Header Ads

Wakurugenzi Bandari wana kesi ya kujibu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imesema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wa zamani, Ephraim Mgawe na Naibu Mkurugenzi Mkuu wake, Hamadi Koshuma wana kesi ya kujibu dhidi ya mashtaka ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka.

Endapo watapatikana na hatia, watumishi hao wa zamani wanaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo.

Mkeha alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa Jamhuri ambao uliita mashahidi watano, mahakama yake imeona washitakiwa wana kesi ya kujibu.

Hakimu alisema washtakiwa wanatakiwa kupanda kizimbani kujitetea ili kuondoa maswali katika ushahidi ulioacha mashaka dhidi yao.

Washtakiwa wataanza kujitetea Mei 16, Mkeha alisema na kwamba dhamana zao zinaendelea.

Ilidaiwa katika kesi ya msingi kuwa Desemba 5, mwaka 2011, washtakiwa wakiwa watumishi wa umma, katika utendaji wao wa kazi, kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kwa kusaini mkataba wa kibiashara bila kuitisha zabuni.

Ilidaiwa kuwa mkataba huo ulikuwa kati ya TPA na Kampuni ya ujenzi ya Communication and Construction ya China (CCCC), ambao ulikuwa unahusu ujenzi wa gati namba 13 na 14 katika bandari ya Dar es Salaam, bila kuitisha zabuni.
Ilidaiwa kuwa, kitendo hicho kiliipa faida Kampuni hiyo ya China na kuitia hasara serikali.
CHANZO: NIPASHE

No comments