Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO - 05


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Mmh! Sikumualika si unajua watu waliokuja hapa mwenye hadhi zao, hivyo angekuwa tofauti na wengine.”
“Mimi nilimualika.”
“Sasa Colin... yule msichana atavaa nini ili alingane na hadhi ya sherehe hii. Inawezekana kabisa John kamzuia getini kutokana na hadhi ya sherehe yako.”
“Kama atakuwa amefanya hivyo atakuwa hakutenda haki kwa vile mimi ndiye niliyemualika.”
SASA ENDELEA...
“Achana naye, si muhimu kama sherehe yako,” mama Colin alijibu kwa mkato huku akichukua glasi ya kinywaji na kupeleka mdomoni.
“Hapana,” Colin alisema huku akielekea getini.
Mama yake hakushughulika naye alimuacha aende, alipofika getini alimuuliza John kama amemuona Cecy.
“Sijamuona, sizani kama anaweza kuja kwenye sherehe ya watu wazito kama hii. Kila mmoja kaja na gari la kifahari, msichana mmoja ndiyo kaja na gari la kukodi, muuza ndizi kama Cecy atakaa wapi?” John alisema kwa dharau.
“John au umemkatalia?” Colin alimuuliza huku akimkazia sauti na macho.
“Hapana bosi,”John aliingiwa hofu.
“Sasa kesho aje aseme umemzuia jihesabu huna kazi.”
“Sijamuona kwa kweli, kama akifika nitamruhusu aingie.”
Wakati Colin akirudi ndani, Cecy alikuwa akitoka msalani na kukutana uso kwa uso. Kwa vile Colin alikuwa na hasira alimuona msichana mrembo lakini akili yake haikumtambua.
Baada ya kusalimiana alimchangamkia kama wageni wengine na kutaka kuelekea ukumbini.
“Colin jamani ndiyo nini?” Cecy alimsemesha.
Sauti ya Cecy ilimshtua Colin na kugeuka na kujikuta akitazamana na msichana mrembo.
“Mungu wangu, nini wewe Cecy?” Colin alishtuka.
“Naam, ni mimi,” Cecy alisema kwa sauti ya kike huku akishika mkono mmoja kiunoni na kunesa kwa madaha na macho kuyarembua.
“Yaani huwezi kuamini, natoka nje kukuuliza.”
“John kasemaje?”
“Cecy ulivyopendeza umetuchanganya wengi, kuanzia mama mpaka John getini amekusahau, anasema hajakuona.”
“Jamani! Ndizi ni kazi lakini umbile kazi ya Muumba, ninyimwe kila kitu? Nimemkosea nini Mungu?” Cecy alisema kwa sauti ya kinanda na kumfanya Colin aamini kama si kutangaza uchumba basi yeye angekuwa chaguo lake.
“Basi nimefurahi kukuona pia hongera umependeza sana na karibu sana.”
“Asante.”
“Wacha niwahi sherehe inanisubiri mimi.”
“Hakuna tatizo tupo pamoja.”
“Nilisahau kamsalimie mama ajue upo.”
“Sawa.”
Cecy baada ya kuagana na Colin alikwenda mpaka alipokuwa amekaa mama Colin na kumsemesha.
“Shikamoo ma’ mkwe,” alimsalimia huku akipiga magoti kwa heshima.
“Ha! Cecy mkwe wangu jamani, nisamehe sana nilikusahau nawe umependeza sana.”
“Ni kawaida yangu.”
“Karibu mkwe.”
“Asante, nipo mbele.”
“Hakuna tatizo.”
Mama Colin alimsindikiza mpaka anakaa na kutikisa kichwa na kujisemea moyoni: “Cecy msichana mzuri sana.”
Sherehe iliendelea kila mmoja akiifurahia huku Mc akieleza kila hatua iliyokuwa ikiendelea. Ilifika wakati wa kukata keti, kama kawaida Mage ndiye aliyekata keki na kumlisha kisha Colin kumlisha Mage.
Kisha keki ilikatwa vipande kisha Colin alipita kila meza ya wageni na kumlisha mojamoja huku akipiga naye picha. Baada ya zioezi lile alimwambia mpigapicha ahakikishe anampiga Cecy picha zaidi ya ishirini za mikao tofauti na kumpelekea.
Mpiga picha alifanya kama alivyoelekezwa kwa kumfuata Cecy na kwenda naye kumpiga picha tofauti.
Baada ya zoezi la kulishana keki kumalizika, Colin aliomba kipaza sauti na kuzungumza machache kuhusiana na sherehe yake kwa kuwashukuru wageni waalikwa.
“Kwanza namshukuru wazazi wangu kunizaa kwa mama yangu mzazi kunilea na baba yangu aliyetangulia mbele ya haki. Pia nawashukuru wageni waalikwa kwa kufika katika sherehe ya kuzaliwa kwangu.
“Leo ni siku muhimu na maalumu katika historia ya maisha yangu, kitakacho kifanya ni hatua moja kuelekea katika maisha yangu ya kujitegemea. Wazazi wangu na wageni waalikwa natumia siku ya yangu ya kuzaliwa ili kumtambulisha mchumba wangu kwa kumvisha pete.”
Kauli ile ilifanya moyo wa Cecy ilipuke pa! Na kufanya mapigo ya moyo kwenda kwa kasi. Alijiuliza kauli ile anayoisikia ni ya kweli au anaota ndotoni. Akili yake ilipata jibu la kupewa nguo nzuri na kualikwa kwenye sherehe ile. Aliiona ndoto yake ya mchana kuwa mke wa Colin ilikuwa ikitimia muda si mrefu.
Alitulia akijipa ujasiri ili kunyanyuka kwenda kuvishwa pete mbele ya umati ule akiitwa. Colin aliendelea kuzungumza huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa mkebe wenye pete ya uchumba.
“Jamani naomba mpenzi wangu wa moyo ambaye anatarajiwa kuwa mama wa watoto wangu asogee mbele.”
Kauli ilimfanya Cecy atake kunyanyuka akiamini kabisa yeye ndiye mchumba wa Colin. Kabla hajanyanyuka kwenda mbele alishangaa kumuona Mage msichana aliyetoka naye ndani akisogea mbele akiwa ameshika kifuani asiamini kilichosemwa.
Baada ya kufika hapo Mc alichukua kipaza sauti na kuongoza zoezi lile.
Wakati huo Cecy alikuwa ameingiwa ganzi mwilini na kuona kama Colin kumuita kwenye sherehe ile ilikuwa amemtendea unyama. Alijiuliza kitu gani alichomtendea Colin mpaka kumfanyia ukatiri kama ule. Alijitahidi kuzuia hali ile kwa kushika mkono kifuani kuzuia mapigo yaliyokuwa yakienda kasi huku kijasho chembamba kikimtoka.
Wakati wa kuvishwa Mage pete kilikuwa kipindi kigumu kwa Cecy, ilikuwa sawa na kupasuliwa moyo wake kwa kisu butu bila ganzi. Bila kujielewa presha ilimpanda alishindwa kuizuia na kujikuta akiona kiza kizito mbele yake , alipiga kelele. “Mungu wangu.” alijikuta akinguka chini kama mzigo na kuwashtua waliokuwa wamekaa naye karibu.
Tukio lile lilizua taharuki na kusababisha sherehe kusimama, wakati huo zoezi la pete lilikuwa limeisha. Colin na mama yake walishtuka kusikia aliyeanguka ni Cecy.
Walikimbia eneo la tukio na kumkuta amezungukwa na watu.
“Vipi?” waliuliza kwa sauti ya mshtuko.
“Hata sijui, nilimuona akishika kifuani na kuhema kwa kasi kisha kufumba macho. Nilipotaka kumuuliza nilimsikia akisema Mungu wangu na kushangaa kumuona akianguka chini. Nilijitahidi kumuwahi nilichelewa tayari alikuwa ameanguka chini,” alisema dada mmoja aliyekuwa amekaa meza moja na Cecy.
“Labda ana kifafa?” mmoja alichangia.
“Hapana kile si kifafa, kwa jinsi nilivyomuona si kifafa,” alijibu aliyekaa naye meza moja.
“Kifafa gani kisicho na povu,” mwingine aliongezea.
“Jamani tumuwahishe hospitali,” mama Colin alisema.
“Mama we’ baki na wageni acha mimi nimpeleke,” Colin alisema huku akipiga magoti na kushika kichwa cha Cecy aliyekuwa ametulia kama amelala.
“Hapana Colin wewe baki na wageni kumbuka sherehe ni ya kwako pia umemaliza kumvisha mchumba wako pete muda mfupi, hivyo unatakiwa kuwa naye karibu. Endeleeni na sherehe mimi ninatosha.”
Colin alikubaliana na mama yake, yeye alibaki na kuendelea na sherehe na mama aliyemchukua Cecy na kumuwahisha hospitali.
***
Cecy baada ya kufikishwaa hospitali alichukuliwa vipimo na kuoneka hana tatizo kubwa ila presha ilikuwa juu. Lilifanyika zoezi kuishusha mara moja na kurudi katika hali ya kawaida.
“Nafikiri tatizo siyo kubwa sana, baada ya kumaliza drip nitamruhusu,” daktari alisema.
“Itachukua muda gani?”
“Si muda mrefu mtaondoka naye.”
Mama Colin alitoka na kukaa kwenye makochi huku amekasirika na kulaumu kitendo cha mwanaye kumualika msichana yule ambaye hakuwa na hadhi ya sherehe ile na kufikia kuharibu starehe yake kwa kuacha shughuli ya mwanaye kwa ajili ya msichana dhalili kama yule.
Alipanga kupiga marufuku ukaribu wa Cecy na Colin kwa vile aliuona unataka kwenda ndivyo sivyo. Yeye alitengeneza utani ambao ulimtia wasiwasi kwa mwanaye kuamini ni kweli, akiwa katikati ya mawazo daktari alimshtua:
“Mama mgonjwa wapo yupo tayari unaweza kumchukua.”
Alinyanyuka na kwenda wadini alipomkuta Cecy amekaa kitandani.
“Vipi mkwe?”
“Nashukuru sijambo.”
“Tatizo nini?”
“Hata najua! Nimejikuta nikiona kiza ghafla,” Cecy alipindisha ukweli.
“Imeisha wahi kukutokea?”
“Hata siku moja, hata mimi najishangaa, ila samahani mkwe kwa kuharibu sherehe ya mwanao.”
“Ujaharibu kitu sherehe inaendelea kama kawaida.”
“Naomba uniende nyumbani.”
“Hapana nitakupeleka.”
Alimchukua na kumuwahisha kwao ili yeye ageuke awahi sherehe. Alipomfikisha alimpa elfu hamsini kwa ajili ya kujiangalizia hali yake.
“Mkwe ugua pole.”
“Asante ma’ mkwe.”
Cecy aliagana na mama Colin na kwenda kugonga mlango, mama yake aliyekuwa hana amani na moyo wake toka aondoke mwanaye kwenda kwenye sherehe za usiku.
Muda wote alikuwa macho, mwanaye alipogonga aliwahi kufungua.
“Umerudi mwanangu?”
“Ndi..ndi..ndiyo mama.”
Kauli ya Cecy iliyochanganyikana kigugumizi na kilio ilimshtua.
“Cecy nini mama?”
“Ningejua nisingeenda,” alisema sauti ya kilio.
“Kwa nini?”
“Yaani wameniita kuniumiza! Nimewakosea nini?”
“Kukuumiza! Kivipi?”
“Mama yaani sijawahi kuumizwa moyo wangu kama leo, najua unaniona mtoto mdogo lakini nina hisia kama mtu mwingine, mama inaumaa,” Cecy alisema kwa uchungu huku akishika mkono kifuani.
“Kuna nini mbona uniweki wazi?” mama yake alishtuka.
“Mama Colin wa kuniita kunionesha mchumba wake?”
“Kukuonesha kivipi?”
Cecy alimweleza kila kitu kilivyokuwa katika sherehe, mama yake alishtuka na kusema:
“Mwanangu unataka kujiua bure, nilikueleza na mapema tajiri na sisi kina pangu pakavu wapi na wapi?”
“Kwa nini mama yake ananiita mkwe wakati mwanaye ana mwanamke mwingine?” Cecy aliuliza macho yakijaa machozi.
“Kuna siku alikutamkia suala la uhusiano kati yake na wewe?”
“Hapana.”
“Sasa kuumia huko kumetoka wapi?”
“Mama! Nampenda sana Colin.”
“Ulimwambia unampenda?”
“Nilikuwa naona aibu.”
“Siku zote moyo ni mfungwa wa mapenzi hasa kumpenda asiyejua anapendwa mdomo wako ndiyo wakili wa kuutetea moyo wako. Bila hivyo upendo wako utateketea kama mwanga wa mshumaa mchana wa jua kali, hakuna atakayeuona mwanga wake.”
“Mama, Colin alionesha ananipenda.”
“Nilikueleza toka zamani ule ni utani tu wala hakuna ukweli wowote.”
“Kwa kitendo walichonifanyia siendi tena kwao kuuza ndizi.”
“Mwanangu nikueleze mara ngapi kila kitu kinatokana na baraka za Mungu. Muombe yeye ndiye atakayekuchagulia mwanaume wa maisha yako.”
“Asante mama kwa kunitia moyo.”
“Basi badili nguo kisha uoge ule ulale.”
“Mama hata hamu ya kula ninayo, wacha tu nikalale.”
Cecy aliingia chumbani kwake kulala na kumwacha mama yake akiwa amesimama na kuyafikiria yote aliyoelezwa na mwanaye. Alimuonea huruma kwa kujiingiza kwenye mapenzi ya kumpenda mtu mwenye mpenzi mwingine anayempenda.
Kingine kibaya ilikuwa hali yao duni ambayo ilikuwa tofauti na matazamo ya familia yenye fedha kuwaangalia matajiri na wasomi wenzao. Alijiuliza kwa hali iliyomtokea mwanaye iliyopelekea kupatwa na presha kupelekea kukimbizwa hospitali itachukua muda gani kumtoa.
Aliamini ingemtesa mwanaye kwa kipindi kirefu na kumfanya akose amani ya moyo wake. Lakini aliamini atampatia ushauri nasaha utakaomrudisha katika hali ya kawaida. Aliachana na mawazo yale na kwenda chumbani kwake kulala.

No comments