Header Ads

Siwema wa Nay ahenyeshwa gerezani!

Mbongo Flava, Emanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’  akiwa na aliyekuwa mpenzi wake  Siwema Edson

DAR ES SALAAM: Kufuatia kifungo cha miaka miwili jela kwa mwanadada Siwema Edson (28) ambaye alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kujipatia pesa kwa njia ya vitisho kutoka kwa kigogo mmoja ambaye jina liko kapuni kwa sasa, madai mapya ni kwamba, mrembo huyo amehenyeshwa gerezani, Risasi Jumatano linakufunulia.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Siwema ambaye ni mzazi mwenzie na nyota wa Bongo Flava, Emanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’, alipofikishwa gerezani tu alinyolewa nywele, akapewa mavazi ya ufungwa na kuoneshwa sehemu za kufanyia usafi.
TWENDE NA CHANZO
“Jamani nimesikia kuhusu Nay ameapa kwamba anamtafuta mwanasheria mkali ili ageuze kibao cha Siwema, badala ya kufungwa apigwe faini.
“Lakini mimi nina habari kwamba, Siwema ameshaanza kutumia kifungo chake, kwani alipowasili tu kwenye Gereza la Butimba alinyolewa nywele, akapewa yale mavazi ya rangi ya machungwa ya wafungwa na kupangiwa sehemu ya kufanya usafi.
“Sasa Nay anaposema anatafuta mwanasheria mbona naona kama amechelewa sana! Lakini pia sijajua kisheria hiyo imekaaje!” alisema mnyetishaji huyo.
SIWEMA ALITEGEMEA FAINI
Akaendelea: “Unajua wakati kesi inaendelea, Siwema alitarajia zaidi kupigwa faini lakini ikawa kinyume, akakumbana na kifungo kabisa cha jela, lakini pia sijajua hapo sheria ikoje! Kwamba lile kosa lake lilikuwa si la faini?”
ALIVYOJITETEA
Siku ya hukumu, mrembo huyo alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba mahakama impunguzie adhabu akidai kwamba ana mtoto mdogo (aliyezaa na Nay) ambaye anamtegemea, pia ana wadogo zake wanaomtegemea.
ALIANGUA KILIO KORTINI
Habari nyingine zinasema kuwa, baada ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Ilemela, mheshimiwa Sumaye kutamka kifungo cha miaka miwili jela kufuatia kumtia hatiani, inadaiwa Siwema aliangua kilio.
SIWEMAGARI41 (1)KIGOGO AONGEA NA RISASI MCHANGANYIKO
Juzi, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta kigogo huyo kwa njia ya simu na kutakiwa kutoa maoni yake kuhusiana na adhabu aliyopewa Siwema ambapo alijibu kwa kifupi:
“Sina mengi ya kusema, sheria imechukua mkondo wake.”
WAKILI ATAFSIRI SHERIA
Mwanasheria mmoja wa jijini Dar alipozungumza na gazeti hili juzi, alisema kosa alilokutwa nalo Siwema lina hukumu mbili.
“Lile kosa lina hukumu mbili, ya kifungo au faini. Sasa kama hakimu wake aliamua hivyo, mimi sijui. Lakini ndugu wakimpigania anaweza kutoka,” alisema mwanasheria huyo akiomba hifadhi ya jina lake.
SIWEMA AMEFIKAJE HAPA?
Mei 2, mwaka jana, Siwema alilala ‘nyuma ya nondo’ (mahabusu) kwa siku mbili katika Kituo Kikuu cha Polisi, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza baada ya kukamatwa nyumbani kwake Lumala, Manispaa ya Ilemela akidaiwa kujipatia mali kwa njia ya vitisho.
Awali ilidaiwa kuwa, Siwema aliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na kigogo huyo kwa ahadi ya kufunga naye pingu za maisha kufuatia kigogo huyo kufiwa na mkewe.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza kwa wakati huo, ACP Charles Mkumbo alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
Nay anasemaje
Mzazi mwenziwe na Siwema, Nay wa Mitego alisema atafanya chini juu kuwatafuta mawakili wawili ili kulishughulikia suala hilo kisheria.
Alisema Siwema alikamatwa baada ya kigogo huyo kutoa taarifa kwa jeshi hilo ambapo walifungua jalada la uchunguzi Mei 2, mwaka jana na siku hiyohiyo walimkamata mtuhumiwa akiwa nyumbani kwake.
“Ni kweli tulimkamata Siwema Edson, mkazi wa Lumala. Ametuhumiwa kujipatia mali kwa njia ya vitisho. Awali alikuja mlalamikaji kabla ya kukamatwa.
“Hawa watu awali walikuwa wapenzi. Katika mapenzi yao, siku moja, Siwema alimpiga picha za utupu mlalamikaji bila yeye kujitambua wala ridhaa yake,” alisema Kamanda Mkumbo.
Alisema baadaye uhusiano wao ulivunjika, ndipo Siwema akatumia picha hizo kumtishia kuwa kama hatatimiza matakwa yake kwa kumnunulia gari na kumpa fedha, basi angezisambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook.
“Mlalamikaji alitimiza matakwa ya mtuhumiwa kwa kumnunulia gari aina ya Honda CVR lenye namba za usajili T103 DDU na akamtumia fedha. Lakini Siwema aliendelea kumtumia vitisho, akimtaka amtumie kiasi kikubwa cha fedha za mtaji, ndipo mlalamikaji akaja kutoa taarifa polisi, likafunguliwa jalada la uchunguzi,” alisema Mkumbo.
Gari hilo lilishikiliwa kituoni hapo huku Siwema akiachiwa kwa dhamana wakati upelelezi ukiendelea. Ulipokamilika alifikishwa mahakamani.
 CHANZO:  RISASI MCHANGANYKO

No comments