Header Ads

Chura wa Mtungi wa Maji Moto - 01

MZEE Mahinya ua Mwarabu alikaa dukani akiongea na mkewe, akaangalia nje kupitia dirishani, ghafla akasimama na kutoka... “Mume wangu vipi tena jamani, umeona nini nje?” mkewe alimuuliza... 


“Nakuja bwana,” alisema mzee Mahinya huku akitoka nje kwa kasi. Mkewe, mama Mahinya naye alitoka huku akisemasema... “Huyu mzee hajatulia kabisa jamani, sijui ana nini?” Alimkuta anaongea na mrembo mmoja aliyekuwa anapita nje ya nyumba hiyo ambapo kuna njia... “Sasa unapokataa kuzungumza na mimi binti una maana gani?” “Sina maana mbaya, wewe najua ni mume wa mtu, sasa mimi wa nini jamani? Au unataka kunitafutia matatizo. Haya mkeo huyo katoka,” alisema mrembo huyo huku akianza kutembea... “We binti malayamalaya  hebu subiri,” mama Mahinya alisema huku akishuka ngazi kwa hasira... 

“Mama ee samahani sana! Huwezi kuniita mimi malayamalaya wakati hujui mume wako alinisimamisha kwa sababu gani?! Je, nikisema malaya wewe na mumeo?” “Wee! Huna adabu, mimi na mume wangu tunaweza kuwa malaya? Umefunzwa kweli wewe?” alikuja juu mama Mahinya. *** Mama Mahinya na mume wake walikuwa wakiishi katika maisha ya ndoa lakini hawakujaliwa kupata mtoto hata wa dawa. Walikuwa wakiendesha maisha yao kupitia biashara ya duka lililokuwa nje ya nyumba kwenye chumba cha nje watu walizoea kusema ‘Dukani kwa Mwarabu’.

 Maisha ya mzee huyo siku zote ni kuvaa msuli na singlendi kwa juu. Siku akivaa suruali na shati labda anakwenda kufungasha bidhaa za dukani. Kilio kikubwa na mke wake ni uhuni, kutoka na wasichana wadogo wa rika ambalo angeweza kuwazaa. 

Hali hiyo ikawa ikimfanya mwanamke huyo kuamini kuwa, huenda wangebahatika kuzaa mzee Mahinya asingekuwa hivyo. Mkewe ameshamfumania mpaka akachoka, akaenda kwao, akarudi na akaendelea kumfumania lakini bado hajamzoea. Siku moja alifumaniwa na binti wa jirani yake, mzee Matata tena kwenye chumba cha binti huyo, ikabidi mzee Mahinya aingie chini ya kitanda kifupi, hivyo aliweza kuingiza kichwa tu lakini sehemu kubwa ya nyuma ilikuwa wazi, watu wakamwona na kumpa jina la chura wa maji moto, kisa cha kupewa jina hilo kiko mbele ya chombezo hili... “We mzee Mahinya ulikuwa unaongea naye nini yule msichana?” mke alimgeukia mumewe sasa... 

“Hakuna kitu, wasiwasi wako tu...” “Kama ni wasiwasi wangu mbona ulitoka ndani ghafla?” “Wewe mke wangu rudi ndani bwana,” alisema mzee Mahinya huku akijifunga msuli sawasawa kwani umekuwa na tabia ya kuashiria kuvuka kila mara na kuudaka. Mke na mume hao walirudi dukani, mke akaingia ndani zaidi kufanya kazi zake... “Mzee Mahinya nataka dawa ya meno,” mteja mmoja alifika kununua... “Dawa ya meno umepata...” “Mzee Mahinya, una majani makubwa ya chai?” mama mmoja alimwuliza.“Yapo!” mzee Mahinya alimjibu. “Haya hela hii hapa nipatie.” “Na mimi mzee Mahinya nataka udi wa mia tano,” mrembo mmoja anayeitwa Siha, alisema... “Unataka udi wewe?” “Ndiyo...” “Ah! Wataka kutoka au?” “Ndiyo...” ‘Ha! Watoka kwenda wapi mtoto mzuri wewe?” “Mtoko tu... kwani vipi?” aliuliza Siha baada ya kuona maswali mengi... “Hata mimi nataka kutoka...” “Kwenda wapi?” “Pahali popote...” “Kwa hiyo na wewe utajipaka udi?” “Hapana, mimi napaka pafyumu ile ya Uarabuni... umewahi kujipaka wewe?” “Wala...si inauzwa bei kubwa sana?” “Sana...bei yake mwaweza kula wewe, baba yako, mama yako na ndugu wengine kwa mwezi nzima.” “Hee! Kumbe...” “Eee! Ukipulizia kwenye nguo hii, haitoki mpaka ufue mara sabini na tano..” “He! Sasa kufua nguo mara sabini na tano hiyo nguo si itakuwa imeshachakaa!?”
Ndiyo maana yake, hiyo pafyumu inatumiwa na watu wenye uwezo ukiwa mchomvu utaishia kunusa harufu tu,” mzee Mahinya alimwambia Siha. Baada ya mzee huyo kusema hivyo, siha akajikuta akisema; “Sasa mimi naitaka, najua nikipulizia nguo mara moja tu...” “...basi huhitaji kupulizia tena,” alidakia mzee Mahinya... “Eee, inapunguza gharama...” alisema Siha... “Sasa wewe kaoge, vaa halafu njoo kabla hujaenda kwenye huo mtoko wako,” mzee Mahinya alisema. Siha aliondoka mpaka nyumbani huku akitupa udi nje, akaingia ndani na kwenda kuoga kisha akavaa harakaharaka ili atoke... “Mwenzetu wewe mbona mbiombio leo, vipi?” mama yake alimuuliza Siha... “Nakuja mama,” alisema Siha huku akitoka kwenda kupuliziwa pafyumu... “Loo...pafyumu nikipuliziwa leo mpaka nguo inachanika halafu niilazie damu, siwezi,” alisema Siha huku akikata mitaa kwenda kwa mzee Mahinya. 
Je, nini kitaendelea? Usikose kusoma tukutane hapa wiki ijayo siku kama ya leo Alhamis..


Mtunzi: Irene M Ndauka

No comments