye uhusiano wa mapenzi
“Watu wanaweza wasiamini lakini ukweli ni kwamba kwa sasa sipo kwenye uhusiano wa mapenzi maana akili yangu haijatulia kutokana na gemu langu kuwa halijasimama vizuri na pia sijampata mtu sahihi wa kuwa naye,” anamaliza Mo music.

 Makala: Boniphace Ngumije/GPL

No comments