Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 16


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Mmh!” mama Colin alishusha pumzi ndefu na kusema:
“Nimekuelewa.”
“Una la ziada?” Mage alimuuliza.
“Mpaka hapo sina, nikuache upumzike.”
SASA ENDELEA...
“Sawa mama msalimie Colin, naendelea kumuombea naye apate mke mwenye mapenzi naye ya kweli.”
“Amen.”
Mama Colin alimwita mama Mage amuage, baada ya kuja alimweleza:
“Dada nikukimbie.”
“Jamani, mbona haraka mmeelewana na mwanao?”
“Tumeelewana na nimemuelewa vizuri sana.”
“Basi nikutoe.”
Waliongozana kutoka nje walipofika nje mama Mage alitaka kujua kama mwanaye amebadili uamuzi.
“Vipi amesemaje?”
“Amesimamia msimamo wake, nami naheshimu alichokisema kwa vile amekuwa mkweli. Japo inauma lakini ndiyo ukweli wenyewe.”
“Bado hatujakata tamaa nitazungumza naye.”
“Muache tu, kwa aliyo zungumza hata kwa mtutu wa bunduki habadili uamuzi wake.”
“Mmh! Sawa, lakini Mage ni mtoto bado nina nafasi kama mzazi,” mama Mage alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
Waliagana na mama Colini aliingia kwenye gari lake kurudi kwake akipata uhakika wa ndoa ya mwanaye kuvunjika.
***
Siku ya pili Mage alimuamsha mama yake aliyekuwa bado amelala, baada ya kuamka alimuaga.
“Mama nasafiri kidogo.”
“Unakwenda wapi?”
“South.”
“Una maanisha Afrika ya kusini?”
“Ndiyo mama.”
“Na nani?”
“Na mchumba wangu.”
“Nani, Colin?’
“Hapana mama, ya Colin yameishafutika moyoni mwangu itabaki kama historia.”
“Unakwenda na Hans?”
“Mama kuna mwingine? huyo ndiye aliyeshikilia maisha yangu.”
“Mmh! Sawa.”
“Bai mama,” Mage alimsogelea mama yake na kumbusu shavuni.
“Mage mwanangu ndiyo umeamua kunivua nguo mbele za watu?” mama yake bado hakuamini.
“Mama nakuahidi nikitoka South barua ya posa inakuja na ndoa itakuwa ya haraka sana. Najua utasahau yote.”
“Mage mwanangu unamuamini vipi Hans mwanaume alikuacha katika wakati mbaya?”
“Lile lilikuwa shinikizo la wazazi wake si uamuzi wake najua kabisa Hans ananipenda sana hata mimi kama ningeolewa na Colin lilikuwa shinikizo letu.”
“Mage mwanangu nani alikulazimisha, si ulikubali kwa hiyari yako?”
“Nilikubali ili kufunika kombe mwanaharamu apite.”
“Mmh! Sawa, safari njema,” mama alisema kwa sauti ya unyonge ambayo haikumshitua Mage.
Mage alitoka hadi nje na kuchukua gari la nyumbani ambalo alikwenda kuliacha uwanja wa ndege. Aliungana na mpenzi wake kwenda Afrika ya kusini kupumzika kwa wiki moja kabla ya kurudi kwa ajili ya maandalizi ya harusi kabambe.
Wakati Mage na zilipendwa wake wakienda kutuliza mawazo Colin naye aliamini kuendelea kuwepo Tanzania kwa muda ule akili yake haitakuwa sawa.
Alipanga siku inayofuata aende Afrika ya Kusini kwa wiki moja ili arudi na mawazo mapya. Kwa vile ndege ilikuwa ikiondoka saa sita mchana Colin alipanga kuondoka saa nne asubuhi ili awahi saa moja kabla ndege haijaondoka baada ya taratibu zote alijiandaa kwa siku ya pili.
Siku ya pili Colin akiwa amejilaza kitandani alikumbuka kitu na kunyanyuka kwenda kwenye kabati na kutoa picha alizompiga Cecy siku ya birth day yake. Alizichukua na kuziweka juu ya kitanda, katika zile picha aliikuta picha moja ya Mage. Alipitia picha mojamoja, aliona kitu cha ajabu mbele ya macho yake Cecy alikuwa msichana mrembo kuliko Mage na kujiuliza kipi kinachomfanya amng’ng’anie Mage wakati kuna almasi juu ya mchanga.
Alitulia akiitazama picha ya Cecy na Mage, mara simu yake iliita, alipoangalia ilikuwa ya rafiki yake Lukonge.
“Niambie Musoti,” alimwita kwa jina alilokuwa akipenda kumtania kutokana na kufanana na umbile la mchezaji wa timu ya Simba, Donald Musoti raia wa Kenya.
“Mzee vipi?”
“Poa za siku?”
“Nzuri naona namba ya South, lini tena huko?”
“Na wiki sasa.”
“Naona mzee umenikumbuka?”
“Kawaida tu, Colin kuna kitu kinanitatiza sina uhakika nacho?”
“Kitu gani?”
“Ngoja nitume picha kwenye WhatsApp kisha utanipa jibu.”
“Poa tuma.”
Baada ya sekunde chache picha iliingia kwenye simu kupitia WhatsApp, aliifungua na kukutana na picha tofauti za Mage akiwa na mwanaume wakiwa katika mkao wa mahaba mazito. Alituliza macho na kushindwa kuelewa picha ile imepigwa lini na Mage yupo wapi. Baada ya muda Lukonge alipiga simu na kuuliza:
“Umeelewa?”
“Ndiyo, hii picha umetoa wapi?”
“Nimezipiga muda si mrefu, huyu si shemeji Mage?”
“Kwani wewe upo wapi kwa sasa?”
“Nipo Hilton hotel hapa Daban.”
“Musoti ni historia ndefu niache kwa muda nitakupigia.”
“Poa.”
Baada ya Lukonge kukata simu, Colin aliziangalia upya zile picha jinsi Mage alivyojiachia na mwanaume Afrika ya kusini. Akiwa katikati ya lindi la mawazo na kumuangalia Mage ambaye aliamini kabisa hakuwa na mapenzi naye na ukweli ilizidi kudhihirika. Mlango uligongwa, aliweka simu pembeni na kunyanyua uso wake kuangali mlangoni bila kusema kitu.
Alijua ni mama yake amerudi baada ya asubuhi kuondoka kwenda kwa mama Mage kutaka kutafuta muafaka. Aliamini picha zile ndizo zitapunguza presha ya mama yake aliyeng’ang’ania kuokoa ndoa yake na Mage ambayo iliisha kufa. Alikumbuka ameacha simu alirudi kitandani na kuichukua ili amuoneshe mama yake zile picha za Mage akiwa na mwanaume nchini Afrika ya kusini.
Baada ya kuichukua simu alirudi hadi mlangoni na kufungua, alishtuka kumuona mwanamke mgeni kwake akitabasamu aliyekuwa na miwani ndogo nyeupe. Aliwekewa kidole mdomoni na kumsukuma kumrudisha ndani, naye hakuwa mbishi alirudi hadi kitandani na kukalishwa. Msichana yule mrembo alifunga mlango na komeo na kugeuka huku akitoa miwani ndogo na kutabasamu.
Colin alikuwa kama anaota baada ya kumuona aliyekuwa amesimama mbele yake ni Cecy hakika alikuwa amependeza sana.
“Ha! Cecy?”
“Ndiyo mimi,” Cecy alijibu kwa madaha.
“Siamini…Siamini Cecy wewe ni mwanamke mzuri sana tena sana.”
“Simshindi Mage.”
“Cecy naomba uachane na kile kichefuchefu.”
“Colin leo unamuona Mage kichefuchefu kwa vile amekukataa?”
“Ilikuwa shinikizo la mama tu lakini ukweli sikuwa na mapenzi naye kama ninavyokupenda,” Colin alijitetea.
“Colin napita nilitaka kujua kama upo,” Cecy baada ya kusema vile aligeuka na kutoka nje.
“Cecy hebu nisikilize.”
“Ungekuwa na shida na mimi ungenifuata nyumbani kwetu.”
Colin aliamini kabisa Cecy alikuwa amechukizwa na kitendo cha kumterekeza na ahadi za uongo. Alitoka mbio kumuwahi Cecy nje, alimkuta amekaribia getini alimfuata na kumshika mkono asiondoke.
“Cecy najua nimekukosea naomba unisamehe.”
“Colin najua hunipendi bali mimi najipendekeza kwako, endelea na Mage wako.”
“Hapana Cecy nakuapia haki ya Mungu wewe ndiye moyo wangu,” Colin alipiga magoti mbele ya Cecy ambaye siku ile alionekana mrembo mara dufu.
“Colin wewe ndiyo wa unifanya hivi au kwa vile mimi ni maskini mbumbumbu sijui lolote, asante,” Cecy alisema kwa sauti ya kilio.
“Ha..ha..Si..si…” Colin alinyamaza baada ya kusikia honi lakini alishindwa kunyanyuka kwa vile alikuwa bado kamshika mkono Cecy akimuomba msamaha.
Geti lilifunguliwa na gari la mama Colin liliingia na kushangaa kumuona mwanaye amepiga magoti mbele ya binti mrembo.
Cecy alipomuona mama Colin akiteremka kwenye gari alimsukuma Colin na kutimua mbio kwenda nje.
“Cecy…Cecy rudi na..na..”
Cecy hakugeuka alitoka hadi nje ya geti, bahati nzuri aliona bajaj inapita aliisimamisha na kupanda kisha alimweleza dereva ampeleke nyumbani kwao. Colin alipotoka nje alikuta ameisha ondoka. Alirudi ndani mbio na kumwambia mlinzi afungue geti, alipanda kwenye gari alilokujanalo mama yake na kumfukuzia Cecy kwa kuamini hasira za Cecy hazikuhitaji kupewa muda zaidi ya kutulizwa haraka la sivyo atakosa bara na pwani.
Mama Colin toka afike alikuwa akijionea vihoja asijue kumetokea nini na yule binti mrembo ni Cecy gani. Alimsogelea mlinzi na kumuuliza.
“Eti yule msichana ni nani?”
“Hata sijui, alikuja na kukuuliza kama upo nikamwambia haupo, akaniuliza Colin nikamwambia yumo ndani. Basi aliingia ndani hata hajakaa niliona akitoka mara nikamuona Colin akimkimbilia na kumshika yule msichana akawa mkali. Nilishangaa kumuona akipiga magoti kumuomba msamaha.”
“Nimesikia anamwita Cecy, ni Cecy yupi?”
“Mmh! Ndiyo leo namuona.”
“Mmh! Sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Hata najua! Labda atakuwa amemfuata huyo msichana.”
Colin aliendesha gari kwa kasi kuitafuta bajaj ambayo ilikuwa imeishapotea kuonesha Cecy alimwambia dereva aikimbize. Aliakanyaga mafuta kuitafuta bajaj kuifuata njia ya kuelekea nyumbani kwao Cecy. Alipokaribia nyumbani kwao alimuona akiteremka kwenye bajaj na kuingia ndani.
Colin alisimamisha gari mbele ya nyumba ya kina Cecy na kuteremka, hakufunga mlango alikimbilia ndani, Cecy alishangaa kumuona Colin pale alimuuliza kwa sauti ya juu.
“Colin umefuata nini hapa kwa masikini?”
“Cecy mpenzi naomba unisikilize.”
“Nikusikilize nini, ni wazi nalazimisha mapenzi nenda kwa Mage mwanamke mwenye uwezo na elimu, niache mimi maskini nisiye na elimu.”
“Ukifanya hivyo utakuwa ukinifunga mikono na kunipiga sitaweza kujitetea, naomba unipe nafasi.”
“Umetudhalilisha vya kutosha kwa kutudanganya kuishi maisha ya peponi leo yapo wapi, najua una chaguo lako naomba uondoke utuache na umaskini wetu.”
“Cecy najua nimewakosea lakini nami ni mwanadamu ninayehitaji kusamehewa kwa vile si mkamilifu.”
Mama Cecy aliyekuwa nyumba ya pili akichota maji aliporudi alishangaa kumkuta Colin kampigia magoti Cecy.
“Kuna nini?” aliuliza kwa mshangao.
“Mama huyu si alikuja hapa kusema nini na alifanya nini?” Cecy aliuliza kwa sauti hasira.
“Mama najua sikuwa mkweli lakini mpango wangu upo palepale.”
“Baada ya kukataliwa na Mage eeh?” Cecy alimuuliza huku amemshikia kiuno.
“Hapana majukumu yalinibana, mama naahidi nikitoka hapa kila nilichoahidi nakitimiza nisipofanya hivyo chukue uamuzi wowote.”
“Tuchukue uamuzi gani ikiwa hatukudai ni hitari yako si lazima,” mama Cecy alisema.
“Mama nilikuwa katika kipindi kibaya ambacho naamini ningelezimisha ningeweza kuwatia kwenye matatizo.”
“Colin, maisha yetu ndiyo haya hatuhitaji msaada wako, hatujaja kwenu kuomba msaada, hata masikini ana nafasi kwa muumba,” Cecy alisema huku machozi ya uchungu yakimtoka.
“Cecy usifike huko, najua unanipenda,nakuhakikishia kulipa upendo mara mbili.”
“Sihitaji,” Cecy alijibu kwa nyodo japo moyo wake wote ulikuwa kwa Colin alitaka kutikisa kibiriti kuona kama kimejaa.
“Cecy najua nimekukosea lakini amini huu ni wakati wako wa kuponya maumivu ya moyo wako.”
“Cecy msamehe mwenzako,” mama Cecy aliingilia kati.
“Basi amka,” Cecy alinyanyua Colin ambaye alikuwa bado amepiga magoti kama muumini aliyekuwa akiungama kanisani.
Colin alinyanyuka na kukumbatiana na Cecy ambaye alijilaza kifuani kwa mpenzi wake, mama yake alikuwa pembeni alitabasamu huku akiomba dua Colin amuoe Cecy ili kutimiza ndoto ya mwanaye.
“Cecy nataka kukuhakikishia mbele ya Mungu, mama yako na mchana wa jua kuwa wewe ndiye mke wangu wa maisha.”
“Muongo Colin unanidanganya,” Cecy alisema kwa sauti ya kudeka.
“Unataka nifanye nini ili uamini ninayosema.”
“Nioe niwe mkeo.”
“Nakuhakikishia kukuoa uwe mke wangu na mimi niwe mumeo.”
“Asante.”
“Naomba sasa hivi twende nyumbani nikamueleze mama mbele yangu.”
“Akikataa?”
“Hawezi, hii ni nafasi yangu ambayo hakuna wa kuiingilia, naomba uniamini.”
“Mmh! Sawa wacha nikaoge ili tuondoke.”
Colin alipewa kiti ili amsubiri Cecy aliyekwenda ndani kubadili nguo, alitoka amejifunga upande wa khanga na kutoka kuelekea bafuni kuoga.
Colin alimsindikiza kwa macho baada ya kupata nafasi ya kuliona umbile la Cecy katika vazi la kanga rangi adimu ya isiyochanganywa madawa ya ngozi.
Aliamini chaguo la kwanza la mama yake lilikuwa sahihi, alijua ni wakati wa mama yake kuamini chaguo la pili halikuwa sahihi bali tamaa ya macho ndiyo iliyompoteza. Cecy baada ya kumaliza kuoga alirudi ndani na kubadili nguo kwa kujipamba kwa vazi la kitenge lililompendeza alionekana mwanamke wa Kiafrika hasa. Alisimama mbele ya Colin na kutabasamu.
“Colin tunaweza kwenda.”
“Duh!” Colin alisema akiwa haamini.
“Ndiye mimi Cecy, mwafrika asilimia ninayejivunia rangi yangu nyeusi.”
“Basi mama inatosha, “Colin alisema huku akinyanyuka na kumshika mkono.
“Mama tunaomba tukukimbie,” Colin alimuaga mama Cecy.
“Haya baba Mungu awatangulie mfike salama.”
“Amina.”
Walishikana mikono na kutoka nje kuelekea kwenye gari, mama Cecy aliwasindikiza kwa macho na kunyanyua mikono juu na kurudi kuomba dua yake ya Colin kumuoa mwanaye ili roho itulie. Hakuteremsha jicho mpaka gari lilipopotea machoni mwake.
Ndani ya gari Cecy moyo wake ulikuwa na furaha nusu kwa vile aliamini lazima Colin atumie nguvu nyingi bila hivyo hakuna mapenzi kwa vile mama yake aliishajenga uadui mapema. Alionekana mtu mwenye mawazo mengi kitu kilichomfanya Colin amshtue.
”Vipi mpenzi?”
“Colin bado moyo wangu una wasiwasi.”
“Wa nini?”
“Jinsi mama yako atakavyonipokea.”
“Ondoa wasi kila kitu niachie mimi.”
Colin alisimamisha gari mbele ya geti na kupiga honi, mlango ulifunguliwa na kuliingiza gari ndani. Alizunguka upande wa pili na kumfungulia Cecy na kumshika mkono kuteremka kwenye gari kwa heshima kisha alielekea naye ndani. Walitembea taratibu kama mtu na mkewe angetokea mtu na kuwaona angejua ni wapenzi wa muda mrefu wanaopendana sana.
Walipofika mlango wa kuingia sebuleni Colin alisema kwa sauti ya unyenyekevu:
“Karibu malkia wangu.”
“Asante mfalme wangu,” Cecy naye alijibu kwa unyenyekevu.
Sauti zile zilimfanya mama Colin aliyekuwa ameinama akisoma biblia kunyanyua macho na kumuona mwanaye na msichana mrembo ambaye aliamini ndiye aliyeondoka muda mfupi uliopita.
“Shikamoo mamkwe!” Cecy alimsalimia mama Colin kwa unyenyekevu huku akipiga magoti ya heshima.
“Marahaba mama, karibu.”
“Asante,” Cecy alijibu huku akinyanyuka na kumfuata Colin aliyekuwa amesimama pembeni yake na kumshika mkono.
Colin alimuongoza Cecy mpaka kwenye sofa na kumkaribisha tena:
“Karibu.”
“Asante,” Cecy alijibu huku akikaa.
“Unatumia kinywaji gani?”
“Chochote utakachonichagulia mfalme wangu.”
“Colin si ungemwita dada wa kazi awahudumie,” mama Colin aliingilia kati.
“Hapana huyu ni mgeni wangu, kila kitu chake nitafanya mimi.”
“Mmh! Haya.”
Muda wote mama Colin alikuwa bado hajaipata picha ya yule msichana mrembo, alituliza macho kwa wizi ndipo alipomgundua kuwa ni Cecy msichana muuza ndizi. Alikunja uso kwa hasira na kuamini kabisa lile si chaguo sahihi kwa mwanaye bali ni papara ya kuachwa na Mage.
Alinyanyuka na kuelekea chumbani kwake, alipotoka eneo la sebule alimwita Colin.
“Colin.”
“Naam mama.”
“Njoo mara moja.”
“Nakuja,” Colin alisema huku akimwekea juisi kwenye glasi na kunywa kidogo kisha alimkaribisha.
“Karibu malkia wangu.”
“Asante mfalme wangu.”
“Samahani namsikiliza mama mara moja.”
“Nenda mpenzi kamsikilize mama.”
Colin alimfuata mama yake kwenye korido alipokuwa amesimama, alimsogelea karibu na kumuuliza:
“Unasemaje maana umenitoka kama kuna kitu?”
“Yule nani?” aliuliza huku akinyoosha kidole sebuleni.
“Mke wangu mtarajiwa chaguo sahihi la moyo wangu.”
“Colin… Colin una tatizo gani wanawake wote wameisha mpaka umfuate huyu maskini mbumbumbu asiyejua kitu. Mwanangu tuna fedha tunaweza kumuona msichana yeyote mzuri mwenye elimu yake kwa fedha yoyote na popote duniani.”

No comments