Header Ads

TOO MUCH! NDOA YA OKWI NA SIMBA MPAKA LINI?


Na David Wambura
Sasa too much ndiyo unachoweza kusema baada ya duru za kimichezo pamoja na kauli mbalimbali za baadhi ya viongozi wa timu ya Simba SC kuanza kuonesha wako tayari kumrudisha klabuni kwao mshambuliaji wao wa zamani Emmmanuel Okwi, hususan kauli za Mwenyekiti wa kamati ya usajili Simba bwana Hans Poppe hivi karibuni kwenye vyombo vya habari.

Hapa naomba nieleweke wazi hakuna asiyejua ubora wa Okwi enzi zake Simba, mimi ni moja ya mashabiki wake wakubwa wa kile amewahi fanya kwenye klabu ya Simba.

Ila hofu yangu kwenye harufu ya songombingo hili ni moja tu, nikiiangalia Simba na viongozi wake wa sasa napata picha huenda wameanza kuamini njia pekee ya kutatua changamoto zao ndani ya uwanja ni kurudisha wachezaji wao wa zamani kitu ambacho si mtazamo sahihi kwa maoni yangu na inasikitisha kama kweli huu ndiyo mtazamo kwani walipaswa kujifunza tayari sababu si mara ya kwanza, kwa nyakati tofauti tumewahi kuwasikia kina Kisiga, Owino hivi karibuni Mgosi, Kazimoto. Wachezaji wote hao kwa nyakati tofauti wamewahi kurudi Simba na kuondoka bila kuongeza lolote la maana na sasa Okwi tena kwa mara nyingne! ni wazi viongozi wa Simba hawajifunzi haraka.

Ukitaka kujua tofauti kati ya taasisi iliyo na mipango sahihi kwenda mbele na taasisi isiyokua na uhakika inakokwenda ni rahisi tu, moja ya dalili za taasisi isiyo na mipango ya uhakika kuisaidia kwenda mbele ni tabia ya taasisi husika kuwa na mazoea ya kurudia matapishi yake yenyewe kwa kuendelea kuamini watu waliowahi kuwa sehemu yake huko nyuma kua ndiyo wenye hati miliki ya kuivusha kwenda mbele hata nyakati mpya zinazohitaji mambo mapya na watu wapya.

Taasisi makini ni ile ambayo kila mara huwa na mpango mahsusi wa kurithishana kutoka kizazi kimoja kwenda kingne bila purukushani (succession plan) lakini hua haitoshi tu kuwa na mpango wa kurithishana mnapaswa kuwa na ujasili wa kuusimamia mpango husika na kuhakikisha unatekelezeka.

Ni kwa misingi hiyo fununu za Okwi kurudi tena Simba kwa mara nyingne zimeweka ukakasi kwenye ulimi wangu, kwani kwangu hiki ni kiashiria cha udhaifu uliopo ndani ya klabu ya Simba kwa sasa, kwangu ni sawa na kuwa na mke anayeweza kuamua muda gani awe nawe muda gani aende kuzurura kwa watu wengine, sababu anajua huna ubavu wa kumkataa, walio wahi kuwa kwenye mahusiano watakubaliana nami kuwa hakuna kitu kibaya kama kuachana na mwenza wako akaenda aendako kwa walionazo akarudi akakuta bado uko palepale huna mbele wala nyuma.

Mbaya zaidi hujajenga hata jeuri ya kimasikini ya kumkataa, na huu ni ukweli mwingne unaouma kuhusu story ya Simba na Okwi, Simba wanakosa jeuri ya kumkataa Okwi kutokana na ukweli kwamba toka Okwi kaondoka, Simba kama klabu hawajapiga hatua ya maana kwenda mbele ndiyo maana ni rahisi kuamini ujio wa Okwi labda unaweza kua suluhisho.hapa Okwi anajiona mwanamke mrembo anayeringa huku Simba ikiwa ni mwanaume aliechoka yuko tee. Ukitaka kujua ukweli wa maneneo yangu na kile nachokiongea jiulize ni mchezaji gani aliyewahi ondoka Yanga miaka mitatu au mininne iliyopita anajeuri ya kurudi Yanga ya sasa?

Lakini pia unaposikia sakata hili ni vigumu kujizuia kufikiri pengine zile kelele za majirani zao Yanga sasa zimewaingia na sasa zimeanza kuathiri uwezo wao wa kufanya maamuzi, kwani moja ya sifa iliyokuwa inawatofautisha Simba na Yanga kwa miaka mingi, ni uwezo wa Simba kufanya mambo yake bila kuathiriwa na ‘pressure’ kutoka Yanga, wakati Yanga wakisajili kwa mbwembwe nyingi na magazeti Simba hujikita kusajili kiufundi na kwa umakini mkubwa kitu ambacho mara zote kimekua kikijidhihirisha kila mara timu hizi kongwe na pendwa zilipokutana huko nyuma.

Lakini sasa inaonekana zile kelele za Muro zimeanza kuwavuruga na sasa pressure iliyojengwa imeanza wafanya wafikirie wanaweza tu kuamka wakawa kama watani zao, ufikiri wa style hii ni ufikiri wa mtu asiyejua anachofanya.

Kwa mtazamo wangu ili klabu ya Simba ipige hatua ya kweli kwenda mbele, kwanza lazima wakubali wanapita kipindi cha mpito kwenye klabu yao (transition period) na wakubali ukweli unaouma kwamba kwa sasa Yanga wako hatua kadhaa mbele yao na kwamba kufika pale inahitaji mipango madhubuti si hii ya ‘unga-unga mwana’ ya kufikiri tu unaweza kulala na kuamka ukamrudisha Okwi ukawa kama Yanga, wakikubali ukweli huu watajikita kuendeleza kikosi cha vijana wenye vipaji walionao sasa, wachezaji kama Hassani Isihaka, Hasan Kessy, Mkude, Ajib, Ndemla hawa ni wachezaji wenye vipaji vikubwa na kama wataandaliwa kwa muda mrefu watakapofika umri wa ku-mature kama wachezaji miaka 24-26 watakua msaada mkubwa kwa timu, kwani vipaji vyao havina shaka.

Ukishakua na uti wa mgongo wa wachezaji makinda wenye vipaji kama niliowataja hapo juu mpango wa pili unapaswa kuwa kuendelea kutafuta wachezaji makinda wenye uwezo kama wao ili kuweza kuunda timu ya kizazi kijacho itakayodumu muda mrefu na si kurudisha wachezaji wa zamani kwa kutaka kulazimisha mafanikio kwa njia ya mkato.

Kwa mfano pesa ambayo ungeweza kumnunua Okwi kwa nini usiende kumchukua Michael Olunga pale Kenya mchezaji kijana mweye kipaji murua, kwa mtazamo wangu Olunga ana kila sifa za foward wa kisasa, mrefu, mzuri hewani na miguuni ana nguvu, anambio anaweza attack space kwa pace yake, si aina ya maforward wa kizamani wanaosimama kwenye box, huyu anaweza ku-patrol channels zote kulia na kushoto uwanjani, ni mchezaji aina ya Ngoma au Mbwana Samatta mchezaji ambae kwa ‘movement’ zake uwanjani anaweza wahamisha mabeki na kutengeneza nafasi kwa wenzie, ningekuwa kiongozi wa Simba ningefikiria kufanya sajili za wachezaji kama Olunga na kuwasubiri watani zangu Yanga baada ya miaka miwili au mitatu kuona nani atacheka sana mwishoni.

Simba haitakua ya kwanza kuwa klabu inayolazimika kukubaliana na ukweli huu kwamba wanapita kipindi cha mpito na kwamba mpinzani wake wa jadi yuko imara kuliko yeye, Barca iliwahi kubali kuwa Madrid ni bora kuliko yeye unakumbuka enzi Figo anatoka Nou Camp anahamia Bernabeu, Galactico ilikua bora sana kabla Madrid na Galactico yake haijapitia kipindi cha mpito pia huku Baraca ya Ridjkad  na Pep Guardiola ikiwa moto hizi ni ‘cycle’ ambazo kila klabu lazima ipitie.

Madrid wamewahi kukusanya wachezaji msimu huu, unaofuata wakatimua karibu wote mfano ni ile Madrid ya kidachi ya kina Rud van Niestroy, Huntelar, Sneidjer, Rubben, Van Devart, pamoja na kina Heinze, Cicinho baadae wakatimua wote hii inaonesha ilivyo ngumu wakati wa kujenga upya timu lakini mwisho wa siku uvumilivu ndiyo neno la msingi.

Kuna mtu anaweza sema Okwi kurudi Simba nini bhana! mbona Scholes alirudi United, yes alirudi na ilikua kipindi pekee Fergie amewahi fanya hivyo na hata hivyo haikuondoa ukweli kwamba kitendo hicho kiliashiria udhaifu kwa upande wake na alilazimika kutumia muda mwingi kujitetea dhidi ya kina Viera na Noise Neighbours waliofananisha hilo na ‘an act of desperation’, lakini tofauti nyingine na Okwi ni kwamba Scholes alistaafu akarudi timu ileile si huyu Okwi anayezerura lakini pia Scholes alienda akarudi mara moja si kwenda kwenda na kurudi-rudi tu kila ukijiskia.

Yote mifano ya Torres na Kaka wamewahi rudishwa timuzao za zamani lakini ni mara moja tu Wenger na mapungufu yake yote aliliona hili kwamba mwamke hata kama akikukuta umechoka vipi ilimradi wakati kwa hiari yake aliona mwingne ni bora kuliko wewe akirudi mwambie ‘seat’ yake keshakaa mwingne hata kama unajua yawezekana yeye bado anaurembo kuliko uliyenae ndiyo alichomfanyia Cesc Fabregas wakati anataka kurudii Arsenal, sasa jaribu kupata picha fedheha Arsenal wangeipata kama wangemlegezea Cesc, akiwa captain wa timu ali-force kuuzwa huku akinunua sehemu ya mkataba wake ku-force lengo lake halafu baadaye aje kirahisi tu, akimwambia Wenger bado anaipenda Asernal?

Simba kama klabu wanapaswa kujiuliza wanataka kuwa kitabu ama ukurasa tu ndani ya kitabu, kama jibu ni kitabu njia ni moja tu waendelee kuuamini mpango wao wa muda mrefu na kuwa na ujasiri wa kuusimamia, kurudi kwenye misingi iliyoijenga na kuisadia klabu hiyo kongwe kwa muda mrefu sasa kama nilivyokkwisha eleza na kuacha kuendesha klabu kwa mihemko ya Muro na pressure ya upande wa pili al maarufu ‘wakimataifa’.

No comments