Header Ads

YANGA wakomaa kibishi na kufanikiwa kuichapa Coastal Union kwao bao 2-1

YANGA wamekomaa kibishi jana Jumapili na kufanikiwa kuichapa Coastal Union katika Kombe la FA lakini mechi hiyo ikavunjwa na vurugu. Haikuwa rahisi hata kidogo kupata ushindi huo, mabao ya Yanga yote yalionekana yana utata.
Bila kujali uchovu wa kucheza siku tatu kabla mechi ngumu ya kimataifa dhidi ya Al Ahly, vijana wa Jangwani walikomaa na kuichapa Coastal kwao.

Hata hivyo, kwa mashabiki wa Coastal ilionekana kama Yanga wamebebwa katika mchezo huo lakini utata kwenye maamuzi huwa upo duniani kote.
Coastal Union walionekana kutibua furaha ya Yanga kwa kuwa walikuwa na dalili zote za kushinda mchezo wa jana.

Coastal Union walianza kupata bao dakika ya 54, lililofungwa na Yusouf Sabo akiunganisha krosi ya Ayoub Semtawa. Dakika sita baadaye, Donald Ngoma aliisawazishia Yanga bao ambalo lilikuwa na utata kutokana na wengi kuamini kuwa alikuwa ameotea. Hata hivyo, marudio ya televisheni yalionyesha kuwa alikuwa nyuma ya beki kabla krosi haijapigwa.
Bao hilo lilisababisha vurugu miongoni mwa mashabiki wa Coastal ambao wengine walirusha chupa uwanjani na kusababisha mpira kusimama kwa takribani dakika saba.

Wachezaji wa Coastal walimzonga mwamuzi Abdallah Kambuzi wakilalamikia bao hilo lakini haikusaidia.
Bao la pili la Yanga nalo lilijaa utata, ilipigwa krosi na Juma Abdul kwenye lango la Coastal, kipa Fikirini Bakari akaruka kuudaka kisha akaukosa kabla ya Amissi Tambwe kukutana na mpira ulioonekana aliusindikiza kwa mkono nyavuni na mwamuzi akaweka mpira kati.

Baada ya hapo, Adeyumu Ahmed alipewa kadi nyekundu dakika ya 104 kwa kuunawa kwa makusudi mpira, ambayo ilikuwa ni kadi ya pili ya njano, alionekana kumrushia konde mwamuzi wakati akilalamika na hata alipokuwa akitoka uwanjani, alionekana pia akimrushia konde mwamuzi msaidizi.
Kuanzia hapo mpira haukuendelea tena, kwani mashabiki wa Coastal walikuwa wakirusha mawe uwanjani, hasa upande wa kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.
Kamisaa wa mchezo huo, Osuri Kosuri, alipofuatwa baada ya mechi hiyo kuvunjika, alisema mwamuzi aliamua kuuvunja kutokana na Oscar Joshua kupigwa jiwe huku Dida naye akipigwa.
Mwamuzi msaidizi Charles Simon naye alipigwa jiwe na mashabiki wa Coastal. Hali ya usalama haikuwa shwari na askari wa kutuliza ghasia, walitanda nje na ndani ya Uwanja wa Mkwakwani.

Alipopigiwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura, kuhusiana na hatima ya mechi hiyo, alisema: “Inategemea na ripoti ya kamisaa, kama mazingira ya kuvunjwa mechi hayakuwa yakizihusu timu zote mbili, maana yake wataenda kumalizia dakika zilizobaki, kama mashabiki wa timu moja wamesababisha vurugu maana yake hiyo timu inapoteza mechi.”
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, alisema: “Ripoti ya kamisaa na refarii ndiyo itakupa majibu, naomba nisiongeze zaidi.”  Yanga iliwakilishwa na Deogratius Munishi ‘Dida’, Kelvin Yondani/Malimi Busungu, Deus Kaseke, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Juma Abdul, Haruna Niyonzima, Vincent Bosou, Oscar Joshua, Issofou Boubacar/Simon Msuva na Donald Ngoma/Amissi Tambwe.
Coastal Union: Fikirini Bakari, Yusouf Sabo, Miraj Adam, Adiyou Ahmed, Hamad Juma, Abdulrahim Humud, Ayoub Semtawa, Mahadhi Juma, Ismail Mohamed, Godfrey Wambura, Ayoub Yahaya.
Habari na Musa Mateja, Abdallah Juma, Tanga na Ibrahim Mussa, Dar./GPL

No comments