Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 10


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Kabla hajajibu Mage alitoka chumbani ili awaone wageni ni kina nani, askari mmoja baada ya kumuona alijua ni Mage alibahatisha kwa kumwita jina.
“Mage.”
“Abee.”
“Upo chini ya ulinzi,” alisema askari wa kike.
“He! Kwa kosa gani?” Mage alishtuka.
“Kutokana na tukio lililomtokea mpenzi wako wa zamani.”
SASA ENDELEA...
“Sasa mimi nahusika kivipi?”
“Utajua yote kituoni.”
“Mi siendi,” Mage alitaka kugoma kwenda.
“We nenda wala usihofu, ila jamani chondechonde mwanangu asiguswe wala kulazimisha kusema uongo tutaelewana vibaya.”
“Hakuna tatizo, atakuwa salama baada ya mahojiano atarudi.”
Ilibidi Mage achukuliwe kupelekwa kituo cha kati cha polisi, mama yake alichukua simu na kumpigia mkuu wa polisi ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa mzee Chogo baba yake Mage.
“Vipi shemeji?” ulipokewa upande wa pili.
“Mwanao Mage amekamatwa na vijana wako sasa hivi.”
“Kwa kosa gani?”
Alimwelezea kila kitu, baada ya kumsikiliza alimjibu.
“Basi hakuna tatizo shemeji nitalishughulikia mwenyewe, yupo kituo gani?”
“Cha kati.”
“Usiwe na wasi waache wamuhoji watamwachia tu.”
“Sawa shemeji kwa hiyo niende.”
“Hapana nitamfuta mwenyewe.”
“Asante shemeji.”
Mama Mage baada ya kukata simu alijikuta njia panda, alijifikiria kumpigia simu Colin lakini alijiuliza akimpigia atamwambia nini. Aliamua kukaa kimya ili kusubiri hatima yake ndipo ajue afanye nini.
***
Mage alipelekwa hadi kituoni na kuingizwa chumba cha mahojiano, Inspekta Koleta alikaa mbele ya meza aliyokuwa amekaa Mage na kalatasi ili kuandika mahojiano yale.
“Unaitwa nani?”
“Mage.”
“Nataka jina kamili.”
“Magreth Chogo,” Mage alijibu kwa sauti ya chini kidogo.
“Una umri gani?”
“Miaka 24.”
“Unamfahamu vipi Hans?”
“Namfahamu kama mpenzi wangu wa zamani.”
“Ulijuaje amepata matatizo?”
Mage alielezea jinsi alivyopigiwa simu na shoga yake Brenda ambaye alipigiwa simu rafiki yake Hans, Ndubukile.
“Wewe ulikuwa wapi?”
“Kwa mchumba wangu.”
“Anaitwa nani?”
“Colin.”
“Inasemekana mlikuwa ikipendana sana na Hans kwa nini hakukuoa akamuoa msichana mwingine?”
“Alichaguliwa na wazazi wake.”
“Unafikiri kwa sababu gani alichaguliwa msichana mwingine wakati wewe ndiye uliyekuwa mpenzi wake kila mtu alijua.”
“Kwa kweli kwa hiyo siwezi kujua.”
“Hans alipoona mwanamke mwingine wewe ulichukuliaje?”
“Sikuwa na jinsi ila roho ilinikuma sana.”
“Ulifikiria kufanya nini baada ya kuachwa na Hans?”
“Nilipanga kutojishughulisha na mapenzi tena.”
“Hukupanga kulipa kisasi?”
“Kisasi cha nini?”
“Kwa vile ndoto zako zilikuwa kuolewa na Hans.”
“Ni kweli ndoto zangu zilikuwa kuolewa na Hans lakini sikuwa chaguo la wazazi wake.”
“Unafikiria kwa nini unahusishwa na matukio ya mauaji na shambulizi la Hans?”
“Hata mimi nashangaa.”
“Kuna ukweli gani umelipa kisasi cha kuachwa kuolewa?”
“Hakuna ukweli wowote kwa vile sasa hivi nami nipo katika maandalizi ya ndoa yangu, kwanza nifanye vile kwa ajili gani kwa vile Hans sijagombana naye ameoa tukiwa tunapendana. Pia sikuwa na kinyongo na familia yake.”
“Unaweza kufikiria nani aliyefanya vile?”
“Mmh! Kwa kweli sijui kwa vile niliisha kata mawasiliano na Hans toka alipooa.”
“Kuna taarifa mlikuwa na penzi la siri na Hans?”
“Si kweli, mara nyingi Hans alinitafuta kuniomba msamaha nilimkatalia kwa vile yeye ni mume wa mtu sikutaka kuonekana naingilia ndoa yake hasa baada ya familia yake kutonihitaji.”
Wakiwa katika ya mazungumzo mkuu wa polisi aliingilia Mr Clarence, Inspekta Koleta alinyanyuka na kupiga saluti. Mage alipomuona alifurahi kwani siku zote alikuwa mtu wa karibu katika familia yao.
“Shikamoo baba.”
“Marahaba, kuna nini?”
“Mkuu kuna tukio la mauaji na mashambulizi ambayo inaonekana mshukiwa wa kwanza ni huyu binti,” alijibu Inspekta Koleta.
“Hebu nipe hiyo kalatasi ya maelezo.”
Mkuu wa Polisi Mr Clarence aliichukua na kuisoma kisha aliomba kuzungumza na Mage kidogo. Baada ya kupishwa alimuuliza mswali kuhusiana na tukio lile.
“Mage.”
“Abee baba.”
“Naomba uniambie ukweli ili nikusaidie hata kama umehusika niambie ili nijue jinsi ya kukusaidia,” Mr Clarence alimwambia kwa upole.
“Baba haki ya Mungu sijui chochote zaidi ya kupigiwa simu asubuhi nikiwa kwa mkweo, kwa vile Hans ndiye aliyekuwa chaguo la moyo wangu pia sikukosana naye bali penzi letu lilivunjwa kwa nguvu ya wazazi wake nilishtuka sana kupata habari ile. Huwezi kuamini taarifa ile ilisababisha nitoke hata bila kumuaga mkweo hivi ndiyo nilikuwa najiandaa kwenda kuzungumza na mkweo japo sikutaka ajue nimekuja kumuona mpenzi wangu wa zamani.”
“Una muda gani ujaonana na Hans?”
“Mmh! Sasa ni mwaka na nusu.”
“Kwa nini?”
“Baba, yeye kaoa na mimi Mungu kanipa wangu kuna umuhimu gani kuendeleza ukaribu?”
“Nimekuelewa, sasa nitawaambia utoke kazi yote niachie mimi.”
“Asante baba.”
Mkuu wa polisi alimwita Inspekta Koleta na kumweleza amwachie Mage na kumweleza waendelee na upelelezi kwa vile Mage ahusiki na matukio yake. Walikubaliana na Mage aliruhusiwa kutoka. Mkuu wa Polisi Mr Clarence alimchukua Mage na kumrudisha nyumbani.
Mama yake alifurahi kumuona mwanaye na Mr Mulisa.
“Asante shemeji.”
“Kawaida, nina imani Hans akipata nafuu kila kitu kitakuwa wazi.”
“Tena Mungu ampe afya ili kuwaumbua wenye roho mbaya wanataka kuiharibu harusi na mwanangu.”
“Usiwe na wasi kila kitu kitakwenda kilivyopangwa na aliyetenda unyama ule atajulikana mkono wa dola ni mrefu.”
Mkuu wa polisi aliaga na kumuacha Mage na mama yake, baada ya kuondoka Mage aliagungua kilio.
“Mama kosa langu nini? Mbona familia ya kina Hans wameniandama hivyo, jamani mimi nimuue mke wa Hans na mwanaye na kutaka kumuua Hans ili iweje?”
“Ndiyo dunia mwanangu, kwa vile baba yako yupo atakusimamia.”
“Unajua mama mi’ nilikuwa na wasiwasi labda aliyefanya vile ni Colin.”
“Wee! Temea chini tena usirudie kusema kitu kama hicho, Hans na Colin wapi na wapi?” Mama yake alikuwa mkali.
“Basi mama nisamehe ni mawazo tu.”
“Tena umeniudhi sana, wee kidogo ufe kwa presha kwa kusingiziwa unataka kumpaka shombo mtoto wa watu.”
“Basi mama nisamehe ulikuwa wasiwasi wangu.”
“Nataka uoge ubadili nguo uende kwa mwenzio ukamtoe hofu usimweleze ya kupelekwa polisi.”
“Sawa mama.”
Mage alikwenda kuoga na kubadili nguo alichukua gari na kwenda kwa Colin, akiwa njiani alijawa na mawazo juu ya familia ya Hans kumshukia yeye katika tukio lile.
Alijiuliza kipi hasa kilichofanya wamfikirie yeye kwanza.
Aliona jinsi gani familia ile jinsi ilivyokuwa ikimchukia na kuamini kauli ya mama yake kuwa hata kama angeolewa asingedumu kwenye ndoa yake kwa vile hakuwa chaguo lao.
Alijikuta taratibu mapenzi yake yote akiyahamishia kwa Colin na kuuapia moyo wake kumpenda kwa nguvu zake zote na kwa akili zake zote. Alipofika nyumbani kwao Colin baada ya kuteremka kwenye gari aliingia ndani huku akikimbia kama mtu aliyepagawa. Sebuleni alimkuta mama Colin, alishtuka kumuona katika hali ile.
“Vipi Mage?”
“Mama, mume wangu yupo wapi?” aliuliza akionesha kuchanganyiwa.
Wakati huo Colin alikuwa akitokea chumbani kwake kuja sebuleni, alipomuona alikimbilia na kumkumbatia.
“Jamani mume wanguu!”
“Vipi mbona hivyo?” Colin alishtuka uchangamfu wa Mage uliopitiliza.
“Najua nimekuudhi nisamehe sana, mama nimemuudhi sana mume wangu,” Mage alisema huku akilia.
“Hujamuudhi chochote,” mama Colin alisema.
“Najua nimemuudhi, Colin naomba twende chumbani.”
Walishikana mikono na kuelekea chumbani na kumuacha mama Colin akiwatazama na kuchekelea moyoni na kusema kwa sauti ya chini. “Kweli wanapendana.” Aliwatazama mpaka walipopotea machoni kwake.
Colin na Mage alikwenda hadi chumbani, alipofika ndani Mage alijifupa kifuani kwa mpenzi wake na kuanza kulia kitu kilichomshtua Colin na kuhoji.
“Vipi mpenzi?”
“Colin nisamehe sana mpenzi wangu.”
“Kwa lipi?”
“Najua leo nimekukosea kwa kuondoka bila kukuaga kitu kilichokufanya usumbuke kunitafuta, kibaya zaidi zijapokea simu zako na kukataa kuzungumza na wewe uliponifuata nyumbani.”
“Kumbe ni hayo? Achana nayo.”
“Hapana najua umenikubalia ili yaishe lakini umejenga picha mbaya juu yangu.”
“Walaa.”
“Colin nihukumu hukumu yoyote lakini elewa nakupenda sana mpenzi wangu, nilitaka kufanya surprise lakini ikaenda ndivyo sivyo. Nilishindwa nikueleze nini kwa vile sikuwa na lakukueleza kwa wakati ule hasa baada ya Brenda kunichanganya.”
“Yote mama alinieleza ndiyo maana nilikuelewa toka asubuhi.”
“Colin lakini si unajua nakupenda?” Mage alimuuliza kwa sauti ya kudeka.
“Najua, ndiyo maana upo hapa.”
“Nashukuru kulifahamu hilo.”
Siku ile Mage alishinda pale na kufanya kazi zote za nyumbani ikiwa pamoja na kupika chakula cha jioni. Colin aljikuta akisahau yote na kujiona kama tayari kaisha muoa Mage.
Siku ile muda wote walikuwa pamoja kama kumbikumbi kwa kufanya kazi kwa kusaidizana. Mama Colin muda wote alikuwa mtu wa tabasamu na kuona ndoa ya mwanaye jinsi itakavyojaa furaha na upendo.
Aliwaangalia walivyopendeza kwa kusaidizana kazi zote za jikoni mtu na mchumba wake. Alifumbata mikono yake na kuomba kwa sauti ya chini.
“Eeh! Mwenyezi Mungu baba nijalie ndoa ya wenetu iwe yenye matunda,” baada ya dua alipiga njia ya msalaba kumshukuru Mungu.
Siku ile ilikuwa ya furaha kwa wapenzi wawili kwa Mage ambaye alihamishia mapenzi yake yote kwa Colin baada ya kujua hata kama angempenda vipi Hans asingekuwa na nafasi ndani ya familia yake. Aliona jinsi gani sivyo mpenda mpaka kumzushia shutuma nzito za mauaji ya shambulio la kuua.
Kingine kilichomuweka njia panda kama Mungu atamsaidia Hans kupona atamchukuliaje, lazima naye atangeamini mhusika ni yeye. Lakini kwa upande wa Hans alijua ni vigumu kumshuku yeye kutokana na ukaribu wao ulivyokuwa.
Angekuwa na wasiwasi kama angekuwa akilipigania penzi la Hans. Kama tatizo lile lingemtokea baada ya kuoa lazima Hans angejua ni yeye, lakini baada ya mkewe kupata ujauzito na kujifungua penzi lake alilizika rasmi.
Aliamini ule ndiyo muda wa kulionesha penzi lake halisi kwa Colin, siku ile alilala tena na kuondoka siku ya pili huku kila mmoja akifurahia penzi la mwenzake.
****
Ukaribu wa Mage na Colin kwa kufuatana muda wote kama kumbikumbi, Ulifanya Colin ashindwe kutekeleza ahadi yake kwa kina Cecy. Baada ya kusubiri kwa wiki bila kuonekana dalili zozote za kutekelezwa ahadi. Cecy aliyekuwa amejilaza kitandani na kukosa usingizi.
Alijikuta akinyanyuka kitandani na kumfuata mama yake aliyeamini ameisha pitiwa usingizi ambaye alikuwa na matumaini ya kuyakimbia maisha ya kulala nyumba ya kuvuja na taa ya kibatari.
Alitoka chumbani kwake na kwenda hadi kwenye mlango wa mama yake na kugonga.
“Mama..mama.”
“Unasemaje Cecy,” alimuuliza bila kuamka kwa vile tayari alikuwa amepitiwa usingizi.
“Kuna jambo nataka tushauliane.”
“Jambo gani, kwani lazima tuzungumze usiku?”
“Ndiyo, asubuhi nikiamka nijue cha kufanya.”
“Mmh! Nakuja.”
Mama yake aliamka na kutoka sebuleni, alimkuta Cecy amesimama, mama yake aliketi kwenye kigoda na kumtazama mwanaye aliyekuwa bado amesimama.
“Unasemaje mama?”
“Mama siku zote japo mdogo lakini huwa nayaamini mawazo yangu japokuwa sina elimu kubwa, lakini busara haina elimu bali kipawa toka kwa Mungu.”
“Ni kweli.”
“Hivi mama tulipokuwa tukifanya biashara zetu tulipungukiwa nini?”
“Hatukupungukiwa kitu, kwani maisha ya mwanadamu Mungu ndiye anayetuongoza.”
“Kwa hiyo hatuwezi kumtegemea mtu?”
“Ndiyo, kwani amelaaniwa kila amtegemea mwanadamu.”
“Nimefurahi sana kulifahamu hilo.”
“Ulikuwa una maanisha nini?”
“Huoni kama tunamkosea Mungu kumtegemea mtu.”
“Tunamtegemea nani?”
“Tumeacha kufanya biashara zetu kwa ajili ya Colin aliyetugeuza watoto kutuahidi pipi, leo ni siku ya ngapi hatufanyi biashara kwa ajili ya kusubiri ahadi yake. Wiki inakatika hakuna cha tofari wala mchanga.”
“Cecy mwanangu Colin, naye binadamu huenda amepatwa na matatizo. Hivyo tulitakiwa kuvuta subira.”
“Mama niliyajua haya mapema, sikutaka kukukata kauli kwa vile wewe ni mtu mzima. Lakini nilijua hakuna kitu, Colin atujengee nyumba kwa kipi cha maana tulichompa?”
“Kwa hiyo ulikuwa unasemaje?”
“Kesho asubuhi nakwenda Mabibo kununua ndizi na kuendelea na kazi yangu inayoniweka mjini.”
“Mmh! Si wazo baya.”
Walikubaliana siku ya pili Cecy aendelee na biashara yake ya ndizi kama kawaida. Kila mmoja alirudi chumbani kwake na kupanda kitandani. Cecy alichelewa kulala huku moyo ukimuuma kwa kitendo cha Colin kuwadhalilisha kwa kuwaahidi kitu kisichowezekana.
Alijikuta akimchukia Colin na kuapa hata zungumza naye siku zote za maisha yake. Kutokana na hasira alijikuta akichelewa kulala.
Siku ya pili Cecy aliamka na mapema na kuwahi kununua ndizi, baadaye alirudi nyumbani na kuoga kisha aliingia chumbani na kuchagua nguo za kuiingia nazo mtaani. Alitafuta gauni lililochoka na upande wa khanga uliopauka na kuvaa.
Alitoka kuelekea nje, alipofika mlangoni alisita kidogo na kujiuliza swali.
“Hivi maisha yangu namtegemea nani? Jibu Mungu, kwa nini niishi maisha kwa ajili ya mtu fulani? Ina maana bila Colin sina maisha? Hapana..hapana,” Cecy alisema huku akirudi chumbani na kuvua nguo chakavu na kufungua sanduku lake na kutoa nguo nzuri na kuzivaa kisha alitoka na kuchukua beseni lake la ndizi na kumuaga mama yake aliingia mtaani kuuza ndizi.
Alishangaa siku ile alimaliza ndizi mapema tofauti na alivyobadili mfumo wa maisha baada ya kuumizwa na penzi la Colin na kuamua kuishi kwa kutojijali. Toka alipoamua kuishi maisha yale biashara yake haikuwa kama awali alijikuta akimaliza biashara zake kwa kutembea umbali mrefu pia kutumia muda mwingi.
Alijikuta akijilaumu kwa kupoteza muda wake mwingi kumuwaza Colin mwanaume asiye na mapenzi naye ambaye tayari alikuwa na mpenzi wake. Moyo wake aliutoa kifungoni na kuwa tayari kupokea penzi jipya ila la mtu atakaye mpenda naye ampende ambaye atakuwa sahihi kwa moyo wake.
Hakuwa tayari kumkubali mwanaume anayetumia umaskini wake kufanya naye ngono. Siku zote aliamini mwenye mapenzi ya kweli hawezi kutanguliza ngono mbele zaidi ya upendo kwanza.
Lakini kwa Colin alikuwa radhi kuupoteza usichana wake hata bila ndoa kwani aliamini penzi la Colin lilizidi furaha ya maisha yake. Baada ya matukio yote aliamini muda wa uvumilivu ulikuwa umepita hivyo alitakiwa kitengeneza mawazo mapya na kuwaza kitu kingine kabisa kigeni katika ubongo wake.
Kila usiku ulipoingia alitumia muda mwingi kuwaza maisha wanayoishi ya kuuza ndizi mwisho wake nini. Aliamini muda ule bado ana nguvu alitakiwa atafute njia mbadala itakayomsaidia kukabiliana na ukali wa maisha aweze kumsaidia mama yake. Wazo lilikuwa kila jioni baada ya kutoka kwenye biashara zake ambazo zilikuwa zikifanya vizuri japokuwa changamoto za wanaume zilikuwa kubwa ambazo alikabiliana nayo.
Wazo kubwa lilikuwa aanze kusoma masomo ya jioni kujifunza kingereza ambacho kingemsaidia kufafuta kazi ya kuajiliwa na kuachana na kazi ya kuzurula huku akila vumbi la barabarani.
Wazo lile alimwambia mama yake ambaye naye aliliafiki, jioni ilipofika alikwenda sehemu moja iliyokuwa ikifundisha twisheni na kuomba kusoma kingereza ambacho aliahidiwa kukijua baada ya miezi mitatu. Alilipa ada na kuanza kusoma siku ileile huku akiwa na ndoto za siku moja naye kuzungumza kingereza.
Itaendelea

No comments