Header Ads

Yanga kuchea na Al Ahly ya Misri leo Taifa

UKIONA NDEVU...
YANGA, leo Jumamosi jioni itacheza kwa tahadhari kubwa mechi yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya pili dhidi ya Al Ahly ya Misri lengo likiwa ni kutokubali kutolewa tena na timu hiyo katika michuano hiyo.
Mwaka 2014 ikiwa chini ya kocha wake wa sasa, Hans van Der Pluijm, katika michuano hiyo, Yanga ilitolewa na Al Ahly kwa penalti 4-3 baada ya kufungwa bao 1-0 katika marudiano jijini Alexandria, Misri, Machi 09, 2014.
Awali katika mchezo wa kwanza Machi Mosi, 2014 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 82.
Ikicheza ugenini kwenye Uwanja wa Harras El-Hedoud, Alexandria, Yanga ilifungwa bao 1-0 na Al Ahly mfungaji akiwa Sayed Moawad, na katika penalti kwa Yanga, Said Bahanuzi na Oscar Joshua walikosa na Al Ahly ikashinda nyumbani kwa penalti 4-3. Moawad sasa ana miaka 36 na amestaafu kucheza.
Mwaka jana, Yanga ilitolewa na Etoile du Sahel ya Tunisia katika raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kwa mabao 2-1, katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, Aprili 18, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Kutokana na historia hiyo, Pluijm raia wa Uholanzi ameliambia Championi Jumamosi: “Tumejipanga kuhakikisha tunaitoa Al Ahly kwa kupata ushindi nyumbani halafu tukapambane ugenini.
“Nashukuru najua mbinu zao nyingi tu za uwanjani na nimeshazifanyia kazi na wachezaji wangu hivyo sina hofu kubwa kukabiliana nao, naomba mashabiki wa Yanga waje wengi uwanjani kutushangilia,” alisema Pluijm.
Pluijm alisema, pia anawafahamu wachezaji hatari wa Al Ahly ambao ni kiungo mshambuliaji chipukizi, Ramadan Sobhi na mastraika Malick Evouna na Emad Moteab.
“Hao jamaa ni hatari kutokana na uwezo wao mkubwa wa kupiga chenga, kumiliki mpira na kufunga mabao, hivyo tayari nina mbinu za kuwazuia tunataka kuiona Yanga ikisonga mbele sasa,” alisema Pluijm.
Yanga kwa wiki nzima ilikuwa kambini kisiwani Pemba kujiandaa na wachezaji wote wapo vizuri kwa mchezo huo isipokuwa Matheo Simon na Mbuyu Twite.
Kwa upande wake, Kocha wa Al Ahly, Martin Jol ambaye timu yake jioni ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam alisema; “Mechi yetu na Yanga siyo nyepesi kama watu wanavyofikiri, ni ngumu na tutacheza kwa tahadhari kubwa ili tusiruhusu bao ugenini.
“Kuangalia video tu siyo kama ndiyo tumemaliza kazi, hapana tunahitaji kufanya kazi ya ziada kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ugenini.”
Tofauti na Pluijm, Jol ambaye pia ni raia wa Uholanzi amewahi kuzinoa klabu kubwa Ulaya zikiwemo Tottenham Hotspur na Fulham (za England), Ajax (Uholanzi) na Hamburger SV ya Ujerumani.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Denis Dembele wa Ivory Coast akisaidiwa na Marius Donatien na Moussa Bayere. Kama Yanga ikifanikiwa kuitoa Al Ahly baada ya marudiano wikiendi ijayo nchini Misri, itaingia katika hatua ya makundi.
Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, tiketi za mchezo huo zilianza kuuzwa jana mchana baada ya kuwasili kutoka Uturuki.
“Tumechapa tiketi zetu nchini Uturuki kwa kuogopa hujuma kwa wachapaji wa hapa Tanzania, pia tutatumia vifaa maalum kuzitambua kuepusha tiketi feki,” alisema Muro.

VIKOSI
Katika mchezo wa leo, vikosi vinatarajiwa kuwa; Yanga: Ali Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Vincent Bossou, Kelvin Yondani, Salum Telela, Deus Kaseke, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Simon Msuva.
Al Ahly: Sherf Ekramy, Ahmed Fathy,  Ahmed Hegazy, Ramy Rabiea, Sabry Rahil, Hossam Ghaly, Hossam Ashour, Sobhi, Momen Zakryia, Abdullah Al Saied na Evouna raia Gabon.

No comments