Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO - 04


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Waaawoo! Itafanyikia wapi?”
“Nyumbani saa moja usiku.”
“Kesho nitakuletea zawadi nzuuri.”
“Nitafurahi sana, nikuacheni muendelee na mazungumzo, mengi tutazungumza kesho.”
“Asante mpenzi nimefurahi sana kusikia sauti yako.”
“Unishindi mimi.”
SASA ENDELEA...
****
Usiku ulikuwa mrefu kwa Cecy, alitamani siku ya pili ifike haraka ili akaijue hiyo zawadi aliyoahidiwa na Colin. Alijikuta akipindua kitandani usingizi ulikimbia kabisa. Kutokana na kukosa usingizi akiwazia zawadi alijikuta akichelewa kuamka, kitu kilichofanya akose ndizi nzuri.
Kwa vile shida yake ilikuwa kufika kwa kila Colin akachukue zawadi, ilibidi anunue ndizi nzuri kwa wenzake ambazo kwake hazikuwa na faida kwa vile angekwenda kuuuza kwa bei ileile.
Hakuchukua ndizi nyingi, alirudi hadi nyumbani. Baada ya kuoga na kujipamba na kuhakikisha amependeza alibeba ndizi zake na kuelekea kwa mama Colin huku akijiuliza Colin anataka kumpa zawadi gani.
Kama kawaida alipofika kwenye mlango wa geti alibonyeza kengele, mlinzi alimfungulia na kuingia ndani.
“Mmh! Cecy muuza ndizi unapendeza kuliko mfanyakazi ofisini!” Mlinzi alimshangaa Cecy kila siku kupendeza na kuonesha uzuri wake.
“John acha ushamba nani alikuambia muuza ndizi anatakiwa kuwa mchafu?”
“Pamoja na hayo, wee umezidi.”
“Kwa hiyo ulitakaje?”
“Walaa, nakupongeza tu.”
“Asante.”
“Ila mama ametoka sasa hivi umechelewa kama dakika mbili.”
“Na..na Colin?” Cecy alishtuka.
“Ye yupo.”
“Ooh! Afadhali!”
Cecy alisema huku akishusha pumzi ndefu kitu kilichomshangaza mlinzi.
“Mbona umeshusha pumzi?”
“John, mbona una maswali mengi kama polisi?” Cecy alimjia juu mlinzi.
“Basi Cecy nisamehe.”
Cecy alisogea mlangoni wa kuingilia nyumba kubwa, aliweka beseni la ndizi chini na kuita kwa sauti.
“Ndiziii.”
Colin alitoka mlangoni akiwa amebeba mfuko mkubwa kidogo mkononi, Cecy alipomuona alijikuta akipoteza kujiamini na mapigo ya moyo kwenda mbio.
“Karibu mchumba,” Colin alimkaribisha huku akitabasamu.
“Asante.”
Colin alisogea hadi beseni na kuchagua ndizi.
“Mbona leo ndizi kidogo?”
“Chukua zote, nilichelewa kuamka.”
“Ooh!Pole.”
Baada ya kuchukua ndizi aliingia nazo ndani huku akiacha mfuko wake pembeni ya Cecy. Cecy alimsindikiza kwa macho huku moyo wake ukiendelea kuteseka juu ya Colin.
Aliutazama mfuko ulioonekana una vitu ndani, alijiuliza ni wake na kama wake kuna zawadi gani? Lakini hakujua kama ndiyo wake. Baada ya muda alitokeza tena Colin akiwa kwenye tabasamu.
“Mmh! Mchumba samahani nilisahau kukusifia umependeza sana.”
“Asante,” Cecy alijibu huku akiwa ametawaliwa na aibu.
“Jana nilikuahidi nini?” Colin alimuuliza Cecy.
“Zawadi.”
Colin alichukua mfuko na kumpa, Cecy aliupokea kwa kupiga magoti kwa heshima mpaka chini.
“Asante mpe...M..chumba,” Cecy aliingia kigugumizi.
“Usijali, sasa ni hivi...leo jioni nitakuwa na sherehe ndogo ya kuzaliwa kwangu.”
“Waaaooo, hongera mchumba.”
“Asante, naomba kila kilichomo ndani ya mfuko huu, uvae leo kwenye sherehe yangu sawa mchumba?”
“Sawa.”
Colin alimpa elfu ishirini, Cecy alishtuka kwa vile ilikuwa nyingi tofauti na malipo ya siku zote ya shilingi elfu tano.
“Colin mbona nyingi?”
“Usiwe na wasi chukua zote.”
“Asante, kwa hiyo sherehe inaanza saa ngapi?”
“Saa moja usiku, ukikosa utaniudhi.”
“Jamani si usiku?”
“Kodi gari.”
“Basi nitakuja.”
Cecy aliondoka na kumuacha Colin akimsindikiza kwa macho. Wakati Cecy akiingia getini Colin alikuwa ghorofani akimtazama. Aligundua Cecy ni mzuri kuliko Mage, lakini alikosa vigezo kutokana na hali ya maisha kuwa ya sayansi na tekinolojia inayomtaka kila mtu kuwa na elimu ili kukabiliana na kasi yake bila hivyo lazima ikuache.
Wakati Cecy anatoka alipishana getini na Mage aliyekuwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser V8. Colin aliyekuwa ghorofani alishtuka kuona gari la kifahari likiingia nyumbani kwao. Hakuteremka chini haraka, alisubiri kumuona nani anaingia. Baada ya gari kusimama kwenye maegesho alishtuka kumuona Mage akiteremka.
Alijikuta akimsahau Cecy ghafla kutokana na jinsi Mage alivyokuwa amependeza kwa vazi la gauni fupi la rangi nyeusi na weupe lililoishia chini kidogo ya makalio.
Alijikuta akijisemea mwenyewe moyoni.
“Mage ni msichana mrembo sana.”
Aliteremka chini kwenda kumpokea, Mage alipomuona alimkimbilia na kumrukia kwa furaha.
“Waaaoo my husband to be.”
“Waaaooo my wife.”
Walishikana mikono na kuelekea ndani kila mmoja akiwa na furaha tele moyoni. Wakiwa wanaelekea ndani Mage alimwambia Colin.
“Baby, naomba ujitayalishe tuna mtoko mdogo.”
“Wapi baby?”
“Surprise.”
“Mmh! Haya.”
Walikwenda wote chumbani kwa Colin, ili kuokoa muda aliingia bafuni kuoga ili watoke. Akiwa bafuni Mage alimfuata.
“Vipi Mage,” Colin alishtuka huku akigeuka nyuma.
“Nimekuja kukuosha mpenzi wangu, au kuna ubaya?”
Colin hakuwa na jinsi alikubali kuoga na Mage, baada ya kuoga waliondoka kuelekea mjini. Mage alimpeleka kwenye duka la nguo na kumtaka mpenzi wake achague itakayo mpendeza kwenye sherehe yake ya kuzaliwa.
“Colin mpenzi nataka uchague suti nzuuuri, itakayokupendeza jioni ya leo. Nami unichagulie nguo nzuri ambayo tukisimama wakati wa kulishana keki kila mtu moyo umchome.”
“Suti nichagulie wewe, nguo yako nitakuchagulia mimi,” Colin alijibu huku akitabasamu na kufanya Mage auone vizuri uzuri wa mpenzi wake.
“Sawa.”
Walikubaliana kila mmoja kumchagulia mpenzi wake nguo nzuri.
***
Cecy baada ya kutoka kwa kina Colin hakuwa na biashara yoyote alirudi moja kwa moja nyumbani kwao akiwa na shauku ya kuiona zawadi aliyopewa.
Alijikuta akianza kuiamini ndoto yake kuwa Colin naye anampenda kama yeye bila kujali elimu yake ya kata.
Kutokana na kuchanganywa na zawadi, alipofika kwao alisahau kumsalimia hata mama yake aliingia moja kwa moja chumbani kwake na kutoa vilivyokuwemo kwenye mfuko na kuviweka kitandani.
Alikuta gauni zuri la rangi ya zambarau lenye mchanganyiko mweusi kwa mbali. Alishtuka kukuta nguo za ndani mbili moja nyekundu na nyingine nyeupe.
Viatu vilikuwa vya kisigino kirefu kidogo chenye mikanda. Alivaa na kuzunguka chumbani kama miss aliyekuwa akitafuta pointi. Aliufungua mkebe kidogo na kukuta mkufu mdogo ya fedha.
Aliivaa na kuchukua kioo na kujikuta akitabasamu huku akiwa na hamu ya kutoka nje ili walimwengu wamuone alivyopendeza.
“Kumbe na mimi mzuri namna hii, kwa nini Mungu umeninyima elimu?” Cecy alijikuta akianza kulia.
Mama yake alikuwa amesimama mlangoni baada ya kupitwa na mwanaye bila kusemesha na kuacha kazi zake kumfuata ili kujua mwanaye amepatwa na kitu gani.
Alipofika alimuona akitoa vitu kwenye mfuko alitulia mpaka aone mwisho wake. Alishtuka kumuona akitoa nguo za gharama na kuvaa. Alijiuliza amezitoa wapi, lakini hakutaka kumuuliza haraka alisubiri aone mwisho wake.
Kauli ya mwanaye ya kujisifia ilimfanya atabasamu, lakini alipoanza kulia huku akimlaumu Mungu kukosa elimu alimshtua.
“Cecy.”
Cecy alishtuka na kugeuka bila kuitikia huku akifuta machozi, alipomuona mama yake aliitikia.
“Abee mama.”
“Unalia nini?”
“Roho inaniuma kukosa elimu pia nipo njia panda kwa Colin.”
“Kwanza nguo hizi umetoa wapi?” mama yake alikaza sauti.
“Kanipa Colin.”
“Ili?”
“Mama alisema atanipa zawadi, nilipofika kwao leo alinipa na ameniomba leo nihudhulie kwenye sherehe yake ya kuzaliwa.”
“Saa ngapi?”
“Saa moja usiku.”
“Utakwendaje usiku na utarudije?”
“Amenipa hela ya gari.”
“Mmh! Haya, mwisho wako na Colin tutauona.”
“Mama unavyonifikiria sivyo,” Cecy alijitetea.
Mama yake aliachana na mwanaye na kurudi nje kuendelea na kazi zake na kumuacha Cecy akibadili nguo. Aliziweka vizuri nguo zake ambazo alitakiwa kuzivaa jioni ya siku ile.
***
Cecy alitumia zaidi ya nusu saa bafuni kuoga na saa nzima kujipamba kuhakikisha ile inakuwa kete ya kumfanya Colin aamini yeye ni msichana mrembo. Kabla ya kutoka alimwita mama yake aongeze kumremba.
“Mmh! Mwanangu inatosha.”
“Mamaa! Sitaki nionekane tofauti na nitakaowakuta si unajua lazima kutakuwa na wageni wengi.”
Mama yake alimtengeneza mwanaye kwa kumpaka vizuri poda lipsitiki na wanja mwembamba na kumfanya Cecy kuwa kama malkia. Baada ya kujiamini amependeza alitembea taratibu kuelekea barabarani na kukodi gari kuelekea kwa kina Colin.
***
Sherehe ilifanyika kwenye ua wa jengo la nyumba ya kila Colin kwa kupambwa vizuri kuwafanya wageni wafurahie mandhali ile. Wageni walifika kwa wakati kila mmoja alionekana ana maisha mazuri kutokana na magari ya kifahari kupaki kwenye maegesho.
Asilimia kubwa ya wageni walikuwa wamefika na kukaa kwenye nafasi zao huku wakiendelea kutumbuizwa na muziki laini. Kutokana na foleni Cecy alikuwa wa mwisho kuingia, ilikuwa dakika chache kabla ya sherehe haijaanza.
Baada ya kuteremka kwenye teksi, alishika gauni lake kwa kulipandisha juu na kusogea mlangoni. Mlinzi alimfungulia bila kumfahamu kama ni Cecy muuza ndizi kwa jinsi alivyokuwa amependeza kupita kiasi.
Aliingia kwa mwendo wa taratibu kuelekea kwenye kiti kilichokuwa wazi, kila mmoja aligeuka kumuangalia Cecy msichana maskini mwenye elimu duni lakini mwenye urembo wa asili.
Mama Colin aliyekuwa amekaa na mama Mage alishtuka kumuona msichana mrembo lakini mgeni machoni mwake. Alimsindikiza kwa macho mpaka alipokwenda kukaa.
Baada ya Mage kukaa na kupatiwa kinywaji, zilipita dakika tano sherehe ya kuzaliwa Colin ilianza kwa Colin kutokeza akiwa ameongozana na Mage.
Moyo ulimshtuka Cecy lakini hakujua yule msichana aliyetoka naye ndani ni nani yake. Lakini hakutaka kuumiza moyo wake kwa kuamini kabisa huenda yule ni mpambe aliyechaguliwa kwa ajili ya kumsindikiza. Alijikuta akiingia wivu kwa kujiuliza kwa nini hakuchaguliwa yeye ndiye awe mpambe wake.
Lakini kwa upande mwingine aliamini huenda kutojua kingereza kulichangia, kwa vile mambo mengine yanayohitaji kuzungumza kingereza yangemshinda. Wazo lile aliliafiki na kujiona ana deni la kwenda twisheni kujifunza maneno mawili matatu ya Kingereza ili aendane sawa na Colin.
Kila alivyomuangalia Colin alivyokuwa amependeza katika vazi la suti, moyo wake ilizidi kuteketea na kutamani siku ile ndiyo ingekuwa siku ya kuvishwa pete ya uchumba na kila mtu kujua yeye ni mchumba wa Colin angekuwa juu zaidi ya mawingu.
Wakati sherehe ikiendelea Colin alishtuka kutomuona Cecy kwenye sherehe ile, pamoja hakuwa mpenzi wake lakini alitokea kumpenda kumuona kutokana na jinsi alivyojiweka na kuwa tofauti na wasichana wengi wanaotoka familia duni.
Alijikuta akiwa na wasiwasi wa kutomuona kwenye sherehe yake wakati alimualika. Aliondoka kwenye kiti chake na kumfuata mama yake kumuuliza kama amemuona Cecy.
“Vipi Colin?” mama yake aliinama kumsikiliza.
“Eti, hujamuona Cecy?”
“Cecy! Yupi?”
“Mkweo.”
“Mmh! Sikumualika si unajua watu waliokuja hapa mwenye hadhi zao, hivyo angekuwa tofauti na wengine.”
“Mimi nilimualika.”
“Sasa Colin... yule msichana atavaa nini ili alingane na hadhi ya sherehe hii. Inawezekana kabisa John kamzuia getini kutokana na hadhi ya sherehe yako.”
“Kama atakuwa amefanya hivyo atakuwa hakutenda haki kwa vile mimi ndiye niliyemualika.”
Itaendelea

No comments