Header Ads

Giza latanda JK kumkabidhi Magufuli uenyekiti CCMMwenyekiti wa ccm Taifa, Jakaya Kikwete (kushoto) akimtambulisha John Magufuli baada ya kuteuliwa rasmi kuwania urais kupitia chama hicho.
 

URITHISHANAJI uongozi kwa hiari ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), unaelekea kukwama baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete, amepata kigugumizi cha kumkabidhi Rais John Magufuli, Juni mwaka huu, kama ilivyotarajiwa.

MWENYEKITI WA CCM TAIFA, JAKAYA KIKWETE (KUSHOTO) AKIMTAMBULISHA JOHN MAGUFULI BAADA YA KUTEULIWA RASMI KUWANIA URAIS KUPITIA CHAMA HICHO.
Hali hiyo inadaiwa kujidhihirisha kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CCM ya iliyokaa mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki ambayo pamoja na mambo mengine, ilitarajiwa kutangaza tarehe ya Mkutano Mkuu Maalum ambao ungetumika kumkabidhi chama Rais Magufuli.
 

Akitoa majumuisho ya kikao hicho juzi mjini Dodoma, msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, alizungumzia mambo mengi bila kutaja tarehe ya mkutano mkuu maalumu.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM kimesema hivi karibuni Baraza la Ushauri la Wazee, linaloundwa na Wenyeviti wa CCM wastaafu na Makamu, litakaa kujadili mambo mbalimbali ikiwAmo makabidhiano ya uongozi wa chama.
 

Baraza hilo linaundwa na Mwenyekiti wake, Raismstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, Marais wastaafu wa Zanzibar, Salmin Amour na Amani Abeid Karume na Makamu wenyeviti wa zamani wa CCM, 

John Malecela na Pius Msekwa.
Chanzo hicho cha uhakika kutoka ndani ya kikao cha kamati kuu kilisema ajenda za kikao hicho cha Kamati Kuu zilikuwa nne, moja ikiwa ni kufungua kikao na kupitisha majina ya wabunge na wawakilishiwanaogombea ujumbe wa halmashauri kuu.
Ajenda nyingine zilikuwa ni Waziri Mkuu kuwasilishahali ya kisiasa bungeni pamoja na ile ya maandalizi ya mkutano mkuu maalumu.
Ajenda ya mkutano mkuu maalum ilitarajiwa kutaja tarehe ya mkutano huo ambao ungetumika kumkabidhi Rais Magufuli uenyekiti wa CCM.
 

Kabla ya kikao hicho cha kamati kuu, imeelezwa, palikuwa na kikao cha ndani kati ya Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Kikwete na Katibu Mkuu wa CCM, Abrahaman Kinana, ambacho kilikubaliana kujadili ajenda hizo kwa kina.
“Kwenye hicho kikao cha watu wanne walikubaliana kabisa kwamba watajadili hayo mambo manne, sasa wakashangaa wamefika kwenye kikao cha Kamati Kuu ajenda zote tatu zimeenda vizuri, ile ya mwishoya mwenyekiti ikapita bila kujadiliwa kwa kina," kilisema chanzo chetu.
 

“Kwa maelezo yake mwenyekiti (Kikwete) anasema bado kuna mambo ambayo hayajakamilika ndiyo maana anataka kusogeza mbele mkutano mkuu maalum wa kumkabidhi (Rais) Magufuli chama,” kilisema.
 

Chanzo kingine kilisema baadhi ya wajumbe wa kikao hicho cha kamati kuu walitaka Kikwete aendelee na nafasi yake mpaka mwakani kama ambavyo katiba yaCCM inamruhusu.
Baada ya hali hiyo, mmoja wa jumbe wa mkutano huo,ambaye pia ni Mbunge wa wabunge wa CCM, imeelezwa, alisimama na kuhoji kwa nini mwenyekiti haonyeshi dhamira ya kukabidhi chama wakati imekuwautamaduni kwa viongozi waliotangulia kufanya hivyo baada ya muda mfupi.
 

Imekuwa desturi kwa viongozi wa CCM kuachiana madaraka kabla ya uchaguzi mkuu wa chama, tofauti na Mwalimu Julius Nyerere ambaye alimwachia Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, uongozi wa chama
baada ya miaka mitano.
 

Nyerere alimkabidhi Mwinyi kijiti cha uenyekiti waCCM Agosti, 1990, licha ya kuwa alianza kuwa Rais mwaka 1985.
 

Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alikabidhiwa chama na Mwinyi mwaka Oktoba, 1996 ikiwa takribani miezi saba baada ya kuchaguliwa, huku naye akimkabidhi Kikwete kiti hicho Juni 2006, ikiwa miezi sita baada ya Uchaguzi Mkuu.
 

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa madai hayo, msemaji wa CCM, Ole Sendeka, alisema jambo hilo halikujitokeza kabisa ndani ya kikao hicho.
 

“Kwanza kama ni mtu anataka kukabidhi chama ni huyu mzee (Kikwete), watu wanataka kumzushia hayo mambo sasa hivi,” alisema na kuongeza ni maneno yasiyo ya kweli ya mitandaoni.
Alipoulizwa ni lini basi mkutano mkuu maalumu wa CCM utakaa kwa ajili ya kurithisha uongozi wa chama kwa Rais Maghufuli, Ole Sendeka alisema maandalizi yanaendelea na yatakapokamilika tarehe itatangazwa rasmi.
 

"Mkutano mkuu si jambo dogo. Maandalizi yanaendelea na hata Mwenyekiti Kikwete amehimiza kuwa yaharakishwe na pale yatakapokamilika basi itatangazwe rasmi," alisema Ole Sendeka.
 

MIZENGWE KATIBU WA WABUNGE
Kampeni za kumpata Katibu wa Wabunge wa CCM zimepamba moto baada ya majina manne ya wanachama watakaowania nafasi hiyo kupitishwa na Kamati Kuu hiyo.
Waliopitishwa ni Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda, Jason Rweikiza (Bukoba Vijijini),Mariam Kisangi (Viti Maalum) na Abdalla Ulega (Mkuranga).
 

Mmoja wa wagombea (jina tunalihifadhi) inadaiwa anapigiwa debe na baadhi ya vigogo wa serikali na CCM ili kuchukua nafasi hiyo.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa siasa za makundi ya urais nazo zimeingia kutokana na baadhi ya viongozi wa CCM kuanza kupanga safu za 'mitandao' yao.
Suala jingine linalofanya vigogo 'kuweka mkono' kwenye uchaguzi huo ni kutaka kudhibiti siasa za wabunge wa CCM Bungeni na kupitisha mambo yao kwa urahisi.

CHANZO: NIPASHE

No comments